Dunia ikiwa bado haijamalizana na janga la COVID-19, ambalo limeondoka na roho nyingi za watu na kukwamisha shughuli nyingi za kiuchumi, sasa kuna taharuki mpya imezuka baada ya Shirika la Afya Duniani (WHO) kutangaza virusi vipya vinavyosababisha ugonjwa wa monkeypox.
Monkeypox ni virusi vinavyoambukizwa kutoka kwa wanyama kwenda kwa binadamu ambapo dalili zake zinafanana na zile zilizoonekana hapo awali kwa wagonjwa wa ndui. Pamoja na kutokomeza ugonjwa wa ndui mwaka 1980 na baadae kukomesha chanjo ya ndui, monkeypox pia umeibuka na kuwa kama ugonjwa unaoleta tishio kubwa kwa afya ya umma.
Ugonjwa wa monkeypox ulizoeleka kutokea kwenye baadhi ya sehemu za Afrika tu, lakini tangu Mei 13 hadi sasa WHO imetangaza zaidi ya maambukizi 550 ya watu wenye monkeypox katika nchi 30 duniani zikiwemo Ujerumani, Sweden, Ubelgiji, Ufaransa, Italia, Ureno, Uhispania na Uingereza, pia kesi hizi zimeripotiwa Uholanzi, Australia, Canada na Marekani.
Kinachotisha zaidi ni kwamba ugonjwa huu sasa unaonesha sura mpya kabisa kwani unatokea katika sehemu nyingi kwa wakati mmoja. Je safari hii dunia itafanikiwa kudhibiti mapema janga hili lisije kuleta balaa kama lililoletwa na virusi vya Corona?
Shirika la Afya Duniani limesema kwamba kwa sasa juhudi zake zote zitaelekezwa katika kudhibiti mlipuko huu wa monkeypox kwa kuzuia kadiri liwezavyo maambukizi kati ya binadamu pamoja na kuchunguza na kudhibiti haraka hali hii inayokua kwa kasi.
Nchi nyingi zinazopitia majira manne ya mwaka yaani ya baridi, spring, joto na mpukutiko (autumn), sasa zimeingia kwenye majira ya joto. Kulingana na uzoefu, haya ni majira ambayo yanakuwa na mikusanyiko mingi ya watu. Hivyo WHO limeonesha wasiwasi wake kwamba ugonjwa huu unaweza kusambaaa kwa kasi zaidi duniani.
Katika kuhakikisha ugonjwa huu unabaki nje na hauingii nchini, mamlaka za forodha nchini China zinaendelea kufanya juhudi kubwa kwa sasa, wakati huohuo huku zikiendelea kupambana na janga la COVID-19. Kwa mujibu wa Idara Kuu ya Forodha (GAC), imeandaa wataalamu wa kutathmini hatari, kutoa tahadhari kuhusu virusi vya monkeypox, na kuchukua hatua kali zikiwemo kupima joto la mwili na kuangalia afya kwa wasafiri wanaoingia nchini.
Tunafahamu kuwa China ina uzoefu mkubwa sana wa kukabiliana na virusi hatari. Waswahili wanasema “Ukiumwa na nyoka ukiona ung’ong’o unashtuka” Kwa kuwa China tayari imeshapitia kwenye milipuko ya magonjwa hatari kama vile Sars na Corona na kufanikiwa kudhibiti kwa ufanisi, bila shaka hata ugonjwa huu wa monkeypox pia kwa juhudi za pamoja za China, naamini endapo utafika nchini basi utadhibitiwa haraka na kwa ufanisi mkubwa.
Wahenga wanasema “Nguo ya Ijumaa hufuliwa Alhamis”, kujiandaa mapema kwa China dhidi ya janga hili, kusiwe sababu ya kufanya mataifa mengine kuanza kukaa chini na kufikiria watunge shutuma gani za kuitupia China. Kwani uzoefu unaonesha kuwa kila linapoibuka janga kubwa linaloathiri mataifa mengi duniani, manung’uniko na kunyoosheana vidole huwa havikosekani.
Ushahidi tosha tuliupata wakati lilipoibuka janga la COVID-19, badala ya nchi kupambana na ugonjwa, ziliamua kuirusha China shutuma na kuipaka matope, hadi kusababisha kuchelewa kudhibiti ugojwa huu katika nchi zao na kupelekea vifo vingi zaidi.
Hadi sasa China haijaripoti mgonjwa hata mmoja wa monkeypox. Ingawa ugonjwa huu unaonekana kuweza kudhibitika na hatari yake sio kubwa sana kama ile ya virusi vya Corona, lakini katika mwaka huu tayari kuna baadhi ya nchi za Afrika zimesharipoti vifo vinavyotokana na ugonjwa huu. Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) imesharipoti vifo 9 mwaka huu, na Nigeria kifo kimoja. Hivyo juhudi za pamoja zinahitajika sasa kuliko wakati mwingine wowote ule, ili kuhakikisha janga la monkeypox linadhibitiwa kwa haraka na ndani ya muda mfupi.