Nimesoma kwenye gazeti lao leo kuwa kuira hiyo iliwekwa na wahuni na wamekanusha kuhusika nayo
Tovuti ya Uhuru yachakachuliwa
Tuesday, 05 October 2010 21:01 newsroom
NA MWANDISHI WETU
WAHUNI wameingilia tovuti ya magazeti ya Kampuni ya Uhuru Publications LTD (UPL) na kuendesha utoaji maoni yanayodaiwa kutoka kwa wananchi, juu ya hali ya kisiasa nchini wakilenga kuhoji utendaji wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Katika utoaji huo wa maoni, wahuni hao wa kisiasa wamepanga kuonyesha utendaji wa serikali si mzuri, na kwamba inahitaji yafanyike mabadiliko, wakilenga kuwalaghai wananchi washawishike kupiga kura za kuikataa serikali ya CCM katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 31, mwaka huu.
Kitendo hicho cha kuchakachua tovuti ya gazeti la Uhuru, kimefanywa kwa makusudi wakidhani wakitumia gazeti hili ambalo wanatambua uhusiano wake na Chama kilichopo madarakani na serikali zake, wataweza kuwayumbisha Watanzania wengi, kwa kuwafanya waamini ghilba hizo za kisiasa, ili wabadili msimamo na kuunga mkono upinzani, hususan chama cha CHADEMA. Wahuni hao wamefanya hivyo wakitambua Chama Cha Mapinduzi ndicho chenye nguvu kubwa nchini, kina hakika ya kushinda kwa kishindo katika uchaguzi mkuu ujao, na hakuna namna yoyote ya kukizuia kuendelea kuunda serikali, ndipo walipobuni mbinu hiyo chafu kwa kupitia tovuti ya gazeti hili ili waweze kuaminika.
Gazeti la Uhuru halijawahi kujihusisha na kura yoyote ya maoni yenye kutaka kuonyesha maoni ya watu juu ya hali ya kisiasa nchini, au kuhoji juu ya utendaji wa serikali, kama ilivyoonyeshwa na wahuni hao. Baada ya uchakachuaji wa maoni hayo na kuwekwa kwenye tovuti ya gazeti hili, na kuonyeshwa pia katika mtandao wa 'bidii forum', baadhi ya magazeti yameyachangamkia kwa nia ya kutaka kuyachapisha matokeo hayo.
Mhariri Mtendaji wa magazeti haya, Josiah Mufungo, alisema jana kuwa mchakato mzima wa maoni hayo hauhusiki na gazeti la Uhuru, kwani huo si utaratibu wake na halina utaratibu wa aina hiyo, ila huo ni usanii wa kisiasa unaopikwa kwa nia ya kuwababaisha Watanzania juu ya imani yao kwa Chama Cha Mapinduzi na serikali zake za Jamhuri ya Muungano, na ya Mapinduzi Zanzibar. Amewataka wananchi kupuuza kinachodaiwa kuwa 'matokeo' ya maoni hayo, ambayo wahuni hao wanataka kuyaonyesha kuwa yametolewa kupitia gazeti hili.