Keizer, Ndege ya Uchumi salaam!
Kwa lugha rahisi, OD ni gia namba 5 ambayo inakupa mwendo uliotulia, wa kasi lakini kwa mzunguko mdogo wa injini (RPM). Hii hukuwezesha kuwa na matumizi madogo ya mafuta pengine kwa kasi zaidi.
Unaweza kuitumia pia ikiwa unataka kuipita motakaa nyingine, mathalan, kwenye kilima ambapo nawe motakaa yako inakuwa umepungua nguvu, hivyo unaweza kuiweka off (hapa unakuwa kama umerudisha namba 4), na injini itabadili kasi ya mzunguko, utaiweka uklisha maliza tena matumizi yake.
Eneo lingine, ni mara gurudumu la motaklaa yako linapopasuka. Ikitokea hivyo, unaweza kuondoa OD, huku ukiwa umeacha kukanyaga pedeli ya mafuta, kwa maana ndiyo utakuwa unaomba mwendo upungue pasi na kukanyaga breki. Katika hali kama hii, utakuwa umesaidia kupunguza mwendo wa gari wakati ukithibiti muelekeo wa motokaa pia.
Watu wengine katika hali kama hii huwa wanakanyaga breki. Kufanya hivi ni hatari, maana unasimamisha kabisa mwendo wa gurudumu lililopasuka, na matokeo yake mwendo wa motokaa, badala ya kwenda mbele, itajaribu kutii amri ya gurudumu linalogomea motokaa kwenda mbele na kuamua kwenda upande wa gurudumu lilipasuka, nikiwa na maana kwamba hapo motokaa itakuwa inaacha njia na au kupinduka.
Kwa giaboksi zenye kujibadili zenyewe, ni vema basi tukaziacha OD zijiendeshe zenyewe, maana kuziondoa hatari yake ni kuwa unaweza kusahau kuiweka tena unapokwenda zaidi ya km 70 kwa saa, mfano barabara ya Nyerere, na kusababisha matumizi makubwa ya nishati ya kuendeshea mtambo.