NI HII 'DEMOKRASIA' YA DEMOCRAT YA MAREKANI TUHIMIZWAYO KUIFUATA?
MY TAKE
Kwanza nakushukuru sana Mkuu Nguruvi3 na wachangiaji wengine kwa kuendelea kuimarisha jukwaa hili kwa juhudi na maarifa. Pili nakushukuru (Nguruvi3) sana kwa kusaidia kwa kiasi kikubwa kuumulika uchaguzi wa Marekani. Kupitia hapa tumeweza kugundua uendeshaji wa uchaguzi wa kidemokrasia ambao tumekuwa tukishauriwa kuufuata hasa katika vyama vyetu vya siasa hapa nchini na hata katika uendeshaji wa serikali. Kwa kila hatua kuanzia kampeni mpaka sasa kwenye kutangaza wagombea wa vyama nilikuwa na furahia kuona namna demokrasia safi inavyofanya kazi hapo Marekani.
Lakini kugundulika kwa upendeleo katika kupata mgombea wa 'democrat', chama kinachojinasibu kwa demokrasia iliyotukuka na kupitia serikali kinayoongoza kinahimiza nchi nyingine za ulimwengu kuifuata, kimenihuzunisha kweli.
Tujifunze wapi sasa demokrasia ya kweli? Sielewi viongozi wetu wa kisiasa walioalikwa kwenye mikutano ya vyama hivyo kama watadhubutu kutueleza ukweli juu ya hili la 'unafiki' wa demokrasia ya kimarekani? Ukweli hili ni doa kwa wahubiri wa demokrasia ya kimarekani.
Jambo la kushangaza pia ni namna wamarekani (CNN) wanavyojaribu kugeuza mapungufu ya demokrasia yao kwa kuihusisha Kremlin. Wameshindwa kuwalaani na hata kushauri wafukuzwe kwenye chama hao walioshiriki kubadilisha matakwa ya wamarekani wengi kwa sababu wanazozijua wao. Pia hata FBI imejikita kutafuta wale waliowezesha kutoa mapungufu haya ya demokrasia badala ya kuwashughulikia wakandamiza demokrasia. Ni ajabu sana hii, kwa nchi (Marekani) tunayohubiriwa inajali haki, utawala bora, na mengine kama hayo katika uendeshaji wake. Wahusika wa kuhujumu matakwa ya wamarekani wanatakiwa kuadhibiwa zaidi ili kuhalalisha ubora wa demokrasia ya Marekani inayoenezwa ulimwengu.
Kama ndiyo hivi hiyo tume yao ya uchaguzi itakwaje, haki itatendeka?
Ya kwangu ni hayo. Tuendelee kueleweshana juu ya Uchaguzi huu wa wamarekani hadi November,2016 na baada ya hapo.
Mkuu ahsante kwa mchango wako. Kuna hoja ningependa kuchangia katika mabandiko mawili yajayo
1. Ni ukweli usiopinga hakuna demokrasia 100% duniani.
Ukamilifu wa Demokrasia ni kwa viwango
Demokrasia haina ufanano. Ni makubaliano ya jamii katika kupanga, kuamua na kuendesha waliyokubaliana. Utimilifu wa demokrasia ni pale makubaliano yanapotekelezwa hata kama si kwa kiwango chote, lakini katika kiwango kinachokubalika
Ni sawa na mtihani,kuna 'bench mark' kwamba aliyefaulu anatakiwa kiwango fulani.
Sasa kama ni 70 , 80 au 90, wote watakuwa wamekidhi haja.
Tofauti na wenzetu, mauza uza yalitokea nchini na hasa Zanzibar yanatutofautisha nao
Uchaguzi wetu ni kwa utaratibu wetu na viwango vyetu.
Hakuna anayepaswa kutuingilia midhali tumekubaliana.
Wanatuingilia pale ambapo hatukubali tulichokubaliana.
Kufutwa kwa uchaguzi Zanzibar ni mfano mzuri.
Wazanzibar walikubaliana kupitia katiba matokeo yabandikwe, na yalibandikwa.
Wakakubaliana mwenye matatizo ayafikishe tume, hakuna aliyefikisha.
ZEC bila sababu ikafuta matokeo bila msingi wa kisheria unaonyesha mamlaka hayo
Kilichofanyika ni kutangaza uchaguzi mwingine ambao kikatiba hauonyeshwi unless awepo anayeweza kutueleza wapi uchaguzi wa marudio wa jumla umetajwa katika sheria gani.
Katika msingi huo, sisi hatukufikia hata ile bench mark tunayosema wenyewe
Hoja kuhusu sisi si kufuata demokrasia yao, bali kutoheshimu makubaliano yetu wenyewe
Wenye nguvu wanatumia kusimamia makubaliano kinyume na makubaliano husika
Demokrasia ni pana,watu wakipinga kwa hoja. Watu wakipewa fursa ya kujieleza na kueleza duku duku zao. vyama vyote vinapopewa fursa sawa.
Ni pana,matokeo yanatangazwa katika kituo na si 'uhariri' kutoka ''central office''
Demokrasia yao haina msimu, watu wanaruhusiwa kufanya siasa kila siku bila kuwaingilia
Ni Demokrasia pana watu wanapokubaliana kutokukubaliana kwa njia za hiari
Demokrasia ni pana pale vyombo vya umma vinapotumika kwa umma na si kundi la watu
Kwa kiwango chochote, wanaweza kutopata 100% lakini wapo kati ya 80 na 100.
Sisi tupo wapi? Tunawezaje kujilinganisha nao?
Hoja ya pili inafuata