Siku ya Kimataifa ya Vazi la Hijabu
Mwili wa Marwa al Sherbini, mwanamke wa Kimisri aliyedungwa kisu mpaka akafa shahidi katika mahakama ya Ujerumaji umezikwa katika mji wa Alexandria nchini kwao. Shughuli ya mazishi ya mwanamke huyo ambaye sasa amekuwa mashuhuri kwa jina la "Shahidi wa Vazi la Hijabu", imehudhuriwa na maelfu ya watu wakiwemo mawaziri wa serikali na wabunge.
Hadhirina waliokuwa na hasira katika mazishi hayo walipiga nara wakilaani siasa na msimamo usiokuwa wa kimantiki wa serikali ya Cairo kuhusu mauaji hayo ya kinyama. Vilevile Waislamu wa Misri wamechukizwa mno na kutohudhuria balozi wa Ujerumani mjini Cairo katika mazishi hayo na kimya cha vyombo vya habari vya nchi za Magharibi kuhusu mauaji hayo ya kigaidi.
Watumiaji wa mtandao wa Islamonline wametoa pendekezo kwamba siku ya kuuawa shahidi Marwa al Sherbini ipewe jina la Siku ya Kimataifa ya Vazi la Hijab
Jinai hiyo ya kutisha ilitokea baada ya Mjerumani mwenye umri wa miaka 28 kwa jina la Alex W. kumshambulia kwa maneno Marwa al Sherbini na kumvunjia heshima kwa matusi kutokana na vazi lake la Kiislamu la hijabu. Mjerumani huyo alimrukia mwanamke huyo na kumvua hijabu huku akimwita kuwa ni gaidi. Bibi al Sherbini aliwasilisha mashtaka mahakamani ambako Mjerumani mchokozi alihukumiwa kulipa faini ya Euro 750. Mhalifu huyo alikata rufaa mahakamani na hapohapo akamshambulia mwanamke huyo aliyekuwa na mimba ya miezi mitatu na kumuua shahidi kwa kumdunga kisu mara 18. Mjerumani huyo pia alimjeruhi mume wa mwanamke huyo. Maafa hayo hayakuishia hapo, bali polisi wa Ujerumani pia alimpiga risasi mbili mguuni mume wa Marwa kwa madai kwamba alidhani ndiye aliyemshambulia raia wa Ujerumani.
Maelfu ya Waislamu wameandamana mbele ya ubalozi wa Ujerumani mjini Cairo wakilaani mauaji hayo na kutaka kuchukuliwe hatua kali dhidi ya mhalifu huyo. Waandamanaji hao wamesisitiza kuwa ugaidi ni mwana aliyezaliwa huko Magharibi na kwamba mauaji ya kikatili ya Marwa, mwanamke Muislamu ambaye kosa lake pekee ni kuvaa vazi la hijabu, ni maafa ya kibinadamu. Tariq al Sherbini, kaka yake marehemu Marwa amesema kuwa mauaji ya mwanamke huyo yameonyesha kwamba ugaidi halisi uko katika nchi za Magharibi. Mwendesha Mashtaka wa mji wa Dresden nchini Ujerumani Christian Avenarius ameyataka mashambulizi hayo kuwa yanatokana na hisia za kibaguzi.
Mhariri Mkuu wa gazeti huru la al Shuruq ameandika kuwa:
'
Dunia ingekubwa na vilio na makelele mengi lau kama angeuawa Myahudi badala ya Bibi Marwa al Sherbini.'
Mauaji ya mwanamke huyo Muislamu nchini Ujerumani tena mbele ya polisi na ndani ya jengo la mahakama yamezidisha wasiwasi kwamba hisia za kupiga vita dini ya Kiislamu na ufashisti vimeanza kukita mizizi barani Ulaya.