SoC03 Elimu na maarifa ni mali ya Umma. Kipaji na ujuzi ni mali binafsi

SoC03 Elimu na maarifa ni mali ya Umma. Kipaji na ujuzi ni mali binafsi

Stories of Change - 2023 Competition

Baba Jenifa

Member
Joined
May 14, 2023
Posts
5
Reaction score
14
Naandika nikiwa nimeketi nyuma kabisa ya darasa lenye zaidi ya wanafunzi mia moja, wote tukingoja shahada miezi kadhaa ijayo. Mbele kidogo yupo fundi wa mpira na medali zake, na mbele kabisa mwandishi wa mashairi na riwaya katupia miwani yake na tuzo za hapa na pale, na kuna mdada mmoja fundi wa kusuka aliyefungua saluni yake na mwingine mwanamitindo kiasi, kashiriki mashindano kadhaa

Tunafanana
Wote tunaingoja Novemba tuvae joho tule kiapo, turushe kofia juu na baadaye tusajiliwe na baraza tuungane na wengine mtaani wenye elimu na maarifa kama yetu. Nakumbuka mara ya mwisho kupigwa fimbo na mzee wangu alisema “nawatandika kwa sababu mnafanana tabia” nani atamkemea mwenzake au kumshauri ikiwa wote mnafanya makosa yale yale??. Basi hakuangaika na fimbo alitumia mkanda wote tukachezea. Nimekua nikatambua kufanana sana si heri bali heri ni kujua kuwa elimu inatufananisha na ujuzi, ubunifu na vipaji hututofautisha.

Mali ya umma na mali binafsi
Hapa darasani kila mtu ameweza kusoma,kuelimika na kupata maarifa mengi, kila mtu katika mia na zaidi, lakini si kila mtu anaweza kucheza mpira na kungára au kuandika na kupokelewa na wasomaji, au kubuni mitindo ya vitu, au kusuka, au kuimba, au kucheza na tukanyanyuka tumuone, au kuigiza, labda na kughani, au kushawishi na tumsikilize yeye tu, vitu vya kipekee sana hivi.

Elimu imetufananisha ni kama huduma ya umma, ujuzi na vipaji vinatutofautisha maana ni mali binafsi

Ni gharama nafuu kupata huduma kutoka katika taasisi za umma na wengi tunaweza kumudu. Kwa upande mwingine ni ghali kupata huduma kutoka katika taasisi binafsi kama hospitali, shule n.k. kwa kifupi mali binafsi ni chache na ni ghali. Uchache na utofauti huongeza thamani pia.
Katika soko la sasa shughuli binafsi zinalipa pengine zaidi ya mshahara. Kuna fursa katika uchache na upekee. Ipo fursa , ipo.

TUFANYE NINI?
  • Watoto wengi wana mbegu za vipaji na ni rahisi kuwapa ujuzi mbalimbali

Tukitazama kwa karibu tunaweza kujua upekee wa watoto wetu. Kuna mzee mmoja alimuambia mkewe “usimchape mwanao akichelewa kutoka mpirani, siku moja mfuatilie uangalie anavyocheza, pengine ni mwanasoka wa baadaye”. Pengine ni mchoraji wa aina yake, au mwanamuziki kwa sauti yake au mwandishi mchanga. Sote tunaona watoto wakiimba katika runinga, wakiandika, wakichora, wakiigiza, si muujiza bali ni jicho la mzazi. Tunaweza kupalilia talanta za watoto wetu na kuwafundisha fani mbalimbali nje ya elimu yao ya shuleni kwani uchache na utofauti huongeza thamani

Kwa maana rahisi pengine kuliko zote, mazingira ni mambo yote yanayomzunguka mtu. Kama mtu huyo ni mtoto basi mazingira ni mambo yote yanayomzunguka mtoto. Na mtu hujengwa na vitu viwili, moja ni yeye mwenyewe na pili ni mazingira yake, mazingira ya mtoto ni pamoja na mzazi, mwalimu, sanaa, ufundi, ubunifu na vinginevyo. Ni rahisi kumkunja angali mbichi, ni rahisi kumfunza

  • Tusome kwa mikono yetu
Pengine tumeelimika, tuna maarifa lakini ni muhimu kuendana kasi na uhalisia. Na uhalisia ni kuwa kichwa hutunza nadharia na mikono hubeba ujuzi. Basi , kama tumeamua kuwa wasomi ni heri tuifunze mikono yetu kufanya vitu. Na pengine fani tunazochagua kusoma na kubobea ziwe za vitendo zaidi. Mikono hukumbuka.
Mazingira yanayotuzunguka yanatulazimu kuchangamka, kuanza na kunyumbulika. Kuchangamka nikuongeza kasi ya kuona fursa , na fursa iliyopo ni kuwa wengi tumesoma, tuna maarifa lakini ubunifu ni hafifu sawa ulivyo ujuzi wa kufanya vitu bora, tena kwa viwango vya juu. Kuanza ni kuacha ahadi, kufungua mikono na kufanya. Kunyumbulika ni kubadilika, kuona uhitaji na kukidhi uhitaji huo.

  • Tuwe watu wa viwango
Tunaweza kuwa na ujuzi mwingi, vipaji vingi lakini ni muhimu kujitengeneza kufikia viwango vya juu. Tusichoke, juu hakuna foleni, tukijitengeneza mpaka viwango vya juu thamani ya ujuzi na vipaji itakua juu pia. Ubora tulionao unakidhi soko, tuna nini cha ziada na kwanini mimi? Nina nini?, tupo wengi tunaoweza kuimba, kucheza, kubuni, kutunga, au kusuka, kunyoa, kusambaza bidhaa, biashara n.k. Kujiuliza hivi ni sawa nakujiuliza kwanini nyama ina ladha tofauti ikipikwa kwa viungo sawa na wapishi tofauti?. Hata kama tunafanana ujuzi, kuna namna ladha itakuwa tofauti. Ladha ya kiwango cha juu huvutia zaidi, vipaji na ujuzi hukua, kisha huwa tabia.

Bwana Yule!, bibi Yule!, asee Yule jamaa noma sana, pale ofisini kwake!, alianza taratibu, akaboresha, sasa imekua tabia yake kutoa vitu bora, bora nitumie gharama kubwa kwa huduma yake. Hivi ndivyo viwango mabibi na mabwana.

JE NINAWEZA KUFANYA NINI KWA KIWANGO CHA JUU BILA KUAJIRIWA?

Namaliza
kwa kujiuliza...
Asanteni sana

Baba Jenny..
 
Upvote 2
Back
Top Bottom