Watuhumiwa EPA wafikia 20 kortini
Halima Mlacha
Daily News; Monday,November 10, 2008 @20:01
Wafanyabiashara watatu jumatatu walifikishwa kwenye Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam kujibu tuhuma za kujipatia mabilioni ya fedha kutoka kwenye Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA) katika Benki Kuu ya Tanzania (BoT), na hivyo kufanya idadi ya watuhumiwa kufikia 20.
Mbali na wafanyabiashara mbalimbali, watuhumiwa wengine waliopandishwa kizimbani hadi sasa, wamo wafanyakazi wanne wa BoT. Akisoma mashtaka dhidi ya washtakiwa wawili ambao ni Ajay Somani na Jai Somani mbele ya Hakimu Mkazi wa Kisutu Victoria Nongwa, Wakili Mwandamizi wa Serikali Fredrick Nakulilo, alidai watuhumiwa hao wanakabiliwa na makosa matatu.
Alidai katika kosa la kwanza wote wawili walikula njama ya wizi wakiwa na watu wengine ambao hawajafahamika ya kuiibia BoT, na kwamba Septemba 2, 2005, waliiba Sh bilioni 5.9 mali ya benki hiyo.
Pia mnadaiwa kujipatia ingizo la fedha kwenye akaunti zenu, na Septemba 2, 2005 jijini Dar es Salaam, kwa nia ya kudanganya mlijipatia kutoka BoT ingizo la fedha shilingi bilioni 5.9 kwa kujifanya Kampuni ya Liquidity Services Ltd imepasiwa deni lenye kiasi hicho kutoka Kampuni ya Society Alsacience De Construction De Mashines Textiles, alidai Nakulilo.
Alidai upelelezi wa shauri hilo haujakamilika na kwamba upande wa mashtaka hauna pingamizi la dhamana iwapo washtakiwa watatimiza masharti yake. Hakimu Nongwa, alitoa masharti ya dhamana kwa washtakiwa hao kuwa dhamana ya kosa zima ni fedha taslimu Sh bilioni 2.9, hivyo kila mshitakiwa atatakiwa atoe nusu yake ambayo ni Sh bilioni 1.4 au mali isiyohamishika yenye thamani ya fedha hizo.
Pia alisema pamoja na fedha hizo, washitakiwa hao wanatakiwa kuwa na wadhamini wawili kila mmoja, ambao ni waajiriwa katika taasisi zinazotambulika na hawatakiwi kutoka nje ya Dar es Salaam na walitakiwa kukabidhi hati za kusafiria. Washtakiwa wote wawili walikana makosa hayo na kurudishwa tena rumande hadi pale watakapotimiza masharti ya dhamana na kesi hiyo itatajwa tena Novemba 25, mwaka huu.
Aidha, mbele ya Hakimu Mkazi Euphemia Mingi, mfanyabiashara Mwesiga Lukaza, alipandishwa kizimbani akiunganishwa na mshtakiwa mwingine Johnson Lukaza, ambaye alishapandishwa kizimbani juzi, kujibu mashtaka ya kujipatia mabilioni ya fedha za EPA.
Akisoma maelezo ya mshtakiwa huyo, Wakili wa Serikali Bwisalo Maganga, alidai mshtakiwa huyo anakabiliwa na mashtaka matatu ya kula njama, kuiba na kujiingizia katika akaunti kiasi cha Sh bilioni 6.3 mali ya BoT. Alidai Septemba 2, 2005 jijini Dar es Salaam, mshtakiwa akiwa na lengo la kurubuni alijipatia kiasi hicho cha fedha kwa kudanganya kuwa Kampuni ya Kernel Ltd imehamishiwa deni kutoka Kampuni ya Marubeni Corporation ya Japan.
Hakimu Mingi alisema dhamana ya kosa hilo ni Sh bilioni 3.1 hivyo mshtakiwa huyo na mwenzake Johnson kila mmoja atatakiwa kutoa fedha taslim Sh bilioni moja na wadhamini wawili wa kuaminika. Mshtakiwa huyo alikana makosa yote na alirudishwa rumande hadi pale atakapokamilisha masharti ya dhamana na kesi hiyo itatajwa tena Novemba 18, mwaka huu.
Watuhumiwa ambao tayari wamefikishwa mahakamani ni Farijala Hussein, Rajab Maranda, Japhet Lema, Bahati Mahenge, Davis Kamungu, Godfrey Mosha, Manase Mwakale na Eddah Mwakale, Devendra Vinodbhai Patel, Amit Nandy, Ketan Chohan, Jayantkumar Chandubahi Patel na Johnson Lukaza.
Wengine ni wafanyakazi wa BoT ambao ni Mkuu wa Idara ya Madeni ya Biashara, Iman David Mwakyosa, Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Madeni, Ester Mary Komu na makaimu Katibu wa benki wawili ambao ni Bosco Ndimbo Kimela na Sofia Joseph Lakila.
Kati ya watuhumiwa hao, ni wawili tu ambao wako nje kwa dhamana baada ya kutimiza masharti ya dhamana hiyo ambao ni Godfrey Mosha na Davis Kamungu. Washitakiwa wengine licha ya dhamana zao kuwa wazi, wanaendelea kusota rumande kutokana na kushindwa kutimiza masharti.