(Part II)
* Kwa kuitumbukiza Tanzania kwenye "Soko la Pamoja" la Afrika Mashariki, huoni kwamba utakuwa umekiuka kiapo ulichokula cha kuulinda uhuru wa, na mipaka ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ?
* Kulikuwa na sababu gani ya kupambana na Idd Amin aliyetaka kipande "kidogo tu" cha nchi yetu, ikiwa leo tunaigawa sandakarawe nchi nzima kwa kisingizio cha soko la pamoja?
* Tanzania itaondoka SADC? (Tayari nchi nyingine za Afrika Mashariki zimeanza kutuamuru tutoke SADC. SADC imeweka bayana kwamba wakati umefika wa kuchagua kati ya EAF au SADC.) Unadhani itakuwa ni busara kuondoka SADC? Kwa nini usitoe tamko kwamba Tanzania ya kesho ni ndani ya SADC?
* Je sisi wananchi wa Watanzania tutaulizwa kuhusu kujiunga na "Soko la Pamoja la Afrika Mashariki" au ni uamuzi uliofikiwa tayari kwamba tutajiunga na soko la pamoja la Afrika Mashariki?
* Huo Mkataba wa EAC/EAF uko wapi ili tuweze kuuona na kuusoma? Ni Watanzania gani waliousoma na kuuridhia kwamba SASA tunaanza kuwa kwenye mchakato wa kuelekea kwenye Shirikisho? (Inaripotiwa kwamba Tume yako ni sehemu tu ya taratibu ‘chovu' za mchakato huo...)
Watanzania tutafanyaje ili kuondoka kwenye EAF, iwapo Tanzania ijajikaanga yenyewe kwa kuingia kwenye EAF? Vipengele vya kujiondoa kwenye EAF viko wapi? Hautakuwa ni uhaini kuzungumzia kujitoa EAF, kama ambavyo si ruksa kuzungumza kujitoa kwenye Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ?
Mheshimiwa Rais Jakaya Kikwete, maswali hayo na mengine mengi yanaleta changamoto kwako binafsi kwamba zawadi kubwa kuliko zote unazoweza kutupa sisi Watanzania, ni kutukabidhi Tanzania yetu yenye "sovereignty" ileile au zaidi ya uliyokabidhiwa pale utakapoacha madaraka mwaka 2010 au 2015, panapo majaaliwa.
Kwa taarifa yako Mheshimiwa Rais , Tanzania ndiye "Mbuzi wa Shughuli" kwenye Shirikisho la Afrika Mashariki. Na mbuzi huyu amepangwa "kuchinjiwa kwenye maji" ili hata ukelele wake wa mwisho usisike. Hawatarudia makosa ya Jumuia ile iliyokufa 1977, kwa kutuacha bado tunafurukututa. Kujiunga kwa Tanzania EAF kwafanana na Punda wa kwenye hadithi moja iliyochapishwa Tanzania ambamo Simba baada ya kujeruhiwa, alishindwa kuwinda; na Sungura, Fisi na Punda wakaenda kumpa pole. Kumbe Fisi na Sungura walikuwa na lao jambo.
"Simba kwa kuwa huwezi kuwinda naomba unile mimi", alianza kusema Sungura. " Asante sana kwa kunijali, siwezi kukula wewe rafiki yangu. Sasa nimefahamu wewe ni rafiki yangu wa kweli katika kipindi hiki kigumu cha dhiki!" alijibu Simba. Fisi naye akajitoa aliwe na Simba, ambaye pia alikataa kumla, akitoa sababu zilezile.
Sasa Punda akawa njia panda: "Nikikaa kimya nitaonekana mbaya kwa Simba. Kwanza Simba mwenyewe kakataa kuwala wenzangu, na mimi atakataa... acha nijisemee tu kwamba najitolea anile..." aliwaza.
Akaropoka, "Simba kwa kuwa huwezi kuwinda naomba unile mi..." Kabla hajamaliza maneno yake alirukiwa na kuraruliwa palepale.
Kenya, Uganda , Rwanda na Burundi zina ajenda kadhaa kwenye EAF: mbali na zile "rasmi" zinazotangazwa hadharani. Ili ajenda zao zitimie, lazima "Punda" Tanzania awemo kwenye EAF ili aweze "kuliwa". Mheshimiwa Rais, ni wajibu na heshima kwako kuhakikisha Tanzania haijiungi na EAF kwa kuwa Tanzania haina ajenda mbali na ngonjera za kisiasa, pengine na posho za vikao kwa baadhi ya watu.
Kwanza Tanzania siyo lazima ijiunge au ikubaliane na kila kitu kwenye ushirikiano wa Afrika Mashariki. Wachache wanaounga mkono kujiunga na shirikisho la afrika mashariki, wanadai upo umuhimu wa kujiunga kwa vile "dunia nzima mwelekeo ni kujiunga pamoja, kama vile Jumuia ya Ulaya, EU". Kama sababu ni hiyo, kwa nini tusibakie SADC tuliko? Hivi tulipigania uhuru wa kusini mwa Afrika ili iweje? Watanzania tulitoa damu zetu, mali na uhai wetu, kukomboa Ndugu zetu walio Kusini mwa Afrika, sasa ukombozi umepatikana, pana wakati gani muafaka zaidi ya huu kuendeleza undugu wetu? Majirani zetu wa Afrika Mashariki tutaendelea kushiriana nao, kama tunavyoendelea kushirikiana na majirani zetu wengine. Kutojiunga kwenye shirikisho siyo maana yake tutakuwa maadui!
Tanzania lazima ikae mbali na EAF, hata ikibidi kwa miongo kadhaa ijayo, ikiwa si moja kwa moja. Kwanza , Muungano wetu wenyewe una "mipasuko" ambayo haijasilibwa bado. Kabla ya kuulizwa kuhusu Shirikisho la Afrika Mashariki, tuulizwe basi kuhusu Muungano wa Tanganyika na Zanzibar . Tanganyika na Zanzibar , mara baada ya kupata Uhuru, hazikutimiza miaka mitano, "zikaishia" na kuwa Taifa moja Tanzania . Sasa jamani, Tanzania hata miaka hamsini haijafikia, nayo "iishie", tena kusikoeleweka? Tanzania ina manufaa tele SADC, kuliko kwenye shirikisho la Afrika Mashariki. Hivi, wakati tulipokuwa "Mstari wa Mbele wa Ukombozi Kusini mwa Afrika", majirani zetu wa Kenya na Uganda walikuwa wapi? Leo hii tukiwakubalia kuondoka SADC, watatuona timamu kweli?
Mheshimiwa Rais Kikwete, kiasi inaeleweka ikiwa unaona pana ugumu wa wewe kuonekana unakwenda tofauti na Watawala wetu waliotutangulia, ambao huenda wanapendelea kuona EAF ikizinduliwa, Tanzania ikiwemo. Lakini mheshimiwa Rais, ndiyo maana kukawa na kikomo cha utawala cha vipindi viwiliviwili! Kwa kuwa umechaguliwa kwa ushindi "wa kishindo", imani yetu Watanzania imekuwa kwako kwamba utaweza kuipeleka Tanzania kule tunakotaka. Na tunakotaka sisi Watanzania siyo kwenye "soko la pamoja la afrika mashariki" wala EAF. Huo Muungano tu wa Forodha wa Afrika Mashariki unatekelezwaje? Matatizo na mizengwe iliyoko panaashiria nini pindi tukiwagaia nchi hii yote kwenye Shirikisho au "soko la pamoja"? Siyo maafa, Mheshimiwa Rais?
Mheshimiwa Rais Kikwete, kwenye Jumuia ya Ulaya --EU, Uingereza na Jamhuri ya Ireland SIYO mataifa yaliyoko kwenye "Mkataba wa Schengen" wa Jumuia ya Ulaya, mkataba unaoondoa mipaka na vizuizi baina ya nchi za Jumuia ya Ulaya kwenye masuala ya Uhamiaji, japo Uingereza na Jamhuri ya Ireland ni wanachama kamili wa Jumuia ya Ulaya. Hii haikuzuia Ufaransa, Uholanzi, Ubelgiji, Ujerumani na nchi nyinginezo za EU zilizokubali kusaini kuendelea na "Makubaliano ya Schengen". Kadhalika , Iceland , Norway na Uswisi zimesaini "Mkataba wa Schengen" japo nchi hizo SI zanachama Jumuia ya Ulaya. Kila taifa linaangalia maslahi yake kama taifa. . Ulipoanzishwa umoja wa Forodha wa Afrika Mashariki takriban karne moja iliyopita, Tanganyika haikujiunga mpaka ilipoona vema kwamba itakuwa ni kwa maslahi yake kujiunga.
Hii haikuzizuia Kenya na Uganda kuanzisha Umoja wao wa Forodha. Tanganyika ilijiunga baadaye! Hata ile Jumuia ya Afrika Mashariki iliyovunjika, ilianzishwa baada ya kupita MIAKA HAMSINI tangu kuanzishwa ule Umoja wa Forodha wa Afrika Mashariki, japo nchi hizi zote tatu zilikuwa zinatawaliwa na Mkoloni mmoja takriban muda wote huo. Haraka ya sasa hivi ya nini? Wanajua wakituachia muda, tukienda hatua kwa hatua, hawataweza tena kuigeuza Tanzania koloni lao.
Tanzania iendelee kuwa mwanachama wa SADC, na kuendelea kuwa imesaini kwa muda makubaliano ya Umoja wa Forodha wa Afrika Mashariki mpaka pale SADC itakapoanzisha Umoja wa Forodha wa SADC, ambapo Tanzania itajitoa kwenye Umoja wa Forodha wa Afrika Mashariki. Au busara zaidi, ni vyema Tanzania ikajitoa SASA HIVI toka Umoja wa Forodha wa Afrika Mashariki, na kuelekeza nguvu zake kwenye SADC. Kenya , Uganda , Rwanda na Burundi zinaweza kuendelea na Umoja wao wa Forodha, Soko la Pamoja na Shirikisho (waliite vyovyote wapendavyo), bila Tanzania kuwemo.
* Mheshimiwa Rais, ukubwa wa eneo la ardhi ya Tanzania ni zaidi ya Jumla ya eneo lote la ardhi ya Kenya , Uganda , Rwanda na Burundi ukizichanganya pamoja -- bila kuzungumzia rasilmali zilizoko. Halafu wanasema tuchanganye ardhi yetu na zao, halafu tugawane sawasawa kwa jina la "Soko la Pamoja la Afrika Mashariki". Hivi tukikubali ujuha huo, ni kwa nini wasituone sisi mazuzu?
Swali kuu tunaloulizwa Watanzania na Tume yako mheshimiwa Rais ni iwapo Watanzania tunaona bado kuna sababu za Tanzania kuendelea kuwa nchi huru ambayo ni "dola", wakati ambapo kuna shinikizo nchi yetu igawe uhuru wake kwa kisingizio cha "soko la pamoja" na "shirikisho la Afrika Mashariki". Tuchukulie kwa mfano, tume itawahoji na kupokea maoni toka kwa watu laki mbili. Kati yao 80% wakasema Tanzania ijiunge kwenye "Soko la Pamoja" na "Shirikisho la Afrika Mashariki", 20% wakasema tusijiunge.
Je, Mheshimiwa Rais, hiyo itakuwa na maana uamuzi utakuwa umesilibwa wa Tanzania kufikia mwisho wake, kwa kujiunga na Soko la Pamoja na Shirikisho la Afrika Mashariki? Je, hutatumia busara kama ilivyotumika kwenye Tume ya Nyalali ya Vyama Vingi pale Tanzania ilipoangalia maslahi ya taifa, na kuruhusu mfumo wa vyama vingi, bila kuangalia asilimia zilizotokana na tume? Ikiwa kweli kabisa umedhamiria kuipeleka Tanzania kwenye mwisho wake machinjioni Afrika Mashariki, kwa nini usiweke KURA YA MAONI kwa kila Mtanzania kupiga kura yake, badala ya kutumia Tume, angalau basi kuchelewesha kwa muda mauti ya Taifa Tanzania? "Soko la Pamoja" na pacha wake "Shirikisho la Afrika Mashariki" maana yake ni mwisho wa uhai wa Taifa la Tanzania .
Ikiwa Tanzania itajinyonga (Mungu apishie mbali!) kwa kusaini mkataba wa "Soko la Pamoja la Afrika Mashariki" au ule wa "Shirikisho la Afrika Mashariki", basi Watanzania tutasahau "maisha bora kwa kila Mtanzania" na itabidi tujiandae kwa "Bora Maisha kwa kila Mtanzania", na kwamba wewe Rais wetu, Jakaya Kikwete, utakuwa umefeli vibaya kabisa jukumu lako la msingi tulilokupa -- kulinda uhuru na umoja wa Taifa la Tanzania na kubakisha Taifa la Tanzania kuwa dola huru kwa manufaa ya Watanzania mpaka pale utakapomkabidhi madaraka ya Urais wa dola la Tanzania huru Mtanzania mwingine.
Kwa kuandika barua hii, imani yetu Watanzania kwako Rais wetu kwamba utaweza kuhimili mashinikizo yote ya nje, na kutusikiliza sisi raia zako, tunaotaka tubakie na taifa letu huru la dola ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania .
Mwenyezi Mungu akujalie. Amin.
Ndimi,
Mlenge Fanuel
Raia na Mwananchi wa Tanzania,
Simu: +255 75 4372902,
Email:
mlenge@yahoo.com,
Dar es Salaam, Tanzania.