UJIO WA SHIRIKISHO LA AFRIKA MASHARIKI
Habari mbaya kwa Watanzania
NA AZIZ MONGI
NIMESHAWISHIKA kuandika makala haya baada ya kushuhudia kisa cha kusikitisha, kati ya vijana wawili wa kiume, na mmoja wa kike. Kisa hiki kilitokea baada ya vijana hao wa kiume kumuonea gere aibu na ajabu! kijana huyo wa kike, eti, amemleta rafiki yake wa kiume mtaani kwao. Hakukuwa na cha ajabu juu ya rafiki huyo wa kiume wa binti huyo, ila, kwao hao vijana, ulikuwa mwiko kwa rafiki huyo kufika mtaani huko (wenyewe wanakuita Uswazi) na motokaa yake. Lakini kabda sijaendelea na kisa hiki murua, naingia moja kwa moja na mada kuu ya makala haya.
Naam! Lile Shirikisho (la kisiasa) la Afrika Mashariki, ambalo limekuwa likizungumziwa katika nyanja mbali mbali, mitaani, kwenye taasisi mbali mbali, na hata Bungeni (hili sina uhakika nalo...), linabisha hodi hapa kwetu. Gazeti moja la kila siku linalochapishwa kwa lugha ya Kiingereza hivi majuzi limechapisha taarifa kuhusu maoni ambayo yamekuwa yakikusanywa na Kamati Maalum ya Kuratibu Maoni ya Watanzania juu ya Shirikisho la Afrika Mashariki. Sikufanikiwa kusoma taarifa hiyo, ila, ninaamini, kwa vyovyote vile, hakuna kizuri ambacho kimetolewa na taarifa hiyo, kuhusu ujio juo wa Shirikisho la Afrika Mashariki.
Kwa maoni yangu narudia, kwa maoni yangu Shirikisho hilo halina habari njema kwa Watanzania, ila, linakaribisha matatizo kwa Watanzania wengi, kutokana na ukweli kwamba Watanzania ni wagumu na wazito kubadilika. Kwenye mijadala mbali mbali ambayo inaendeshwa na vijana wa Kitanzania, hususan kwenye mtandao wa Intaneti, kumekuwa na maoni mbali mbali juu ya Shirikisho hilo, lakini cha msingi ambacho ndicho ninachokiamini mimi ni kwamba, Watanzania sio tu kwamba ni wavivu, bali pia, ni wazembe na wasiojali kujituma hata kama wanaambiwa baada ya kujituma huko kwao watapata zawadi lukuki.
Tuambizane ukweli. Iko mitaa ambayo siku hizi utawakuta vijana wa kiume wakicheza bao, huku wazee wakikerwa na tabia hiyo mbaya, kiasi cha kuwafukuza mitaani hapo. Wazee hao wamenukuliwa wakisema kwamba hawaoni sababu ya vijana wenye nguvu kushindwa kutwa wakicheza bao, huku wakilia kwamba hawana pesa. Wazee hao wamechukizwa na vitendo hivyo kwa kusema kwamba kuna misitu na mapori ambayo, kama vijana hao wangejituma kuyakata na kujilimia mashamba, wangevuna mazao mengi na kuyauza, hatimaye kupata fedha ambazo wamekuwa wakizililia. Wazee hao wamewapiga marufuku vijana hao kucheza bao, kwani mchezo huo ni kwa wastaafu peke yao, sio vijana wenye nguvu.
Mara nyingi nikiwa ninakatiza mitaa ya kati kati ya Jiji la Dar es Salaam, binafsi, ninalazimika kuomba njia kutoka kwa vijana wenzangu, wa kike na wa kiume, ambao ninawakuta wakizubaa mitaani, kupiga gumzo lisilokuwa na tija, hivyo kuziba njia chache ambazo zimebakia kwa waenda miguu kutokana na wingi wa motokaa kwenye Jiji hili. Inanishangaza, kuona vijana wenzangu wakipoteza muda wao mwingi kuongea mambo yasiyokuwa na maana, wakisimama mitaani kupiga gumzo, wengi wakidai wanapanga dili... wakamtapeli fulani, wakamwibie fulani, wakachomoe kifaa fulani kwenye gari fulani... mambo ambayo, ukiangalia, kwanza ni uhalifu, na pili, ni hasara isiyo kifani ambayo haiwezi kukubalika. Na hawa ni wale vijana ambao, pengine, walisomeshwa kule Mlimani kwa gharama kubwa, walizembea masomo, hawakufaulu, sasa wako mishe mishe wakingojea ujio wa Nuhu kuwashushia neema. Nuhu alikwishafanya kazi yake, hatarudi tena.
Shirikisho la Afrika Mashariki litawakuta vijana wengi wa Kitanzania wakiwa wamelala usingizi mzito, tena wa pono, jambo ambalo litawafanya hata wale walio kwenye ajira kupoteza ajira hizo kutokana na sababu zifuatazo.
Mosi: Uvivu na uzembe ukweli ni kwamba Watanzania wengi ni wavivu na wazembe. Kwenye kampuni nyingi binafsi hapa nchini, waajiri hulalamika kwamba wafanyakazi wao hutumia muda mwingi kuongea, kufanya shughuli binafsi, badala ya kufanya kile ambacho wameajiriwa. Iko mifano mingi, kwa mfano, kazi ambayo ingefanyika kwa muda wa siku moja, inafanyika kwa muda wa siku tatu. Mifano mwingine ni pale ambapo kazi fulani ingetakiwa kufanywa na mtu fulani, mtu huyo anatafuta sababu au anakwepa kutokuifanya kazi hiyo (kwa sababu anazozijua yeye mwenyewe), labda akidai kwamba kazi hiyo haina hadhi ya kufanywa na mtu kama yeye. Anamtafuta mwenzake (ambaye pengine hana ujuzi wa kutosha kufanya kazi hiyo) aifanye badala yake, jambo ambalo, hatimaye linasababisha hasara kubwa, kwani, mara nyingi kazi hiyo hufanyika katika kiwango cha ubora wa hali ya chini kabisa, na mara nyingi zaidi, kazi hiyo haifanyiki kabisa, kutokana na aliyepewa kuifanya kutokujua aanzia wapi na amalizie wapi. Ni sawa na kumtafuta mwalimu bingwa wa Hisabati, na kumpa darasa la lugha ya Kifaransa. Ni bingwa wa Hisabati, lakini kwenye Kifaransa anatoka kapa.
Pili: Ukosefu wa uzalendo jambo hili ambalo ni muhimu mno kwa taifa letu, hivi leo limetufikisha katika hali mbaya, wengi wetu hatujui kwamba tuko kwenye hali mbaya. Wengi wetu tunadhani hali tuliyonayo imetokea tu, na kwamba ni stahili yetu kuishi katika hali hii mbaya. Ninazungumzia hali halisi inayotukabili mitaani kwetu; uchafu uliokithiri kwenye mazingira yetu, uhalifu uliokubuhu, dhulma, unyanyasaji wa wanawake na watoto, wizi, unyanganyi, ukahaba, uendeshaji madanguro, uoneshaji wa picha za sinema za ngono (ambapo pia watoto wadogo huruhusiwa kuona picha hizo, jambo ambalo ni uhalifu), na hili ambalo limekuwa sugu zaidi, yaani, fujo zilizokithiri za madereva wa daladala wawapo mitaani.
Ninasema uzalendo haupatikani tena hapa nchini, kwani, sio tu kwamba umepotea, ila, Watanzania wanajua wajibu wao, ila hawaoni sababu ya kuwajibika. Sio kazi yangu, wanadai. Au Mimi nahusika vipi hapa? Kuna majibu mengi zaidi.
Inashangaza kuwaona wakimchapa kwa bakora, kumpiga kwa mateke, mawe, mapanga na nondo, kijana ambaye atakamatwa kwa wizi wa kuku mtaani kwao (huku yule Mzungu wa Unga akikodoa macho dirishani kwake...), hatimaye kijana huyo kuishia kupata adhabu isiyostahili kosa alilolifanya... kifo kwa kuunguzwa na moto wa petroli. Kesho yake, magazeti yanachapisha habari juu ya kijana aliyeaminika kuwa mwizi aliuwawa na watu wenye hasira baada ya kuchomwa moto na mwili wake kutupwa barabarani..., watu wananunua magazeti hayo, wanasoma, kisha wanafungia vitumbua, maandazi na chapati, siku imeisha. Yule Mzungu wa Unga anayewaharibu vijana wengi kwa kuwauzia madawa ya kulevya bado yuko pale pale, mtaani pale pale, anajulikana, lakini hakuna anayethubutu kutoa taarifa kwenye vyombo husika, kwa kuwa ... sio kazi yake..., vijana wazidi kuteketea. (Labda kwa kuwa askari polisi wanakula rushwa, na wanawataja watoa taarifa za siri?)
Jambo la ajabu ni kwamba, uhalifu unaofanywa na vibaka unaonekana kuwa uhalifu mbaya zaidi kuliko uhalifu unaofanywa na madereva wa daladala. Dereva wa daladala akivunja sheria kwa kupita pembeni, kwenye eneo la wapita miguu, abiria wanafurahi, kwa kuwa wanawahi. Dereva akitanua upande wa kulia wa barabara, abiria wanakenua meno kwa furaha, kwa kuwa wanawahi. Wanawahi wapi? Kuzimu? Kwa nini uhalifu wa kuvunja sheria za barabara unaofanywa na dereva wa daladala usiwe uhalifu, ila, ule unaofanywa na kibaka sugu wa mtaani ndio uonekane uhalifu, tena wa kuishia kuchomwa moto na kibaka yule kupoteza maisha yake? Huu ni unafiki unaosababishwa na ukosefu wa uzalendo.
Tatu: Kushindwa kuweka kipaumbele cha maisha. Ni kweli kabisa, Watanzania wengi hawajui waanzie wapi kuweka kipaumbele cha maisha yao. Ukienda vijijini, kunakodaiwa kuwa na maisha magumu, utaona jinsi watu wanavyoendesha maisha yao kiholela. Wanaishi kwenye nyumba za udongo na miti, wasione kwamba nyumba hizo hazifai kwa maisha ya binadam. Mvua kubwa zilizonyesha hivi karibuni zilizomba nyumba za namna hiyo mkoani Shinyanga na kuwaacha maelfu ya wakazi wa mkoa huo kukosa makazi. Ukirudi mijini, ambako kuna maisha magumu zaidi, hali ni mbaya zaidi. Watu wako radhi kufakamia bia na ulabu badala ya kuwekeza kidogo kidogo, kufyatua matofali mawili au matatu kwa siku, kununua viwanja vya kujenga... ni kweli, mimi binafsi sijajenga, najikosoa pia... tumeshindwa kuweka kipaumbele cha maisha. Ni jambo gani muhimu? Starehe au kuwa na nyumba bora za kisasa? Mbona tuko tayari kuchangishana mamilioni ya fedha kwa ajili ya karamu kubwa ya siku moja Harusi ama Send off wakati tungechanga fedha hizo kuwasomesha watoto wetu kwenye shule bora zaidi, hata nje ya nchi? Hatukujifunza kwa majirani zetu wa Kenya, ambao mpaka leo wanaendesha Harambee ya kuwasomesha watoto wao ughaibuni?
Nne: Kushindwa kujiamini. Hili ni tatizo kubwa sana kwa Watanzania walio wengi. Tatizo hili haliangalii uwezo wa kielimu wa mtu mmoja mmoja, au uwezo wa kiuchumi. Linaangalia ujasiri wao, kama wanaamini kwamba wanaweza kufanya wale ambayo wanakusudia kuyafanya, ama la. Ukweli ni kwamba, wengi wa Watanzania hawajiamini kabisa katika kujaribu mambo mapya. Wako radhi kumsubiri mtu afanye jambo, nao waige. Utakuta, mtaa mmoja dada anafungua salon de coiffeur yake, ama chumba cha kurekebishia nywele, basi, akina dada wengine watafungua saluni hizo bila kujali kama wateja waliopo watawatosheleza, yaani, kutakuwa na uwiano sahihi kati ya watoa huduma na wateja. Hatimaye, inafikia kugombania wateja wachache waliopo, na wengine hata kufanyiana mambo mabaya yasiyofaa kutajwa hapa. Hawakuangalia nini maana ya kuwa mjasiriamali, kwani, mjasiriamali hufanya utafiti na kubaini ni huduma gani ambayo inakosekana katika sehemu fulani, kisha yeye kuchukua fursa ya kuitoa huduma hiyo ili watu wafaidike nayo. Mambo ya kuiga, kweli yanatokea mitaani, kwa sababu Watanzania wameshindwa kujiamini na kujitosa kikamilifu kwenye biashara. Kushindwa kujiamini huku nako kumefikia hata kwa waidhinishaji mikopo, ambao wanaona kwamba watu wenye ngozi nyeusi Waafrika hawana uwezo wa kufanya biashara zinazohitaji mitaji mikubwa, hivyo, wajasiriamali wadogo, mathalan, wachimba madini wadogo, wanapopeleka michanganuo yao kwenye benki mbali mbali, haiyumkini wao kunyimwa, kwa kuwa tu ni Waafrika. Kutokujiamini kunatokea hata kwa waidhinishaji mikopo, ambao hawana imani na wao wenyewe, hivyo, kudhani kwamba hata wachimba madini wadogo watashindwa kuendeleza miradi yao. Lakini akija mzungu? Kwani mzungu peke yake ndiye aliyepangiwa kufanya bishara kubwa kubwa?
Hizi ni sababu tatu kuu ambazo zinatutofautisha sisi Watanzania na majirani zetu wa Kenya na Uganda, ambao wamesonga mbele miaka mingi iliyopita. Hizi ndizo sababu ambazo zitatufanya sisi Watanzania tumezwe na wenzetu hawa, kwa kuwa wana mtazamo tofauti wa maisha. Sisi, ambao tuko kwenye Nchi ya Neema, tumesahau kabisa kwamba tuna utajiri kupita wao, ardhi bora zaidi kupita wao (sehemu kubwa ya Kenya ni jangwa...), na mali asili nyingi zaidi kupita wao (Tanzanite hupatikana Tanzania pekee, lakini Kenya ndio inaongoza kwa mauzo yake duniani...), na kadhalika.
Afrika Mashariki itakapoingia rasmi, tusishangae kujikuta vibarua, tutakaoajiriwa na majirani zetu kutoka Kenya na Uganda. Wao wakiwa mabosi, sisi makuli, mambo yatakuwa mazuri zaidi au mabaya zaidi kwetu?
Nikimalizia, wale vijana niliowaona wakimsarandia yule dada aliyepata ugeni wa ghafla mtaani kwake, kumbe walikuwa wamekunywa pombe kali aina ya gongo. Hivyo, ilikuwa tafrani kubwa mtaani hapo. Badala ya kukaa na kupanga mipango makini ya nini wafanye, wao wanaishia kutwa kulewa mchana, jioni kupora wapita njia. Hayo ni maisha gani? Kijana, fanya kazi, usimwonee wivu dada anayejituma, anayefanya kazi. We unabakia kalaghabaho? Yakhe! Haifai hiyo, mwanaume kumfuatia mambo yake binti anayejituma sio fresh. Huo ni sawa na umbea! Mwanaume mwenye tabia ya umbea hafai kwenye jamii ya siku hizi. Angalau, tunaweza kumvumilia mwanamke mwenye tabia hiyo, ingawa hata kwa wanawake pia tabia hiyo sio nzuri. Umbea haufai! Tufanye kazi, Afrika Mashariki hiyo inakuja, tutamezwa tukitazama bila kuwazuia.
Tuamke! Usingizi mtamu, lakini mbaya!