Pata jinsi wenye ufahamu wanavyoongea:
Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kupitia wilaya ya Lindi mjini Mama Salma Kikwete amewaomba wananchi kuipigia kura ya ndiyo katiba inayopendekezwa kwa kuwa ni bora na imezingatia mahitaji ya makundi yote ya jamii.
Mama Kikwete ambaye ni Mke wa Rais Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete ametoa ombi hilo jana wakati akiongea na wananchi waliohudhuria mkutano wa hadhara uliofanyika katika tawi la Mikumbi Magharibi kata ya Wailes wilayani humo.
Alisema katiba inayopendekezwa ni ya watanzania wote na imegusa maeneo yote muhimu kwa ustawi wa wananchi, inazungumzia haki za wanawake, wazee, wavuvi, watoto na watu wenye mahitaji maalum.
"Katiba iliyopo sasa nayo ni bora, lakini hii inayopendekezwa ni bora zaidi kwani imezitaja haki za mwanamke, mtoto, kijana,mzee na watu wenye mahitaji maalum lakini katika katiba hii ya sasa makundi haya hayatajwi. Msipoteze nafasi, siku ikifika jitokezeni kwa wingi mkaipigie kura ya ndiyo", Mama Kikwete alisema.
MNEC huyo pia aliwahimiza wananchi hao kujitokeza kwa wingi kujiandikisha katika daftari la kudumu la wapiga kura ili waweze kuipigia kura katiba inayopendekezwa na kushiriki katika uchaguzi mkuu utakaofanyika mwishoni mwa mwaka huu wa kumchagua Diwani, Mbunge na Rais.
Alisisitiza, "Zoezi hili la uandikishaji katika daftari la kudumu la wapiga kura ni jipya, hata kama unakitambulisho cha zamani ni lazima ukajiandikishe ili uweze kupata kitambulisho kipya kwakuwa hicho cha zamani hakitatumika tena",.