Colly 7
Member
- Jul 27, 2022
- 93
- 446
Tanzania ni moja kati ya nchi ambazo mpaka sasa elimu yake kwa kiasi kikubwa ni ya kinadharia. Tangu shule ya awali na ya msingi, mwanafunzi hupimwa zaidi uwezo wake wa kuelewa masomo husika kwa nadharia zaidi na sii kwa vitendo, ambapo akimaliza darasa la saba, na hata kidato cha nne, hawezi kujiajiri au kuajiriwa kwa sababu hakufundishwa stadi za maisha au ujuzi fulani, bali alifunzwa masomo mbalimbali (kama jiografia, sayansi, na mengine) kwa nadharia zaidi.
Hali hii huwafanya vijana wengi wanaohitimu darasa la saba na kidato cha nne ambao hawakupata nafasi ya kuendelea na ngazi nyingine, kujikuta njia panda, hivyo baadhi yao kuangukia kwenye magenge ya madawa ya kulevya, wizi/uporaji (Mfano, "Panya Road"), na kwa watoto wa kike - kujiunga na ukahaba, kupata mimba za utotoni, na ndoa za mapema.
Mfumo wa elimu kwa sasa unatoa ujuzi kuanzia ngazi ya chuo kikuu au vyuo vya ufundi stadi. Katika ngazi hii (hasa vyuo vikuu), bado nadharia hutawala zaidi kuliko vitendo, na ndio maana wahitimu wengi hushindwa kujiajiri au kuajiriwa. Huko nyuma, wafanyabiashara wadogo (maarufu kama Wamachinga) walikuwa ni vijana waliohitimu darasa la saba au ambao hawakusoma kabisa, kwa sasa wamachinga wengi ni wahitimu wa vyuo mbalimbali. Jambo hili halina tija kwa vijana wenyewe na wala kwa serikali, kwa kuwa wapo katika mfumo usio rasmi unaowapatia kipato kidogo sana na ambapo serikali haiwezi kukusanya kodi.
Historia ya Elimu ya Tanganyika kabla ya Uhuru
Kwa mujibu wa jarida la Elimu, Sauti Mtwara la Juni 2018, Elimu iliyotolewa wakati wa ukoloni kwa watanganyika ililenga katika kukidhi haja na mahitaji ya wakoloni. Elimu wakati huo iliendeshwa na Waarabu, wamisionari, Wajerumani na Waingereza.
Elimu wakati wa Waarabu
Madhumuni ya elimu ya Waarabu yalikuwa; Kueneza dini ya kiislamu; Kufunza KKK (Kusoma, Kuandika na Kuhesabu), (Taasisi ya Elimu Tazania [TET], 2002).
Elimu ya Wamisionari
Wamisionari walianzisha shule kwa ajili ya watumwa walioachiwa huru, ambapo shule za kwanza zilijengwa Bagamoyo na Zanzibar ambapo walifundisha kilimo, ufugaji, useremala na uashi. Malengo ya elimu ya wamisionari yalikuwa; Kupata waumini wa jinsi zote; Kufunza stadi za KKK; Kufunza ufundi wa aina mbalimbali.
Elimu wakati wa ukoloni wa Wajerumani
Mitaala ilifunza stadi kama uashi, useremala, ukarani, upigaji chapa, ufundi cherehani, ushonaji viatu na uaskari. Kuanzishwa kwa shule za wajerumani kulifanya kuwepo na mifumo miwili ya shule; shule za wamisionari na shule za serikali (TET, 2002).
Malengo ya elimu yalikuwa ni pamoja na: kuinua maisha ya wananchi kwa ujumla; Kuwapatia mbinu bora za kilimo; Kuanzisha na kuendeleza viwanda vitumiavyo malighafi ya hapa nchini; Kuboresha afya za wananchi; Kuandaa watumishi wa serikali za mitaa; na Kupata mabwenyenye uchwara (TET, 2002).
Vilevile, elimu iliyotolewa kipindi cha ukoloni wa Mjerumani na Mwingereza (kuanzia ngazi ya elimu ya msingi), pamoja na stadi nyingine iliwapatia wanafunzi ujuzi wa kilimo, ufundi (kama useremala, uashi, kushona viatu, kushona nguo, nk, na elimu ya afya.
Stadi hizi ziliwezesha wahitimu wa ngazi zote za elimu kuweza kujiajiri na kuajiriwa; mfano, watu walioshia darasa la nne waliweza kuajiriwa katika maofisi mbalimbali ikiwa ni pamoja na kampuni ya Garimoshi kama matarishi, makarani, nk. Na wengine waliweza kujiajiri au kuajiriwa katika sekta ya ufundi kama useremala, uashi, nk.
Elimu baada ya Uhuru
Kwa mujibu wa makala ya Bw. Stephen Maina (Novemba, 2011), baada ya kupata uhuru mwaka 1961, tulirithi mfumo wa elimu uliokuwa wa kibaguzi, ambapo shule ziligawanyika katika makundi matatu: Shule za Wazungu; za Waasia (hasa Wahindi) na za Waafrika.
Mabadiliko katika Mfumo wa Elimu Bw. Steven anaendelea kusema, Elimu ya ufundi ilisimama na kukawa na shule tatu za ufundi ambazo zilikuwa ni Dar es Salaam, Ifunda na Moshi. Tatizo ninalolizungumzia katika makala haya, linaanzia hapa; kwani uamuzi wa kusitisha elimu ya ufundi na stadi nyingine, umesababisha upungufu wa mafundi wa kutosha wa ngazi za kati katika fani za kilimo, ufugaji, afya, umeme, uashi, useremala, ufundi magari nk. Hii ndio hali inayoathiri vijana wengi na taifa kwa ujumla mpaka leo.
Nini kifanyike?
Pamoja na mabadiliko mengi chanya yaliyofanyika katika mfumo wa elimu hapa Tanzania baada ya uhuru, yaliyopelekea watanzania wengi kupata elimu katika ngazi mbalimbali, ni vyema mfumo huu ukaangaliwa upya na serikali, ikiwa ni pamoja na kurejesha elimu ya ufundi na stadi za maisha kuanzia elimu ya msingi na kuendelea. Hii inapaswa kwenda sambamba na kuimarisha elimu ya KKK (Kusoma, Kuandika na Kuhesabu), bila kusahau sanaa na michezo. Ninaamini kila binadamu ni mahiri katika eneo fulani, elimu hii ikirejeshwa, kila mhitimu atafaulu. Elimu ya sasa humpima mwanafunzi katika maeneo machache tena kwa nadharia zaidi, na hivyo wahitimu wengi kuonekana kutofaulu; lakini hawa ndio huwa wafanyabiashara wazuri, mafundi mahiri katika fani mbalimbali, wanamichezo wazuri, au wasanii maarufu sana. Je, hawa wamefundishwa wapi na nani?
Kurejeshwa kwa elimu ya ufundi na stadi za maisha katika mfumo wa elimu kutawezesha watoto kugundua vipaji vyao mapema na kuanza kuvitndea haki. Kwa muktadha huu, kila mhitimu wa ngazi yoyote ya elimu, kuanzia shule ya msingi, atakuwa ana thamani kubwa, kwani atakuwa na wigo mpana wa kuchagua cha kufanya, aidha kuendelea na ngazi nyingine ya elimu, kuajiajiri au kuajiriwa katika fani mbalimbali, n.k. na tatizo la ajira nchini litapungua sana, kama sii kuisha kabisa. Kwa sasa mhitimu wa darasa la saba na hata kidato cha nne, ambaye hakupata fursa ya kuendelea ngazi nyingie, hujiona kama hakusoma, na hata kama anafanya biashara au kazi za ufundi, bado hujidharau na kusema nafanya kazi hizi kwa kuwa sikusoma!
Hitimisho
Elimu ya ufundi na stadi za maisha ikirejeshwa, thamani ya mhitimu wa kila ngazi ya elimu itarejea, na vijana wengi watajiajiri, na taasisi mbalimbali rasmi zitapata shida ya kupata watumishi, na hivyo zitafikia hatua ya kuajiri wahitimu wa ngazi ya elimu ya msingi. Hali hii itasisimua zaidi sii tu uchumi wa mtu mmoja mmoja, bali pia uchumi wa nchi kwa ujumla.
Rejea
HakiElimu (Aprili, 2013), Tamko la HakiElimu kuhusu Bajeti ya Sekta ya Elimu ya mwaka wa Fedha 2013/2014.
mtanzania.co.tz (Januari, 2017), Wasomi waoredhesha yanayodumaza Elimu nchini.
Stephen Maina (Novemba 04, 2011), Historia fupi ya Elimu Tanzania.
Elimu, SAUT-Mtwara, (Juni 10, 2018), Historia ya Elimu ya Tanganyika kabla ya Uhuru

Upvote
33