SoC02 Elimu Bure Imeifikisha hapa Sekta ya Elimu

SoC02 Elimu Bure Imeifikisha hapa Sekta ya Elimu

Stories of Change - 2022 Competition

Ri ri

Senior Member
Joined
Aug 28, 2022
Posts
141
Reaction score
219
Utangulizi
Sera ya elimu bure hapa nchini ilianza kutekelezwa na Serikali ya awamu ya tano. Sera hiyo ya elimu bila malipo inahusisha shule zote za Umma za msingi na sekondari. Ndani ya miaka mitano (2016-2020) ya utekelezaji wake, Idadi ya wanafunzi wanaoandikishwa katika shule zote hapa nchini imekuwa ikipanda mwaka hadi mwaka. Idadi ya uandikishaji wa wanafunzi wa shule za msingi iliongezeka kwa takribani asilimia 5.8 kila mwaka wakati uandikishaji wa wanafunzi wa sekondari uliongezeka kwa wastani wa asilimia 10.3 kila mwaka.(Takwimu za Msingi, Tanzania 2020).


pic-shule.jpg

(picha kutoka mtandaoni)

Kuongezeka kwa idadi ya wanafunzi kila mwaka bila kuwepo maboresho yoyote ya mazingira ya kujifunzia na kufundishia kumesababisha mfumo wa utoaji elimu kulemewa na kuzidi kuzorota siku hadi siku.


Shule hizi zimegeuka kuwa sehemu ambapo wanafunzi wanaenda kukutana na kusogeza siku wakisubiri kuhitimu na siyo kujifunza tena.

Sera ya elimu bure imeongeza mwitikio wa wazazi/walezi kuandikisha wanafunzi shule na kupunguza idadi ya watoto waliokuwa wanakaa mitaani bila kwenda shule, japokuwa mazingira ya kujifunzia ni kikwazo.

Hali ni mbaya mno katika shule zetu hizi ambapo wanafunzi wanafika hadi darasa la 3 bila kujua kusoma, kuhesabu na kuandika.


Hali hiyo inasababishwa na darasa kuwa na idadi kubwa ya wanafunzi ambayo mwalimu anashindwa kuimudu, ingawa tatizo la utoro nalo linachangia ambapo wazazi hawatimizi majukumu yao ya kufuatilia maendeleo ya watoto wao na kudhani serikali imemaliza kila kitu kwa kuondoa ada.

Ukosefu wa mahitaji muhimu kama chakula unaotokana na umaskini unachangia wanafunzi kushindwa kuhudhuria masomo na mwisho wake kuacha shule kabisa.


Wanafunzi kuacha shule ni changamoto kubwa mno ambapo takwimu zinaonesha mwaka 2019 watoto takribani 167834 wa shule za msingi nchini waliacha shule kwa sababu mbalimbali kama vile utoro, kurudia darasa, umbali wa shule, ukosefu wa mahitaji muhimu na mimba za utotoni.(Takwimu za Msingi za elimu 2020).

Ingawa ripoti ya BEST 2021 imebaini wanafunzi wanaoacha shule kwa sababu ya mimba imepungua toka wanafunzi 1135 mwaka 2019 hadi wanafunzi 989 mwaka 2020 kwa shule za msingi. Shule za sekondari pia idadi imepungua toka wanafunzi 5398 mwaka 2019 hadi wanafunzi 4543 mwaka 2020, lakini namba hizo zinaonyesha dhahiri bado safari ni ndefu.


Utofauti wa ubora wa elimu kati ya mijini na vijijini ni janga lingine hapa nchini, ambapo tukiangalia mazingira ya kufundishia na kujifunzia yaliyopo vijijini ni tofauti na mazingira ya kufundishia na kujifunzia yaliyopo mijini.

Ukifuatilia kiundani utagundua kuwa walimu na wanafunzi wa maeneo ya pembezoni wana changamoto zao ambazo hazipo shule za mijini. Uhaba wa walimu kupitiliza, kukosekana makazi ya walimu na huduma za afya, shule kutokuwa na madarasa ya kutosha ambapo wanafunzi wengine hulazimika kusomea nje, hakuna vyoo, madawati wala mifumo ya maji na umeme, wakati shule zilizopo maeneo ya mijini zina ahueni zikiwa na walimu wa masomo yote, madarasa ya wanafunzi, vyoo,huduma za afya, mifumo ya maji na umeme.

Tukiangalia sera ya elimu na mafunzo ya mwaka 2014 inapendekeza uwepo wa fursa za elimu na mafunzo nchini kwa usawa kinyume na hali ilivyo ambapo shule za pembezoni zinaachwa nyuma.

Upungufu mkubwa wa walimu uliosababishwa na ongezeko la wanafunzi kila mwaka. Kwa mujibu wa ripoti ya CAG ya mwaka 2021, tathmini ya uwiano wa walimu na wanafunzi iliyofanyika katika mamlaka 48 za serikali za mitaa ilibaini upungufu wa walimu 16577 ambao ni sawa na asilimia 41.


Pia kuna mabadiliko ya mitaala yasiyohusisha walimu na wadau wengine wa elimu, mfano mwaka 2015 kulikuwa na mabadiliko ya mtaala kwa darasa la 1 na la 2 bila kuwaandaa walimu, hali iliyopelekea walimu kurudi katika ufundishaji wa mtaala wa zamani.

Mapendekezo
·Kuanzishwe mafunzo endelevu ya walimu wa shule zote hapa nchini pamoja na wakufunzi wa vyuo vya elimu ya ufundi. Mafunzo hayo yatawanoa walimu hao kuendana na mabadiliko ya sayansi na teknolojia pamoja na mahitaji ya mitaala.
·Matumizi ya tafiti na takwimu katika kufanya maamuzi na kutatua changamoto katika sekta ya elimu, ili kuepuka kupeleka walimu na nyenzo za kujifunzia maeneo yasiyokuwa na uhitaji. Mwaka 2014 ripoti ya CAG ilibainisha walimu zaidi ya 2960 wa masomo ya sanaa walipelekwa katika shule zisizo na uhitaji wa walimu hao huku shule zenye uhitaji zikiachwa solemba.
·Serikali kugharamia huduma ya chakula ili huduma hiyo ipatikane bila malipo (bure) katika shule zote nchini.Hatua hii itawapa hamasa wanafunzi kuhudhuria masomo hivyo kuongeza ufaulu na kupunguza utoro na idadi ya wanafunzi wanaoacha shule.
·Serikali kuajiri walimu wapya ili kuenda sambamba na ongezeko la wanafunzi na kufikia uwiano wa mwalimu 1 kwa wanafunzi 45 uliopendekezwa na Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014.
·Kuboreshwa kwa miundombinu ya kujifunzia na kufundishia katika shule zote nchini kama ifuatavyo,
-ujenzi wa nyumba za walimu, kuongeza madarasa, matundu ya vyoo pamoja na kuongeza mishahara ya walimu ili kuwapa motisha katika kutimiza majukumu yao,

-kuhakikisha uwepo wa maabara za sayansi pamoja na vifaa vya majaribio katika shule zote za sekondari,
-kuhakikisha upatikanaji wa huduma za maji na umeme katika shule zote nchini,
-kuhakikisha shule zote za msingi na sekondari nchini zinakuwa na maktaba na vipindi vya wanafunzi kujisomea wenyewe ili kujenga tabia ya wanafunzi kupenda kujifunza.
·Pia napendekeza utekelezaji wa mipango ya maendeleo ya sekta ya elimu kutoa vipaumbele kwa shule za vijijini ili kuondoa utofauti uliopo hivi sasa na kuleta uwiano sawa wa ubora wa elimu kati ya mijini na vijijini.
·Serikali kuandaa mpango endelevu wa utoaji wa elimu ya afya ya uzazi katika shule za msingi (darasa la 6 na 7) na sekondari nchini ili kupunguza idadi ya mimba za utotoni, mikoa ya Morogoro, Arusha, Mwanza na Dodoma ipewe kipaumbele.
·Mwisho niwaombe wazazi/walezi tutimize wajibu wetu kwa kushirikiana na walimu kufuatilia mienendo na maendeleo ya watoto wetu, pia jamii kwa ujumla tuonapo mtoto mwenye umri wa kutakiwa kuwepo shule anarandaranda mitaani tusilifumbie macho suala hilo.

Hitimisho
Natoa wito kwa Serikali kuongeza bajeti katika sekta ya elimu ili kuboresha miundombinu ya elimu sambamba na kujenga utamaduni wa kufanyia tafiti mipango/sera/matamko ya maendeleo kabla ya utekelezaji, Kama sera ya elimu bure ingefanyiwa utafiti kabla ya kutekelezwa, Serikali ingejiandaa kuboresha miundombinu ya kujifunzia na kufundishia kabla ya utekelezaji na isingeleta athari kubwa katika ubora wa elimu kama hali ilivyo hivi sasa.
 
Upvote 3
Back
Top Bottom