Gonjwa lisiloponyeka bila dawa

Gonjwa lisiloponyeka bila dawa

NAXFRA

JF-Expert Member
Joined
Jul 28, 2011
Posts
392
Reaction score
74
Ukiachana na magonjwa ya kisaikolojia, kiakili, kimwili, kiroho na mengineyo mengi yale yanayozidi kubainika na kuongezeka siku hadi siku katika kizazi cha ulimwengu wa sasa; lipo gonjwa la muda mrefu, ambalo limedumu karne kwa karne. Gonjwa hili sugu ni kongwe kuliko magonjwa mengine baadhi yaliyoibuka hivi karibuni.



Gonjwa hili hakika linatisha, maana ukilipata tiba yake inahitaji kujikana nafsi, bila hivyo, linaweza kukutesa hadi wakati wa kufa, unakufa nalo na marehemu asiweze kukumbukwa kwa lolote juu ya dunia hii. Ukiachana na magonjwa mengine unayoyafahamu; gonjwa hili kwa namna ya ajabu huwapata watu wenye afya zao nzuri, wenye nguvu tele za kufanya kazi, wasio na ulemavu wo wote katika miili wala akili zao. Hakika ni gonjwa la pekee na la ajabu sana.

Gonjwa hilo linaandikwa na kutamkwa kwa herufi nne; gonjwa hili ninalolizungumzia linaitwa ‘‘uvivu’’. Neno uvivu ni neno ambalo haliwezi kubadilika maana yake hata kama utalisoma kinyumenyume, au ukitumia kioo; na ndani ya kioo litasomeka vilevile bila kupoteza maana yake halisi. Uvivu ni hali inayompata mtu na asiweze kujituma katika kufanya kazi au kukosa uwezo au ari ya kufanya kazi kwa bidii; uvivu ni uzembe, na kinyume cha uvivu ni kutofanya kazi kwa bidii.

Uvivu kwa mtu mmoja mmoja huzalisha umasikini kwa mtu mmoja mmoja, hatimae umasikini huo hupanda ngazi katika familia na mwishowe katika taifa zima kwa ujumla. Taifa lolote likiwa na watu wa vivu; taifa litegemee kuwa na kiwango kikubwa cha umasikini maana watu wake hawana ari, bidii, na moyo katika kufanya kazi. Taifa la wavivu huzaa taifa legelege lenye watu ombaomba na tegemezi hadi ngazi ya kitaifa.

Sifa na Tabia za Mtu Mvivu Pamoja na Changamoto Zake: Endapo mtu ni mvivu lakini ni mwenye afya, nguvu, hana ulemavu wowote wala matatizo ya kiakili mara nyingi huwa na sifa na tabia bainishwa zifuatazo:



1. Mtu mvivu hupenda kulala na huthamini usingizi kuliko kujituma:
Mvivu yeyote hutumia muda mwingi kulala (usiku na mchana) kama ilivyo nafsi yake, jua huchomoza yeye bado yupo kitandani kila siku. Usingizi kwake ni starehe. Mvivu anaependa usingizi, njaa kwake ni sawa maana hutumia muda mwingi kulala kuliko kutafuta mkate (chakula) wake wa kila siku.



2. Mtu mvivu hafanikiwi, kwa sababu hana moyo wa kujituma: Yeyote aliye mvivu kufanikiwa kwa jambo lolote kwake ni nadra sana, hiyo ni kutokana na kukosa ari ya kujituma kwa bidii katika kufanya kazi yo yote ile na nafsi yake imefanyika kutopata na kutofanikiwa. Tofauti na mvivu, mwenye bidii hubarikiwa na hufanikiwa katika kujibidisha kwake.



3. Mtu mvivu ni mzembe wa kutupwa; hata kwa vitu au kazi isiyohitaji nguvu na maarifa yeye humshinda: Mvivu hata ukimsogezea fursa mlangoni kwake umefanya kazi bure.; hata kama fursa zipo kila mahali, mvivu hawezi kuthubutu katika kujisumbua kufanya jambo lo lote, maana yeye kila jambo kwake ni kero na usumbufu. Mtu mvivu ni sawa na mtu asiyeweza kufunga goli katika mpira wa miguu wakati mlinda mlango (goal keeper) hayupo.



4. Mtu mvivu hujiona sahihi kwa hali aliyonayo, hata kama akishauriwa hachukui hatua: Mvivu hawezi akashaurika kwa jambo lolote la mafanikio yake, hujiona sahihi jinsi alivyo, hata ufanye jitihada zipi hawezi akabadirika, maana kwake uvivu ni tatizo linalomshambulia daima.



5. Mvivu kutumika au kujitumakwake ni kuchungu: Daima mvivu hapendi kutumika na kujituma katika bidii ya kazi. Mvivu hukeleka na huumia pale aambiwapo kufanya kazi au kutumwa kufanya kazi, na huwa mkali au hulalamika sana apewapo majukumu ya kufanya kazi.



6. Mvivu hutawaliwa, hufanywa mtumwa na wale wenye bidii na waliofanikiwa: Mvivu haheshimiki, hugandamizwa na kunyanyaswa na wale waliofanya bidii katika maisha yao na kufanikiwa. Kwa kuwa uvivu huleta umasikini, basi mvivu ni mtumwa kwa wale walifanikiwa au kujibidisha katika kazi.



7. Mtu mvivu ni ombaomba; hali na kutumia vya jasho lake mwenyewe: Mvivu hawezi kujibidisha ili apate pesa, vitu, au mali itokanayo na nguvu zake; bali yeye haishi kuomba kila kukicha. Kwa kukosa fikra yakinifu za kujitambua pamoja na kujituma katika kutafuta na kufanya kazi, mvivu haishi kuombaomba kwa wale wenye kuzitafuta pesa na mali kwa nguvu zao.



8. Maisha ya mtu mvivu huwa ni magumu na ya shida: Mtu aliyeathirika na uvivu, kwake siku zote maisha ni magumu na ya shida sana maana hawezi akapata ahueni ya maisha, kwa sababu yeye hana kasumba ya kujishughulisha katika kutafuta ili afanikiwe; bali hutumia muda mwingi kwa mambo yasiyo ya msingi, kama vile sitarehe au anasa na kulala kwingi.



9. Mtu mvivu hupenda maisha rahisi, hapendi kujitesa katika bidii ya kutafuta:
Mvivu hapendi kujisumbua, kujibidisha katika kazi, wala kuteseka ili hapo baadae afanikiwe na kufaidi matunda yake; bali yeye (mvivu) hupenda maisha rahisi na mepesi. Maisha ya kupanda mlima kwa mvivu ni machungu mno tena ni zaidi ya pilipili kichaa.



10. Mikono ya mtu mvivu hufanya kazi kwa ulegevu: “Kwa sababu ya uvivu paa hunepa; Na kwa utepetevu wa mikono nyumba huvuja” (Mhubiri 10:18). Kutokana na kukosa moyo au ari ya kufanya kazi kwa bidii, mtu mvivu hufanya kazi kizembe tena kwa ulegevu na utepetevu wa mikono wa mikono. Mikono ya mtu asiyependa kazi ni milegevu na haitaki daima kutenda kazi.



11. Mtu mvivu hawezi kuthubutu, kuvumilia wala kuzikabili changamoto ili ayafikie mafanikio: Mvivu ni mvivu hata katika kufikiria, hawezi kufanya kazi, biashara wala jambo lolote bila kusukumwa au kusaidiwa. Mvivu huzungukwa na mashaka, wasiwasi, pamoja na uoga uliokithiri, hivyo hawezi kuthubutu kwenye kazi au jambo linalohitaji ushupavu wa moyo, nguvu, akili na uwezo wa maarifa, pamoja na ustahimilivu kubwa.



12. Mtu mvivu huharibu, hatunzi, hutumia kwa pupa na kwa uharibifu vitu au mali zilizotafutwa na wengine: Kutokana na kutojua uchungu, mateso, usumbufu, gharama na jasho lililotoka katika kuvipata vitu au mali zilizotafutwa na watu wengine; mtu mvivu azikutapo mali hizo au vitu hivyo yeye hutapanya, hufuja, huharibu, hutumia kwa pupa na fujo (mali zilizokwishatafutwa na watu wengine).



13. Mtu mvivu ni mzigo na hunyonya wengine: Tabia ya uvivu, utegemezi, kuombeleza vitu na mali za wengine; humfanya mtu mvivu awe mzigo kwa ndugu, marafiki, jamii hata taifa kwa ujumla. Mvivu ni mzigo mkubwa na mnyonyaji kwa watu wengine wanaojibidisha katika kufanya kazi na kutafuta, wale ambao usingizi, raha wala anasa kwao hazina thamani, maana kila siku, kila saa, kila muda nafsi zao, damu zao, fikra zao huwaza na kusema “kazi tu”.



14. Mtu mvivu hupenda kufuatilia mambo na mafanikio ya wengine: Mvivu asiyefanya kazi; masikio yake, macho yake, miguu yake na mdomo wake huwa makini katika kufuatilia na kusema mambo na mafanikio ya wengine (yasiyomhusu hata kidogo). Kutokana na kukosa kazi, shughuli na mambo ya kufanya, mvivu hufuatilia ya watu wengine na kuyatapanya mtaani au kuyasambaza kwa watu wengine. Tabia hii ya mtu mvivu, huzaa tabia ya umbea, uongo, usengenyaji na kuchunguza chunguza maisha ya wengine.



15. Mtu mvivu hawajali wala kuwahudumia na kuwatunza walio wa familia yake: Kutoka na athiri ya uvivu, mtu mvivu hukwepa majukumu na hawezi kuwahudumia wala kuwatunza vyema wale walio wa familia yake kwa kiwango kinachotakiwa. Familia inayomtegemea mtu mvivu haina uhakika wa maisha ya kesho wala kesho kutwa; familia haikosi njaa, haina akiba wala matunzo yanayokidhi.



16. Kazi, mali, na vitu vya mtu mvivu havipo katika utaratibu, matunzo na mpangilio maalumu: Kila jambo, kila kazi, na kila kitu cha mtu mvivu kipo ovyoovyo; hakuna matunzo, hakuna mpangilio, hakuna utaratibu. Mvivu hana kipi kianze na jambo lipi lifuatie baada ya jingine; muda gani jambo au kitu gani kifanyike na kifuatiwe na kitu gani kingine; kazi ipi ifanyike vipi, muda gani na kwa namna gani ianzwe na imalizike; kitu gani kitunzwe na kihifadhiwe kwa namna ipi?



17. Mvivu hapendi wengine wafanikiwe, anataka wabaki kama alivyo yeye: Kushindwa kwake, mvivu hutamani na wengine washindwe ama wasifanikiwe kama alivyo shindwa yeye. Kwa maana nyingine; mvivu huwaonea wivu wale wanaofanikiwa na hujenga kinyongo na chuki juu yao.



18. Kwa tabia ya uvivu, mvivu hawezi akathaminika wala kuheshimika: Mara zote mvivu haheshimiki, kutokana na matendo, mienendo na tabia zake zisizokuwa na uelekeo wala malengo. Tabia ya uvivu humpunguzia mtu hadhi ya kuheshimika, kwani kila jambo yeye huwa anashindwa; kiuchumi, kibidii, kimafanikio, kiubunifu na kimaarifa.



19. Mvivu ni mvivu hata kujifunza maarifa mapya ili aweze kubadirika:
Kutokana na uvivu kumtawala; mtu mvivu ni mvivu hata kujifunza maarifa mapya ili aweze kufanikiwa na kujikwamua kimaisha. Hata kama atapatiwa elimu, ushauri na maarifa mapya anaweza kushindwa kutokana na kuwa mvivu katika kusimamia, kutekeleza na kujibidisha kwa kile alichojifunza au kushauriwa na wengine.



20. Mvivu anatatizo la kuahirisha ahirisha kazi na mambo yake: Mtu mvivu huwa na changamoto ya kuahirisha-ahirisha kutimiza, kutekeleza mambo na shughuli zake kwa wakati. Tatizo la kuahirisha-ahirisha mambo kwa luhga ya Kingereza linaitwa “Procrastination”. Tatizo hili huwakabili watu wengi walio wavivu na huchukua sehemu kubwa ya maisha yao. Kuwaza na kusema “nitafanya tu” ndiyo kauli mbiu ya mtu mvivu mwenye tabia ya kuahirisha-ahirisha mambo, kazi, majukumu.



21. Mvivu hujipatia pesa, vitu na mali kwa njia zisizo halali:
Mtu mvivu hudhulumu, hutapeli, hukaba, huiba; hunyang’anya vitu, mali, au pesa, hivyo, njia azitumiazo mtu mvivu kujipatia mali, vitu, pesa huwa ni njia zisizo halali. Mvivu anaweza akadhuru, akaua, akateka ili mwisho wa yote apate kitu, mali au pesa kwa njia hatarishi zilizo kinyume na Mungu, ubinadamu, sheria na taratibu.
 

Attachments

Back
Top Bottom