Msumari wa mwisho wapigiliwa jeneza la General Tyre
- Ni kilio na kusaga meno kwa wafanyakazi 317
- Serikali yakatisha rasmi ajira zao
MWAKA 2003 mmoja wa wafanyakazi vijana wa kiwanda cha kutengeneza matairi cha General Tyre East Africa Ltd cha Arusha alifichua tuhuma za ufisadi mkubwa uliokuwa ukifanywa na menejimenti ya kiwanda hicho kwa kuwaeleza baadhi ya wafanyakazi wenzake.
Mfanyakazi huyo hakuishia kueleza wenzake tu, lakini pia alichukua hatua za kuvujisha habari hizo katika vyombo kadhaa vya habari; lengo likiwa ni kuiamsha bodi ya wakurugenzi na serikali ambayo ndiyo yenye hisa nyingi katika kampuni hiyo kuhusu ufisadi huo.
Ufisadi huo uliokuwa unatishia ustawi na uhai wa kiwanda hicho ulikuwa unafanywa na meneja wake, Deven Lohan - raia wa Nepal kwa kushirikiana na wakuu wa idara mbalimbali ambao ni wazawa.
Vyombo kadhaa viliripoti habari za ufisadi katika kiwanda hicho lakini kwa mwamko kidogo wa serikali yetu; hakuna hatua za maana zilizochukuliwa huku Wizara ya Viwanda na Biashara, ambayo wakati huo ilikuwa chini ya Waziri Basil Mramba (Awamu ya Tatu), ikikalia mada hayo bila kuyachunguza.
Hata hivyo, pamoja na kuonyesha uzalendo wake, mfanyakazi huyo hakupata kuungwa mkono na wenzake katika kufichua ufisadi huo, na badala yake baadhi walimchongea kwa wakubwa ambao nao walichukua mara moja hatua za kumfukuza kazi.
Wafanyakazi hao walimwona mwenzao kama mtu msumbufu na vijana wa sasa ambao wanakosa nidhamu katika sehemu za kazi wenye tabia za kujaribu kuhoji kila jambo. Hata hivyo, jambo ambalo wafanyakazi hao hawakulijua ni kwamba ufisadi huo ungekuja kuwa "gharika" katika maIisha yao ya baadaye.
Baada ya kuachishwa kazi, mfanyakazi huyo alipata kazi katika moja ya makampuni ya simu za mkononi mkoani Arusha, na hadi leo bado anaendelea kufanya kazi na kampuni hiyo.
Lakini miaka mitano (mwaka 2007) baadaye, ufisadi huo mkubwa ulisababisha kiwanda hicho kusitisha uzalishaji na wafanyakazi wakawa wanalipwa mishahara bila kuzalisha chochote kwa miezi sita hadi mwaka 2008 kiwanda kilipofungwa kabisa.
Kiwanda hicho kilifungwa baada ya kushindwa kuagiza mali ghafi ya kutengeneza matairi, kukatiwa umeme na maji na wafanyakazi walipelekwa likizo isiyokuwa na malipo.
Tuhuma za ufisadi zilizokuwa zimeibuliwa kuhusu meneja huyo ni kutumia fedha za mkopo wa Shilingi bilioni 10 zilizotolewa na Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) kwa matumizi mengine badala ya kufufua kiwanda hicho kwa kuongeza uzalishaji.
Baada ya kiwanda kupata fedha hizo huku kikidhaminiwa na serikali, menejimenti ilipa kiasi cha fedha kwa madeni waliyokuwa wanadaiwa lakini kiasi cha Dola za Kimarekani milioni 3.5 zinaelezwa kutumika bila vielelezo vyovyote.
Imeelezwa kuwa meneja huyo alitumia fedha nyingi kwa matumizi binafsi yakiwemo ya kuwaleta ndugu zake kutoka Nepal na mmoja wa wana wa mfalme wa nchi hiyo kutembelea mbuga za wanyama za Ngorongoro, Serengeti na Manyara kwa gharama za kiwanda hicho!
Aidha, kiasi kingine cha fedha kilitumika kwa sherehe za kidini zilizofanywa na meneja huyo katika mikoa ya Tanga na Dar es Salaam.
Meneja huyo kabla ya kuondoka nchini na kurudi kwao pia aliuza nyumba nne za kampuni zilizokuwa katika eneo la Corridor katika manispaa ya Arusha kwa bei ya kutupa; huku moja akijiuzia mwenyewe kwa kwa kiasi cha Shilingi milioni 100.
Wakati Meneja huyo akifanya vitendo hivyo, ambavyo kwa ujumla vilionekana kama hujuma, wakuu wa idara nao hawakuwa nyuma katika "udokozi"; kwani inaelezwa kuwa kila moja katika idara yake alifuja kiasi alichoweza wakitumia mwanya wa udhaifu wa menejimenti.
Baadhi wanadaiwa kuiba vipuri mbalimbali vya mashine za kuzalisha matairi na wakati mwingine wakinunua vipuri feki ambavyo vilishindwa kufikia viwangi vinavyotakiwa.
Kufuatia mlolongo huo wa matukio ya ufisadi uliochukua zaidi ya miaka mitano sasa, wafanyakazi hao wapatao 317 wamekumbwa na hali ya hofu, mashaka na wasiwasi baada ya serikali kukatisha ghafla mikataba yao ya ajira kuanzia wiki iliyopita; huku wakiwa hawajalipwa mishahara kwa zaidi ya mwaka mmoja.
Uamuzi huo wa kusitisha ajira za wafanyakazi hao ambao umekuja ghafla na bila kutarajiwa ulitangazwa wiki iliyopita na Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Dk.Shaban Mwijaki wakati alipofanya mkutano na wafanyakazi hao.
Wafanyakazi hao wamepewa notisi ya kulipwa mshahara wa mwezi mmoja pamoja na mafao yao yatakayolipwa na serikali ambayo ndiyo yenye hisa nyingi katika kiwanda hicho.
Serikali inamiliki hisa karibu asilimia 80 za kiwanda hicho wakati kiasi cha hisa kilichobakia kinamilikiwa na kampuni ya Continental ya nchini Marekani.
Kwa mujibu wa baadhi ya wafanyakazi, mafao ya serikali kwa mujibu wa sheria ni kidogo sana, na kuna uwezekano hakuna mfanyakazi atakayelipwa zaidi ya shilingi milioni 2 bila kujali muda ambao mfanyakazi husika amefanya kazi.
"Kuna waliofanya kazi miaka 17 wanaambullia Shilingi 700,000 na wengine milioni 1.2….sasa hapo utaona ni kwa kiwango gani wafanyakazi wanapata hofu ya maisha watakaporudi mitaani", alisema mmojawao mwishoni mwa wiki.
"Kwa kweli wafanyakazi wote wamepata hofu hasa wengi ambao tuna umri mkubwa ambao si rahisi kupata ajira serikalini na hata makampuni binafsi tunaweza kumudu gharama za maisha wakati hatujalipwa mafao ya maana", aliongeza mfanyakazi huyo.
Wafanyakazi hao wanadai kuwa wao hawahusiki na ubadhirifu huo na hatua zilizochukuliwa na serikali ni sawa na kuwapa adhabu kwa makosa ambayo hawakutenda.
Mwenyekiti wa Chama cha wafanyakazi (TUICO), tawi la kiwanda hicho, Lukio Tulule alikataa kutoa ufafanuzi kuhusu utaratibu na sheria inayotumiwa na serikali kulipa mafao kwa wafanyakazi hao kwa madai kuwa jambo hilo limemfanya achanganyikiwe.
"Ndugu yangu, sielewi chochote naomba uniache tu suala hilo limenichanganya sana….nipigie simu Jumatatu nitakuwa nimepitia nyaraka zilizopo na nitajua utaratibu uliotumika kulipa mafao yetu", alisema.
Akizungumzia hatua ya kukatisha ajira za wafanyakazi hao, Katibu Mkuu huyo alieleza kuwa serikali imechukua uamuzi huo kutokana na ukweli kuwa kwa sasa kiwanda hicho hakiwezi tena kuzalisha matairi hadi hapo serikali itakapopata mbia mwingine.
"Kutokana na kiwanda kuwa na madeni makubwa na ufisadi uliofanywa na menejimenti, serikali imeona ni vyema kiwanda hiki kikafungwa kwanza na wafanyakazi kulipwa mafao yao wakati tukijipanga upya kutafuta hatua za kuchukua", alisema.
Kufungwa kwa kiwanda hicho kunahitimisha kuwepo kwa viwanda vya umma katika mkoa wa Arusha vilivyokuwa vimeanzishwa katika miaka ya 70 na 80 na ambavyo karibu vyote vilikuwa vimebinafsishwa wakati wa serikali ya awamu ya tatu kwa wawekezaji mbalimbali, lakini vingine vikiwa vimetelekezwa na kubakia magofu.
Viwanda hivyo, ambavyo viliufanya mkoa wa Arusha kuwa ni mkoa wa pili kwa kuwa na uchumi mzuri baada ya Dar es Salaam, ni pamoja na kiwanda cha bia, kiwanda cha madawa ya binadamu cha TPA, kiwanda cha kusindika nafaka cha NMC, Baby Food, kiwanda cha nguo cha Kiltex, kiwanda cha sabuni cha EMCO na kiwanda cha mbao cha Fibreboard.
Source: Raiamwema.
Hii habari kwa kiasi kikubwa imejaa uzushi.
Kijana anayezungumziwa kwamba alifichua ufisadi uliokuwa ukifanywa na managemant ya GT kwa kuwaeleza wafanyakazi wenzake na baade vyomba vya habari si za kweli hata kidogo tena zimejaa ubabaishaji na uvivu wa hali ya juu kwa mwandishi wa habari hii. Gazeti la Raiamwema linapaswa kuwaomba radhi wasomaji wake kwa kuandika habari pasipo kufanya utafiti wa kutosha.
Kwa sisi tuliowahi kufanyakazi GT uliposoma hii habari tulijua moja kwa moja kijana anayezungumziwa anaitwa Antony Mhandiki.
Kilichomwonda A Mhandiki si kwasababa alifichua ufisadi uliokuwa ukifanywa na managemant ya General Tyre bali kugombea ulaji baina yake yeye na L Mgoyo [Purchasing Manager]
Bwana A Mhandiki alikuwa Ag Marketing Manager kuanzia mwaka 2004 mpaka alipoondolewa mwaka 2007. Kama mkuu wa division ya masoko Bwana Mhandiki alihusika na uhagizaji wa vifaa vya promotion [t-shirt, kofia,key holder na vifaa vya michezo] kupitia idara ya ununuzi [Purchasing]. Kampuni ya Zizou ilipata tender ya kuleta vifaa vyote vyenye thamani ya zaidi ya tsh 250 milioni,ugomvi wa Bwana Mhandiki na Bwana Mgoyo ulisababishwa na kutokugawana kwa usawa 10% na mgawo wa fedha za vifaa ambavyo kampuni ya Zizou hawakuweza kusupply.
Bwana Leonard Mgoyo alitumia vyema fursa iliyokuwepo wakati huo, vyombo vya habari hasa gazeti la RAI na baadaye Mwahalisi yalikuwa yakitoa habari za ufisadi uliokuwa ukifanywa na Bwana D Lohani.
Bwana L Mgoyo kwa uchungu wa kunyimwa ulaji alikwenda kujengea hoja kuu mbili kwa manaja mkuu aliyeanza kulemewa na kashfa za ufisadi.
[1] Kwakuwa Bwana A Mhandiki aliwahi kufanyakazi katika gazeti la Daily news ni rahisi kwake kujuana na wanahabari na kuwa yeye anahusika na uvujaji wa habari zilizokuwa zikihihusisha General Tyre na ufisadi.
[2] Gazeti la RAI wakati huo lilikuwa na wanahabari wengi wahaya/wanaotoka mkoa mmoja na Bwana A Mhandiki.
Hoja hizi mbili zilisababisha Bwana A Mhandiki kuachishwa kazi General Tyre, ingawa manaja mkuu alikuja kukiri baadae alifanya kosa kubwa kumwachisha A Mhandiki kazi kwasababu bado habari za ufisadi ziliendelea kutoka kwenye vyombo vya habari.
Najua waandishi wa habari wa gazeti la Raiamwema wanatembelea sana hapa jamvini itakuwa jambo la maana kama mtaweza kuirekebisha habari mliyoitoa bila kuifanyia utafiti wa kutosha. Tuliokuwa tunazitoa habari za ufisadi tuko bado hatujafa tena tunafahamiana sana. A Mhandiki alikuwa ni sehemu ya viongozi waliosababisha General Tyre ikafikia hapo ilipo.
Naomba kuwasilisha.