na Mwandishi Maalumu, Port of Spain, Trinidad & Tabago
WAZIRI wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, amesema ripoti iliyotolewa hivi karibuni, inayodai kuwa Tanzania inawapa silaha waasi wa kikundi cha FDLR Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), ili kuwadhuru wananchi wenye asili ya Rwanda na Congo wanaoishi katika eneo hilo ni ya uzushi, uzandiki wa makusudi na jitihada za kuchafua jina zuri la Tanzania.
Amesema kutokana na uongo huo, Tanzania inastahili kuombwa radhi na wote wanaohusika kuiandaa ripoti hiyo iliyoandaliwa na kikundi cha wataalam watano wanaohusishwa na Umoja wa Mataifa (UN).
Waziri Membe alisema ni jambo lisiloingia akilini kuwa nchi kama Tanzania iliyofanya mambo mengi na kujitolea mhanga kwa kila hali kuleta amani na kujenga usalama katika eneo la Maziwa Makuu, inaweza kushutumiwa kwa kutoa silaha kwa waasi wa FDLR.
Alitoa ufafanuzi huo alipozungumza na waandishi wa habari mjini hapa kuhusiana na habari za ripoti hiyo ambazo zimekuwa zinatangazwa katika vyombo vya habari.
Waziri Membe yuko mjini hapa akiandamana na Rais Jakaya Kikwete kuhudhuria mkutano wa wakuu wa nchi wanachama wa Jumuia ya Madola unaoendelea.
"Ripoti hiyo ni uongo wenye nia mbaya kwa Tanzania ambayo imetungwa kwa kuchochewa na nia ya kulichafua jina zuri la Tanzania na serikali yetu," alisema.
Alisema Tanzania haijapata na kamwe haitapata kufikiria kujiingiza katika vitendo vya ovyo, visivyokuwa na maana na vya kutojali vya kushiriki katika biashara ya silaha kwa nia ya kuchochea vurugu dhidi ya majirani rafiki kama Rwanda na DRC.
"Tofauti na madai hayo, Tanzania itaendelea kufanya mema katika hali ya machafuko na vurugu. Tanzania itaendelea kushirikiana na wengine katika jitihada za kumaliza, na wala si kuchochea vurugu na migogoro. Kamwe hatutamwaga petroli kwenye moto.
"Hii ndiyo kazi ambayo Tanzania imekuwa inaifanya, na inaendelea kuifanya, katika miaka 15 iliyopita. Rekodi yetu katika hili inajulikana na inajisemea na kujithibitisha yenyewe. Tanzania kamwe haiwezi kushiriki katika unafiki," alisema.
Aidha, alisema tokea kutoka kwa ripoti hiyo, Tanzania imekuwa inashangaa ni wapi inapata silaha hizo.
"Kwa bahati mbaya sana, ripoti hiyo haisaidii kutoa mwelekeo katika jambo hilo. Inachofanya ripoti hiyo ni kukariri watu wasiotajwa, kusema uzushi na kufikia maamuzi yasiyokuwa na msingi.
"Kazi ya kikundi hiki imeiacha Serikali ya Tanzania ikishangazwa na kiwango cha kutisha cha ukosefu wa ufanisi na ukosefu wa weledi iliyofanywa na kikundi kilichoundwa na Umoja wa Mataifa, taasisi ambayo Tanzania inajua kuwa ni makini na yenye kuheshimika sana.
"Serikali ya Tanzania inakuwa haina jingine la kufikiria isipokuwa kuichukulia ripoti hiyo kama madai yanayostahili kudharauliwa na yenye nia mbaya," alisema Wazir Membe.
Aliongeza kwa kueleza kuwa, Tanzania haina maduka ya kuuza silaha za kivita na hairuhusu maduka hayo. Licha ya kutokuwa na mipango ya kufanya hivyo sasa ama siku zijazo.
Alisema katika Tanzania, silaha za namna hiyo zimo mikononi mwa majeshi ya taifa, hivyo kikundi hicho kuihusisha Tanzania na vitendo vya kudharauliwa kama hivyo, inamwacha mtu kuanza kuamini kuwa silaha hizo zimetoka mikononi mwa majeshi ya ulinzi ya Tanzania.
"Nataka kumhakikishia kila mtu kuwa jambo hilo halijatokea na halitatokea kwa sababu serikali kamwe haiwezi kuliruhusu kutokea. Kwa hakika, hakuna hata ripoti za kupotea kwa silaha kutoka kwenye maghala ya silaha za jeshi letu la ulinzi ama polisi wetu.
"Ndiyo maana nasema kwa nguvu zote kuwa, ripoti hii imetungwa makusudi kwa nia mbaya dhidi ya Tanzania. Tanzania siku zote imekuwa mwanachama mwenye wajibu mkubwa katika eneo letu na katika familia ya Umoja wa Mataifa. Tanzania imefanya mengi kutafuta na kudumisha amani katika eneo la Maziwa Makuu na nje ya eneo hilo," alisema.
Kwa mujibu wa Jarida la Africa Confidential ambalo huchapishwa London, Uingereza, kikundi hicho cha wataalam cha UN kinaundwa na watu watano kutoka Ubelgiji, Guinea, Marekani, Italia na Uingereza.
Jamani nawashauri mawaziri wajihadhari na research za western countries mara nyingi zina ukweli kwasababu hawa mabwana wanahifadhi their academic integrity. Je unayosema mkuu kuna ukweli ndani? au wao wanasema ukweli? na Meremeta je!!!!!