Overdrive inatumika ili kuifanya gari ikupe namna fulani ya gia za juu na kama vile gia fulani ya ziada unapokuwa kwenye spidi za juu. Tuseme gari yako ya Automatic ikiwa na gia 6, Overdrive ni kama inakupeleka gia za 5,6 na namna fulani kama vile gia ya 7. Sasa mara nyingi, wengi huwa tunaendesha gari likiwa tayari kwenye Overdrive toka tunapoondoka (taa ya OD inakuwa haiwaki pale kwenye dashboard), yaani hatuweki Overdrive off. Hilo sio tatizo. Ina maana kwamba, unakuwa umeipa gari uamuzi wa kukuweka kwenye gia za chini ukiwa mwendo mdogo na zile za juu na ya ziada kila ikifikia spidi ya juu, hasa kuanzia 70km/hr. Hilo ni nzuri, kwa sababu gari itakapoingia kwenye Overdrive ina maana inapunguza mzunguko wa injini inapofikia spidi ya juu, na hii inafanya gari itumie mafuta kidogo, na hata muungurumo unakuwa wa chini.
Lakini sasa, ukiondoa Overdrive kwa kui-switch off (yaani taa ya OD inakuwa ON), ni sawa na kuiambia gari nataka usinipeleke kwenye zile gia za ziada za juu (kama ya tano, sita na saba) kwa sababu nataka injini inipe nguvu zaidi, na hasa pale ninapotaka ku-accelerate haraka, kama ku-overtake.
Kwa lugha nyepesi, ikiwa gari iko kwenye Overdrive, inaweza kukupeleka kwenye gia za juu wakati wewe bado unataka injini ikupe nguvu au acceleration ya haraka, ambapo unaweza kukuta gari haichanganyi vizuri wakati unataka ku-overtake haraka. Ni sawa na ukiwa na gari la manual, urudi gia namba tatu wakati wa ku-overtake, lakini wakati uko katikati ya ku-overtake ubadili gia toka gia ya tatu kwenda ya tano. Sasa ukiweka Overdrive off, ni sawa na unaiambia gari isije ikaingiza gia toka ya tatu kwenda ya tano kwa sabau tu imehisi tayari umefikia spidi ya juu kwa hiyo ikakuchagulia gia za Overdrive hata wakati bado unahitaji injini ikupe power ya ku-overtake.
Ila ni vizuri ukisha overtake urudishe gari kwenye Overdrive.
Sasa, kuna wakati ni vizuri tu kui-switch Overdrive off muda wote. Kwa mfano gari ni automatic na limebeba mzigo mkubwa. Au kwa mfano unaendesha gari katika barabara mbaya ambapo hata kufika spidi ya 80km/hr ni shida, basi ni vema ku-switch overdrive off. Na pia ukiwa na mzigo mkubwa au hata bila mzigo unateremka mteremko mkali au mteremko kwenye barabara mbaya, au ya matope, ni vema kutoa Overdrive, na hata kuirudisha gia toka D kwenda 2. Ukiacha gari kwenye Overdrive inaweza ikafikia mahali ikawa kama unashuka mteremko mkali na gari ya manual wakati uko gia ya tano au sita, hata kama mwendo wako sio mkali. Gari inakuwa nyepesi sana, na inakuwa haina breki ya injini.
Kwa mfano, basi au lori ambalo lina gia automatic, dereva kushuka Kitonga wakati yuko kwenye Overdrive ni kutafuta ajali mbaya. Ina maana gari itakuwa inashuka mteremko na wewe unaipunguza mwendo kwa kutumia breki peke yake, bila injini kusaidia kupunguza spidi ya gari. Matokeo ni kwamba breki zitaanza kupata moto sana na kuungua (utasikia harufu mbaya sana kama vile clutch inaungua) na inaweza hata kutokea breki zikafeli. Ukigusa rim ya tairi utakuta ina mto vibaya sana na tairi inaweza kupasuka kwa kuyeyuka!
Kuna sehemu fulani kule Mbeya kwenda Tukuyu mteremko unaitwa Uwanja wa Ndege, ukiwa na lori au basi automatic ukashusha nalo ule mteremko ukiwa kwenye Overdrive, unaweza ukakuta inafikia breki hazishiki tena, zimeungua! Kushuka mteremoko kama ule na lori au basi liko kwenye Overdrive ni sawa na kushuka mteremko ukiwa na lori au basi la gia manual wakati uko gia ya sita, huku unapunguza spidi kwa breki!!!
Kwa loli au basi la automatic, unaposhuka milima ya Lushoto au Kitonga au Uwanja wa Ndege (kwenda kule Tukuyu) lazima u-switch off Overdrive, na hata zaidi uitoe gari kwenye D na kwenda kwenye 2.
Nadhani nimekusaidia kukuelewesha suala la Overdrive mkuu.