MPANGAJI 17
By CK Allan, 0746 266 267
Sasa Bwana Yahaya Kidude alikua akitabasamu huku akimpa mkono Sele ambaye hata hakushughulika kuushika,
“bwana Kidude, naomba kujua alipo mke wangu tafadhali” aliuliza Sele huku akisogea
“sikiliza Bwana Gift ni makosa kidogo yalitokea lakini nilitaka tu tuongee kidogo wewe na mke wako na kukupa pole kwa haya yote yaliyokukuta” alisema Bwana kidude akikaa chini
“tafadhali naomba kujua mke wangu alipo” alirudia tena Gift na sasa Bwana kidude akamkonyeza mlinzi wake mmoja ambaye aliingia chumba kingine na na kutoka na Esta,
Gift alimuona mke wake akiwa mzima kabisa na kumkimbilia na kisha wakakumbatiana
“Bwana Gift kama ujuavyo sisi tunatetea haki za watanzania nikaona walau nikuite ili kama kuna chochote naweza kukusaidia katika harakati zako hizi” alisema Bwana Kidude
“kunisaidia huko kwa kuniteka mimi na mke wangu ndio nini?” aliuliza Gift
“kama nilivyokuambia ni kuwa ni makosa madogo tu yamejitokeza lakini lengo tukae pamoja mimi na wewe”
“huu ni ujinga na tafadhali kaa mbali na maisha yangu” alisema Gift akimshika mke wake mkono na kutoka nje
“nafurahi sana kusikia hivyo Gift tuko pamoja” alipaza sauti Bwana kidude
Gift alitoka nje na kumfungulia mke wake mlango kisha akazunguuka haraka na kuondoa gari kwa kasi kuelekea nyumbani kwao
“imekuwaje kwani mbona sielewi” alianza Esta
“hata mimi pia Sielewi” alisema Gift
“ulipoondoka tu na wale jamaa hawa wakaja wakasema kuwa wamekuteka wewe na hivyo nikikataa kuongozana nao tu wanakuua kule kule, lakini pia nashangaa walikua wananilazimisha nitembee vizuri kana kwamba hakuna kitu!” Esta alisema
Sele nae alikumbuka walimuambia maneno hayo hayo
“tutajua tu lengo lao hawa watu,lakini siamini kama wametuchukua vile ili kutuambia ule upuuzi tu” alisema Sele
Tayari ilishafika majira ya saa 10 waliegesha katika mgahawa mmoja na kupata chakula cha mchana,
Sele alifungua sehemu aliyokua anahifadhi vitu vyake vidogo vidogo na ndipo akastuka kuona bahasha ya kaki ikiwa imekunjwa, kwakuwa tayari Esta alishatangulia hakuona ni busara kuifungua ile bahasha muda ule hivyo alichukua tu wallet yake na kushuka kisha wakaagiza chakula na baadae wakarudi kwenye gari kuendelea na safari yao kurudi nyumbani
“vipi kama hii bahasha ina mambo ambayo si Vyema Esta ayaone?” Sele aliwaza
“au pengine kuna kitu kibaya hapa nikifungua tunakufa wote?” aliwaza
Alikuwa na uhakika ile bahasha hakuweka yeye na hivyo lazima amewekewa na wale jamaa
“sele!”
“sele!” Sasa Esta alikua anamtingisha kumstua kwani tayari alikuwa mbali mawazoni
‘basi tu kuna jambo nawaza hapa” alisema Sele sasa akikaribia maeneo ya Mbweni kule wanapoishi
kwa mbali waliona gari la polisi karibu na nyumbani kwao
“itakuwa Mr K alinitafuta sana akanikosa ndio maana akatuma polisi” alisema Sele
“hapana ni mimi nilifanikiwa kumtumia ujumbe kuwa tumetekwa” alisema Esta
“kwa jinsi gani?” aliuliza
“tutaongea nyumbani nimechoka sana sele” alisema Esta sasa akitabasamu kufika kwake
Walifika getini kwao na kukuta tayari polisi wanne wakiwa mlangoni wanawasubiri
“kweli leo imekuwa siku mbaya” aliwaza Sele akishuka
“Bwana Sele sisi ni maafisa wa Polisi na huyu mwenzetu ni mwakilishi kutoka makao makuu ya taasisi ya kupambana na Rushwa, upo chini ya ulinzi kwa kupokea Rushwa ili kumchafua raisi mstaafu pamoja na familia yake, na hapa tuna kibali cha kupekua nyumba pamoja na gari yako!” alisema Yule polisi akitoa hati ya upekuzi
“subiri kwanza nimpigie mwanasheria wangu!” alisema Sele
“unaweza kumpigia tukutane kituoni lakini kwasasa wewe ni mtuhumiwa tayari” alisema sasa wakianza kupekua gari kuanzia kwenye buti ya gari kisha wakaingia ndani na kupekua na kutoa bastola na vitu kadhaa na ile bahasha!
‘Sele kitu gani kinaendelea” aliuliza Esta akihamaki
“sijui Esta”
Wale polisi sasa walisogea na kuanza kufungua ile bahasha ya kaki na kutoa mabunda matano ya fedha dola za kimarekani
“Ohh shit, kidude!’ aliwaza Sele sasa akiwa amekata tama
“Bwana Sele uko chini ya ulinzi”
Walisema sasa huku pingu zikipita mikononi mwa sele
Na kisha wakawaongoza kwenye gari la Polisi na safari ya kuelekea kituoni ilifika
Walifika kituo cha polisi huku sasa taarifa zikisambaa kila kona ya nchi na tayari waandishi wa habari walikua nje ya kituo kikuu cha polisi kwa ajili ya kusubiri wakati sele na mkewe wakiwa wanaletwa chini ya ulinzi mkali, mara baada ya kufika tu waliingizwa kwenye vyumba viwili tofauti na mahojiano yalianza huku Sele akikanusha kila hoja,
Baadae Sele alikataa kutoa ushirikiano akisubiri mwanasheria wake aje, na hivyo hakukua na budi kumsubiri ambaye alifika baada ya masaa matatu,
Aliingia huku akiwa akiwa na huzuni, tofauti na miaka yote ambayo Sele alimjua mwanasheria wake huyo katika baadhi ya kesi chache binafasi na zile za kampuni , leo sio Yule mwanasheria wake aliyekuwa akimjua siku zote
‘hei Rapha, kunani kitu gani kinaendelea?” aliuliza Sele akisimama
“usiwe na shida kaka, ninajaribu kufanya niwezalo lakini niambie ukweli broo” alisema Rapha akiweka begi lake chini lililokuwa na nyaraka zake
“tupishe!” alisema Rapha akimwambie Yule polisi aliyekuwa akimhoji Sele
‘kwa uhalisia unaweza kuona nimechelewa kuja, lakini nilikua nafuatilia kila jambo, Mpaka sasa jamaa wana ushahidi wa kutosha Sele” alianza kusema
“unasemaje wewe?” aliuliza sele alifoka
‘kamera za nyumbani kwako, na kamera za kule nyumbani kwa Kidude zinaonyesha kabisa hakukua na utekaji wowote!, na mbaya zaidi kidude hajulikani alipo mpaka sasa!’alisema Rapha
Sasa sele alifunguka akili zake na kumsimulia hadithi yote mwanzo mapka mwisho
“na mke wangu nae wakamwambia vile vile, kwahiyo walikua wanajua kabisa wanachokifanya ooh no!” alimalizia Sele
“ulishakutana na Bwana kidude au jamaa yoyote kabla ya leo?” aliuliza Rapha
“hapana”
“jamaa wametumia akili sana kutengeneza hii kesi”
“iko hivi, polisi wanasema walipata taarifa kuwa mheshimiwa kidude ndie aliyepanga mambo yote yale kwa kukutumia wewe ili aweze kujipatia umaarufu wa kisiasa, na kumbuka ni yeye aliibua hii kesi hata kipindi kile cha kampeni miaka kadhaa iliyopita, kwahiyo polisi wakawahi kule nyumbani kwake na wengine wakaenda nyumbani kwake,kwa bahati pale kulikua na jamaa yangu mmoja hivi ndio akanijulisha kuwa wewe unatafutwa,
Sasa jamaa wametengeneza mchoro mmoja mzuri sana,ila bado tunaweza kuwashinda, kwasasa tujaribu tuwezavyo upate dhamana” alisema Rapha
Ni kweli nje ya kituo cha polisi tayari watu walikuwa wamejaa na wengine wakifuatilia kwenye mitandao ya kijamii,
Mr K pamoja na watu wengine wa kampuni ya We4u Walifika polisi na kuangalia namna ya kuweza kumtoa Sele na mke wake kwa siku ile lakini jitihada zao ziligonga mwamba.
Kesho yake kupitia vyombo vya habari sasa mke wa raisi mstaafu mama Joan alikua akizungumza na waandishi kuhusu habari hizo
“Tangu siku ya kwanza nilikua nawaambia watu hizi ni tuhuma za Bwana Kidude na wenzake kuchafua yale mambo mazuri yaliyofanywa na Rais Tupa, mimi namjua mume wangu vizuri, hajawahi kuchepuka na wala hakuwahi kuwa na mahusiano yoyote nje na hakuwahi kuwa na mtoto, niwasihi polisi waendelee kumshikilia huyo mwanaharamu mpaka ataje wenzake wote na sheria kali zichukuliwe ili kuwa funzo kwa wengine, na vile vile huyo bwana Kidude aliyetoroka akamatwe haraka” alisema mama Joan huku akiondoka na walinzi wake
Mzee Tuppa wakati akifuatilia habari hiyo alijikuta akitetemeka na kutupa glasi ya maji aliyokua nayo mkononi mwake, kwa mara nyingine tena mke wake huyo alikua anachukua points tatu hivi hivi asingekubali kirahisi alimuita mlinzi wake Joshua
“sasa ni wakati wetu, siwezi kukubali upuuzi mwingine utokee, imetosha” alisema akimshika bega Joshua