Gazeti hilo limenukuu zaidi ya nyaraka 1,300 za siri kutoka Wizara ya Ulinzi ya Marekani, zikionesha kwamba mashambulizi mengi ya anga yaliyofanywa na jeshi la Marekani katika nchi za Mashariki ya Kati yaliwekewa alama kuwa “makosa makubwa ya kijasusi”, na yalisababisha vifo vya maelfu ya raia, wakiwemo wanawake na watoto wengi. Nyaraka hizo zinaonyesha kuwa tangu mwaka 2014 hadi mwaka 2019, Marekani ilifanya mashambulizi zaidi ya 50,000 ya anga katika nchi mbalimbali zikiwemo Iraq, Syria na Afghanistan, bila ya maandalizi mazuri. Kutokana na upelelezi hafifu na vitendo vya haraka, jeshi la Marekani halikuweza kuhakikisha watu walioshambuliwa ni magaidi au raia.
Mara kwa mara serikali ya Marekani imekuwa ikidai kwamba kwa sababu ya matumizi ya ndege zisizo na rubani na silaha zinazoongozwa kwa usahihi mkubwa, jeshi lake linaweza kuepuka majeruhi ya raia wasio na hatia katika mashambulizi ya anga. Hata hivyo, kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na jeshi hilo, wakati wa vita dhidi ya magaidi nchini Iraq na Syria, raia 1,417 waliuawa katika mashambulizi ya anga yaliyofanywa na jeshi la Marekani, na tangu mwaka 2018, mashambulizi ya anga ya Marekani yamesababisha vifo vya raia 188 nchini Afghanistan. Lakini kutokana na takwimu za jumuiya ya kimataifa, idadi halisi ya vifo vya raia katika mshambulizi ya jeshi la Marekani ni zaidi ya mara 10.
Tukio jipya la vifo vya raia nchini Afghanistan kutokana na mashambulizi ya Marekani lilitokea Agosti 29 mwaka huu. Wakati huo jeshi la Marekani lilifanya mashambulizi ya ndege zisizo na rubani baada ya kundi la Taliban la Afghanistan kuteka mji wa Kabul. Hapo awali Wizara ya Ulinzi ya Marekani ilidai kuwa shambulio hilo lilifanikiwa kuwaua magaidi wengi, lakini baadaye kutokana na ripoti za vyombo vya habari, Marekani ilikiri kuwa hakuna gaidi aliyeuawa katika shambulio hilo, badala yake lilisababisha vifo vya raia 10 wakiwemo watoto 7.
Hivi karibuni Marekani ilitangaza matokeo ya uchunguzi huo, na kusema hakuna Mmarekani yeyote anayestahili adhabu kutokana na tukio hilo, kwani hakuna uzembe, makosa au uongozi mbaya.
Mwezi Machi, 2020, Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu ilitangaza uchunguzi kuhusu uhalifu wa kivita na kibinadamu uliofanywa na jeshi la Marekani nchini Afghanistan. Mwezi Septemba mwaka huo, Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani ilitangaza kuweka vikwazo vya upande mmoja kwa Fatou Bensouda, mwendesha mashtaka mkuu wa Mahakama hiyo, pamoja na maafisa wengine kadhaa waandamizi.
Kwa muda mrefu, Marekani imeanzisha vita nyingi dhidi ya nchi nyingine kwa kisingizio cha demokrasia na haki za binadamu, lakini vita hizo zimesababisha idadi kubwa ya vifo vya raia. Marekani inapaswa kujibu kwa dhati wito wa jumuiya ya kimataifa, na kuchunguza kwa dhati vitendo vya majeshi yake vya uhalifu wa kivita, ili kufidia watu waliouzwa bila ya hatia.