UTU: Hekima na Kanuni Sahihi ya Maisha
Kwa kuwa mtu si mnyama tu kama walivyo wanyama wengine, kila siku ya uhai wake anafaya shughuli mbali mbali katika namna ambayo ni ya kiutu. Mtu hatarajiwi kufanya kazi kwa ajili ya kujidhuru yeye mwenyewe. Ni pale tu utu wa kawaida unapomtoka anapoweza kuamua kuidhuru nafsi yake, au pale maarifa aliyonayo yanapokuwa ni finyu kiasi kwamba hatambui kuwa anachokifanya kitamletea madhara. Kadhalika mtu hatarajiwi kwamba katika shughuli zake kwa maksudi atafanya mambo yaliyo na madhara kwa watu wenzake. Kwa sababu ni mtu mwenye utu atafanya shughuli katika namna ya kiutu na kuwatendea wenzake mambo ya kiutu. Kinyume chake ni vitendo vya kinyama, kikatili, kibinafsi, kidhuluma na mambo mengine yanayofanana na hayo.
Vile vile shughuli za kiutu za mtu ziko katika namna ambayo si ya madhara kwa viumbe wengine na chochote kilichomo katika mazingira. Mtu mwenye utu, hachukulii udhuru wa mahitaji yake yatokanayo na mazingira kumfanya awe mharibifu wa kila kilichomo katika mazingira yake, bali mahitaji ya kiutu hutoshelezwa kwa namna ya kistaaarabu. Hayawani wasio na utu, hawashangazi wanapokuwa wakatili katika harakati zao za kujitafutia mahitaji na wala hawatambui kama wanafanya ukatili. Chukulia mfano wa chui katika mbuga za Serengeti na kwingine, jinsi maisha yake yanavyoongozwa na sirika ya kuua takribani kila mnyama mnyonge anayekatiza mbele yake hata kama tayari amekwisha kupata kimtoshacho kwa ajili ya siku. Ataendelea kuua tu hata asivyovihitaji, na huo ndio uhayawani halisi.
Mtu mmoja mmoja mwenye utu ndiye hatimaye huunda jamii yenye utu. Utu katika jamii inayoundwa na watu wenye utu hujidhihiri katika mahusiano baina yao, katika shughuli zao za uzalishaji mali/ shughuli za kiuchumi, imani zao, mipangilio yao ya kisiasa na hata katika utamaduni wao wa siku hadi siku kwa ujumla wake.
Katika jamii yenye utu zipo amali za jamii za kiutu na yapo maadili ya kiutu ambayo yanaheshimika, yanazingatiwa na kuenziwa miongoni mwa watu na taasisi zao. Hii ni jamii ambayo heshima ya kila mmoja ni ya kipekee,wema unashamiri miongoni mwa watu, kujali na kutunza ni sifa ya kila mmoja, ukarimu na upendo haviwapigi chenga, kutakiana heri hakuko katika maneno tu bali hata katika vitendo. Ni jamii ambayo matendo ya udanganyifu, rushwa dhuluma, utapeli, uonevu, udhalilishaji na maovu mengine ya aina hii inayawekea alama ya ukengeufu wa utu na kuyatungia sheria na kanuni za kuyadhibiti.
Katika siasa za jamii hii, uongozi unachululiwa kuwa ni alama ya mfano wa uadilifu na utu uliotukuka. Uongozi unakuwepo ili kuzidi kuiekeza jamii katika kiwango kikubwa zaidi cha utu na kuwezesha kuurithishwa utu huo toka kizazi hata kizazi. Wanasiasa na wote wanaopewa dhamana ya kuongoza, jamii inawatarajia katika kauli zao mbele ya watu, katika utekelezaji wa majukumu yao, na katika maisha yao binafsi wawe vinara wa utu. Hawatarajiwi viongozi hawa kuwa upande wa dhuluma za kiwango na aina yoyote ile, bali wazingativu wa sheria na kanuni za utu.
Ni bahati mbaya kwamba kwa sababu ya baadhi ya wanajamii na baadhi ya viongozi kutokuwa na utashi wa kutambua na kutenda utu, dunia imekuwa pahala pa unyama, kudhuriana na kudhulumiana. Utu kamwe hauwezi kukubaliana na utaratibu wa maisha unaoongozwa na dhana ya mwenye nguvu mpishe/mwenye nguvu ndiye anaishi (survival of the fittest). Utu hauwezi kuendana na ubepari ambao umesheheni ushindani umnufaishao anayenyakua fursa ilihali jirani yake akidhulumika stahili yake. Utu hauwezi kukumbatia kumgeuza mtu aliyezaliwa na mwanamke (heshima mbele), kuwa mtumwa. Utu hauwezi kuendana na kanuni za kiuchumi zinazokuza uchumi wa watu wachache na kuwaacha wengi wakiwa hohehahe. Utu hauwezi kuvumilia kuona mchanganyiko wa wakwasi na mafukara katika jamii moja. Palipo na utu hapana migogoro na migongano.
Leo hii katika ulimwengu, tunapoendelea kushuhudia machafuko, vita na mauaji ya mtu mmoja mmoja na ya kimbali, ugaidi, uvamizi, ukaliaji wa kimabavu wa nchi moja dhidi ya nyingine, utengenezaji wa silaha za maangamizi, nyukilia, za kibaiolojia na nyinginezo, tatizo linadhihirka kuwa moja tu, mtu kakengeuka kutoka kwenye utu wake.
Leo hii mataifa yanapoendelea kushuhudia ongezeko la ufisadi, rushwa nene, ubadhilifu na uchafu mwingine miongoni mwa viongozi, watumishi wa umma na wetendaji katika sekta mbalimbali, kinachogomba hapo ni tatizo moja kuu; wamepoteza utu. Fisadi (weka jina la fisadi yoyote hapa) hana utu, vinginevyo asingeyafungamanisha maisha yake na kuiridhisha nafsi yake kwa gharama ya kuwadhulumu wengine; asingeweza kujilimbikizia fedha na mali asizozihitaji kana kwamba yeye ni hayawani wa porini.
Leo hii jamii inapoendelea kushuhudia matendo ya kishirikina, udhalilishaji wa akina mama na watoto, ni dhihirisho jingine la kuondokewa na utu kunakowapata wahusika wa matendo hayo machafu. Ni ajabu kwamba hata wanyama na uayawani wao hawafanyi haya watu wasio na utu wanayoyafanya.
Leo hii tunapoendelea kulia na ongezeko la joto duniani, uharibifu wa mazingira na kadhalika, tatizo ni kwamba mtu kaacha au kapunguza uhusiano wake wa kiutu na mazingira yake. Mtu mwenye utu si mtumiaji wa rasilimali kana kwamba hakuna kesho, ufujaji wa aina yoyote ile si utu. Mtu mwenye utu hawezi kuthubutu kuanzisha moto wa pori ili uteketeze mbuga, misitu, viumbe anuai, na vyazo vya maji. Mtu mwenye utu hawezi kudiriki kuachia tak zenye sumu ziiharibu ardhi, ziyachafue maji na hewa chafu iendelee kuzalishwa kwa wingi toka viwandani. Kukosekana kwa utu kunamfanya mtu asione mbele na wala asitambue uhusianao wa uhai wake na uhai wa viumbe wengine. (balance of the eco system, and biodiversity)
Mtu mwenye utu hawezi kufanya vitendo vya kimaendeleo bila kuzingatia manufaa yake kiutu. Maendeleo ya viwanda na technolojia, kama ni ya madhara kwa watu, basi hayo si maendeleo ya kiutu bali matumizi ya kiayawani ya karama ya maarifa. Ugunduzi wa technolojia sio ukamilifu wa mambo bali ukamilifu wake ni uboreshaji wa utu wa mtu.
Kwa ujumla katika jamii ya watu wenye utu kuna utambuzi kwamba maisha sio tu kuwa na chakula, mavazi, nyumba magari na mali nyinginezo (material wealth) bali utu ni zaidi ya kuwa na mali maana maisha si ya mwilini tu, maisha yako katika nafsi na katika roho pia. Mtu hukamilika kwa roho, nafsi na mwili. Roho siku zote hutaka kutenda mema, lakini mwili una shida ya tamaa; hapo ndipo palipo na fursa ya nafsi kuingilia kati na kufanya utashi wa kutenda utu.
Utashi ndio mwamuzi wa falsafa ya maisha ya mtu mmoja mmoja. Jamii zetu tayari zina utashi huu, zikitarajia kila mmoja wetu aongozwe na falsafa ya UTU, ndio maana si nadra kusikia wanajamii wakimkosoa mtu akosaye utu, wakilalamikia viashiria vya kupungua kwa utu wanavyoviona na kuvisikia katika matukio mbalimbali.
itaendelea...