Hadithi Kali: Kilele Kiitwacho Uhuru

Hadithi Kali: Kilele Kiitwacho Uhuru

Filipo Lubua

JF-Expert Member
Joined
Nov 18, 2011
Posts
339
Reaction score
578
Ilikuwa ni mchana wa jua kali, miti yote ikiwa imepukutisha majani yao na kuifanya ionekane kama mtu aliyesimama uchi. Sauti za ndege wa aina mbalimbali zilisikika zikilalama huku na kule, kama zilizokuwa zikilaani ukame ulioivamia nchi. Mara kadhaa sauti hizo zilifunikwa na sauti mbaya zaidi za nyani na tumbili ambao walilia bila mpangilio wowote. Nyani na tumbili hawa walikuwa wakilia ovyo kwa sauti nzito na za kuogofya, wakati wengine, labda walikuwa ni watoto wao, wakilia kwa sauti zilizokuwa zikifanana na miluzi mibaya; ilikuwa ni kama miluzi ya vijana wa mtaani, wasiokuwa na kazi, wakimzomea ama kumshangilia msichana aliyepita karibu nao akiwa amevaa sketi fupi au suruali ya kubana.

Katikati ya mbuga hii maarufu – Mbuga ya Mahandaki – hapakuwa na dalili zozote za kuwepo binadamu aliyekuwa akiishi hapa. Chemichemi zilizokuwa zikitiririsha maji majira yote ya mwaka, sasa zilikuwa zimekauka. Miti ilikuwa imepukutisha majani yake na wala hapakuwa na mti uliokuwa na matunda. Hata miti yenyewe, ilionekana kushangaa hali ilivyokuwa mwaka ule. Kiangazi kikuu kilichoikumba nchi ya Marumere mwaka ule kilifanya eneo hili la nyika, lionekane kama jehanamu ndogo.

Msitu huu ulikuwa maarufu kwa jina la Mbuga ya Mahandaki maana katika vita iliyopiganwa zamani kidogo dhidi ya nchi jirani, askari wa nchi ya Marumere walichimba mahandaki yao kwa ajili ya shughuli za kijeshi. Ni mbuga hiihii ambayo miaka ya zamani wazee wa kimila waliitumia kufanya matambiko yao wakati jamii ilipopata matatizo mbalimbali kama ukosefu wa mvua au kutabaruku miungu yao wakati wa mavuno. Ni mbuga ambayo miaka michache iliyopita ilikuwa maarufu sana kwa shughuli za utekaji magari zilizofanywa na maharamia kutoka nchi jirani ya Somalia wakishirikiana na Wamarumere wachache.

Katika hali ya kushangaza, leo kuna basi kubwa la abiria likiwa limeegeshwa kandokando ya barabara. Lilikuwa ni basi kubwa lenye rangi ya njano na kijani ambazo zilikuwa zimeshachujuka na kuliacha basi likiwa nyang’anyang’a. Lilikuwa ni basi lililoonekana la zamani kabisa, chakavu na kuukuu; lilionekana zahiri shahiri kuwa lilishakunywa lita nyingi za mafuta kama sio kula chumvi nyingi. Kioo cha dirisha la upande mmoja kilionekana kutengemezwa katika mbao ndogo na kufungwa kwa kamba ya manila ili kisianguke huku usukani nao ukiwa umefungwa kwa matambara. Kwa kulitazama basi lile, mtu asingeshawishika kuwa lina uwezo wa kubeba abiria kutoka sehemu moja kwenda nyingine.

Abiria walikuwa wamekaa pembeni wakiwa na mioyo iliyopukutika putiputi kama vile miti iliyopukutisha majani yake wakati wa majira ya kiangazi. Wanawake wajawazito walikuwa wamelala chali pembeni kwenye kivuli huku wakionekana wamekata tamaa. Watoto wadogo nao walikuwa wamelazwa vivulini huku kanga walizotandikiwa chini zikiwa zimefunikwa na vumbi jekundu. Watu walionekana kama wako matangani, kwenye msiba wa mtu maarufu katika kijiji cha watu wanaopendana. Wanaume, kwa upande wao, walikuwa kama hawajali sana; wengine walikuwa wakihangaika na utingo wa basi kufanya hiki na kile wakati wengine walikuwa kwenye vikundi vidogovidogo wakiongea, wakicheka na wengine kuonekana kupandwa na hasira.

Abiria wote walikuwa wanavuja jasho huku miili yao ikiwa imetapakaa mavumbi. Mchanganyiko wa mavumbi na jasho lililokuwa likiwavuja viliwafanya waonekane kanakwamba walijipaka matope. Urembo! Ah! Afadhali ungekuwa ni urembo. Wote walikuwa wananuka sana. Nguo zao – kama basi zilikuwa zikistahili kuitwa nguo – zilikuwa zimejaa kila aina ya uchafu. Kwani basi zilikuwa nguo! Au nguo inastahili kuitwa nguo kama itakuwa haijamsitiri mvaaji? Mbona hizi zilikuwa zimeraruka kanakwamba walikuwa wamenusurika kutoka kwenye makucha ya simba…..? Ah! Labda makucha ya chui….!

Wakinamama na wakinadada wazuri walikuwa nyang’anyang’a. Ndio, walikuwa ni wazuri maana macho yao na maumbo yao yalikuwa yanafanana au yanazidi ya wale waliokuwa wakisifika kwa uzuri kule mjini. Hata hivyo uzuri wao ungetambuliwa tu na mtu anayeweza kuchunguza vizuri na wala si mtu wa kuangalia mavazi. Wengi wa wanawake na wakinadada walikuwa wamevalia mavazi ambayo sio tu yalikuwa hayawapendezi bali pia yalikuwa makuukuu. Mavazi yao yalikuwa yamewasitiri tu sehemu za kifuani na kiunoni huku sehemu nyinginenyingine za miili yao zikiwa wazi. Hiyo ilikuwa ni kawaida na wala hakuna aliyeshangaa! Hayo ndiyo yaliyokuwa mavazi ya safari hasa safari hii ya kupita barabara hii ya vumbi. Wengi wao walikuwa na nguo mbili au tatu nyumbani kwao kwa ajili ya kuendea sehemu muhimu kama msikitini, kanisani au kwenye harusi.

Tofauti na wengi wao, walikuwepo kinadada wawili ambao walikuwa wamevalia suruali za kubana na vitopu vilivyolala sambamba na miili yao na kuacha milima miwili iliyolingana ikionekana barabara vifuani mwao. Hawa walikuwa kama siafu mwekundu katikati ya msafara wa chunguchungu weusi. Walikuwa wamekaa pembeni mwa kiti cha dereva, wakiwa hawajali kitu chochote kilichokuwa kikiendelea. Dereva alikuwa ameegemea usukani wa basi huku akionekana anauchapa usingizi. Hakutaka bughuza wala tafrani kutoka kwa mtu yeyote. Mara kwa mara msichana mmoja kati ya wale wawili alionekana akimchua dereva yule mgongoni kwa mchuo wa kupendeza na kuliwaza. Walikuwa wanaonekana wameshibana haswa.

Wakinababa na wavulana hawakuwa na tatizo sana. Walishazoea kutembea vifua wazi wakiwa wamevalia kata-mikono. Nyingi ya kata-mikono walizokuwa wamezivaa, zilikuwa ni nyeupe wakati ziliponunuliwa. Hata hivyo, pengine kwa kuvaliwa sana, kufuliwa bila sabuni au kutokufuliwa kabisa, zilikuwa zimebadilika rangi na kuchukua rangi ya udongo. Vifua vyao vilikuwa vimejaa ukurutu haswa. Hawakuwa na sabuni ya kuogea kila siku, licha ya ile ya kufulia nguo zao. Hata hivyo balaa lilowapata siku ile liliwafanya waonekane wachafu zaidi. Haijalishi. Hawa ni wanaume; wanaume wa kazi!

Wanaume hawa walikuwa wakiongea kwa jazba sana, huku wengi wakionekana kumzonga kondakta wa basi lile.
“Nyie ni wapumbavu sana! Hamwezi kutufanya wajinga kiasi hiki,” alisema kijana mmoja wa makamo. “Mmetunyonya vya kutosha, hata damu imeshakauka kwenye mishipa yetu. Au mwataka mtule na nyama kabisa?”

“Mnataka mtugande kooni kama ruba ili hata pumzi tunayovuta iende kwenye mapafu yenu?” Alilalama mwanaume mwingine. “Japokuwa nimeishia darasa la saba najua kuhesabu vizuri. Ndio, ni miaka hamsini sasa. Nakumbuka mwalimu wangu wa darasa la tano alinifundisha kuwa ikifika miaka mia moja huitwa karne. Sasa ni nusu karne! Mtu huzaliwa akaota mvi na kuwa na wajukuu. Tumechoka sasa na huu m-basi wenu, na kuanzia leo sipandi basi hili tena….!” Alimalizia yule mwanaume aliyeonekana kujawa na hasira pomoni. Alikuwa akihema kama mbwa aliyetoka mawindoni; au kama kuku aliyekuwa na hasira ya kuchukuliwa kifaranga wake na mwewe.

*********************Itaendelea nikiona mmeipenda wadau*****************************
 
Umetumia kiswahili kigumu but nzuri
 
hapo hilo basi tu ni kama ma sisiemu vile mana huko kuchoka ni hatari sana.
 
Mkuu tushushie basi part two ya hiyo story,tu enjoy.
 
hapo hilo basi tu ni kama ma sisiemu vile mana huko kuchoka ni hatari sana.
Mkuu, hayo ni ya kwako tu. Mimi hadithi nimeandika kuhusu basi, hiyo habari ya masisiemu mimi siijui. Labda tu ni matukio yamefanana
 
Nilifurahia hadithi yako ya basi - na ninasubiri kwa shauku kusoma sehemu ya pili.

Lakini mimi ndiye mwanafunzi wa kiswahili tu, na nina maswali machache kuhusu msamiati wa hadithi hii. Labda una nafasi kuyazingatia yafuatayo:

1. Uliandika "kutengemezwa". Labda ulikusudi kuandika "kutengenezwa"?

2. Uliandika "balaa lilowapata". Labda "balaa iliyowapata" ilikusudiwa?

Maneno yaliyobaki ni maneno ambayo nimekosa kuona katika kamusi zangu, kwani kamusi hazina maneno mengi ya kisasa.

3. "nyang’anyang’a" ni nini ?

4. "zahiri shahiri" ?

5. "putiputi" ?

6. "vitopu" ?

7. "bughuza" ?

Ningekushukuru sana kuandika ufafanuzi mfupi sana kwa maneno haya.

Asante.
 
Nilifurahia hadithi yako ya basi - na ninasubiri kwa shauku kusoma sehemu ya pili.

Lakini mimi ndiye mwanafunzi wa kiswahili tu, na nina maswali machache kuhusu msamiati wa hadithi hii. Labda una nafasi kuyazingatia yafuatayo:

1. Uliandika "kutengemezwa". Labda ulikusudi kuandika "kutengenezwa"?

2. Uliandika "balaa lilowapata". Labda "balaa iliyowapata" ilikusudiwa?

Maneno yaliyobaki ni maneno ambayo nimekosa kuona katika kamusi zangu, kwani kamusi hazina maneno mengi ya kisasa.

3. "nyang'anyang'a" ni nini ?

4. "zahiri shahiri" ?

5. "putiputi" ?

6. "vitopu" ?

7. "bughuza" ?

Ningekushukuru sana kuandika ufafanuzi mfupi sana kwa maneno haya.

Asante.

Yote uliyoyasema mkuu yaliandikwa kwa usahihi kabisa. Wakati mengine ni maneno ya Kiswahili cha Kisasa, mengine ni takriri na mengine yametoholewa tu. Nadhani nikupe hiyo kama kazi ya nyumbani. Unaweza kuomba msaada kwa jirani akusaidie.
 
Yote uliyoyasema mkuu yaliandikwa kwa usahihi kabisa. Wakati mengine ni maneno ya Kiswahili cha Kisasa, mengine ni takriri na mengine yametoholewa tu. Nadhani nikupe hiyo kama kazi ya nyumbani. Unaweza kuomba msaada kwa jirani akusaidie.

Sawa mwalimu, nitaendelea kufanya kazi yangu ya nyumbani. 🙂 Lakini, kwa bahati mbaya, tangu niliporudi nyumbani Marekani sina majirani wanaoweza kunisaidia na Kiswahili! Labda wanachama wengine wa JF wanaojaribu kuboresha Kiswahili chao watatoa mawazo yao juu ya msamiati wako wa juu, ili kufaidisha wote.
 
Sawa mwalimu, nitaendelea kufanya kazi yangu ya nyumbani. 🙂 Lakini, kwa bahati mbaya, tangu niliporudi nyumbani Marekani sina majirani wanaoweza kunisaidia na Kiswahili! Labda wanachama wengine wa JF wanaojaribu kuboresha Kiswahili chao watatoa mawazo yao juu ya msamiati wako wa juu, ili kufaidisha wote.

Kumbe wewe ni wa Marekani! Basi niambie uko mji na jimbo gani ili nikuelekeze kwa mtu anayeweza kukusaidia. Watu wamejaa kila kona
 
Kumbe wewe ni wa Marekani! Basi niambie uko mji na jimbo gani ili nikuelekeze kwa mtu anayeweza kukusaidia. Watu wamejaa kila kona

Kweli, unajua kuhusu jamii ya Kiswahili Marekani? Mimi ninaishi Sacramento, California. Ningependa sana kuona chama cha wasemao Kiswahili hapa. Marafiki zangu wote wasemao Kiswahili ni Watanzania, wanaoishi Tanzania. Nimewauliza maswali mengi ya Kiswahil (kwa barua pepe), lakini ingekuwa nzuri zaidi kumkuta mwalimu wa Kiswahili hapa.
 
Ngoja nitarudi, nine athari za ukame
 
Kweli, unajua kuhusu jamii ya Kiswahili Marekani? Mimi ninaishi Sacramento, California. Ningependa sana kuona chama cha wasemao Kiswahili hapa. Marafiki zangu wote wasemao Kiswahili ni Watanzania, wanaoishi Tanzania. Nimewauliza maswali mengi ya Kiswahil (kwa barua pepe), lakini ingekuwa nzuri zaidi kumkuta mwalimu wa Kiswahili hapa.

Tembelea hapa: Chaukidu | Chama cha Kiswahili Duniani
Kama unahitaji msaada zaidi, tafadhali usisite kunijulisha. Mimi niko Ohio
 
Back
Top Bottom