Mjumbe Maalum wa China anayeshughulikia Mambo ya Pembe ya Afrika Xue Bing alipewa Cheti cha Shukrani na Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed katika hafla hiyo, ambapo alisema, China siku zote inaona kuwa mazungumzo ndiyo njia sahihi ya kutatua tofauti na mizozo, na mchakato wa amani wa Ethiopia ni mfano mzuri wa kuigwa na nchi nyingine za kikanda katika kutatua migogoro kwa njia ya amani.
Ethiopia ni nchi kubwa ya pili kwa idadi ya watu barani Afrika. Tangu mwezi Novemba mwaka 2020, ilikumbwa na mapigano makali kati ya vikosi vya serikali na vikosi vya TPLF, na kusababisha mamilioni ya watu kukabiliwa na janga la kibinadamu. Kutokana na usuluhishi ulioongozwa na Umoja wa Afrika, tarehe 2 mwezi Desemba mwaka jana, serikali ya Ethiopia na TPLF zilitangaza kufikia makubaliano ya kumaliza vita vilivyoendelea miaka miwili. Hivi sasa, makubaliano hayo yanatekelezwa vizuri, na Ethiopia imefanikiwa kurejesha amani na maendeleo.
Kufikiwa kwa amani nchini Ethiopia sio kama tu kumesuluhisha migogoro nchini humo, bali pia ni mfano mzuri wa kuigwa kwa nchi nyingine za Afrika Mashariki kutatua mizozo kwa njia ya mazungumzo. Kwa muda mrefu uliopita, kumekuwa na migogoro ya mara kwa mara katika eneo la Maziwa Makuu, ambayo inahusisha Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Rwanda, Burundi, Uganda na nyinginezo. Hivi karibuni, makundi yenye silaha katika eneo la mashariki mwa DRC yameendelea kufanya ghasia, na hali ya wasiwasi imeongezeka tena. Wakati huo huo, mzozo mkubwa pia umezuka nchini Sudan. Tarehe 15 mwezi huu, Vikosi vya Serikali ya Sudan vinavyoongozwa na mkuu wa majeshi Jenerali Abdel Fattah Al Burhan na Vikosi vya Msaada wa Dharura vikiongozwa na naibu wake Jenerali Mohammed Hamdan Dagalo vilianzisha mapigano makali katika mji mkuu Khartoum na maeneo mengi nchini humo. Hadi sasa mapigano hayo yamesababisha vifo na majeruhi ya maelfu ya watu.
Kufikiwa kwa amani kwa njia ya mazungumzo nchini Ethiopia ni ushindi wa watu wote nchini humo. Pande zilizozozana zimezingatia maslahi ya taifa na wananchi, na kuchagua kusuluhisha tofauti zao kupitia njia ya kisiasa.
Nchi nyingine zenye migogoro katika eneo la Afrika Mashariki zinapaswa kujifunza uzoefu wa Ethiopia, kujitahidi kufikia amani kupitia njia ya mazungumzo, ili kulinda utulivu wa maisha ya watu na amani ya kikanda.