Vyombo vya habari vilikuwa tegemeo kubwa la Kikwete kuingia madarakani mwaka 2005.
Mwaka 2010, tegemeo kubwa ni : kizuri chajiuza na kibaya chajitembeza. Sasa hivi hahitaji sana vyombo vya habari kwa sababu wanyonge wameshaelewa kazi yake. Na silaha kubwa kati ya zote ni mzunguko wa pesa ulivyo rahisi na kumuwezesha kila mwenye ari ya kufanya kazi kujiwezesha. Wavivu ndio wanaokiona katika serikali hii ya Kikwete. Na nchi yeyote huendelea pale wananchi wake watapokuwa na juhudi ya kazi. Na kazi ya serikali ni kuwapa mianya hiyo na kuwawezesha.
Tamko hilo la mzunguko wa pesa utalisikia katika kila mkoa uendao, kitu ambacho chaonyesha jinsi watanzania wanavyoujua uchumi. Wale wanaodhaniaa watanzania ni wajinga, basi hawawaelewi watanzania. Watanzania walio wengi ni watu wavumilivu, makini, wasio na ndoto za ajabu na ni watu waishio katika uhalisia. WATANZANIA HAWAISHI KATIKA ULIMWENGU WA ABUNUASI. Wao ni wajuzi wa kutenganisha kati ya kampeni za uchaguzi na ukweli halisi kiutendaji. Na kwa mantiki hii ndio baadhi ya watanzania hukurupuka na kuwatukana watanzania kuwa ni wajinga.
Suala la kutotimiza ahadi zote wanazoahidi wagombea, si tatizo la Afrika au Tanzania tu, bali ulimwenguni kote hata huko Ulaya. Michezo hii ya kuigiza ya kukimbia nchi nzima na kucheza Zekamedi kwa kuahidi Paradise, wakati wote wanafahamu haiwezekani ndio ilizozifanya nchi kama China kukataa Demokrasia ya aina hiyo. Na Urusi ikavunja vunja upinzani na kuzingatia uchumi tu, huku ikipiga Gelesha kwa west kuwa wanavyama vingi.
Katika yote yatazungumzwa lakini tofauti kubwa ya utawala wa Mkapa na Kikwete ni MZUNGUKO WA PESA. Wakati wa Mkapa uchumi ulikuwa lakini mzunguko wa pesa ulikuwa mgumu sana ukilinganisha na sasa. Na njia pekee ya kuwasaidia wanyonge ni kuhakikisha kuwa kuna urahisi wa mzunguko wa pesa. Hii inamuwezesha mkulima kuuza mazao yake kirahisi, mjenzi vile vile, muuza vitambaa naye atafaidika sawa na mshonaji, halikadhalika kwa kuli na muuza madafu. Na huu ndio mtaji wa Kikwete kuelekea uchaguzi 2010.