Abdi, ambaye anahudumu katika kampuni ya sheria ya Abshir & Njagi Advocates, aliripotiwa kuonekana mara ya mwisho alfajiri ya Jumapili, Novemba 1, 2026, katika eneo la Muchai Road, karibu na Ngong Road, Kilimani.
Kwa mujibu wa nyaraka za Mahakama zilizowasilishwa na kaka yake, Zakaria Abshir, watu wasiojulikana waliokuwa wamejihami na kuvaa mavazi yanayofanana na sare za kijeshi walimfuata wakili huyo kabla ya kumchukua kwa nguvu na kumuingiza katika gari aina ya Toyota Land Cruiser Prado TX.
Nyaraka hizo zinaeleza kuwa gari lake jeupe aina ya Toyota Premio lilipatikana limeachwa kando ya barabara hiyo, likiwa na mikwaruzo na uharibifu.
Familia pia imewasilisha madai kuwa Abdi amewahi kupokea vitisho kutokana na nafasi yake katika kesi ya jinai inayoendelea katika Mahakama za Makadara, ambako anatajwa kuwa shahidi. Kwa mujibu wa kaka yake, baadhi ya watu waliodaiwa kuwa maafisa wa usalama walikuwa wamemtaka ajiondoe katika kesi hiyo.
Familia inataka Mahakama izilazimishe taasisi za usalama kumwasilisha Abdi mbele ya mahakama ndani ya saa 24 na kueleza iwapo kuna hati au amri yoyote ya kisheria iliyoidhinisha kukamatwa au kuzuiliwa kwake. Pia imeomba kuhifadhiwa kwa picha za kamera za CCTV, taarifa za mawasiliano na rekodi nyingine zinazoweza kusaidia kubaini kilichotokea
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Mohamed Amin, amekanusha madai kuwa maafisa wa polisi walihusika katika kutoweka kwa wakili huyo. Amesema timu ya wachunguzi imeundwa kuchunguza tukio hilo na kuitaka Chama cha Mawakili nchini (LSK) kushirikisha polisi taarifa zozote walizonazo zinazoweza kusaidia uchunguzi.
.
LSK nayo imeeleza wasiwasi wake kuhusu uwezekano wa kutoweka kwa Abdi kuhusiana na kazi yake ya kisheria na kutaka uchunguzi huru ufanyike ili kubaini waliohusika. Chama hicho kimesisitiza kuwa usalama wa mawakili ni muhimu katika kulinda uhuru wa taaluma ya sheria na utawala wa sheria.
Kutoweka huku kunaibua maswali mazito kuhusu usalama wa watu wanaoshiriki katika kesi za Mahakamani, hasa pale ambapo madai ya vitisho yanahusishwa na utekelezaji wa majukumu yao ya kitaaluma.
Je, ni hatua zipi zinapaswa kuchukuliwa kuhakikisha usalama wa Mawakili na mashahidi wanaoshiriki katika kesi zinazohusisha madai dhidi ya maafisa wa umma?