Rais Jakaya Kikwete amekiri kuwa matatizo yanayojitokeza katika mikataba mbalimbali ambayo serikali imeingia na wawekezaji, yanasababishwa na uwezo mdogo wa baadhi ya wataalamu wa kitanzania wanaoshiriki katika majadiliano ya mikataba hiyo.
Rais Kikwete aliiomba serikali ya Norway kuwapatia mafunzo na mbinu za kisayansi wataalamu hao zitakazowapa uwezo wa kujadiliana na wawekezaji kwa kuweka mbele maslahi ya taifa.
Alitoa ombi hilo juzi alipofanya mazungumzo na Waziri wa Maendeleo na Ushirikiano wa Norway, Bw. Erick Solhein, katika siku yake ya mwisho ya ziara rasmi ya kiserikali nchini hapa.
Alisema Tanzania inawahitaji wataalamu na wakufunzi kutoka Norway, kwa kuwa huko nyuma waliwahi kutoa msaada mkubwa sana wakati wa majadiliano ya mikataba, kiasi cha kuwafanya wakubwa katika taasisi fulani ya kimataifa ya fedha kutofurahiwa na umakini ulioonyeshwa kwa upande wa Tanzania.
`Nakumbuka tulipata mtaalamu mmoja mzuri sana kutoka kwenu, alitusaidia sana kiasi cha kuwaudhi wakubwa kwa wale waliokuwa upande wa mwekezaji, na walipoona wanazidiwa kete walimfanyia njama na kumwondoa. Tunawahitaji tena wataalamu kama yule waje kuwafundisha watu wetu,` alisisitiza Rais.
Alifafanua kuwa hivi sasa Tanzania inaendelea kufanya ugunduzi wa rasilimali nyingi zikiwamo za gesi asilia na madini, hali aliyosema kuwa umakini na utaalamu wa hali ya juu unahitajika ili hatimaye mikataba itakayohusu uendelezwaji wa rasilimali hizo ifanyike kwa umakini na kwa uangalifu mkubwa.
Norway kupitia waziri wake huyo imekubali kulifanyia kazi ombi hilo pamoja na lile la kuisaidia kiuwezo na vifaa Taasisi ya Kuzuia Rushwa (TAKURU).
Katika mazungumzo yao, Waziri huyo alimweleza Rais kwamba, Tanzania ndio nchi inayoongoza kwa kupewa umuhimu wa pekee katika masuala ya misaada ya kimaendeleo kuliko nchi yoyote barani Afrika ukiacha Msumbiji.
Alisema Tanzania ni nchi iliyo karibu sana na Norway na kwamba uhusiano kati ya nchi hizo mbili na watu wake haujawahi kutetereka tangu ulipoanza wakati Tanzania ilipopata uhuru wake.
Bw. Erick Solhein alisema Umoja wa Kitaifa, utawala unaozingatia demokrasia na haki za binadamu, utamaduni wa viongozi kuachiana madaraka, maendeleo ya kiuchumi na kijamii, kunaifanya Tanzania kuwa nchi ya kupigiwa mfano Afrika.
Alisema Watanzania wanatakiwa kuuenzi Umoja wa Kitaifa ambao uliasisiwa na Baba wa Taifa, kwa kuwa una umuhimu mkubwa katika maendeleo yao na ya nchi yao.
Katika hatua nyingine akiwa hapa nchini pamoja na kukutana na kufanya mazungumzo na viongozi wakuu wa serikali na utawala wa wafanyabiashara, Rais Jakaya Kikwete pia alikutana na kufanya mazungumzo na Watanzania wanaoishi na kusoma hapa Norway.
Katika salamu zao kwa Rais, wanafunzi wa Kitanzania, walisema kuwa wanaunga mkono, uamuzi wa serikali wa kupitia upya majina ya wanafunzi waliopewa mikopo ili kubainisha wenye uhalali na wasio na uhalali wa kupata mikopo hiyo.
Wanafunzi hao walilalamikia tabia ya baadhi ya waajiri serikalini ya kutowapatia ruhusa wafanyakazi ambao wamepata ufadhili wa kwenda kusoma.
Aidha, walisema kuwa wafanyakazi hao hata pale wanaporejea baada ya kuhitimu mafunzo yao, hawatambuliwi wala kupandishwa vyeo.
Kwa upande wa Watanzania wanaoishi hapa, nao katika salamu zao kwa Rais zilizosomwa na mwakilishi wao Bw. Mafta Himid Yusuf, wao waliiomba serikali kuharakisha utoaji wa vitambulisho vya uraia, kwa kile walichosema kuwa vitambulisho hivyo ni muhimu sana katika ulinzi na usalama wa Watanzania na nchi yao.
Aidha, walipendekeza kuwa serikali itilie mkazo uendelezwaji wa matumizi ya lugha ya Kiswahili kama ambavyo mataifa mengine yanavyotoa kipaumbele kwa lugha zao za kitaifa.
Waliishauri pia serikali iwe makini katika mchakato wa uundwaji wa Shirikisho la Afrika Mashariki huku wakisisitiza wananchi waelimishwe kwa kina kuhusu mchakato huo.
Akijibu hoja hizo na nyingine, Rais alielezea kushangazwa na taarifa za kuwapo kwa watendaji serikalini wanaowazuia watumishi wao kwenda kusoma.