“Period pain ni kawaida.” Kwa miaka mingi, kauli hii imewafanya wanawake wengi kuvumilia maumivu makali bila kujua kuwa huenda kuna tatizo kubwa zaidi linalohitaji matibabu.
Simulizi ya Natalie Githinji imefungua tena mjadala kuhusu endometriosis nchini Kenya. Natalie, ambaye amekuwa akizungumza hadharani kuhusu safari yake ya miaka kadhaa, alilazwa hospitalini mwezi Agosti 2026 baada ya kupata endometriosis flare-up na baadaye kufanyiwa upasuaji baada ya kubainika kuwa ana Stage 4 endometriosis. Ameeleza pia mzigo mkubwa wa kifedha unaoambatana na matibabu yake.
Lakini nyuma ya jina Natalie kuna wanawake wengi ambao hawana jukwaa la mitandao ya kijamii, uwezo wa kulipia matibabu ghali au mtu wa kuwasemea.
Endometriosis ni nini?
Endometriosis ni ugonjwa sugu ambapo tishu zinazofanana na zile zinazopatikana kwenye ukuta wa kizazi hukua nje ya kizazi. Hali hii inaweza kusababisha maumivu makali wakati wa hedhi, kutokwa damu nyingi, maumivu ya nyonga, matatizo ya mfumo wa chakula au mkojo na changamoto za kupata ujauzito.
WHO inakadiria kuwa takribani 10% ya wanawake walio katika umri wa kupata watoto duniani, sawa na takribani milioni 190, wanaishi na hali hii.
Tatizo kubwa ni kwamba maumivu haya mara nyingi hupuuzwa kama “maumivu ya kawaida ya hedhi.”
Kenya: Miaka ya kutafuta jibu
Utafiti uliowachunguza wanawake 37 wenye endometriosis kutoka Nairobi na Kiambu ulitaja changamoto kuu tatu: unyanyapaa na kuvurugika kwa maisha ya kila siku, vikwazo katika kupata huduma bora za afya, na kutegemea nguvu binafsi pamoja na msaada wa wengine.
Baadhi ya wanawake walieleza kutembelea madaktari wengi na kupata utambuzi usio sahihi kabla ya kugunduliwa. Mmoja alisema ilimchukua takribani miaka 7–8 kupata utambuzi sahihi.
Hii ina maana kwamba kwa mwanamke wa kawaida, safari inaweza kuwa ndefu: maumivu, kliniki, vipimo, dawa, kurudi hospitalini na wakati mwingine kuambiwa avumilie—wakati ugonjwa ukiendelea kuathiri maisha yake.
Gharama: Mwananchi anaishije?
Endometriosis haiishii kwenye maumivu. Inaweza kuathiri uwezo wa mwanamke kwenda kazini, kusoma, kufanya biashara au kutunza familia.
WHO inaeleza kuwa maumivu makali na dalili nyingine zinaweza kusababisha mtu kukosa kazi au shule, kupoteza kipato na kukabiliwa na gharama za matibabu kutoka mfukoni.
Katika kesi ya Natalie, alieleza kuwa upasuaji wa laparoscopic unaweza kugharimu kati ya takribani KSh350,000 hadi zaidi ya KSh1.5 milioni, kutegemea ukubwa wa ugonjwa na hospitali.
Kwa familia inayotegemea mshahara mdogo, biashara ndogo, hustle ya kila siku au kipato kisicho na uhakika, kiasi kama hicho kinaweza kumaanisha kuuza mali, kukopa au kuahirisha matibabu.
Ndiyo maana mjadala kuhusu endometriosis haupaswi kuishia kwa “tumuombee Natalie.” Swali kubwa ni: mwanamke ambaye hana umaarufu, mtandao wa watu na uwezo wa kuomba msaada mtandaoni anafanya nini?
Uzazi nao huathirika
Endometriosis inahusishwa na ugumba. WHO inaeleza kuwa miongoni mwa wanawake wenye changamoto za kupata ujauzito, endometriosis inaweza kuwa mojawapo ya sababu.
Katika jamii ambako mwanamke mara nyingi ndiye anayebebeshwa lawama anapokosa mtoto, hali hii inaweza kuongeza presha, unyanyapaa, migogoro ya ndoa na msongo wa mawazo.
WHO pia inaonya kwamba changamoto za kupata mtoto zinaweza kuleta unyanyapaa, msongo wa kihisia, wasiwasi, huzuni na hata matatizo ya kifedha kutokana na gharama za matibabu.
Tatizo si maumivu pekee—ni ukimya
Kuna wanawake wanaoendelea kwenda kazini wakiwa na maumivu makali. Kuna wanafunzi wanaokosa masomo. Kuna mama anayelazimika kulala siku nzima badala ya kuwatunza watoto wake. Kuna mfanyabiashara anayefunga kibanda kwa sababu hawezi kusimama. Na kuna wengine wanaovumilia kwa miaka wakiamini kwamba “wanawake wote hupitia hivyo.”
Utafiti wa Kenya unaonyesha wazi hitaji la kuongeza uelewa wa umma na kuweka njia rahisi, salama na zinazopatikana kifedha za utambuzi na matibabu ya endometriosis.
Serikali na mfumo wa afya wanapaswa kufanya nini?
Mjadala ulioibuliwa na hali ya Natalie umefikia pia suala la SHA, huku viongozi wakitaka kuchunguzwa kama mfumo huo unagharamia kwa kiwango kinachotosheleza mahitaji halisi ya wanawake wanaoishi na endometriosis.
Kwa mwananchi, mahitaji ni rahisi kueleweka: utambuzi wa mapema, wahudumu wa afya wenye ujuzi kuhusu endometriosis, vipimo vinavyopatikana, wataalamu wa kutosha, matibabu yanayomudu gharama na bima inayosaidia kupunguza mzigo.
WHO inasema wastani wa muda wa kupata utambuzi wa endometriosis duniani unaweza kuwa kati ya miaka 4 hadi 12, huku kuchelewa kwa utambuzi na upatikanaji mdogo wa huduma ukiwa changamoto kubwa katika nchi zenye kipato cha chini na cha kati.
Natalie ametukumbusha nini?
Safari ya Natalie imesaidia kuifanya endometriosis iongelewe zaidi. Lakini lengo halipaswi kuwa kumwangalia yeye pekee.
Lengo liwe mwanamke wa Mathare, Kibera, Kisumu, Mombasa, Nakuru au kijiji cha mbali ambaye anaamka kila mwezi na maumivu makali lakini hajui kinachoendelea mwilini mwake.
Maumivu makali ya hedhi hayapaswi kubezwa. Mwanamke anayesema anaumwa anapaswa kusikilizwa.
Kwa sababu endometriosis si “period pain tu”.
Ni suala la afya, kipato, elimu, uzazi, familia na haki ya mwanamke kupata huduma bora za afya.