Hashpower7113
JF-Expert Member
- Sep 26, 2011
- 1,353
- 2,142
Na Hash Power
Kuna msemo mmoja kwamba ukipenda kazi unayoifanya, lazima ufanikiwe maishani mwako! Gene Deitch, ni miongoni mwa mifano inayoishi ya jinsi kujituma, kupenda unachokifanya na kuelekeza nguvu zako kwenye hicho kitu, kunavyoweza kukutoa maishani.
Yawezekana jina la Eugene Merril Deitch au kwa kifupi Gene Deitch likawa geni masikioni mwako, lakini sidhani kama kuna mtu hazijui katuni za Tom and Jerry!
Hizi ni miongoni mwa katuni ambazo zinapendwa mno na watoto, hasa hawa wa kizazi cha dotcom, lakini pia wapo hata watu wazima wanafurahishwa sana na katuni hizi!
Kwa kifupi ni kwamba Tom and Jerry ni katuni zilizojijengea umaarufu kwa miaka chungu nzima, huku zikioneshwa karibu katika chaneli zote kubwa duniani hasa zile zinazohusu mambo ya ucheshi na michezo ya watoto. Kuanzia Chaneli ya Cartoon Network, Disney Kids, Nickelodeon na kadhalika, kote Tom and Jerry ndiyo habari ya mjini.
GENE DEITCH NI NANI?
Alipozaliwa Agosti 8, 1924, Chicago nchini Marekani, wazazi wake Joseph Deitch aliyekuwa mfanyabiashara na mama yake Ruth Delson, walimpa jina la Eugene Merril Deitch ingawa baadaye alipokuwa mkubwa, aliamua kulifupisha jina lake na sasa akawa anafahamika kama Gene Deitch.
Mwaka 1929, familia yao ilihamia California ambako alianza masomo yake huko Hollywood. Baadaye alijiunga na shule ya sekondari ya Los Angeles high School ambako alihitimu mwaka 1942.
Baada ya kuhitimu masomo yake ya sekondari, Deitch alianza kufanya kazi kwenye Shirika la North American Aviation, kazi yake kubwa ikiwa ni ‘kudizaini’ michoro ya ndege kwa ajili ya shirika hilo kwani alikuwa na kipaji cha hali ya juu cha uchoraji.
Kutokana na uwezo wake mkubwa, shirika hilo liliamua kumpeleka chuo kusomea urubani lakini akiwa anaendelea na masomo yake, alipata ugonjwa wa Nimonia na kusababisha akose sifa za kuendelea na masomo ya urubani, akaacha masomo mwaka uliofuatia.
AJIKITA KWENYE UCHORAJI
Ni hapo ndipo alipoanza kuchorea Jarida la The Jaza Magazine, akishiriki kuchora picha za kupambia jarida hilo sambamba na michoro mingine ya ndani na alioifanya kazi hiyo kwa zaidi ya miaka kumi, kuanzia mwanzoni mwa miaka ya 1940 mpaka mwaka 1951.
Baadaye alijiongeza na kusomea masomo ya utayarishaji wa midundo ya muziki (audio engineer), akapata ajira nyingine kwenye Studio za Connie Converse. Hata hivyo, hakuwa akifurahishwa na kazi yake hiyo mpya, miaka michache baadaye akaachana na kazi hiyo na kurudi kwenye uchoraji.
UCHORAJI WA KISASA
Safari hii alirudi kivingine kwenye uchoraji, akaanza kutengeneza katuni za wanyama na kuzivalisha uhalisia wa kibinadamu au kwa kitaalamu ‘animation’.
Mwaka 1955, aliamua kujiongezea maarifa zaidi kwenye fani ya animation na ni hapo ndipo alipojiunga na masomo ya ‘animation’ kwenye chuo kilichokuwa kinamilikiwa na Studio ya United Productions of America (UPA), na baadaye akaanza kufanya kazi na studio hiyo, akiwa mbunifu wa vibonzo na muundaji wa herufi.
AAMUA KUFUNGUA STUDIO ZAKE
Agosti, 1958, kulitokea kutoelewana kati yake na uongozi wa Studio ya United Productions of America (UPA) alikokuwa akifanyia kazi zake, akafukuzwa kazi na akaamua kwenda kufungua studio yake jijini New York, aliyoipa jina la Gene Deitch Associates, Inc ikiwa inajihusisha na utengenezaji wa matangazo ya biashara na utengenezaji wa katuni mjongeo (animations).
Baadaye, aliamua kuhama nchini Marekani na kuelekea Prague, Czechoslovakia (Chekoslovakia) ambako alifungua tawi jingine la studio yake na hapo ndipo nyota yake ilipoanza kung’ara.
NYOTA YAANZA KUNG’ARA
Kazi yake ya kwanza akiwa Prague, ilikuwa ni ‘animation’ ya Munro ambayo ilianza kuoneshwa kwenye televisheni za nchi hiyo. Ni katika kipindi hicho pia ndipo alipokutana na mkewe, Zdenka.
Katuni ya Munro ilianza pia kurushwa kwenye runinga za nchini Marekani mwaka 1961 na ikaingia kuwania tuzo, mwaka huohuo akashinda tuzo yake ya kwanza ya Academy Award for Best Animated Short Film.
Huo ulikuwa ni kama mwanzo wa milango yake ya mafanikio kuanza kufunguka, akapata dili la kushirikiana na Kampuni ya Rembrandt kuongoza filamu nyingine ya katuni iliyopewa jina la Popeye.
KATUNI ZA TOM AND JERRY
Mwaka mmoja baadaye, alipata shavu jingine la kushirikiana na Kampuni ya MGM kutengeneza na kuongoza katuni za Tom and Jerry.
Katuni hizo zilimpatia umaarufu mkubwa na kuanzia hapo, nyota yake ikawa imeng’ara kwelikweli, akawa anaendelea kubuni visa kwa kuwatumia wahusika hao wawili, Tom na Jerry na kama ulikuwa hujui, basi ni katika kipindi hicho ndipo umaarufu wa katuni hizo ulipoanza kuongezeka duniani kote.
Mfululizo wa visa vya Tommy and Jerry vilivyopata umaarufu mkubwa duniani kote ni Switchin' Kitten, Down and Outing, It's Greek to Me-ow!, High Steaks, Mouse into Space, Landing Stripling, Calypso Cat, Dicky Moe, The Tom and Jerry Cartoon Kit, Tall in the Trap, Sorry Safari, Buddies Thicker Than Water na Carmen Get It!
UTAJIRI WAKE
Katika kipindi chote cha uhai wake, Gene Deitch alikuwa akitajwa kama mchora katuni mwenye mafanikio makubwa zaidi kuliko wengine, huku pia akiwa ameshinda tuzo kibao, ikiwemo Tuzo ya Oscar ya Best Animated Feature kupitia katuni za Tom and Jerry.
Lakini pia katika siku za mwisho za uhai wake, alitunukiwa tuzo ya Annie Award iliyotolewa na ASIFA Hollywood kutokana na mchango wake wa muda mrefu katika tasnia ya ‘animations’.
KIFO CHAKE
Deitch alifariki hivi karibuni, April 16, 2020 jijini Prague akiwa na umri wa miaka 95, kifo ambacho kinatajwa kusababishwa na umri mkubwa pamoja na maradhi ya tumbo ya muda mrefu.
Ameacha watoto watatu, Kim, Simon na Seth Deitch na dunia nzima itaendelea kumkumbuka kwa jinsi kazi zake za Tom and Jerry zilivyowafanya watoto wengi duniani kuwa na furaha kwa miaka chungu nzima.