Tatizo la uhaba wa Walimu wa Masomo ya Sayansi na Hisabati kwa Shule za Sekondari mkoani Geita limefikia asilimia 56 hadi sasa, hali inayosababisha wanafunzi wengi kutofanya vizuri kwenye masomo hayo na kuathiri maendeleo ya elimu mkoani hapa.
Akitoa taarifa ya elimu mkoani hapa wiki iliyopita, Ofisa Elimu Mkoa wa Geita, Anton Mtweve alisema hadi mkoa huo una uhitaji mkubwa wa walimu wa masomo ya sayansi 1,715, huku waliopo ni 744 na upungufu ni walimu 972.
Alisema pia shule za sekondari mkoani hapa zinakabiliwa na upungufu wa walimu wa masomo ya sanaa 430 ambapo kwa sasa kuna walimu wa masomo hayo 2,106 ikilinganishwa na mahitaji ya walimu 2,416.
Mtweve alisema kwa upande wa shule za msingi mkoani hapa nazo zinakabiliwa na upungufu wa walimu 7,565 kwani waliopo ni 8,796 ikilinganishwa na mahitaji ya walimu 16,361 sawa na asilimia 46.2.
"Tofauti ya uwiano kati ya walimu na wanafunzi ni kubwa sana ikilinganishwa na mwaka jana, hali hiyo imesababishwa na ongezeko la uandikishaji wa wanafunzi wa darasa la awali na darasa la kwanza mwaka huu," alisema.
Akitoa taarifa ya hali ya ufaulu kwa shule za msingi na sekondari mkoani hapa, Mtweve alisema ndani ya kipindi cha miaka mitatu (2018-2020), kiwango cha ufaulu kwa mtihani wa taifa wa darasa la saba na kidato cha nne umekuwa wa kupanda na kushuka.
"Kwa mtihani wa taifa wa darasa la saba mwaka 2018 ufaulu ulikuwa asilimia 88.53, mwaka 2019 asilimia 79.12 na mwaka jana ulifikia asilimia 82.49, huku kwa mtihani wa taifa wa kidato cha nne mwaka 2018 ufaulu ulikuwa asilimia 91.7, mwaka 2019 asilimia 87.13 na mwaka jana ufaulu ulifikia asilimia 89.15," alisema.
Akizungumzia changamoto ya uhaba wa walimu wa masomo ya sanyansi, Mkuu wa Mkoa wa Geita, Rosemary Senyamule aliziagiza halmashauri zote kuangalia namna ya kupata walimu wa muda wanaoweza kupunguza ukubwa wa tatizo hilo na kuinua ufaulu wa masomo hayo.