UTPC
Journalists' Union
- Apr 17, 2026
- 51
- 38
Utangulizi
Baada ya kuangazia ukubwa wa tatizo, vyanzo, na athari za ukataji miti hovyo katika Halmashauri ya Wilaya ya Chunya Mkoani Mbeya kupitia makala mbili zilizopita, sehemu hii ya tatu na ya mwisho inajikita katika kuchambua hatua za kuchukua ili kudhibiti hali hii.
Hatua hizi ni muhimu katika kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi ambayo tayari yameanza kuathiri mazingira na maisha ya wananchi wa wilaya hii. Bila hatua madhubuti, misitu ya Chunya iko hatarini kutoweka kabisa, jambo linalohatarisha usalama wa viumbe hai na binadamu.
Kilimo Himilivu: Jibu la Mabadiliko ya Tabia Nchi
Kutokana na uharibifu wa misitu unaochochewa na kilimo cha tumbaku na uhaba wa mvua, wataalamu wanashauri wakulima kubadili mfumo wa kilimo na kujikita katika mazao yanayostahimili ukame.
Mtaalamu wa Kilimo katika Kata ya Sangambi, Raymond Choga, anaeleza kuwa mabadiliko ya tabia nchi yameleta changamoto ya mvua zisizotabirika—nyakati nyingine zikiwa nyingi kupita kiasi na nyakati nyingine zikiwa chache mno. Ili kukabiliana na hali hii, sasa hivi wanafundisha mbinu za "Kilimo Himilivu" (Climate-Smart Agriculture).
Mbinu hizi zinawataka wakulima kufuata kanuni bora za kitaalamu, kufuatilia taarifa za utabiri wa hali ya hewa, na kutumia mbegu bora zinazokomaa haraka na zinazovumilia ukame.
Kuongeza Nguvu Kazi na Ajira ya Misitu
Kwa mujibu wa Sheria ya Misitu Namba 14 ya Mwaka 2002, Kifungu cha 26, mamlaka inatolewa kwa vijiji na jamii kusimamia misitu yao. Hata hivyo, utekelezaji wake unakabiliwa na changamoto ya rasilimali watu.
Mhifadhi wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) Wilayani Chunya, Elias Malima, anasisitiza kuwa ili kudhibiti uvunaji haramu wa misitu, Serikali inapaswa kuajiri watumishi wengi zaidi watakaoweza kusambaa na kukagua wilaya nzima ya Chunya.
Anasema kuwa doria zinazofanyika hivi sasa zinakamata kiasi kidogo tu cha uharibifu unaofanyika maeneo ya ndani ya misitu kutokana na jiografia ya eneo hilo kuwa kubwa na ngumu kufikika.
Malima pia amebainisha changamoto kubwa ya usafirishaji wa mkaa kwa kutumia pikipiki. Amefafanua kuwa pikipiki zinazobeba mkaa mwingi na kufunika gari au kuzuia uono wa nyuma ni haramu na ni tishio kwa usalama wa barabarani.
TFS kwa kushirikiana na vyombo vya usalama barabarani imekuwa ikiendesha oparesheni za kuwakamata wasafirishaji hawa wanaokwepa vizuizi rasmi kwa kupita njia za panya.
Suluhisho la Ajira kwa Vijana na Mikopo ya Vikundi
Mbali na hatua za kisheria, wadau mbalimbali wanasisitiza kuwa suluhisho la kudumu la kulinda misitu ni kutoa ajira mbadala kwa vijana.
Diwani wa Kata ya Chokaa, Joshua Mlambalala, anaipongeza TFS kwa oparesheni za kudhibiti uharibifu lakini anashauri kuwepo kwa mikopo ya vikundi vya vijana.
Mlambalala anafafanua kuwa kupitia mikopo ya Halmashauri (asilimia 10), vijana wanaweza kupewa mitaji ya Shilingi milioni 5 hadi milioni 10 ili kuanzisha biashara halali.
Hatua hii itawasaidia kuacha kutegemea biashara haramu ya mkaa na ukataji miti, kwani vijana wengi wanajihusisha na uharibifu huo kwa kisingizio cha kukosekana kwa ajira.
Naye Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Chunya, Kelvin Jackson, amesema Halmashauri imejipanga kusimamia sheria za mazingira na kuanzisha mkakati wa kuhakikisha kila kata inakuwa na shamba la miti.
Pia, Halmashauri itashirikiana na wataalamu ili kuhakikisha kila mwananchi anayekata mti kwa matumizi yoyote, anawajibika kupanda mti mwingine badala yake.
Changamoto ya Siasa katika Uhifadhi
Pamoja na mikakati hiyo, kikwazo kikubwa kimebainishwa kuwa ni mwingiliano wa masuala ya kisiasa katika utekelezaji wa sheria. Mbunge wa Jimbo la Lupa, Masache Kasaka, amekemea vikali tabia ya baadhi ya wanasiasa wanaovamia maeneo ya hifadhi au kuwalinda wahalifu wa misitu kwa kisingizio cha kulinda kura zao wakati wa uchaguzi.
Kasaka amesisitiza kuwa sheria ni msumeno na haipaswi kuangalia chama, wadhifa, wala umaarufu wa mtu. Ameweka wazi kuwa oparesheni za kuwaondoa wavamizi wote waliopo ndani ya misitu ya hifadhi wilayani Chunya zitakuwa endelevu na hazitatazama masuala ya kisiasa.
Nishati Mbadala: Ushauri kwa Serikali
Katika ngazi ya kitaifa, Katibu Mkuu Kiongozi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Mhandisi Zena Ahmed Said, akizungumza jijini Mbeya, amebainisha kuwa nishati mbadala ni nguzo muhimu katika kulinda misitu. Lengo la tatu la Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050 linalenga kuifanya Tanzania kuwa nchi inayohifadhi rasilimali za asili kwa uendelevu.
Mhandisi Zena ameshauri kuwa ili kuhamasisha matumizi ya gesi badala ya mkaa, Serikali inapaswa kuangalia uwezekano wa kupunguza bei ya mitungi ya gesi ili wananchi wa kipato cha chini wamudu kuinunua.
Pia, amewasihi wananchi kujenga tabia ya kuweka akiba ndogo ndogo za fedha kwa ajili ya kujaza gesi mara inapoisha, badala ya kurudi kwenye matumizi ya kuni na mkaa.
Hitimisho
Mapambano dhidi ya mabadiliko ya tabia nchi na ukataji miti hovyo wilayani Chunya yanahitaji ushirikiano wa dhati kati ya jamii, viongozi wa vijiji, na vyombo vya dola.
Kupitia kilimo himilivu, utoaji wa ajira mbadala kwa vijana, udhibiti wa siasa kwenye uhifadhi, na upatikanaji wa nishati mbadala ya bei nafuu, misitu ya Chunya inaweza kuokolewa kwa ajili ya kizazi cha sasa na cha baadaye.
Andiko la: Mwanaisha Makumbuli
Makala imeandaliwa na Mwandishi anayeshiriki katika programu maalum ya kukuza uandishi wa maslahi kwa umma (Public Interest Journalism Fellowship) inayoratibiwa na UTPC kwa kushirikiana na IMS.