Mbunge Kenya awatoa hofu Watanzania
Na Mwandishi Wetu
MWENYEKITI wa Wabunge wa Kenya anayemaliza muda wake, Kadis Motela, amewataka Watanzania waache kuwahofu wenzao katika Afrika Mashariki, kwamba mipaka ikifunguliwa ajira zao zitapokonywa na wageni.
Alisema badala yake nafasi za ajira zitaongezeka kwani kufunguliwa kwa mipaka kunaenda na kumiminika kwa rasilimali kutoka nje ya nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Motela alisema hayo, alipokuwa anazindua kitabu cha Politics of Partnership kilichotungwa na Mbunge wa Afrika Mashariki kutoka Tanzania, Dk. George Nangale kueleza siasa ya Muungano wa nchi hizo tatu, kwa kutumia uzoefu wa miaka mitano aliyotumikia bunge hilo.
Hafla hiyo, ilifanyika juzi jioni katika ukumbi wa Karimjee na kuhudhuriwa na baadhi ya wanasiasa na wasomi maarufu kama vile, Dk. Pius Ngwandu, Zitto Kabwe, Paul Rupia, Hulda Kibacha, Dk. Harrison Mwakyembe, Kate Kamba na Profesa Raphael Mwalyosi.
Hulda na Kate walikuwa na Dk. Nangale, katika Bunge la Afrika Mashariki.
Pia, Motela alizungumzia suala la ardhi akitaka iwekwe sera nzuri za kusimamia ardhi nchini, ili kufungua milango kwa wawekezaji kuja kuendesha shughuli zao nchini na kupanua nafasi za ajira na uzalishaji kitaifa.
Mtu akizalisha kahawa Tanzania itakuwa kahawa ya Tanzania, acheni ardhi iwe ya Watanzania. Woga huu unatuchelewesha kuendelea, alisema Motela na kuongeza: Kinachotakiwa, tengenezeni sheria nzuri ziwalinde vizazi vijavyo.
Kuhusiana na kitabu kilichotungwa, Motela alisema ni cha kipekee, kwani kitakuwa cha manufaa kwa wanasiasa na watu wa Afrika Mashariki na kuwa mtunzi amefanya jambo la kipekee kati ya wabunge wote wa Afrika Mashariki.
Dk. Nangale kwa upande wake, alisema baada ya uzinduzi atazunguka katika vyuo vikuu mbalimbali vilivyo Afrika Mashariki na kupata mawazo zaidi ili afanye mapitio ya kuboresha kitabu hicho.
Pia, Dk. Ngwandu aliyejitambulisha kama baba wa ukoo wa Dk. Nangale, alimshauri mtunzi kufanya uzinduzi wa kitabu katika miji mbalimbali nchini na nchi nyingine za Afrika Mashariki ili kukipatia umaarufu.
Baadhi ya waliopewa nafasi ya kuzungumza, akiwemo mbunge Kabwe na Profesa Mwalyosi, walielezea kuvutiwa na kazi nzuri ya mwansiasa huyo.
Chanzo: Gazeti la Uhuru la tarehe 28 Oktoba 2006