Liundi akosoa utaratibu wa utoaji ruzuku
2008-12-26 14:21:27
Na Simon Mhina
Msajili wa kwanza wa vyama vya siasa nchini, George Liundi amekosoa utaratibu wa ugawaji rukuzu kwa vyama vya siasa vyenye wabunge pekee na kusema utaratibu huo sasa haufai kwa vile unalenga kukitajirisha Chama Cha Mapinduzi (CCM)
Liundi ambaye kitaaluma ni mwanasheria, alienda mbali zaidi na kusema utaratibu huo, unaonekana zaidi kukineemesha CCM na kuvidumaza vyama vya upinzani, hasa vile vipya vinavyoanzishwa.
Akizungumza na Nipashe jijini Dar es Salaam Liundi alisema ni kweli yeye ndiye aliasisi utaratibu huo, lakini ulikuwa wa mpito katika kipindi cha kujifunza kwa vile utaratibu wa vyama vingi ulikuwa mgeni nchini.
Alisema fedha zinazochotwa na CCM zinatosha kabisa kukitajirisha, achilia mbali kuendesha shughuli zake huku vyama vingine `vikifa njaa`.
Akifafanua, Liundi alitoa kauli ambayo wakati fulani iliwahi kutolewa na Mwenyekiti wa TLP Augustine Mrema, kwamba hata kama chama kingekuwa na viongozi wajanja na maarufu kwa kiasi gani, hakiwezi kufanya shughuli zake bila kupata fedha.
Alisema kwa msingi huo, vyama vinahitaji ruzuku kwa vile michango ya shilingi mia mia toka kwa wanachama haiwezi kuendesha chama.
Alisema inabidi vyama vyote vyenye usajili wa kudumu vipewe kiasi fulani cha fedha, bila kujali kina wabunge au la.
Pia alisema ruzuku inayozidi itolewa kwa mujibu wa idadi ya wanachama na ofisi za Chama husika nchi nzima.
Alisema kigezo kingine cha kutoa ruzuku ni jinsi chama kinavyowajibika kisiasa na kura wanazopata katika chaguzi mbalimbali.
Pia alisema ruzuku inatakiwa pia kutolewe kwa vyama kwa kuangalia namna vilivyofanikiwa kupata wabunge na madiwani.
``Kigezo cha ubunge na udiwani, kiwe kigezo cha mwisho cha kukipatia chama ruzuku,`` alisema na kuongeza: ``Vyama vipya vitapataje madiwani na wabunge bila kufanya shughuli za kisiasa kwanza na shughuli za kisiasa ndio hizi ambazo zinategemea fedha? Lazima utaratibu huu tuubadili,`` alisema.
Alipoulizwa kwa nini katika enzi zake hakuubadilisha, alisema ili kuboresha vyama, alishabadilisha mfumo wa utoaji ruzuku mara mbili.
Alisema mwanzoni mwaka 1995 kila mgombea alipewa ruzuku yake ya Sh 500,000 kabla ya uchaguzi, na kiasi hicho baadaye.
Akasema utaratibu huo ukaonekana kuwa na kasoro, hivyo ukabadilika kuwa wa kutoa ruzuku kwa chama chenye wabunge.
``Wakati wangu ulikuwa wa kujifunza, mfumo huu wa vyama vingi ulikuwa mgeni mno, hivyo inabidi kubadilika kila wakati ili kuuboresha ,`` alisema.
SOURCE: Nipashe