Roving Journalist
JF Roving Journalist
- Apr 18, 2017
- 3,984
- 13,760
- MAELEZO MAFUPI (DONDOO) KUHUSU UKEKETAJI NA MAADHIMISHO YA SIKU YA KIMATAIFA YA KUTOKOMEZA UKEKETAJI
- Maana ya Ukeketaji
Chimbuko la Maadhimisho
Tarehe 6 Februari ya kila mwaka, Tanzania huungana na mataifa mengine Duniani katika kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Kutokomeza Ukeketaji kwa Wanawake na Watoto. Historia ya ukeketaji imeendelea kuwepo kwa takribani karne 21 sasa. Ilipofika mwaka 2003 Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa lilidhinisha tarehe 6 Februari ya kila mwaka kuwa siku rasmi ya maadhimisho ya kutokomeza ukeketaji Duniani. Kwa upande wa Tanzania maadhimisho haya yameanza kufanyika mwaka 2010.
Maadhimisho hayo yanatoa fursa kwa Serikali na Wadau wa masuala ya ukeketaji kujitathmini hatua iliyofikiwa katika kutekeleza afua za kutokomeza ukeketaji nchini, ikiwa pamoja na mafanikio na changamoto katika utekelezaji wa afua hizo. Aidha, kubadilishana uzoefu wa namna bora zaidi ya kukabiliana na vitendo vya ukeketaji unaofanywa na baadhi ya jamii zetu hapa nchini.
Vichocheo vya Ukeketaji
Kichocheo kikuu cha vitendo vya ukeketaji hapa nchini ni mila na desturi za baadhi ya makabila katika jamii za kumvusha rika mtoto wa kike kutoka usichana na kuwa mwanamke kamili. Jamii inayokeketa huamini kuwa msichana aliyekeketwa anakuwa tayari kuolewa, sababu hii imepelekea ongezeko la mimba na ndoa za utotoni. Sababu nyingine ni mila ya kutambika ikiwa pamoja na kutii masharti ya mizimu ya baadhi ya jamii kuamini kuwa ukeketaji huondoa mikosi katika familia. Vilevile, zipo sababu za kiuchumi ambapo ngariba na wazee wa mila hulipwa fedha au mali ili kutimiza azma hiyo. Kadhalika, wazazi wa watoto wanaokeketwa huwa na matarajio ya kuwaoza mabinti zao kwa lengo la kupata kipato kupitia mahari inayotolewa.
Madhara ya Ukeketaji
Ukeketaji una madhara makubwa kwa wanawake na watoto wa kike ikiwa ni pamoja na athari za kisaikolojia kama msongo wa mawazo kwani vitendo hivyo hufanywa bila ridhaa ya wahusika. Madhara ya kiafya yanayoweza kusababisha kutokwa damu nyingi wakati wa kujifungua na baadhi yao kupelekea kupoteza maisha. Madhara mengine ya kiafya ni maambukizi ya magonjwa ya zinaa na Virusi vya UKIMWI ikiwa vifaa vinavyotumika kukeketa havitatakaswa vyema. Madhara mengine ya ukeketaji ni pamoja na maumivu makali wakati wa ukeketaji kwa kuwa hakuna utaalamu unaotumika kupunguza maumivu wakati wa zoezi lote la ukeketaji. Aidha, ukeketaji unaweza kusababisha ugonjwa wa fistula yaani kutokwa na haja ndogo bila kujizuia mara baada ya kujifungua.
Jitihada za Serikari na Wadau katika kupinga ukeketaji
Serikali na Wadau katika kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na watoto nchini ni kuanzishwa kwa Kamati za Ulinzi wa Wanawake na Watoto 18,618 kwenye Mikoa, Halmashauri, Kata hadi ngazi za Vijiji/Mtaa. Aidha, tumeanzisha nyumba salama (Safe homes) 9 kwa ajili ya kuwatunza wanaokimbia na wahanga wa ukeketaji kwenye Mikoa yenye kiwango cha juu cha ukeketaji, kuanzishwa kwa vituo vya mkono kwa mkono (one stop centres) 32 Tanzania Bara na kuanzishwa kwa Dawati la Jinsia na Watoto katika vituo 420 vya Jeshi la Polisi nchini. Aidha, jumbe za kuelimisha jamii juu ya vitendo vya ukeketaji na madhara yake zimeandaliwa na kurushwa kwenye vituo vya redio nchini.
- Adhabu kwa kosa la Ukeketaji
Kanuni ya Adhabu, Sura ya 16 kifungu cha 169A (2) kinaeleza kuwa, adhabu yake ni kifungo cha miaka isiyopungua 5 na isiyozidi miaka 15 au faini isiyozidi shilingi milioni 1 au vyote kwa pamoja na kuamriwa kulipa fidia ya kiasi kitakachoamriwa na mahakama kwa yule aliyetendewa kosa hilo kwa maumivu yaliyosababisha mtu huyo.
Sheria ya Mtoto, Sura ya 13 Kifungu 158 A kinaeleza kuwa, adhabu ya mtu atakayekiuka kifungu cha sheria, adhabu yake ni faini isiyopungua milioni 2 au kifungo kisichopungua miaka 5 lakini kisichozidi miaka 15 au vyote kwa pamoja na kuamriwa kulipa faini isiyozidi shilingi milioni 1 au vyote kwa pamoja na kuamriwa kulipa fidia ya kiasi kitakachoamriwa na mahakama kwa yule aliyetendewa kosa hilo kwa maumivu aliyosababisha mtu huyo.
- Ujumbe kwa Jamii kuhusu Madhara ya Ukeketaji
- Kumvusha rika mtoto wa kike kutoka usichana na kuwa mwanamke kamili siyo lazima kumkeketa. Jamii inapaswa kuelewa kuwa mila na desturi hii ina madhara kwa kundi hili, tuiache.
- Msichana anaweza kuolewa umri ukifika bila kukeketwa, aliye keketwa kisiwe ni kigezo. Ukeketaji ni moja ya chanzo cha ndoa na mimba za utotoni. Tuzuie vitendo vya ukeketaji ili kumlinda mtoto.
- Mtoto wa kike asitumike kama chanzo cha mapato katika familia, zuia ukeketaji na ndoa za utotoni ili mtoto wa kike asome na kutimiza ndoto zake. Tumlinde na tumwendeleze mtoto wa kike kwa faida yake na Taifa kwa ujumla.
- Ukeketaji husababisha msongo wa mawazo kwa aliye keketwa kwa kuwa hufanyika bila ridhaa yao. Msongo wa mawazo una athari kubwa katika makuzi na maendeleo ya Mtoto na unaweza kudumu katika kipindi chote cha maisha yake. Tumwepushe mtoto na vikwazo vya maendeleo yake.
- Wakati wa kukeketwa damu nyingi hupotea, inaweza kupelekea kupoteza maisha. Tuache ukeketaji kwani ni hatari kwa usalama wa msichana na mwanamke.
- Ukeketaji unafanyika kwa kutumia vifaa visivyo takaswa vyema, hivyo kuna hatari ya kupata zinaa na maambukizi ya Virusi vya UKIMWI. Tuache ukeketaji.
- Ukeketaji unaweza kusababisha ugonjwa wa fistula yaani kutokwa na haja ndogo mfululizo bila kujizuia mara baada ya kujifungua. Tuache kukeketa kumlinda mwanamke dhidi ya ugonjwa wa fistula.