Nakupa Taarifa hii hapa ndogo uisome
HATIMAYE Serikali imekalimisha ujenzi wa Barabara ya Kusini yenye urefu wa kilomita 504, ambayo kwa miaka na miaka imekuwa kero kubwa kwa wananchi wa mikoa minne, kufuatia kuzinduliwa kwa kipande cha kilomita 60 cha kati ya Ndundu na Somanga katika sherehe iliyofanyika , Ijumaa, Agosti 7, 2015.
Aidha, kuzinduliwa kwa kipande hicho cha barabara kumeiwezesha Serikali ya Rais Jakaya Mrisho Kikwete kukamilisha ujenzi wa miradi 13 mikubwa katika Ukanda wa Maendeleo wa Mtwara (Mtwara Development Corridor).
Vile vile, kwa kukamilisha kipande hicho cha barabara ambayo ni sehemu ya Barabara Kuu ya Dar es Salaam-Kibiti-Lindi hadi Mingoyo, kunaifanya Serikali ya Awamu ya Nne kutumia kiasi cha shilingi trilioni tisa katika miaka 10 ya uongozi wa Rais Kikwete.
Kilomita 60 za Ndundu-Somanga ni sehemu pekee iliyokuwa imebakia katika kukamilisha ujenzi, kwa kiwango cha lami, barabara kuu iendayo mikoa ya kusini ambayo kabla na baada ya uhuru imekuwa kero kwa wananchi wa Mikoa ya Dar es Salaam, Pwani, Lindi na Mtwara.
Sherehe ya uzinduzi wa kipande hicho cha barabara umefanywa na Rais Kikwete katika eneo la Marendego, Wilaya ya Kilwa, mpakani kwa mikoa ya Pwani na Kilwa na kuhudhuriwa na mamia ya wananchi wakiwemo mawaziri na Naibu Mawaziri sita akiwemo Waziri wa Ujenzi John Pombe Joseph Magufuli.
Akizungumza katika sherehe hiyo kabla ya kumkaribisha Rais Kikwete kuzindua barabara hiyo, Waziri Magufuli amesema kuwa chini ya uongozi wa Rais Kikwete,miradi 13 mikubwa ya barabara imetekelezwa na inaendelea kutekelezwa katika Ukanda wa Maendeleo wa Mtwara ambao unaunganisha nchi za Tanzania, Malawi na Mozambique.
Waziri Magufuli ameitaja miradi hiyo kuwa ni ujenzi wa Daraja la Umoja ambao umekamilika, ujenzi kwa kiwango cha lami wa barabara ya Songea-Namtumbo yenye kilomita 72 ambao umekamilika, ujenzi kwa kiwango cha lami wa barabara ya Peramiho Junction-Mbinga yenye kilomita 78 ambao umekamilika na upembuzi yakinifu na usanifu wa kina kwa ajili ya ukarabati wa barabara ya Mtwara-Mingoyo-Masasi yenye urefu wa kilomita 200 ambao umekamilika na ujenzi kwa kiwango cha lami wa barabara ya Masasi-Mangaka yenye kilomita 54 ambao umekamilika.
Miradi mingine ni ujenzi kwa kiwango cha lami wa barabara ya Mangaka-Mtambaswala yenye kilomita 65.5 ambao unaendelea, ujenzi wa kiwango cha lami wa barabara ya Mangaka-Nakapanya wenye kilomita 70.5 ambao unaendelea, ujenzi kwa kiwango cha lami wa barabara ya Nakapanya-Tunduru wenye urefu wa kilomita 66.5 ambao unaendelea, ujenzi kwa kiwango cha lami wa sehemu ya Tunduru-Matemanga yenye kilomita 58.7 ambao unaendelea na ujenzi kwa kiwango cha lami wa barabara ya Matemanga-Kilimasera yenye urefu wa kilomita 68.2 ambao unaendelea.
Waziri Magufuli ameitaja miradi mingine kuwa ni ujenzi wa kiwango cha lami wa barabara ya Kilimasera-Namtumbo wenye kilomita 60.7 ambao unaendelea, upembuzi yakinifu wa barabara ya Mtwara-Newala-Masasi yenye kilomita 221 ambao umekamilika na tenda tayari imetangazwa kwa ajili ya ujenzi kwa kiwango cha lami cha sehemu ya Mtwara-Mnivata yenye kilomita 50, maandalizi ya nyaraka ya zabuni kwa ajili ya ujenzi kwa kiwango cha lami wa barabara ya Mbinga-Mbamba Bay wenye kilomita 66 ambao unagharimiwa na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB).
Waziri Magufuli amesema kuwa miradi hiyo na mingine mingi ya ujenzi ambayo imejengwa na inaendelea kujengwa wakati wa uongozi wa Rais Kikwete imegharimu kiasi cha sh. trilioni tisa, ambacho ni kiwango kikubwa kuliko vyote vilivyopata kutumika kwa miradi ya ujenzi katika muongo mmoja katika historia ya Tanzania.
Waziri Magufuli amesema kuwa miradi hiyo ni pamoja na madaraja makubwa 12 ambao yamejengwa na kukamilika katika kipindi hicho ambayo ni Rusumo (Kagera), Umoja (Mtwara), Mwanhuzi (Simiyu), Kikwete (Kigoma), Nangoo(Mtwara), Ruhekei (Ruvuma), Mbutu (Tabora), Mwatisi (Morogoro), Ruvu (Pwani),(Nanganga (Mtwara), Maligisu (Mwanza) na daraja la waendao kwa miguu la Mabatini (Mwanza).
Waziri Magufuli pia amesema kuwa jumla ya madaraja mengine madogo zaidi ya 7,200 yamejengwa na kukamilika na madaraja mengine makubwa saba yapo katika hatua mbali mbali za ujenzi ambayo ni Kigamboni (Dar es Salaam), Kilombero (Morogoro), Kavuu (Katavi), Sibiti (Singida), Ruvu Chini (Pwani), Lukuledi 11 (Mtwara) na Kolo (Dodoma).
Amesema kuwa madaraja mengine makubwa ambayo yako katika maandalizi ya kujengwa ni Momba, Mwiti, Simiyu, Wami, Ruhuhu, Daraja jipya la Salendar, Daraja jipya la Wami Chini, Pangani,na daraja la wandeao kwa miguu la Furahisha.
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania - Tovuti Rasmi ya Rais