WAKATI baadhi ya wananchi, wakihoji juu ya uhalali wa Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Gray Mgonja, kuingilia kazi zisizomhusu kwa kusaini barua ya Ikulu, Spika wa Bunge, Samuel Sitta amejitokeza na kumtetea.
Akizungumza na mwandishi wa gazeti hili jana mjini hapa, Spika Sitta alisema Mgonja, ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Hazina, hakuvamia kazi za Ikulu, kama inavyohojiwa na watu hao.
Spika Sitta alitoa kauli hiyo alipotakiwa kufafanua kuhusu taarifa ya maandishi ya maamuzi yake (Spika) kuhusu Mbunge wa Bukoba Vijijini, Nazir Karamagi (CCM) iliyonukuu barua ya Mgonja ya Juni 18, mwaka huu, ikithibitisha kuwa uamuzi wa kuongezwa muda mkataba kati ya Kitengo cha Kupakia na Kupakua Makontena Bandarini (TICTS) na serikali, ulifuata taratibu zote.
Barua hiyo ya Mgonja pamoja na kauli ya Spika Sitta ya kuitaja Ikulu, ndivyo vilivyowafanya wananchi na vyombo vya habari waibue mjadala wakihoji uhusiano wa Mgonja kama Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Ikulu.
Katika ufafanuzi wake jana, Spika Sitta alikiri kuwa ofisi yake ilipokea barua ya Mgonja inayothibitisha kwamba, mkataba wa TICTS ulifuata taratibu za maamuzi serikalini.
Barua hiyo ya Mgonja, ni moja ya ushahidi uliowasilishwa na Karamagi kwenye Ofisi ya Spika kuthibitisha kauli yake kuhusu mkataba huo.
Ushahidi mwingine uliowasilishwa na Karamagi kwa mujibu wa taarifa ya maamuzi ya Spika, ambayo Mwananchi inayo nakala yake, ni barua yenye Kumbukumbu Na. TYC/A/400/386 ya Oktoba 25, mwaka 2005 iliyosainiwa na Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Peniel Lyimo kwenda kwa Ofisa Mtendaji wa TICTS.
Spika Sitta alisema, baada ya Mgonja kuwasilisha ushahidi huo, ofisi ya Bunge iliona kuwa zina upungufu na hivyo, Katibu wa Bunge akawasiliana na Ikulu kupata ukweli kuhusu suala hilo.
Alisema baada ya mawasiliano hayo, Ikulu ilimwelekeza Mgonja aiandikie Ofisi ya Spika kuelezea suala hilo kwa vile Hazina ndiyo inayoshughulikia raslimali za nchi, ikiwamo bandari.
Wakati huo huo, Mbunge wa Maswa, John Shibuda (CCM), alimweza mwandishi wetu nje ya Ukumbi wa Bunge mjini hapa kwamba, hashangazwi na majibu ya Ikulu kuhusu mkataba wa TICTS.'' Sishangai kwa sababu hata maovu yana msemaji wake,'' alisema.