Ethiopia yakumbatia mifuko ya karatasi wakati marufuku ya matumizi ya mifuko ya plastiki ikianza kutekelezwa

Ethiopia yakumbatia mifuko ya karatasi wakati marufuku ya matumizi ya mifuko ya plastiki ikianza kutekelezwa

ldleo

JF-Expert Member
Joined
Jan 9, 2010
Posts
1,310
Reaction score
1,265
VCG111363794809.jpg


Katika eneo la Alembank, pembezoni mwa mji mkuu wa Ethiopia, Addis Ababa, mmiliki wa duka dogo anayeitwa Meseret Molalgn anawasalimia wateja wake wanaonunua sukari, mkate na mahitaji mengine ya kila siku.

Mpaka siku chache zilizopita, alikuwa akitumia mifuko ya plastiki kufungasha bidhaa za wateja wake bila malipo. Anasema karibu wateja wake wote walikuwa wanakuja dukani bila mifuko ya kubebea vitu walivyonunua, na ilikuwa kawaida kwake kuwafungashia mahitaji yao katika mifuko ya plastiki bila kuwatoza malipo ya ziada.

Hata hivyo, sasa hali imebadilika. Mwishoni mwa mwezi uliopita, serikali ya Ethiopia ilianza kutekeleza marufuku ya uzalishaji, uingizaji, uuzaji na matumizi ya mifuko ya plastiki inayotumika mara moja, kufuatia kipindi cha mpito cha miezi sita chini ya tangazo la kitaifa la usimamizi wa taka ngumu na utupaji wa taka.

Akitangaza hatua hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Uhifadhi wa Mazingira ya Ethiopia (EPA), Lelise Neme, aliitaka jamii kuchukua hatua za haraka, akisisitiza kuwa athari za matumizi ya mifuko ya plastiki zinaweza kuathiri kizazi cha sasa na kijacho. Chini ya sheria hiyo mpya, watu watakaokamatwa wakitumia au kusambaza mifuko ya plastiki watatozwa faini ya hadi dola za Kimarekani 32, huku wazalishaji, waingizaji na wauzaji wakikabiliwa na adhabu kali zaidi. Licha ya kampeni za uhamasishaji zilizofanywa kote nchini, sheria hiyo imepokelewa kwa hisia mseto. Wamiliki wengi wa maduka na wateja wanaunga mkono lengo la kulinda mazingira, lakini wana wasiwasi kuhusu ongezeko la bei.

EPA inahusisha ongezeko la taka za plastiki nchini Ethiopia na ukuaji wa kasi wa miji, ongezeko la idadi ya watu na mabadiliko ya mtindo wa maisha. Aidha, utupaji hovyo wa taka umechangia kuzorota kwa hali hiyo, huku mifuko ya plastiki iliyotupwa ikiziba mifereji ya maji, kusambaa mitaani na kuchafua vyanzo vya maji.

Katika ripoti ya mwaka 2024 ya Mkakati na Mfumo wa Kitaifa wa Usimamizi wa Taka za Plastiki, serikali ya Ethiopia ilieleza kuwa matumizi ya plastiki yameongezeka, huku chini ya asilimia 60 ya taka za plastiki zikikusanywa. Matumizi ya plastiki kwa mwaka yalikadiriwa kuwa kati ya tani 280,000 na 300,000, ambapo mifuko ya plastiki ya matumizi ya mara moja ilichangia karibu asilimia 70 ya kiasi hicho.

Wakati huohuo, mabadiliko kutoka plastiki yanafungua fursa mpya za kibiashara. Yishak Miruk, mjasiriamali kijana, hivi karibuni alizindua kiwanda cha kutengeneza mifuko ya karatasi baada ya kupata mashine kupitia mpango wa serikali kwa karibu birr milioni 1.2, miezi kadhaa kabla ya sheria mpya kuidhinishwa na bunge la Ethiopia. Mwanzoni, mahitaji yalikuwa madogo sana kiasi kwamba kampuni yake ilipunguza uzalishaji kutoka mifuko 2,000 kwa siku hadi 200.

Hata hivyo, tangu marufuku hiyo kuanza kutekelezwa, mahitaji yameongezeka kwa kasi. Miruk anasema hatua hiyo ni uamuzi mzuri, kwani umeongeza matumizi ya mifuko ya karatasi na pia umeimarisha uelewa wa umma kuhusu athari za mifuko ya plastiki kwa mazingira na afya.

Chanzo: Xinhua
 
Back
Top Bottom