Hadithi : Nitakapokufa

MTUNZI: NYEMO CHILONGANI.
MAHALI: DAR ES SALAAM.
SIMU: 0718 069 269.

NITAKAPOKUFA 12

Katika kipindi chote Samiah hakuonekana kuwa na furaha kabisa, kitendo cha kupewa talaka na mume wake, Yusufu kilionekana kumuumiza kupita kawaida. Kila siku akawa mtu wa kulia tu, hakujua sababu ambayo ilimfanya mume wake kupinga kwa nguvu zote kupata ujauzito. Wakati mwingine alikuwa akijuta kile ambacho alikuwa amekifanya cha kuruhusu ujauzito.
Mtoto alionekana kuwa baraka katika familia nyingine lakini kwake akaonekana kuwa kama laana. Muda wote Samiah alikuwa mtu wa kulia tu. Wazazi wake, Bwana Hussein pamoja na mama yake, Bi Warda walikuwa na kazi kubwa ya kumbembeleza kila siku. Moyoni aliumia kupita kawaida, maumivu makali ambayo wala hakuwa akiyategemea kabla.
Mara zote alikuwa akijifungia chumbani. Kutokana na kuwa na msongo mkubwa wa mawazo huku akiwa na ujauzito, mara kwa mara Samiah alikuwa akiumwa. Kila alipokuwa akipelekwa hospitalini madaktari walikuwa wakimwambia apunguze mawazo na pia awe anakula sana lakini maneno ya madaktari wale hayakubadilisha kitu chochote kile.
Mwili wake ukanyong’onyea, kila wakati alikuwa akimfikiria mtalaka wake, Yusufu ambaye katika kipindi hicho alikuwa ameamua kuishi maisha ya peke yake. Siku ziliendelea kukatika mpaka katika kipindi kile ambacho akaanza kujisikia uchungu na kupelekwa katika hospitali ya mkoa ya Dodoma na kisha kujifungua salama mtoto wa kiume.
Kwa kiasi fulani furaha yake ikaonekana kurudi tena moyoni mwake, mtoto wake huyo ambaye aliamua kumpa jina la Nasri ambaye alionekana kumpa furaha katika kipindi hicho. Kila alipokuwa akimwangalia, alifanana nae sana huku baadhi ya maeneo akiwa amefanana na Yusufu. Samiah akapokea zawadi mbalimbali kutoka kwa ndugu, jamaa na marafiki ambao walikuja hospitalini pale.
Waandishi wa habari hawakutaka kupitwa, mara baada ya kupata taarifa kwamba Samiah alikuwa amejifungua, wakasafiri mpaka Dodoma na kisha kuchukua habari na kuwapiga picha. Taarifa hiyo ndio ambayo ilionekana kuuza sana magazeti hasa pale watu ambapo wangesikia na hatimae kutaka kumuona mtoto huyo, Nasri.
Kama ilivyotarajiwa na ndivyo ilivyotokea. Magazeti yakanunuliwa sana mitaani kiasi ambacho kiliwashangaza hata wamiliki wa magazeti hayo. Kila mtu alikuwa akitaka kumuona mtoto wa Yusufu au The Ruler kama jinsi ambavyo alivyokuwa akijuliakana katika kipindi hicho.
Mwezi wa kwanza ukapita, mwezi wa pili ukapita. Yusufu hakuacha mawasiliano pamoja na mtalaka wake, Samiah kwani mara kwa mara alikuwa akipeleka fedha za matumizi kama kuepuka lawama lakini huku moyo wake ukiwa na hasira na Samiah kwani aliona muda si mrefu angeweza kunyang’anywa kila alichokuwa nacho.
****
Yusufu akaamka kutoka usingizi, jasho lilikuwa likimtoka kupita kawaida. Akaanza kuangalia huku na kule, alikuwa akiweweseka sana. Mapigo yake ya moyo yalikuwa yakidunda kupita kawaida. Macho yake akayapeleka katika simu yake, ilikuwa saa tisa usiku. Hofu ikaanza kumjia moyoni, hakuelewa sababu yoyote ambayo ilimpelekea kuwa katika hali ile.
Huku akiwa anajiuliza, ghafla chumba kikawa na giza kubwa, taa ambayo mara kwa mara alikuwa akiiwasha ikajizima, mwanga mkali ukaanza kumulika kutoka katika kile kioo ambacho kilionekana kuwa kama mlango wake wa kuingilia katika ulimwengu wa giza. Yusufu alizidi kuogopa kupita kawaida, hali ambayo ilikuwa imetokea katika kipindi kile haikuwahi kumtokea hata siku moja.
Ghafla, sauti kali na nzito ikaanza kusikika kutoka katika kioo kile ambacho hakukuwa na mtu ambaye angeweza kukiona zaidi yake. Sauti ile ilikuwa ikimtaka kuelekea katika ulimwengu ule wa giza. Bila kujiuliza au kuleta mgomo wowote ule, akainuka na moja kwa moja kuanza kukifuata kioo kile.
Mianga kama ya radi nangurumo za ajabu zikaanza kusikika, kwa sababu ngurumo zile alikuwa amekwishazizoea, hakuogopa, akaelekea katika kioo kile na kisha kutokea katika upande wa pili. Mwendo wa Yusufu ambao alikuwa akitembea siku hiyo ulikuwa ni wa tofauti sana, kichwa chake kilikuwa kikijua wazi kwamba kitendo cha kuvunja moja ya masharti ndicho ambacho kilisababisha yale yote.
Mara baada ya mwendo fulani akaifikia nyumba ile na kisha kuingia ndani. Muonekano wa nyumba ile siku hiyo ulikuwa ni wa tofauti kabisa. Kwanza nyumba ilionekana kubwa sana kwa ndani siku hiyo, hata idadi ya watu ambao walikuwa ndani ya nyumba ile siku hiyo walikuwa wameongezeka zaidi.
Watu zaidi ya themanini walikuwa ndani ya nyumba ile, mavazi yao yalikuwa yametofautiana. Wapo ambao walikuwa wamevaa nguo nyeusi na wengine nyekundu. Mavazi yao hazikuwa suruali, zilikuwa kama mashuka makubwa ambayo walikuwa wakiyavaa kuanzia chini mpaka kufunika vichwa vyao.
Yusufu akabaki akiwa amesimama mlangoni, katikati ya watu wale kulikuwa na chombo ambacho kilikuwa kikiwaka taa huku pembeni kukiwa na kisu ambacho kilionekana kuwa na ncha kali sana. Yusufu hakutaka kupiga hatua zaidi, alichokifanya ni kuanza kuelekea mbele kabisa huku watu wote ambao walikuwa mahali pale wakiwa wameinamisha vichwa vyao huku kwa mbali sauti zao zikisikika mahali pale.
Mara baada ya kufika mbele kabisa, mtu mmoja ambaye alionekana kutisha sana akaanza kumfuata pale alipokuwa amesimama na kisha kuanza kumwangalia usoni. Macho ya mtu yule hayakuwa ya kawaida kabisa, yalikuwa mekundu kabisa huku meno yake yakiwa na ncha kali kupita kawaida.
Alichokifanya mtu yule mara baada ya kumwangalia Yusufu kwa muda fulani, akaanza kuelekea kule kulipokuwa na kisu na kisha kukichukua na kumgawia Yusufu. Yusufu hakujua kazi ya kisu kile, alibaki akitetemeka huku akijua kwamba alitakiwa ajichome na kujiua kama adhabu ambayo aliambiwa angepewa.
“Umevunja moja ya masharti yetu” Mwanaume yule alimwambia Yusufu kwa sauti nzito iliyokuwa na utetemeshi mkubwa.
Watu wote ambao walikuwa wameinama chini wakainua vichwa vyao na kisha kuanza kumwangalia Yusufu. Yusufu aliwaangalia watu wale, alikuwa akiwatambua sana huku akionekana kushtuka, hakuamini hata viongozi wengine wa nchi pamoja na matajiri wengine nao walikuwa katika ulimwengu ule.
“Tunakuadhibu” Mtu yule alimwambia Yusufu.
Mara ghafla mbele ya Yusufu kikatokea kioo kimoja kikubwa, kilikuwa mara mbili zaidi ya kile kioo ambacho kilikuwa chumbani kwake. Yusufu hakuelewa maana ya kioo kile, alibaki akikiangalia tu. Baada ya sekunde kadhaa, sura za wazazi wake, mzee Kessi na Bi Fatuma zikaonekana katika kioo kile kitu ambacho kilimfanya Yusufu kushtuka.
“Tunakuadhibu. Tunamtaka mtu mmojawapo” Mtu yule alimwambia Yusufu.
Yusufu akaanza kutetemeka, hakuamini kama adhabu ambayo alikuwa akipewa kwa wakati huo ilikuwa ni kumuua mmoja wa wazazi wake. Ule ukaonekana kuwa mtihani mkubwa sana kwake, hakujua ni mzazi gani ambaye alitakiwa kumuua katika kipindi hicho. Akabaki akiwaangalia wazazi wake kwa muda hata kabla hajaamua ni yupi alitakiwa kumuua kwa mkono wake katika kipindi hicho.
Mawazo yake yakaanza kurudi nyuma kabisa. Akaanza kukumbuka katika kipindi ambacho wazazi wake hao walivyokuwa wakiangaika sana kila siku kwa ajili yake. Hakuamini kama siku hii ya leo alitakiwa kufanya uamuzi mmoja mgumu, uamuzi wa kumuua mmoja wa wazazi wake ambao walikuwa wamejitoa sana katika maisha yake.
Alibaki kwa muda wa dakika tano akawa bado hajatoa uamuzi wowote ule. Alikuwa akiendelea kukumbuka mambo mengi ambayo yalikuwa yametokea katika maisha yake ya nyuma ambayo alikuwa amelelewa sana na wazazi wake hao. Japokuwa uamuzi ulikuwa mgumu sana kwake lakini alitakiwa kufanya kitu kimoja tu, kumuua mtu mmojawapo.
Yusufu hakuwa na jinsi, alitakiwa kufanya kile ambacho alitakiwa kukifanya mahali hapo. Akaunyanyua mkono wake ulioshika kisu. Machozi yalikuwa yakitiririka mashavuni mwake, maumivu makubwa sana yakaukumba moyo wake. Alichokifanya mahali hapo ni kuchoma taswira ya baba yake, mzee Kessi ambayo ilikuwa ikionekana katika kioo kile.
Mzee Kessi akaonekana akianza kuangaika katika kioo kile, damu nyingi zikaanza kumtoka kwa sekunde kadhaa na kisha kutulia. Yusufu akabaki akilia, hakuamini kama katika kipindi hicho alikuwa amemuua baba yake kwa mikono yake mwenyewe. Adhabu ile ikaonekana kuwa kubwa kwake, hakuamini kama baba yake ambaye alikuwa amemlea katika kipindi chote kile ndiye ambaye alikuwa amemuua kwa mkono wake mwenyewe.
Hapo hapo akapokonywa kisu kile. Yusufu akapiga magoti chini na kuanza kulia kwa uchungu mkubwa. Japokuwa watu wengine walikuwa wamekwishaanza kuondoka mahali hapo lakini Yusufu hakuondoka, bado alikuwa amepiga magoti chini huku akiendelea kulia. Ghafla akajikuta akisafirishwa kutoka katika ulimwengu ule na kutokea katika kitanda chake huku akiwa amepiga magoti vile vile. Yusufu alibaki akilia tu, hakuonekana kuamini kile ambacho alikuwa amekifanya kipindi kile, kumuua baba yake kwa mkono wake mwenyewe.
****
Siku hiyo usiku ukaonekana kuwa usiku mgumu kuliko siku zote alizowahi kuishi ndani ya dunia hii. Alijitahidi sana ili aweze kupata usingizi lakini usingizi ukagoma kabisa kuja. Mawazo yake yalikuwa yakimfikiria baba yake tu, mzee Kesy ambaye alikuwa akiishi mjini Bagamoyo. Moyo wake ulikuwa ukimuuma sana, hakuamini kama utajiri, umaarufu na mvuto ambao alikuwa nao ndio ambao ulikuwa umesababisha siku hiyo kumuua baba yake.
Yusufu alilia sana usiku huo, japokuwa hakuwahi kwenda msikitini lakini kwa kufikia hatua hiyo akaanza kumuomba Mungu aweze kumnusuru baba yake ili kile ambacho alikuwa amekifanya kule kwenye ulimwengu wa giza, kitendo cha kumuua baba yake kisiweze kufanikiwa. Hakujua angeishi vipi baada ya hapo, hakujua ni hali gani ambayo angekuwa nayo mara baada ya kusikika kwamba baba yake, mzee Kessi alikuwa amefariki.
Masaa yalizidi kwenda mbele mpaka kulipopambazuka, bado Yusufu alikuwa macho na wala hakuwa na nguvu za kutoka kitandani ambako alikuwa amelala tu. Kwa upande wake mmoja wa moyo wake ulionekana kujuta kwa kile ambacho alikuwa amekifanya lakini upande mwingine ulikuwa ukimpongeza kutoka na kitendo kile ambacho kingeufanya utajiri wake, umaarufu na hata mvuto kubaki navyo vile vile.
Saa 1:07 asubuhi, simu yake ikaanza kuita. Alichokifanya ni kuichukua na kisha kuangalia kioo cha simu ile. Jina lala ‘Dear Mom’ lilikuwa likionekana katika kioo cha simu ile. Hata kabla ya kupokea simu ile Yusufu akajua ni kitu gani ambacho kilikuwa kimetokea. Kinyonge akabonyeza kitufe cha kijani na kisha kuipeleka simu sikioni.
“Baba yako amefariki” Ilisikika sauti ya mama yake simuni hata kabla ya salamu.
Japokuwa alikuwa akijua kwamba kitu kile kingetokea lakini kwa wakati huo baada ya kupewa taarifa ile moyo wake ukamlipuka, mapigo ya moyo yakaanza kudunda kwa kasi kupita kawaida, mzunguko wa damu yake ulikuwa ukizunguka kwa kasi sana. Yusufu hakuongea kitu, machozi yalikuwa yakitiririka katika mashavu yake, moyo wake ulijisikia uchungu kupita kawaida.
“Ninakuja huko huko” Yusufu alisema na kisha kukata simu.
Akabaki akiwa amepigwa na butwa kitandani pale, moyo wake ulikuwa ukifikiria zaidi kuhusiana na baba yake, kosa alilolifanya mke wake ambaye alimpa talaka, Samiah likaonekana kuwa kubwa kwake na ndilo ambalo ilikuwa limesababisha yale yote kutokea. Alichokifanya Yusufu ni kumpigia simu Kelvin na kumtaarifu kile ambacho kilikuwa kimetokea kwamba baba yake alikuwa amefariki.
Ndani ya dakika ishirini, Kelvin akafika mahali hapo huku akitangulizana na marafiki wengine na kisha kuanza safari ya kuelekea Bagamoyo huku wakiwa pamoja na Yusufu. Kila mmoja ndani ya gari alikuwa akimfariji, hawakujua kwamba huyo huyo Yusufu ndiye ambaye alikuwa amemuua baba yake kwa mikono yake mwenyewe.
Walichukua dakika arobaini na tano mpaka kufika Bagamoyo ambapo wakaanza kuelekea katika sehemu ilipokuwa na nyumba hiyo. Tayari watu walikwishaanza kufika mahali hapo, vilio vilikuwa vikisikika katika eneo la nyumba hiyo. Yusufu akashindwa kujizuia, akaanza kulia tena jambo ambalo liiwafanya hata marafiki zake kulengwa na machozi.
Yusufu akaanza kuelekea ndani ya nyumba yao ambapo akakutana na mama yake, Bi Fatuma na kisha kumkumbatia. Wote walikuwa wakilia, walionekana kuumia kupita kawaida. Kadri muda ulivyozidi kwenda mbele na ndivyo ambavyo watu walivyozidi kujaa ndani ya eneo la nyumba hiyo. Waandishi wa habari hawakuwa mbali, nao wakafika mahali hapo na kisha kuanza kupiga picha kila kilichokuwa kikiendelea.
Taarifa zikatangazwa kwenye vituo vya redio pamoja na televisheni. Kila mtu ambaye aliisikia taarifa ile alishtuka. Hawakuamini kama Yusufu yule yule ambaye alikuwa amepata sana umaarufu ndiye ambaye alikuwa akipitia katika mambo magumu namna ile. Wananchi wakaanza kuamini ushirikina kwa kuona kwamba kulikuwa na mtu ambaye alikuwa amesababisha hayo yote.
“Mmmh! Miezi mitano iliyopita alitalikiana na mke wake, leo hii baba yake amefariki. Nina wasiwasi kuna mkono wa mtu hapa. Kuna mtu ambaye hapendi kumuona akipata mafanikio haya” Mwananchi mmoja alisikika akimwambia mwenzake.
“Yaani na mimi nilitaka niseme hivyo hivyo. Yaani sjui kwa nini Watanzania tuna roho za kwa nini, yaani hatutaki kuwaona watu wakifanikiwa maishani mwao” Jamaa mwingine alimwambia mwenzake.
Mapenzi kwa Yusufu yalikuwa makubwa sana, hakukuwa na mtu yeyote ambaye alifahamu kwamba Yusufu huyo huyo ndiye ambaye alikuwa katika kila kilichoendelea mahali pale. Machoni mwa watu alionekana kuwa mtu asiye na hatia yoyote ile. Uso wa majonzi ambao alikuwa akiuonyesha siku hiyo ndio ndio ambao uliwaonyeshea watu kwamba alikuwa hausiki kabisa na kile ambacho kilikuwa kimetokea.
Vitu vingine viliendelea kama kawaida mhali hapo mpaka pale ambapo Shekhe Oswald alipofika msibani hapo na kisha kuongea maneno machache na mwili kupelekwa msikitini kuswaliwa na kisha kuruudishwa nyumbani ambapo harakati zote za mazishi zikaanza kufanyika mahali hapo.
Ilipofika saa 10:15 watu zaidi ya mia saba ambao walikuwa wamekusanyika mahali hapo wakaanza kuupeleka mwili wa mzee Kessi makaburini kwa ajili ya kuzikwa. Wakinamama walibaki majumbani wakilia, Bi Fatuma hakuamini kama mume wake ambaye alikuwa akimpenda kwa wakati huo alikuwa amefariki dunia na mwili wake ulikuwa njiani ukipelekwa makaburini.

Je nini kitaendelea?
Je nini kitatokea katika maisha ya Yusufu?
Umaarufu atakuwa nao zaidi au utampotea?
Je ataweza kuishi bila kuvunja masharti?
 
MTUNZI: NYEMO CHILONGANI.
MAHALI: DAR ES SALAAM.
SIMU: 0718 069 269.

NITAKAPOKUFA 13

Watanzania walikuwa wakimuonea huruma Yusufu kwa msiba mkubwa wa kumpoteza baba yake ambao ulikuwa umemkumta. Muda mwingi Yusufu alionekana kuwa mnyonge kupita kawaida. Marafiki pamoja na mashabiki mbalimbali walikuwa wakimtumia salamu za pole kwa kile ambacho kilikuwa kimemkuta katika maisha yake.
Kila mmoja alijua fika kwamba Yusufu alikuwa katika kipindi kigumu sana, kipindi ambacho alihitaji faraja kubwa sana kutoka kwa marafiki zake pamoja na mashabiki zake. Japokuwa katika kipindi hicho mazishi yalikuwa yamekwishafanyika lakini Yusufu hakutaka kurudi jijini Dar es Salaam, alihitaji muda mwingi wa kukaa na mama yake kwa ajili ya kufarijiana.
Bado kila kitu kilibaki kuwa siri, hakukuwa na mtu ambaye alijua kwamba Yusufu huyo huyo ndiye ambaye alikuwa amemuua baba yake tena kwa mkono wake mwenyewe. Moyoni aliumia kupita kawaida lakini lawama zote hizo alikuwa akimpa mke wake, Samiah kwa kufanya kitu ambacho yeye alikiona kuwa cha kijinga, kuruhusu kufanya mapenzi katika siku za hatari za kupata ujauzito. Yusufu hakutaka kuwasiliana na mkewe tena kwani aliamini kwamba kama angeendelea kufanya hivyo, alikuwa akizidi kuumia na kumkasirikia zaidi na zaidi.
“Mungu amemchukua baba yako” Bi Fatuma alimwambia Yusufu kwa sauti ya chini iliyojaa maumivu makali.
“Kazi yake haina makosa. Kila mmoja yupo safarini kuelekea huko. Yatupasa kujiandaa kwani hatujua muda wala saa” Yusufu alimwambia mama yake, Bi Fatuma.
Yusufu alikaa Bagamoyo kwa wiki moja na ndipo ambapo aliamua kurudi jijini Dar es Salaam. Watu walipojua kwamba siku hiyo ndio ilikuwa siku ambayo alikuwa akirudi kutoka Bagamoyo, zaidi ya watu elfu tatu walikuwa wamekusanyika Mwenge jijini Dar es Salaam kumfanyia mapokezi ambayo kwake yangeonekana kuwa ya mshtuko mkubwa.
“Unasemaje?” Yusufu alimuuliza rafiki yake, Abdul ambaye alikuwa amempigia simu.
“Ndio hivyo. Watu wamekusanyika hapa Mwenge, wote wanataka kukupokea” Abdul alimwambia Yusufu ambaye bado alikuwa kwenye mshtuko mkubwa.
“Sasa nifanye nini hapa manake natumia usafiri binafsi?” Yusufu aliuliza.
“Naomba usiwaangushe. Unajua wanakukubali sana na ndio maana wameamua kufanya hivi. Naomba usiwaangushe” Abdul alimwambia Yusufu.
Mapenzi ya watu kwa Yusufu yalikuwa makubwa sana kiasi ambacho mpaka yeye mwenyewe alikuwa amechanganyikiwa. Hakuamini kama angeweza kufikia hatua ya kupendwa namna ile kwamba hata kama alikuwa akitoka Bagamoyo watu wangekuwa wamekusanyika wakimsubiria, kwa wakati huo alijiona kuwa mtu mwenye umaarufu mkubwa hata zaidi ya rais wa nchi.
“Nani huyo?” Kelvin alimuuliza Yusufu huku akiendesha gari.
“Abdul”
“Anasemaje?”
“Mashabiki wangu wamekusanyika Mwenge kwa ajili ya kunipokea”
“Unasemaje?”
“Ndio hivyo. Kwa hiyo hapa tunachotakiwa kukifanya tukifika Mwenge ni kuonana na mashabiki hao” Yusufu alimwambia Kelvin.
“Alisema wapo sehemu gani pale Mwenge?”
“Hilo sikumuuliza. Ila nafikiri tukifika pale, tutawaona kwani wapo zaidi ya elfu tatu” Yusufu alimwambia Kelvin.
Bado safari ilikuwa ikiendelea kama kawaida, baada ya dakika arobaini, wakaanza kuingia Mwenge. Kwa mbali idadi kubwa ya watu ilikuwa ikionekana huku wakiwa wameshika mabango mengi ambayo yalikuwa yakimtakia pole Yusufu. Yusufu akashindwa kuvumilia, akajikuta akianza kutokwa na machozi, kila kilichokuwa kikionekana kwake kilionekana kuwa kama ndoto fulani ambapo baada ya muda fulani angeamka kutoka katika usingizi mzito.
Watu walipoliona gari la Yusufu, wakaanza kupiga kelele, waandishi wa habari ambao walikuwa wamekusanyika mahali hapo wakachukua kamera zao na kisha kuanza kupiga picha. Watu walionekana kuchanganyikiwa kupita kawaida, kurudi kwa Yusufu kulionekana kuwapagawisha watu ambao walikuwa mahali hapo.
Askari wa barabarani wakapata wakati mgumu sana katika kuyaongoza magari yaliyokuwa barabarani, watu ambao walikuwa mahali hapo walikuwa wamefunga barabara zote. Gari la Yusufu lilipokaribia, Yusufu akafungua juu na kisha kutoka nusu mwili na kuanza kuwapungia watu mkono. Watu wakaonekana kuchanganyikiwa zaidi, kwa wale ambao walikuwa na simu zenye kamera wakaanza kumpiga picha, kwao, Yusufu alionekana kuwa mpya.
Kwa wakati huo Yusufu akaonekana kuwa kama rais, umaarufu wake nchini Tanzania ukaonekana kuwa kama wa Michael Jackson katika kipindi kile ambacho alikuwa akivuma sana miaka ya tisini. Kelvin akalisimamisha gari, Yusufu hakuonekana kuridhika, alichokifanya ni kutoka kabisa garini. Watu wakaanza kumfuata, kila mtu alikuwa akitaka kumshika Yusufu.
Hata kwa watu ambao walikuwa kwenye daladala nao wakashindwa kuvumilia. Mtu ambaye mara kwa mara alikuwa akiopnekana kwenye televisheni pamoja na kusikika redioni leo hii alikuwa akionekana Mwenge, nao wakajikuta wakishuka na kuanza kumfuata Yusufu. Kila mtu alipokuwa akimshika, alionekana kuridhika kabisa. Mvuto ambao alikuwa nao Yusufu ukaonekana kuwa mkubwa mara kumi ya ule ambao alikuwa nao kabla ya baba yake, mzee kessi kufariki, damu ya baba yake ambayo alikuwa ameimwaga ikaonekana kumzidishia kila alichokuwa nacho.
“Mimi ni kama mungu wa Tanzania” Yusufu alisema kwa sauti ya chini ambayo hakukuwa na mtu aliyeisikia.
Yusufu alijiona kuwa juu, juu zaidi ya Mungu. Kupendwa na watu wengi kiasi kile kulionekana kumpa kiburi kikubwa sana, hakuona kama Mungu alipendwa kama alivyokuwa akipendwa yeye. Kiburi chake kikamfanya kujiona kuwa juu, hakukuwa na mtu ambaye alikuwa akifahamu kwamba miongoni mwa watu waliokuwa wamekusanyika mahali hapo, hata majini yalikuwepo huku wakiwa na kazi ya kuwafanya watu kumuona Yusufu kuvutia na hata kuwa na kiu ya kutaka kumsogelea.
Uwepo wa Yusufu pale Mwenge ukawa umesimamisha kila kitu, kituo cha daladala cha Mwenge kilikuwa cheupe kabisa, kila mtu alikuwa amekwenda barabarani kwa ajili ya kumuona Yusufu, mtu ambaye alikuwa na umaarufu mkubwa sana katika kipindi hicho. Watu walikuwa wakizidi kuongezeka kiasi ambacho kikawafanya wanajeshi ambao walikuwa karibu na eneo hilo kuanza kusogea kwa ajili ya kuwatuliza watu ambao walionekana kama wamechanganyikiwa kutokana na kumuona Yusufu kwa macho yao katika kipindi hicho.
“Ingia ndani ya gari” Mwanajeshi mmoja alimwambia Yusufu.
“Hiyo ngumu mkuu. Watu wanaonekana kuchanganyikiwa sana. Naomba mniruhusu kufanya kitu kimoja” Yusufu alimwambia mwanajeshi yule.
“Kitu gani?”
“Nahitaji kutembea kwa miguu mpaka Ubungo kwani naamini hivyo ndivyo watu wataridhika. Ila nitahitaji sana ulinzi wenu” Yusufu alimwambia mwanajeshi yule ambaye alionekana kumshangaa.
“Haiwezekani kabisa. Ingia ndani ya gari na uondoke katika eneo hili” Mwanajeshi yule alimwambia Yusufu ambaye akatii na kuingia garini.
Kazi ikabaki katika kuliondoa gari hilo. Watu hawakutaka kutoka barabarani na kuliruhusu gari lile kuondoka barabarani hapo, walikuwa wamesimama mbele huku wakiwa wamelizuia. Japokuwa wanajeshi walikuwa wakiwataka watu hao kuondoka na kuacha barabara nyeupe lakini watu hawakuonekana kuwaelewa, walichokuwa wakikitaka ni kumuona Yusufu akiteremka kutoka garini.
“Imeshindikana. Watu wengi halafu sisi wachache. Tufanye nini sasa?” Mwanajeshi mmoja alimuuliza mwenzake.
“Bado sijajua kifanyike nini. Ila nilikuona ukiongea nae mwanzo. Ulikuwa ukiongea nae nini?” Mwanajeshi mmoja alimuuliza yule mwanajeshi ambaye alikuwa ameongea na Yusufu kipindi kichache kilichopita.
“Alisema kwamba anataka atembee kwa mguu kutoka hapa mpaka Ubungo” Mwanajeshi yule alijibu.
“Ili iweje?”
“Kuwaridhisha watu. Ila kama asipofanya hivyo, watu hawa kuondoka mahali hapa itakuwa ngumu sana”
“Sawa. Inabidi umruhusu. Haina jinsi”
Mwanajeshi yule akaanza kulifuata gari la Yusufu. Watu waliokuwa mahali hapo bado walikuwa wakiimba huku wakimtaka Yusufu kuteremka kutoka garini vinginevyo wasingeondoka mahali hapo. Mara baada ya mwanajeshi yule kulifikia gari lile, Yusufu akashusha kioo.
“Vipi?” Yusufu aliuliza.
“Shuka. Fanya ulichotaka kufanya” Mwanajeshi yule alimwambia Yusufu.
Yusufu akaufungua mlango na kutoka nje ya gari, watu wakalipuka kwa kelele, Yusufu akanyoosha mikono yake juu na kisha kuwataka watu wanyamaze kwani alikuwa na kitu ambacho alikuwa akitaka kukiongea mahali hapo. Watu wote wakabaki kimya.
“Nahitaji kufanya kitu kimoja. Kwa sababu wengi mmekuwa mkitamani sana kuwa pamoja nami, naomba nifanye kitu kimoja kama kuwaridhisha na kisha mniache niende nyumbani kupumzika” Yusufu alisema huku akiwaangalia watu hao na kuendelea.
“Nitataka kuelekea Ubungo kwa miguu pamoja nanyi. Nitaingia garini mara baada ya kufika Ubungo. Mko tayari” Yusufu alisema na kuuliza.
“Ndiooooooooo” Watu waliitikia kwa sauti kubwa na kuanza kushangilia..
“Ila naomba mfanye kitu kimoja. Sitopenda fujo zitokee. Kwa anayetaka kunigusa nitampa ruhusa hiyo wakati tunatembea, ila sitaki fujo” Yusufu alisema na watu wote kuanza kushangilia.
Hapo hapo safari ya kuelekea Ubungo kwa miguu ikaanza. Kila mtu alikuwa akitaka kumgusa Yusufu kwa wakati huo. Watu ambao walikuwa njiani, walipoona kwamba mtu ambaye alikuwa pamoja na watu hao alikuwa Yusufu, nao wakaongezeka katika msafara huo.
Polisi hawakuwepo katika msafara huo, watu waliojiona kwamba walikuwa na miili mikubwa ndio ambao wakajipa kitengo cha kuzuia fujo mahali hapo. Kila mmoja alionekana kuchanganyikiwa kwa furaha, mbele ya macho yao, Yusufu alionekana kama Malaika ambaye alikuwa ameshushwa duniani kwa kuwaletea Neema.
Walitembea kutoka Mwenge mpaka Ubungo, kwa mtu ambaye alitaka kumgusa, siku hiyo alimgusa, kwa aliyetaka kumpiga picha, alimpiga picha. Muda wote huo, waandishi wa habari walikuwa bize wakimpiga picha Yusufu kwa ajili ya kuziweka katika magazeti yao siku inayofuata. Watu bado walikuwa wakiendelea na safari ya kwenda Ubungo huku nyimbo mbalimbali za Yusufu zikiimbwa.
Idadi hiyo kubwa ya watu ikaonekana kuziba barabara yote, kwa yale magari ambayo yalikuwa nyuma ya watu hao, yalisimama huku mengine yakiendeshwa kwa mwendo wa taratibu sana. Mpaka wanafika Ubungo, tayari askari wa barabarani wa Mwenge walikuwa wamekwishawasiliana na askari wa Ubungo, hivyo magari yaliyokuwa yakitumia barabara ile ya Sam Nujoma yalikuwa yamekwisharuhusiwa.
Mara baada ya kufika Ubungo. Yusufu akawaaga watu na kisha kuingia ndani ya gari na kuondoka mahali hapo. Hayo yakaonekana mapokezi makubwa kupita mapokezi mengine ya msanii yeyote yule, awe wa Tanzania au nje ya Tanzania, Yusufu alionekana kufunika. Baada ya watu kuliona gari la Yusufu likiondoka mahali hapo, wakanza kulipungia mikono na kumtakia safari njema huku wengine wakiwa wameshindwa kujizuia na kujikuta wakilia kutokana na furaha kubwa ya kumuona Yusufu mbele ya macho yao pamoja na kumgusa.
****
“Unamfahamu yule msichana?” Hilo lilikuwa swali kutoka kwa Yusufu akimuuliza Abdul.
“Msichana yupi?” Abdul aliuliza.
“Yule aliyevaa raba nyeupe, kipedo cha blue pamoja na fulani nyeupe.
“Yeah! Namfahamu”
“Anaitwa nani?”
“Christina Tobias. Anaishi Sinza” Abdul alimjibu Yusufu.
“Naweza kuongea nae?”
“Ngoja nikakuitie” Abdul alisema na kuanza kumfuata Christina
Yusufu alikuwa akiangaliana sana na Christina katika kipindi hicho ambacho walikuwa katika sherehe ya kuzaliwa ya msanii Mapac Jnr ambayo ilikuwa ikifanyika Mbalamwezi Beach Resourt. Katika sherehe hiyo, Yusufu alikuwa miongoni mwa watu ambao walikuwa wameitwa kushiriki katika sherehe hiyo.
Msanii Mapac Jnr alikuwa ametoa tiketi mia moja kwa watu wa nje ambao si ndugu, jamaa na marafiki kushiriki katika sherehe yake hiyo ya kuzaliwa. Watu hawakuwa wakionekana kujali, ila mara baada ya kutangaza kwamba hata Yusufu alikuwa kwenye sherehe hiyo, watu wakaanza kuzitafuta hizo tiketi ambazo ndani ya saa moja tu, tiketi zote zilikuwa zimekwisha na hivyo watu kutaka tiketi nyingine zaidi ziongezwe.
Mapac hakutaka kuongeza tiketi nyingine, zile ambazo zilikuwa zimetolewa zilionekana kutosha sana. Kwa watu wengi ambao walikuwa wameingia ndani ya sherehe hiyo baada ya kununua tiketi, walikuwa wakimtafuta Yusufu na kisha kutaka kupiga nae picha. Kila mmoja alionekana kuvutiwa na Yusufu, wasichana wengi walikuwa wakimwangalia kwa macho ya mahaba lakini Yusufu hakuonekana kuwajali, mtu ambaye alikuwa akimjali kwa wakati huo alikuwa msichana, Christina ambaye alikuwa akitumia muda mwingi kuangaliana nae.
Abdul akamfuata Christina na kuongea nae kwamba alikuwa akihitajika na Yusufu, kwanza Christina hakuonekana kuamini kama kweli Yusufu ndiye ambaye alikuwa akimuita kwa wakati huo. Akamwangalia vizuri Abdul na kisha kuyapeleka usoni mwa Yusufu ambaye alikuwa akimwangalia kwa tabasamu pana.
Kwa mwendo wa mapozi, Christina akaanza kumfuata Yusufu ambaye alionekana kama simba mwenye njaa kali, alipomfikia, akasimama karibu nae. Hata kabla hawajaongea kitu chochote kile, Yusufu akaanza kumwangalia Christina kuanzia chini mpaka juu na kisha kutoa tabasamu pana. Mapigo ya moyo wa Christina kwa wakati huo yalikuwa yakidunda kupita kawaida, hakuamini kwamba mtu ambaye alikuwa amesimama mbele yake alikuwa Yusufu au The Ruler kama alivyojulikana.
“Umependeza” Yusufu alimwambia Christina.
“Asante. Nawe umependeza pia” Christina alimwambia Yusufu huku nae akionyesha tabasamu.
“Ningependa sana usiku wa leo uwe wa kipekee sana kwangu. Ningependa sana kama tutatumia usiku wa leo pamoja” Yusufu alimwambia Christina ambaye alikuwa akijisikisikia aibu.
“Kwa leo itakuwa ngumu” Christina alijibu huku akionekana kutomaanisha alichokuwa akikiongea.
“Kwa nini?” Yusufu aliuliza.
“Nawahi nyumbani”
“Unaishi wapi?”
“Naishi Sinza”
“Sinza kubwa sana”
“Vatican City” Christina alijibu.
“Usijali. Nitakurudisha nyumbani. Ninachokitaka ni kuwa nawe usiku wa leo. Hata masaa mawili tu yanatosha” Yusufu alimwambia Christina ambaye alikuwa akiangalia chini huku akionekana kuwa mwingi wa aibu.
Yusufu hakutaka kuchelewa, alichokifanya kwa wakati huo ni kumchukua Christina na kisha kuanza kuelekea nae nje. Kwa kiasi cha pombe ambacho kilikuwa kimemchukua kwa wakati huo, hakuonekana kujali macho ya watu ambayo yalikuwa yakimwangalia kwa mshangao, alichokijali kwa wakati huo ni kuondoka na Christina tu.
Mara baada ya kufika nje, akalifuata gari lake na kisha kulifungua. Katika kipindi chote hicho, Christina hakuonekana kuamini kama kweli alikuwa na Yusufu kwa wakati huo. Moyo wake ulikuwa na furaha kupita kawaida, kuwa pamoja na Yusufu kulimfurahisha kupita kawaida.
“Usiogope” Yusufu alimwambia Christina.
“Usijali” Christina alisema huku akiufungua mlango na kukaa kitini.
Hata kabla Yusufu hajaliondoa gari mahali hapo, akamsogelea Christina na kisha kuanza kubadilishana nae mate. Kwa Yusufu, kila kitu kwa wakati huo kilionekana kuwa kama mteremko mkubwa, umaarufu mkubwa ambao alikuwa nao, fedha nyingi ambazo alikuwa nazo katika kipindi hicho zilikuwa zikifanya kila kitu kuwa rahisi kwa upande wake. Walifanya kile kitendo kwa dakika kadhaa huku wakichezeana katika baadhi ya maungo yao na kisha kuondoka mahali hapo.
Safari hiyo ilikuwa ni kuelekea nyumbani kwake, Kijitonyama ambapo mara baada ya kufika, wakateremka na kisha kuanza kuelekea ndani. Kila alipokuwa akimwangalia Christina, Yusufu alizidi kuvutiwa nae zaidi na zaidi, umbo lake la kimiss, weupe ambao alikuwa nao ulionekana kumdatisha kupita kawaida. Mara baada ya kuufikia mlango wa kuingilia sebuleni, akaufungua huku mlinzi akibaki kumwangalia Christina kwa macho ya mshangao, uzuri wake ulimdatisha hata yeye mwenyewe.
“Hapa magumashi. Twende chumbani” Yusufu alimwambia Christina na bila ubishi wowote ule, Christina akakubaliana nae.
Alichokifanya Yusufu ni kumbeba Christina na kisha kuelekea nae chumbani kwake huku akiendelea kubadilishana nae mate. Walipofika chumbani, akamtupa kitandani na kisha kuanza kumvua nguo zote. Kwa kila kitu ambacho kilikuwa kikiendelea mahali hapo, bado Christina hakuwa akiamini kama siku hiyo alikuwa akitaka kufanya mapenzi na Yusufu, mwanaume ambaye alikuwa akipenda sana kusikiliza nyimbo zake pamoja na kutamani hata siku moja kumgusa.
“Mbona unahema sana?” Yusufu alimuuliza Christina.
“Siamini” Christina alisema kimahaba.
“Hauamini nini?”
“Kuwa na wewe kitanda kimoja. Siamini The Ruler” Christina alimwambia Yusufu huku dhahiri akionekana kutokuamini.
“Amini kwamba leo upo pamoja nami Christina, amini kwamba leo unakwenda kuuona mwili wangu wote nikiwa mtupu, amini kwamba leo tunafanya mapenzi pamoja” Yusufu alimwambia Christina na kisha kuanza kufanya ngono, tena mbaya zaidi bila kutumia mpira, hakukuwa na aliyejali kwamba wangeweza kuambukiza magonjwa au Christina kupata ujauzito, walichojali kwa wakati huo ni kupeana mapenzi moto moto kitandani.


Aya sasa Yusufu kaanza kazi.
Je nini kitaendelea?
 
MTUNZI: NYEMO CHILONGANI.
MAHALI: DAR ES SALAAM.
SIMU: 0718 069 269.

NITAKAPOKUFA 14

Mapenzi yakawa yamewateka wote wawili, tangu siku ya kwanza walipofanya mapenzi wakajikuta wakianza kupendana zaidi na zaidi. Yusufu akazidi kuwa karibu na Christina jambo ambalo lilimfanya kuwa na furaha kupita kawaida. Mara kwa mara walikuwa pamoja, walikuwa wakitoka mitoko ya usiku pamoja huku katika kila safari ambayo Yusufu au The Ruler alipokuwa akienda kwa ajili ya matamasha mbalimbali, Christina alikuwa pamoja nae.
Wasichana wengine walimuonea wivu Christina, kitendo cha kuwa katika mahusiano ya kimapenzi pamoja na Yusufu kilionekana kuwa kitu cha bahati sana ambacho msichana yeyote yule angefurahi kuwa nacho. Magazeti hayakuchoka kuandika kuhusiana na mahusiano hayo ambayo yalionekana kuwa machanga lakini yenye kasi kubwa, watu hawakuacha kujiuliza kuhusiana na maisha ya Yusufu ambaye alionekana kusahau kabisa kama alikuwa na mtoto ambaye alihitajika kumlea katika kipindi chote.
Mapenzi ya Christina kwa wakati huo yakaonekana kumchanganya kupita kawaida, kila siku alikuwa akiongea nae simuni lakini hakuwa akichoka, alimthamini sana Christina, alimuona kuwa mwanamke bora hata zaidi ya alivyokuwa Samiah ambaye alikuwa mke wake wa ndoa aliyempa talaka na kumrudisha nyumbani kwao.
Katika kipindi hiki, maisha ya Yusufu yaliendelea kupata mafanikio makubwa zaidi, watu waliendelea kujiuliza juu ya mafanikio hayo lakini hakukuwa na mtu ambaye alikuwa akifikiria kuhusiana na maisha ya upande wa pili ambayo alikuwa akiishi kwa wakati huo.
“Nataka unioe” Christina alimwambia Yusufu.
“Usijali. Cha msingi kwanza tuendelee kuchunguzana” Yusufu alimwambia Christina ambaye alionekana kushtuka.
“Tuendelee kuchunguzana tena mpenzi. Kwani hii miezi sita tuliyokuwa pamoja haijatosha kuchunguzana?” Christina alimuuliza huku akionekana dhahiri kushtuka.
“Mbona muda mchache sana huo mpenzi. Tuendelee tu kuchunguzana” Yusufu alimwambia Christina huku akimbusu busu katika maeneo mengi mwilini mwake.
“Au bado unampenda mtalaka wako?” Christina aliuliza.
“Naomba usinikumbushe kuhusu huyo mpumbavu, utanifanya kesho nisafiri niende nikamuue” Yusufu alisema huku akionekana kuanza kukasirika.
“Pole mpenzi. Sikudhani kama ungeweza kukasirika namna hiyo” Christina alimwambia Yusufu.
“Usijali”
Maisha hayakuishia hapo, starehe ndio yalikuwa aina ya maisha ambayo walikuwa wakiishi katika kipindi hicho. Wasichana wengi walikuwa wakitamani sana kuwa pamoja na Yusufu lakini wala hakuonekana kuwa radhi kuwa na msichana mwingine, kwake, Christina alionekana kuwa msichana wa ndoto katika maisha yake.
Mara kwa mara Yusufu alikuwa akisafiri na kuelekea katika nchi mbalimbali kwa ajili ya kufanya shoo mbalimbali. Katika soko zima la Afrika Mashariki, Yusufu alikuwa ameliteka. Tanzania, Kenya, Uganda na nchi nyingine za Afrika Mashariki walikuwa wakipenda sana kumuita Yusufu kwa ajili ya kufanya shoo ambazo zilikuwa zikiendelea kuwaingizia fedha nyingi kupita kawaida. Yusufu akafanikiwa na kuwa mwanamuzi tajiri kuliko wote Afrika mashariki, akanunua magari ya kifahari pamoja na kujenga nyumba tano za kifahari jijini Dar es Salaam.
Yusufu hakuishia hapo, akaanzisha studio yake ambayo aliipa jina la Nasri Record, huku akiwa amechukua jina la mtoto wake aliyezaa pamoja na mtalaka wake, Samiah. Pamoja na kuanzisha studio hiyo, pia Yusufu akaongeza biashara nyingine nyingi kama maduka mengine ya nguo, maduka ya vipodozi, akafungua sehemu ya kuuzia magari pamoja na biashara nyingine nyingi. Maisha ya kimasikini ya kuishi ndani ya chumba kimoja pamoja na rafiki yake, Kelvin yalionekana kusahaulika katika maisha yake, kwa wakati huo yalikuwa ni maisha ya kula starehe tu.
“Kuna siku watu hawa wataniabudu tu” Yusufu alimwambia Kelvin mara baada ya kuona watu wamefurika katika uwanja wa taifa kwa ajili ya kuangalia tamasha lake ambalo lilikuwa limetangazwa sana Afrika mashariki, tamasha ambalo lilikuwa ni la kusaidia watoto waliokuwa katika maisha ya kimasikini, hasa ya mitaani.
“Hiyo inawezekana. Umetokea kupendwa mpaka mimi mwenyewe unanishtua” Kelvin alimwambia Yusufu au The Ruler kama ambavyo alikuwa akijulikana kisanii.
“Baada ya miaka miwili, nitaanzisha msikiti wangu mwenyewe. Msikitini huo utakuwa maalumu kwa ajili ya watu kuniabudu tu. Nadhani nitapata watu wengi sana” Yusufu alisema huku akionekana kutania.
“Utawafanya hata mashehe kuja kukuabudu ukianzisha huo msikiti. Jiandae kwani muda wowote utapanda jukwaani” Kelvin alimwambia Yusufu.
Siku hiyo ilionekana kuwa siku ya kitofauti na ya kuweka historia katika nchi ya Tanzania. Uwanja wa taifa ambao ulikuwa ukifanyikia tamasha hilo kubwa la kusaidia watoto waliokuwa wakiishi katika mazingira magumu ya mitaani ulikuwa umejaa kupita kawaida. Watu zaidi ya elfu sitini walikuwa wamekusanyika ndani ya uwanja huo huku kiingilio cha chini kikiwa ni shilingi elfu kumi na tano.
Watu walionekana kuchanganyikiwa kwa kumuona Yusufu, kila mtu akaonekana kuwa na ndoto moyoni mwake, ndoto ya kumuona Yusufu akisimama jukwaani na kuanza kuimba. Baada ya wasanii wengine wengine kumaliza kuimba, ikawa zamu ya Yusufu. Uwanja mzima ukaanza kulipuka kwa furaha, vitambaa vikaanza kurushwa hewani katika kipindi ambacho Yusufu alikuwa akipanda jukwaani hapo. Watu wengine wakaonekana kushindwa kuvumilia, wakaanza kutokwa na machozi.
Yusufu hakuonekana kuwa mtu wa kawaida, upendo ambao alikuwa akipendwa na mashabiki zake uliwafanya watu kuchanganyikiwa kabisa. Katika kipindi hicho, Yusufu alionekana kama msanii Michael Jackson ambaye kila alipokuwa akipanda jukwaani watu walikuwa wakilia na hata wengine kuzimia. Alipopanda jukwaani, Yusufu akaanza kunyoosha mkono juu kama ishara ya kuwasalimia.
“Piga keleleeeeeeeeeee” Yusufu alisema kwa sauti kubwa kwenye kipaza sauti.
Uwanja mzima ukapiga kelele kubwa kupita kawaida. Uwepo wa Yusufu au The Ruler katika jukwaa lile uliwafanya watu kuchanganyikiwa kupita kawaida. Wapiga picha hawakuwa mbali, walikuwa wakiendelea kupiga picha kwa kila kitu ambacho kilikuwa kikiendelea jukwaani. Damu ya baba yake ilionekana kumuongezea zaidi mafanikio katika maisha yake, katika kipindi hicho, The Ruler ndiye alikuwa msanii ambaye alikuwa akivuma kupita kawaida.
Tamasha hilo likaonekana kuwa tamasha la tofauti kuliko matamasha mengine ambayo yaliwahi kufanyika nchini Tanzania. Yusufu alijitoa kwa kuimba kwa nguvu zote kuliko siku nyingine katika matamasha mengine. Watu wakaburudika kupita kawaida, siku hiyo ikaonekana kuwa siku maalumu kwa ajili ya Yusufu ambaye alikuwa akipendwa kuliko hata raisi katika kipindi hicho. Mpaka tamasha linakwisha, watu walikuwa wameburudika vya kutosha.
“Siku ya leo imebakia kuwa historia katika maisha yangu” Jamaa mmoja alimwambia mwenzake.
“Hata mimi aisee. Makamuzi aliyoyafanya The Ruler, sijawahi kuyaona kwa msanii yeyote hapa nchini. Halafu naweza kusema ni zaidi ya wasanii wote wa Marekani ambao waliwahi kuja nchini kwa matamasha mbalimbali. The Ruler ametisha ile mbaya” Jamaa mwingine alimwambia mwenzake.
Siku hiyo ikabaki kuwa siku ya historia kwa watu wote ambao walikuwa wamehudhuria tamasha hilo. Kwa wale watu ambao walikuwa wametoka katika nchi nyingine ndani ya Afrika Mashariki hawakuoneka kujutia nauli zao pamoja gharama nyingine ambazo walikuwa wametumia mpaka kufika nchini Tanzania na kuingia katika uwanja huo kwa ajili ya kuangalia tamasha hilo. Siku hiyo, Yusufu akaonekana kuvunja rekodi, akaweka historia kwa tamasha ambalo alilifanya kuingiza watu wengi kupita kawaida, kwa wakati huo, wasanii wengine ambao walikuwa wametumbuiza katika tamasha hilo hawakuonekana kusikika kabisa midomoni mwa watu, kila mtu alikuwa akimzungumzia The Ruler tu.
“Umetisha aisee” Papaa Pipo alimwambia Yusufu katika kipindi ambacho walikuwa katika hoteli ya Serena usiku.
“Kuna wakati mwingine najiona kuwa mungu mtu. Nadhani huu ni wakati ambao watu wanatakiwa kuniabudu sasa” Yusufu alimwambia Papaa Pipo.
“Kwa hiyo inatubidi tuanzishe msikiti. Au wewe unaonaje?” Papaa Pipo alimuuliza Yusufu.
“Poa. Ila unavyoona msikiti huo ujengwe wapi hapa jijini Dar es Salaam?”
“Kama vipi tuujenge kule Tandale au Tandika, sehemu ambayo ina mkusanyiko mkubwa wa watu” Papaa Pipo alimwambia Yusufu.
“Hilo sawa. Kama vipi, ujenzi uanze hata mwaka kesho”
“Poa poa”
Siku hiyo ilikuwa ni ya kula na kunywa ndani ya hoteli hiyo. Wote wawili, maisha yao yalikuwa ni ya fedha tu, walikuwa wakimiliki kiasi kikubwa cha fedha mpaka wakati mwingine wakajiona kama watachanganyikiwa. Fedha kwao yalikuwa kama majani kwamba sehemu yoyote ile ungeweza kuyachuma. Maisha yao ya kuuza nafsi zao kwa shetani yakaonekana kuwaletea faida kubwa sana katika maisha yao. Japokuwa Yusufu alikuwa akijitahidi sana kuwa muaminifu kwa mpenzi wake, Christina lakini kuna kipindi kikatokea kuchoka, kujigonga kwa wasichana kulionekana kumpa mshawasha wa kutaka kutembea nao.
Yusufu akaanza kuvunja amri ya sita na wasichana hao, uhusiano wake na Christina ukaonekana kuwa si kitu katika maisha yake. Alitembea na wasichana ambao alikuwa akitaka kutembea nao katika kipindi hicho, na hata Christina alipokuja kugundua mambo aliyokuwa akiyafanya Yusufu, tayari Yusufu alikuwa ametembea na wasichana wasiopungua ishirini, wote alikuwa akifanya nao mapenzi kama kawaida yake.
“Kwa nini unautesa moyo wangu? Kwa nini umeamua kunitesa namna hii The Ruler?” Christina alimuuliza Yusufu huku akianza kulia.
“Wanawake ni vyombo vya starehe tu. Nimetembea na wewe kwa sababu wewe ni miongoni mwa vyombo hivyo vya starehe. Kuna ubaya hapo?” Yusufu alisema kwa dharau na kuuliza.
“Unanidharirisha Yusufu. Unanidharirisha kwa kuniita mimi ni chombo cha starehe. Leo hii umenichoka na kuamua kuzungumza maneno makali namna hiyo, yaani umesahau kila kitu ambacho tulikuwa tukifanya pamoja? Umesahau kila kitu ambacho tulikuwa tukichangia pamoja? Leo hii unaniita mimi chombo cha starehe!” Christina alisema huku akiendelea kulia.
“Wewe ulitaka niseme nini sasa? Kwanza jiangalie Christina halafu niangalie na mimi. Una hadhi ya kutembea na mimi?” Yusufu alimuuliza Christina kwa kebehi.
“Hata kama sina hadhi lakini si kuniambia maneno hayo. Haujui ni kwa jinsi gani ninaumia moyoni mwangu” Christina alimwambia Yusufu.
“Maumivu yako hayanihusu. Nadhani maumivu yako yangenihusu katika kipindi ambacho tulikuwa pamoja, ila kwa sasa hivi, hayanihusu kabisa” Yusufu alimwambia christina huku akichukua mvinyo na kisha kupiga pafu moja.
Maneno yale yalionekana kuwa kama msumali wa moto moyoni mwa Christina, alimwangalia Yusufu mara mbili mbili huku akionekana kutokuamini kile ambacho alikuwa akikisikia kutoka mdomoni mwake. Ni kweli maneno yale yalikuwa yamemuumiza sana kuliko kitu chochote kile, machozi ya uchungu ambayo yalikuwa yakimtoka, Yusufu hakuonekana kuyajali kabisa.
“Leo ninalia Yusufu huku wewe ukifurahia. Ila kumbuka, kuna siku wewe utalia na mimi kufurahia” Christina alimwambia Yusufu.
“Kama kulia, utalia milele na mimi kama kufurahia, nitafurahia milele na kuna siku utakuja kuniabudu. Upende usipende, utaniabudu tu kwani nimekwishakuwa mungu mtu katika maisha yako” Yusufu alimwambia Christina huku akiendelea kunywa mvinyo.
“Sawa mungu mtu. Ninaondoka na ninakuahidi kwamba utanitafuta tu” Christina alimwambia Yusufu.
“Nikutafute? Kwa lipi? Kipi nilichosahau kwako? Nimekwishakupiga alama nyingi sana mapajani kwako, nimeshaona kila kiungo cha mwilini mwako. Nakuhakikishia kuwa sijasahau kitu chochote kile kwako. Kwa hiyo hakuna umuhimu wa kukutafuta katika maisha yangu” Yusufu alimwambia Christina.
“Sawa. Nimekubaliana na wewe. Ila ningependa kukushauri kitu kimoja tu” Christina alimwambia Yusufu ambaye alitulia akimsikiliza na kuendelea.
“Labda unafikiri nilipenda fedha kwako au umaarufu, unaweza kuwa sahihi juu ya hilo. Ila ushauri wangu ambao ningependa kukupa, onana na daktari wako mapema ili aweze kukupa vidonge vya kuishi kwa matumaini. Mwenzako naishi kwa matumaini. Nakukaribisha mungu mtu katika ulimwengu huu wa kuishi kwa matumaini” Christina alimwambia Yusufu huku akianza kuondoka sebuleni hapo. Alipoufikia mlango, akaufungua na kisha kuondoka zake.
Yusufu akabaki kimya, maneno ambayo aliyaongea Christina mahali hapo yakaonekana kumchanganya. Yusufu akabaki akiwa amesimama tu kama nguzo, ghafla, kijasho chembamba kikaanza kumtoka, akauhisi mwili wake ukianza kutetemeka, alijihisi kama kupigwa sindano ya ganzi. Hapo hapo akajikuta akikaa kochini na kisha kuinamisha kichwa chake chini. Kwa kasi kama mtu aliyekurupushwa kutoka katika lindi la mawazo, akasimama na kisha kutoka nje ya nyumba yake na kulifuata gari lake.
“Fungua geti....fungua geti” Yusufu alimwambia mlinzi huku akiufungua mlango wa gari lake na huku akionekana kuwa mwenye haraka.
Kwa haraka haraka mlinzi akalifungua geti. Yusufu akawasha gari na kuondoka mahali hapo kwa kwa kasi. Njiani, ndani ya gari, Yusufu alionekana kuwa na mawazo kupita kawaida, tayari maneno ambayo aliongea Christina yalionekana kumchanganya kupita kawaida. Foleni za barabarani zilionekana kumkasirisha kupita kawaida, kwa wakati huo alikuwa akitaka kufika katika hospitali binafsi ya Dr Lyimo iliyokuwa Mikocheni B.
Magari yalikuwa yakitembea kwa taratibu sana, mvua ambayo ilikuwa imenyesha siku hiyo ilisababisha foleni kubwa barabarani hapo jambo ambalo lilimfanya Yusufu kushikwa na hasira. Magari yaliporuhusiwa, aliendesha kwa mwendo wa kasi mpaka alipofika Sayansi ambapo akakata kushoto na kuchukua barabara iliyokuwa ikielekea Mikocheni.
Bado Yusufu alionekana kuchanganyikiwa kupita kawaida, maneno yale ambayo alikuwa ameambiwa na Christina yakamfanya kutaka kujua hali yake ilikuwa vipi. Tayari moyoni mwake alijiona kuanza kujuta kwa uamuzi ambao alikuwa ameuchukua wa kutembea na msichana yule, Christina ambaye alionekana kuwa mrembo kwa kumwangalia, kumbe alikuwa mwanamke hatari sana ambaye alikuwa na mipango kabambe ya kumuangamiza Yusufu.
Yusufu alichukua dakika ishirini mpaka kufika katika eneo la hospitali hiyo, hospitali ambayo mara kwa mara alikuwa akitibiwa kila alipokuwa akiumwa. Huku akionekana kuchanganyikiwa, akateremka kutoka garini na kuanza kuelekea ndani ya jengo la hospitali hiyo. Siku hiyo hakuonekana kuwa katika hali nzuri, akajikuta akipita moja moja katika sehemu ya mapokezi na safari yake kuishia katika ofisi ya Dokta Lyimo ambaye alikuwa akijiandaa kuwafanyia kazi wagonjwa wengine ambao walikuwa wamekuja katika hospitali hiyo.
“Nimekuja dokta” Yusufu alimwambia Dokta Lyimo hata kabla ya salamu.
“Kuna nini tena Yusufu? Umeingia ghafla ghafla bila kugonga hodi. Kuna kitu gani?” Dokta Lyimo alimuuliza Yusufu.
“Nimekuja unipime” Yusufu alimwambia Dokta Lyimo huku akionekana kuchanganyikiwa.
“Nikupime. Nikupime nini tena? Hebu tulia kwanza Yusufu. Naona una haraka sana kiasi ambacho hatutoweza kuelewena” Dokta Lyimo alimwambia Yusufu.
“Tafadhaliiiii. Naomba unipime” Yusufu alimwambia Dokta Lyimo huku akimshika koti.
“Nikupime nini tena?”
“Nipime damu yangu. Nataka unipime Dokta nijue afya yangu kama nimeathirika au la. Nipime dokta” Yusufu alimwambia Dokta Lyimo.
Alichokifanya Dokta Lyimo ni kumwambia asubiri mahali hapo na kisha kuondoka kuelekea katika sehemu ya dawa na kuchukua sindano pamoja na vitu vingine ambavyo vilihitajika kwa mtu ambaye alikuwa akitaka kupimwa damu yake. Yusufu alibaki ndani ya ofisi ile huku akionekana kuchanganyikiwa, hakuonekana kuwa na amani hata kidogo, maneno ambayo aliyaongea Christina yalionekana kumchanganya kupita kawaida.
Mara baada ya dakika kadhaa, Dokta Lyimo akarudi ofisini hapo huku akiwa na vifaa vyote. Alichokifanya ni kumfunga Yusufu mkanda fulani karibu na mwisho wa mkono kwa kutaka kuona mishipa ya damu na kisha kumchoma sindano kwenye moja ya mishipa ya damu ambayo ilikuwa ikionekana na kisha kuchukua damu.
“Ngoja nikaiangalie” Dokta Lyimo alimwambia Yusufu na kisha kuondoka ndani ya ofisi hiyo.
Yusufu alibaki kwenye kiti huku akitetemeka kwa woga, kijasho chembamba kikaanza kumtoka huku akionekana kukosa amani kabisa. Furaha yote ya utajiri, umaarufu ikawa imeondoka moyoni mwake, kwa kipindi hicho alikuwa akifikiria kuhusiana na majibu ambayo angekuja nayo Dokta Lyimo kutoka katika chumba cha uchunguzi.
“Nikikutwa nao, nitaua mtu” Yusufu alijisemea huku akionekana kuwa na hasira.
Kwa wakati huo akaanza kujuta, kwanza akaanza kujutia hatua ambayo alikuwa ameichukua ya kumuacha mke wake, alijua kwamba Samiah alikuwa amefanya kosa kubwa la kuruhusu ujauzito lakini hakukuwa na umuhimu wa kumpa talaka kwani tayari kosa lilikuwa limekwishafanyika na hivyo ulikuwa muda wa kuganga mambo yajayo.
Yusufu alikaa katika chumba kile kwa dakika kadhaa na ndipo Dokta Lyimo kurudi katika ofisi ile. Mapigo ya moyo ya Yusufu yakaongezeka kasi katika udundaji, kijasho chembamba kilichokuwa kikimtoka kikaongezeka zaidi na zaidi. Kitendo cha kumuona daktari akiwa amerudi katika chumba kile huku akiwa na karatasi kadhaa mikononi mwake.
“Vipi?”
“Subiri kwanza Yusufu. Hautakiwi kuwa na haraka” Dokta Lyimo alimwambia Yusufu ambaye alionekana kuwa na kiu ya kutaka kujua majibu ya damu yake.
“Niambie kwanza. Majibu yako vipi?” Yusufu aliuliza.
“Kwanza tulia kitini” Dokta Lyimo alimwambia Yusufu.
Akili ya Yusufu kwa wakati huo wala haikutulia, akakaa chini huku akiwa na presha kupita kawaida, kitu ambacho alikuwa akitaka kusikia kwa wakati huo ni majibu ya damu yake tu. Alimwangalia Dokta Lyimo mara kadhaa usoni, alikuwa akiona kama anamchelewesha tu, alichokifanya ni kumnyang’anya ile karatasi ambayo iliandikwa majibu ya damu yake.
Yusufu akaanza kuiangalia karatasi ile kwa haraka haraka. Japokuwa hakuwa amesoma shule lakini alifahamu fika kwamba mtu ambaye alikuwa ameambukizwa virusi vya UKIMWI majibu yake yalisomeka POSITIVE. Akaangalia karatasi ile na maneno ambayo yaliandikwa, chini kabisa akakutana na neno ambalo alikuwa akitarajia kuliona muda huo, POSITIVE.
Yusufu akajiona kama mtu aliyepigwa na shoti ya umeme, ghafla, akasimama na kisha kuondoka ndani ya chumba kile huku akiwa kama mtu aliyechanganyikiwa zaidi na huku mkononi akiwa na karatasi ile ya majibu. Kuambukizwa ugonjwa wa UKIMWI na mtu ambaye alikuwa akimpenda na kumuamini, Christina kulionekana kumuumiza kupita kawaida. Tayari machozi yakaanza kutiririka mashavuni mwake.
Watu wote ambao walikutana nae katika hospitali ile walionekana kumshangaa, Yusufu hakuwa akieleweka kwa wakati huo, alionekana kama mtu aliyechanganyikiwa. Watu wakabaki midomo wazi, ni kweli kwamba walikuwa na hamu ya kumuona Yusufu au The Ruler kama alivyokuwa akijulikana lakini katika hali ambayo alikuwa akionekana kwa wakati huo, hakuonekana kama kuwa katika hali nzuri.
“The Ruler” Msichana mmoja alimuita lakini Yusufu huku akionekana kutokuamini lakini Yusufu hakuweza kugeuka.
Alipofika katika sehemu ambayo alikuwa ameegesha gari lake, akaufungua mlango na kuingia ndani. Hata kabla hajaliwasha, akaulalia usukuni wa gari lile na kisha kuanza kulia. Moyo wake ulikuwa kwenye maumivu makali mno, moyoni alikuwa akijilaumu kutembea na Christina ambaye alionekana kuwa mwanzo wa matatizo yale ambayo alikuwa amekutana nayo kwa wakati huo. Huku akiendelea kulia ndani ya gari lake, Dokta Lyimo akatokea mahali hapo na kuanza kukigongagonga kioo cha gari lake huku akitaka kusikilizwa.
Yusufu hakutaka kuongea kitu chochote, alijihisi kwamba kama angeongea kitu chochote kile na Dokta Lyimo ndivyo ambavyo angeshikwa na hasira zaidi na kuumia zaidi na zaidi moyoni mwake, alichokifanya ni kuwasha gari lake na kisha kuondoka mahali hapo. Njia nzima alikuwa akilia kama mtoto mdogo, kuugua ugonjwa wa UKIMWI katika umri ambao alikuwa nao kulionekana kumuumiza kupita kawaida.
Safari yake kwa wakati huo ilikuwa ni kwenda nyumbani kwa Papaa Pipo ambaye alikuwa akiishi Kijitonyama. Alitumia muda wa dakika chache kutoka hapo Mikocheni B mpaka Kijitonyama ambapo baada ya kufika katika geti la nyumba ya Papaa pipo, akaanza kupiga honi na mlinzi kufungua geti na hivyo kuliingiza gari lake. Baada ya kulipaki, Yusufu akateremka na kisha kuanza kuufuata mlango wa kuingilia katika sebule ya nyumba hiyo.
Kwa jinsi alivyokuwa amechanganyikiwa katika kipindi hicho, Yusufu hakuona kama kulikuwa na mlinzi ambaye alikuwa amemfungulia geti katika nyumba hiyo, alijiona kama kuwa peke yake. Alipoufikia mlango ule, akaufungua na kisha kuingia ndani. Papaa Pipo hakuwepo sebuleni pale kitu kilichomfanya Yusufu kuanza kuita, Papaa Pipo aliyeitikia chumbani kwake, akamwambia kwamba angekuja sebuleni pale
Papaa Pipo alipofika sebuleni, akashangaa mara baada ya kumuona Yusufu akiwa katika hali aliyokuwa nayo. Hakuonekana kuwa na furaha kama siku nyingine ambazo alikuwa akifika nyumbani hapo, siku hiyo alionekana kuwa tofauti sana na siku nyingine. Macho yake, yalikuwa mekundu sana hali ambayo ilionyesha alikuwa akilia katika kipindi kichache kilichopita.
“Kuna nini tena Yusufu?” Papaa pipo alimuuliza Yusufu.
Yusufu hakujibu chochote kile, alichokifanya ni kumpa karatasi ile Papaa Pipo. Papaa Pipo akaanza kuiangalia karatasi ile na kila kitu kilichoandikwa, alipofika chini chini mwa karatasi ile, akaonekana kushtuka. Akayatoa macho yake katika karatasi ile na kisha kumwangalia Yusufu usoni.
“Immpossible (Haiwezakani)” Papaa Pipo alimwambia Yusufu.
“Nimeathirika Papaa” Yusufu alimwambia Papaa Pipo kwa sauti ya chini yenye majonzi.
“Mungu wangu! Nani amefanya hivi?”
“Christina. Christina ameamua kuniua. Christina ameniua Papaa” Yusufu alisema huku akianza kulia tena.
Papaa Pipo akabaki kimya, kwa jinsi Yusufu alivyokuwa akiongea mahali hapo kulionekana kumuumiza kupita kawaida. Akaanza kuiangalia tena karatasi ile huku akirudia zaidi na zaidi, alijiona kama kutokuona vizuri kile ambacho kilikuwa kimeandikwa katika karatasi ile.
“Vipimo vimekosea. Umekwenda kwenye hospitali gani?” Papaa Pipo alimuuliza Yusufu.
“Nimekwenda kwa daktari ambaye kila siku amekuwa dokta wangu wa kipindi kirefu, dokta ambaye amekuwa akinitibia kila siku. Hawezi kudanganya, vipimo vyake haviwezi kusema uongo. Ningefikiri kwamba vinasema uongo endapo ningekwenda kupima bila kuambiwa kwamba nimeathirika” Yusufu alimwambia Papaa pipo.
“Kumbe uliambiwa! Nani alikwambia?”
“Christina mwenyewe”
“Huyu mwanamke ni wa kumuua kabisa. Yaani kakuambukiza ugonjwa huu halafu amekupa taarifa kwamba amekuambukiza ugonjwa huu! Huyu ni wa kumuua kabisa” Papaa Pipo alisema huku akionekana kuwa na hasira.
“Hapana. Kosa si lake” Yusufu alimwambia Papaa Pipo.
“Kosa si lake. Sasa unafikiri kosa ni la nani?” Papaa Pipo aliuliza.
“Kosa ni la wakubwa wetu wa ibadani. Wamenisaliti” Yusufu alimwambia Papaa Pipo.
“Wamekusaliti? Kivipi?”
“Haukumbuki kile ambacho waliniambia?
“Kipi?”
“Kwamba wangeilinda afya yangu”
“Nakumbuka”
“Sasa kwa nini wameruhusu hili kutokea? Kwa nini wameruhusu mimi kuupata ugonjwa huu wa UKIMWI?” Yusufu aliuliza maswali mfululizo.
“Bado sijajua”
“Haiwezekani. Ni lazima niende kule kuuliza. Wamenisalitiiii” Yusufu alisema huku akionekana kuwa na hasira”
****
Usiku wa siku hiyo, Yusufu hakutaka kulala, usiku kucha alikuwa akifikiria jinsi ambavyo majibu ya afya yake yalivyokuwa. Bado karatasi ya majibu alikuwa nayo mkononi, mara kwa mara alikuwa akiiangalia huku akiamini kwamba kuna wakati majibu yale yangeweza kubadilika na kusomeka NEGATIVE. Yusufu alikesha usiku mzima huku akiwa na ile karatasi ya majibu yale lakini hakikubadilika kitu.
Ilipofika saa saba usiku, kioo kile ambacho kilikuwa kikitumika kama mlango wake wa kuingilia katika ulimwengu wa pili kikaanza kuonekana mianga kadhaa ya radi pamoja na miungurumo ambayo alikuwa akiisikia yeye tu. Hapo hapo Yusufu akasimama na kisha kuanza kukisogelea kioo kile na kisha kuingia ndani ya kioo kile na kutokezea katika ulimwengu wa pili, ulimwengu ambao aliamua kuiuza roho yake ili apate mafanikio makubwa katika maisha yake.
Mwendo wake siku hiyo ulikuwa ni wa haraka haraka, kichwa chake kilionekana kuwa na maswali mengi ambayo alitaka kuuliza katika usiku huo. Alitembea kwa muda fulani na kisha kuifiki nyumba ile na kuingia ndani. Ndani ya nyumba ile siku hiyo ilionekana kuwa tofauti na siku nyingine, hakukuwa na mtu hata mmoja zaidi ya meza ile ambayo ilikuwa katika sehemu ambayo ilionekana kuwa kama ukumbi.
Yusufu akainamisha kichwa chini kama kutoa heshima ya kuingia ndani ya nyumba ile na kisha kuanza kuelekea katika moja ya viti ambavyo vilikuwa vimezunguka meza ile na kutulia. Wala hazikupita sekunde nyingi, mwanaume mmoja ambaye hakuwahi kumuona hata siku moja akafika mahali hapo na kuanza kumwangalia Yusufu huku akitabsamu.
Japokuwa mwanaume huyo alionekana kuwa kama binadamu wa kawaida lakini kwa mbali alikuwa na mabadiliko kiasi. Macho yake yalikuwa makubwa zaidi ya saizi ya macho ya mwanadamu wa kawaida, kichwani hakuwa na nywele, alikuwa na upara huku mdomo wake ukiwa mkubwa mara mbili ya mdomo wa kawaida.
“Nimekuja kuuliza kitu”Yusufu alimwambia mwanaume yule ambaye alikuwa amesimama wima akimwangalia Yusufu.
“Kitu gani?” Mwanaume yule aliuliza kwa sauti ya chini lakini iliyojaa utisho mkubwa ambayo kwa kiasi fulani ilimfanya hata Yusufu kusisimka.
“Kwa nini mmenisaliti?” Yusufu aliuliza huku akimwangalia mwanaume yule usoni.
“Hatujakusaliti. Bado tunaendelea kukulinda” Mwanaume yule alimwambia Yusufu.
“Hamjanisaliti! Hamjanisaliti na wakati nimekwishaambukizwa ugonjwa wa UKIMWI! Ulinzi wenu upo wapi sasa juu ya afya yangu? Kama hamjanisaliti, ninapaswa kutumia neno gani hapo?” Yusufu aliuliza. Maswali mfululizo.
“Tunaendelea kukulinda. Kamwe hautodhoofika. Utakuwa hivyo hivyo na wala hakuna mtu ambaye atajua kama umeathirika kwa kukuangalia. Utaishi maisha yako yote na hakuna atakayegudua kitu chochote kile juu ya afya yako” Mwanaume yule alimwambia Yusufu.
“Ina maana sitokonda? Ina maana sitoanza kuharisha? Ina maana sitoopatwa na vidonda?” Yusufu aliuliza.
“Hakuna kitakachokupata. Cha msingi ni kutovunja masharti yetu tu. Ukivunja basi hatuna budi kuuruhusu ugonjwa huu kufanya kazi katika mwili wako” Mwanaume yule alimwambia Yusufu.
“Nashukuru sana. Naahidi sitoweza kuvunja masharti” Yusufu alimwambia mwanaume yule na kisha kuinuka kitini na kutaka kuondoka.
“Subiri kwanza” Mwanaume yule alimwambia Yusufu na kisha kuanza kumsogelea.
“Tunawahitaji watu wengi iwezekanavyo. Utakachotakiwa kukifanya ni kufanya mapenzi na wanawake wengi iwezekanavyo. Kwa kila mwanamke ambaye utafanya nae mapenzi, hatochukua mwezi mmoja, ataanza kuziona dalili za ugonjwa huu katika mwili wake. Fanya mapenzi na wanawake wengi uwezavyo. Tutakachokifanya, tutakupa nguvu ya mvuto wa kimapenzi, hakuna mwanamke ambaye atakukataa. Hakikisha unafanya mapenzi na wanawake wengi uwezavyo” Mwanaume yule alimwambia Yusufu.
“Ila kwa nini umenihusia sana kufanya hivyo?” Yusufu aliuliza.
“Tunahitaji sadaka yako zaidi. Mvuto tuliokupa ni mkubwa sana kiasi ambacho hatujawahi kumpa mtu yeyote yule na ndio maana uliupokea ndani ya usiku mmoja tu. Kama malipo ya kila kitu, fanya nilichokwambia” Mwanaume yule alimwambia Yusufu.
“Nitafanya hivyo”
“Sawa sawa. Ila kumbuka kutovunja masharti yetu. Endapo utavunja, tutakupokonya pete zetu zinazokuingizia kila kitu” Mwanaume yule alimwambia Yusufu.
“Nitafanya kila kitu bila kuvunja masharti”
“Sawa. Unaweza kwenda” Mwanaume yule alimwambia Yusufu ambaye akaondoka mahali hapo.

Je nini kitaendelea?
 
MTUNZI: NYEMO CHILONGANI.
MAHALI: DAR ES SALAAM.
SIMU: 0718 069 269.

NITAKAPOKUFA 15

Maisha ya Yusufu yakaanza kubadilika, hapo ndipo alipoanza rasmi kutembea na wasichana mbalimbali. Kitu ambacho aliamua kukifanya kwa wakati huo ni kuchukua daftari lake dogo kwa ajili ya kuandika jina la kila msichana ambaye alikuwa akitembea nae na kumuambukiza ugonjwa wa UKIMWI ambao ulikuwa ukizidi kushika kasi nchini Tanzania.
Kwa sababu alikuwa na fedha nyingi na kwa sababu alikuwa mtu maarufu ambaye alijulikana sana Afrika Mashariki, tena zaidi ya mwanaumuziki yeyote yule, Yusufu akawapata wasichana wengi ambao walikuwa wakipenda kutembea na watu wenye fedha na maarufu. Kadri alivyokuwa akitembea na wasichana hao na ndivyo ambavyo umaarufu wake pamoja na mvuto ulivyozidi kuongezeka zaidi na zaidi.
Kila kitu ambacho kilikuwa kimepangwa katika ulimwengu wa giza ndicho ambacho kilikuwa kikitokea, kwa kila msichana ambaye alikuwa akitembea nae katika muda huo na kumwambukiza ugonjwa wa UKIMWI, ndani ya mwezi mmoja, msichana huyo alikuwa akibadilika na kuonyesha dalili zote za kuathirika na kuanzia hapo wala hakuchukua muda mrefu, anakufa kwa maumivu makali kitandani.
Yusufu hakuonekana kuhuzunika kwa kile ambacho alikuwa akikifanya, kazi yake ilikuwa ni kukamilisha kile ambacho alikuwa ameambiwa kukifanya katika ulimwengu ule. Mwili wake haukupungua wala kuonyeha dalili za kuwa na ugonjwa ule, kila siku mwili wake ulikuwa ukinawiri kupita kawaida jambo ambalo ilikuwa ni ngumu sana kugundua kama alikuwa na ugonjwa wa UKIMWI.
Wanawake walizidi kujigonga kwake, na kama kawaida yake, alikuwa akitembea nao kama kawaida yake. Yusufu alijua kwamba kuna siku maisha yake yangekatishwa na ugonjwa ule japokuwa alijua kwamba alikuwa akilindwa na watu wale, hata kabla hajafa, alitaka kuondoka na wengi, hasa wale wasichana ambao walikuwa wakiwashobokea watu waliokuwa na umaarufu pamoja na fedha nyingi.
Kulala na wanawake hakukuisha, kila siku alikuwa akilala nao hata zaidi ya watatu na kisha kuachana nao. Hakutaka kurudia kulala na wanawake mara mbili, mara moja ilikuwa inatosha kabisa. Wasichana wengi warembo ndani ya jiji la Dar es Salaam wakaanza kufa kwa ugonjwa wa UKIMWI, mdudu mbaya wa ugonjwa huo akaonekana kulivamia jiji la Dar es Salaam.
“Unamuona yule mrembo wa Kinondoni?” Yusufu alimuuliza Kelvin.
“Mzuri sana. Nilibahatika kuongea nae jana pale Blue Pearl. Alisema angefurahi sana kama angeweza japo kuongea nawe” Kelvin alimwambia Yusufu.
“Alikupa namba yake ya simu?”
“Yeah! Alisema nikupe kama ungependa kuongea nae” Kelvin alimwambia Yusufu.
“Anaitwa nani?”
“Veronica”
“Poa. Nipe tu. Unajua wananifagilia sana hawa wanawake. Ngoja niwape wanachokihitaji” Yusufu alisema huku akiichukua namba ya simu ya Veronica.
Yusufu hakutaka kuchelewa, alichokifanya mahali hapo ni kumpigia simu Veronica na kisha kupanga mikakati ya kuonana nae. Kwa wakati huo, wanawake wengi ndani ya jiji la Dar es Salaam walikuwa wakivutiwa na Yusufu, kama ilitokea siku Yusufu akampigia simu msichana na kuomba kuonana nae, msichana huyo alijiona kuwa miongoni mwa wasichana wenye bahati sana nchini Tanzania.
Hakukuwa na msichana ambaye alikuwa akifahamu kile ambacho Yusufu alikuwa akikifanya kwa wakati huo, hakukuwa na msichana ambaye alikuwa akifahamu kwamba Yusufu alikuwa ameathirika na hivyo alikuwa akifanya hivyo kama njia mojawapo ya kuwaambukiza ugonjwa huo na kuwaua baada ya mwezi mmoja. Wasichana walijiona kuwa na bahati ya kutembea na Yusufu, kwao, kutembea na mtu maarufu ilionekana kuwa sifa kubwa katika maisha yao.
Mara baada ya kupanga sehemu ya kuonana, Yusufu na Veronica wakaonana katika hoteli ya La Vista Inn Magomeni. Muda mwingi Veronica alikuwa haamini kama kweli kipindi hicho alikuwa akiongea na Yusufu au The Ruler kama ambavyo alikuwa akijulikana na watu wengi nchini Tanzania.
“Una ndoto gani Vero?” Yusufu alimuuliza Veronica.
“Nataka kuwa mrembo wa Tanzania” Veronica alijibu huku kwa mbali akionekana kujisikia aibu.
“Safi sana. Kwa hiyo ndoto yako imeishia hapo?” Yusufu alimuuliza.
“Hapana. Nataka pia kuwa mrembo wa Dunia au hata Afrika kama alivyokuwa Nancy Sumari” Veronica alijibu.
“Safi sana. Napenda kuwa na urafiki na msichana ambaye anakuwa na ndoto za mafanikio” Yusufu alimwambia Veronica.
Bado walikuwa wakiendelea kupiga stori za hapa na pale huku muda ukizidi kusonga mbele. Katika kipindi chote hicho, Veronica bado alikuwa akijihisi kuwa na bahati sana. Waliongea mengi siku hiyo huku wakila na kunywa. Yusufu hakutaka kuchelewa, alichokifanya mahali hapo, akakisogeza kiti chake karibu na kiti alichokalia Veronica na kisha kuanza kumshikashika mapaja.
Veronica hakuonekana kushtuka, kile ambacho kilikuwa kimetokea mahali hapo alikuwa amekwishakifahamu toka pale alipokuja mahali hapo, kwa hiyo alichokifanya ni kuonyesha ushirikiano. Waliendelea na mchezo ule mahali pale kwa muda mrefu mpaka ilipofika saa saba usiku kuamua kuchukua chumba ndani ya hoteli hiyo.
“Hii ni ndoto ya kwanza ambayo nilikuwa nayo” Veronica alimwambia Yusufu huku akiwa amemruhusu Yusufu kumvua nguo alizokuwa nazo.
“Ndoto gani?”
“Kufanya mapenzi na wewe” Veronica alimwambia Yusufu.
“Nakukamilishia ndoto yako ya kwanza maishani mwako” Yusufu alimwambia Veronica na kisha kuanza kufanya mapenzi.
Hiyo ndio ilikuwa siku ambayo Veronica alizifuta ndoto zake zote ambazo alikuwa nazo katika maisha yake. Kwa kuamini kwamba alikuwa akikamilisha moja ya ndoto yake katika maisha yake, alikuwa akipoteza zile ndoto nyingine ambazo alikuwa amezipanga kukamilisha katika maisha yake.
Usiku huo ulikuwa ni usiku wenye furaha kwa Veronica lakini ni usiku ambao ulikuwa ukisababisha kilio kikubwa katika maisha yake. Hakujua ni kwa namna gani Yusufu alikuwa akitamani sana kumuambukiza ugonjwa ule kwa kuamini kwamba kutokana na urembo wake basi ilikuwa ni lazima hata wanaume wengine ambao walikuwa na tamaa ya kuwa na wanawake warembo wateketee kwa ugonjwa huo.
****
Maisha yalikuwa yakiendelea kama kawaida, Yusufu hakuacha kutembea na wasichana warembo, kila siku alikuwa na kazi kubwa ya kubadilisha wasichana kama ambavyo alikuwa akibadilisha mavazi katika mwili wake. Yusufu hakuishia ndani ya jiji la Dar es Salaam tu, alikuwa akisafiri mpaka mikoani huku akiendelea na kazi yake kama kawaida.
Yusufu alipoona kwamba kwa Tanzania alikuwa ametembea na wasichana si chini ya mia moja na hamsini ndani ya miezi nane, hapo ndipo alipoamua kusafiri na kwenda Kenya na Uganda pamoja na nchi nyingine za Afrika Mashariki. Yusufu alipokelewa kwa mikono miwili bila kujua kwamba alikuwa amekuja na kitu kingine, ugonjwa ambao ungewafanya watu wengi sana kufa katika maisha yao ya mbeleni.
Huko napo kazi ilikuwa ile ile. Hakukuwa na msichana ambaye alikuwa na ubavu wa kumkatalia Yusufu. Alitembea na wasichana wengi warembo, alitembea na wasichana ambao wazazi wao walikuwa na fedha nyingi na za kutosha, kitu ambacho walikuwa wakikitaka katika maisha yao ni kutembea na mtu maarufu tu.
“Unarudi lini Tanzania?” Papaa Pipo alimuuliza Yusufu simuni katika kipindi ambacho alikuwa nchini Uganda
“Bado kabisa. Ndio kwanza nimetembea na wasichana ishirini hapa Uganda na Kenya nilipotoka wiki iliyopita” Yusufu alimjibu Papaa Pipo.
“Rudi Tanzania kwanza”
“Kuna nini tena?”
“Mambo yameharibika huku” Papaa Pipo alimwambia Yusufu maneno ambayo yalionekana kumshtua.
“Kivipi tena?”
“Tetesi zinaenea kwamba unasambaza ugonjwa wa UKIMWI. Magazeti ya udaku yanaandika sana habari yako kuhusu jambo hilo” Papaa Pipo alimwambia Yusufu.
“Nakuja. Nakuja leo hii. Nitapanda ndege jioni kuja huko. Jambo hili ni lazima limalizwe haraka iwezekanavyo” Yusufu alimwambia Papaa Pipo na kisha kukata simu.
Yusufu akaonekana kama mtu aliyechanganyikiwa kwa wakati huo. Alichokifanya ni kwenda katika ofisi za shirika la ndege la Uganda Airways na kisha kukata tiketi ya safari ya kuondoka nchini hapo siku hiyo. Tetesi zile zilionekana kumshtua kupita kawaida, tayari akaona kwamba kulikuwa na watu ambao walikuwa wamevumisha suala lile. Katika kipindi hicho, majina ya watu wawili ndio ambayo yalikuwa yamemjia kichwani.
Mtu wa kwanza kabisa kumfikiria katika kipindi hicho alikuwa msichana Christina ambaye alikuwa amemuambukiza ugonjwa huo kwa makusudi na wakati alijua fika kwamba alikuwa ameathirika. Mtu wa pili kumfikiria alikuwa Dokta Lyimo ambaye alikuwa amempima miezi kadhaa iliyopita. Hao ndio watu ambao walionekana kueneza habari ile, alichokiona kufaa kukifanya kwa wakati huo, ni kuwatafuta watu hao tu.
Saa nane mchana Yusufu alikuwa ndani ya ndege akirudi nchini Tanzania huku akionekana kuwa na mawazo kupita kawaida. Ndege ile ilichukua masaa mawili ikaanza kukanyaga katika ardhi ya Tanzania. Yusufu akateremka na kisha kuanza kuelekea katika sehemu ya kuchukua mizigo na kuchukua begi lake ambalo lilikuwa miongoni mwa mabegi ya wasafiri ambayo yalikuwa yakichunguzwa.
Yusufu akaanza kupiga hatua kuelekea nje ya jengo la uwanja ule, kila mtu ambaye alikuwa akimuona kwa wakati huo alikuwa akimpiga picha huku wengine wakimuita kwa lengo la kutaka kupiga nae picha. Alipotoka nje ya jengo lile, macho yake yakatua usoni mwa Papaa Pipo ambaye alimtaka kuingia ndani ya gari lake.
“Mambo yameharibika. Hebu soma haya magazeti” Papaa Pipo alimwambia Yusufu huku akimpa magazeti ya udaku ambayo yalikuwa yameandika mengi kuhusiana na habari zake.
‘YUSUFU AWAMALIZA WANAWAKE KWA GONJWA LA AJABU, KILA MWANAMKE ANAYETEMBEA NAE NI LAZIMA AONJE MAUTI, WANAWAKE WANAOTEMBEA NA YUSUFU WAZIDI KUTEKETEA’ Hivyo vilikuwa vichwa mbalimbali vya habari ambavyo vilikuwa vikionekana katika magazeti matatu ya udaku ambayo alikuwa ameyashika Yusufu.
Aliuhisi mwili wake ukitetemeka, kijasho chembamba kikaanza kumtoka, hasira zikaanza kumpanda kwa kuona kwamba watu walewale ambao walikuwa wakifahamu kwamba alikuwa amehusika ndio watu ambao walikuwa wameeneza habari ile ambayo ilionekana kuaminika kwa baadhi ya watu.
“Nitawaua wote” Yusufu alimwambia Papaa Pipo.
“Wakina nani?” Papaa Pipo alimuuliza.
“Wanaoeneza haya”
“Unawajua?”
“Hapana. Ila nawahisi”
“Wakina nani?”
“Yule Dokta Lyimo na yule malaya, Christina” Yusufu alijibu.
“Hata mimi nilihisi hivyo hivyo. Acha tuwafunge midomo milele” Papaa Pipo alimwambia Yusufu.

Je nini kitaendelea?
Je watafanikiwa kuwauawa Dokta Lyimo na Christina?
Hadithi bado mbichi sana.
 
MTUNZI: NYEMO CHILONGANI.
MAHALI: DAR ES SALAAM.
SIMU: 0718 069 269.

NITAKAPOKUFA 16

Mipango ya kufanya mauaji kwa Dokta Lyimo pamoja na msichana Christina ikaanza kufanyika huku Papaa Pipo ndiye ambaye alikuwa akishughulika na mipango yote. Alichokifanya Papaa Pipo ni kuwaita vijana watatu ambao aliona kwamba hao wangeweza kuifanya kazi ile kwa malipo ya kiasi cha shilingi milioni kumi ambazo zilitolewa na Yusufu.
Kila kitu kwa wakati huo kilitakiwa kuwa siri, haikutakiwa kujulikana kwa mtu yeyote kwamba Yusufu ndiye ambaye alikuwa amepanga mipango hiyo. Papaa Pipo akaanza kuongea na vijana wale ambao alitaka kazi hiyo ifanyike kwa haraka sana. Kitu alichowapa Papaa Pipo ni nusu ya malipo na kisha kuwaahidi kumalizia malipo katika kipindi ambacho wangemaliza kazi ile.
Papaa Pipo akawapa maelekezo juu ya mahali ambapo dokta yule alikuwa akipatikana kwa urahisi, katika hospitali yake ambayo ilikuwa ikipatikana Mikocheni B pamoja na msichana Christina ambaye alikuwa akipatikana Sinza Vatican City nyumba namba 689.
Siku iliyofuata, vijana wale, Puma, Mchina na Os D walikuwa wamelipaki gari lao mbali na eneo la hospitali ya Dokta Lyimo maeneo ya Mikocheni B huku wakisubiri muda wa kufunga hospitali hiyo ufike na hivyo kukamilisha kile ambacho walikuwa wamepanga kukifanya katika wakati huo.
“Kama bosi alivyosema. Akitoka tu, ni kumfuata ndani ya gari lake na kisha kumuua” Puma aliwaambia wenzake.
“Kwa hiyo tumuue vipi sasa? Kwa bunduki au visu?” Os D aliuliza.
“Kwa visu. Kama tukimuua kwa kumfyatulia risasi, milio ya risasi itaweza kusikika na hivyo kuwa hatari kwetu” Puma aliwaambia.
“Hapo nimekuelewa mkuu. Ngoja tusubirie” Os D alimwambia Puma.
Puma na wenzake waliendelea kusubiri mahali pale huku kila mmoja akiwa na hamu ya kumuona Dokta Lyimo akitoka ndani ya hospitali ile na kisha kufanya kile ambacho walikuwa wamedhamiria kukifanya mahali pale, kumuua na kisha kumfuata msichana Christina na kumuua pia. Waliendelea kukaa sehemu ile ndani ya gari lao kwa takribani masaa manne na ndipo kwa mbali wakamuona Dokta Lyimo akitoka ndani ya hospitali ile huku ikiwa imetimia saa tatu kasoro usiku.
Kwa haraka haraka bila kupoteza muda, Puma na Mchina wakateremka katika gari lao na kisha kuanza kupiga hatua za haraka haraka kumfuata Dokta Lyimo ambaye alikuwa akilifuata gari lake. Mara baada ya kufungua mlango wa gari lake, Puma akamshika na kisha kumsukumia ndani ya gari lile. Kutokana na kutokuwa na watu ndani ya eneo lile, hakukuwa na mtu yeyote ambaye alikuwa ameliona tukio lile.
Mchina akaingia ndani ya gari kwa kupitia mlango mwingine na kisha Puma kumbana Dokta Lyimo huku akiuziba mdomo wake asiweze kupiga kelele zozote zile. Mpaka katika kipindi hicho, Dokta Lyimo alikuwa akishangaa tu, hakuelewa ni kitu gani kilikuwa kikiendelea mahali hapo.
“Tulia” Puma alimwambia Dokta Lyimo ambaye akakaa kimya.
Hawakuwa hapo kwa ajili ya kupoteza muda kwa kuhojiana maswali, hawakuwa hapo kwa ajili ya kuuliza ni kitu gani ambacho kiliwapelekea waandishi wa habari kujua kile ambacho kilikuwa kimeendelea katika mwili wa Yusufu, na wala hawakuwa hapo kwa ajili ya kuhoji kitu chochote kile, kitu ambacho kilikuwa kimewafanya kuwa mahali hapo ni kukamilisha kile ambacho kilikuwa kimewaleta mahali hapo, kumuua Dokta Lyimo tu.
Puma hakutaka kuchelewa, kitendo cha kukaa hapo na kuanza kuhoji maswali kilionekana kama kingempotezea muda, alichokifanya ni kukichukua kisu chake ambacho kilikuwa kiunoni na kisha kumchoma Dokta Lyimo mara tatu tumboni mwake huku Mchina akiwa amemfumba mdomo kwa kiganja chake kipana. Hakukusikika kelele kutoka kwa Dokta Lyimo, kila alipokuwa akijaribu kulia kwa maumivu, sauti yake haikutoka kabisa mpaka pale ambapo akafa katika maumivu makali na kisha Puma na Mchina kuteremka kutoka ndani ya gari lile na kulifuata gari lao na kuondoka mahali hapo.
Kila kitu ambacho walikuwa wamekipanga walikuwa wakitaka kifanyike usiku huo huo tena kwa haraka sana. Kwa wakati huo walikuwa na safari ya kuelekea Sinza huku lengo lao kubwa likiwa ni kutaka kumuua Christina na kisha kumpelekea taarifa Papaa Pipo ambaye alikuwa amewatuma kufanya kazi ile. Os D alikuwa akiendesha gari kwa kasi huku lengo lao likiwa ni kutaka kufika Vatican City Sinza haraka iwezekanavyo hata kabla usiku haujawa mkubwa.
Njia ambayo walikuwa wamepita ilikuwa ni ile ya Sayansi kuelekea Mtogole ambapo baada ya kufika katika njia iendayo shule ya Sekondari ya Salma Kikwete, Os D akakata kona na kuichukua barabara ile ambayo wakaenda nayo mpaka Sinza Darajani ambapo wakakata kulia na kuanza kukipandisha kilima kidogo katika barabara hiyo mpaka pale ambapo walifika Sinza, Vatican City na kukata kulia na kisha kuchukua barabara ya vumbi ambayo ikawapeleka mpaka katika nyumba ambayo ilikuwa imezungushiwa ukuta.
Alichokifanya Puma ni kuteremka na kisha kulifuata geti la nyumba ile na kisha kuanza kuligonga. Wala haukupita muda mrefu, mfanyakazi wa ndani wa nyumba ile akafika mahali pale na kisha kulifungua geti lile na macho yake kutua usoni mwa Puma ambaye kwa kumwangalia tu, alijifanya kuwa mtu mwema ambaye wala hakuwa na tatizo lolote lile.
“Samahani. Sijui nimekuta mzee Tobias?” Puma aliuliza kwa sauti ya upole iliyokuwa na unyenyekevu ambayo ilimfanya mfanyakazi yule wa ndani kumuona mtu mwema.
“Ndio”
“Sawa. Naweza kumuona?”
“Hakuna tatizo. Karibu ndani” Msichana yule alimkaribisha Puma bila kuuliza swali lolote lile jambo lililoonekana kuwa kosa kubwa.
Hapo hapo Puma akaanza kupiga hatua kumfuata mfanyakazi yule. Os D na Mchina hawakutaka kubaki garini, walichokifanya ni kuteremka na kisha kuanza kumfuata msichana yule pamoja na Puma. Msichana yule alipogeuka nyumba kumwangalia Puma, akashtuka kuona mdomo wa bunduki ukiwa umemuelekezea usoni. Hapo hapo akatakiwa kuufungua mlango bila kupiga kelele zozote zile.
“Fungua mlango kimya kimya. Ukipiga kelele tu, naumwaga ubongo wako” Puma alimwambia msichana yule kwa sauti nzito isiyokuwa na utani.
Msichana yule akafungua mlango na wote kuingia. Mzee Tobias na mkewe walikuwa sebuleni wakiangalia televisheni, wakaonekana kuwa na mshtuko mkubwa mara baada ya kuona msichana wa kazi akiingia pamoja na watu ambao walikuwa na bunduki mikononi mwao. Wote wakaamriwa kubaki kimya, kwa wakati huo walitakiwa kufanya kila kitu ambacho vijana wale walitaka kifanyike.
“Laleni chini na mikono ikiwa kichwani” Puma aliwaambia na hivyo kutii.
“Christina yupo wapi?” Puma aliuliza kwa sauti ya ukali.
“Yupo chumbani kwake” Bi Stella, mama yake Christina alijibu huku akionekana kuwa na hofu.
“Chumba kipi?”
“Chumba cha nne upande wa kulia” Bi Stella alijibu.
Puma hakutaka kuendelea kubaki mahali hapo, alichokifanya ni kuelekea katika ukumbi wa nyumba ile na kuanza kuhesabu vyumba vilivyopo na alipofikia kile chumba ambacho aliambiwa kwamba ni chumba cha Christina, akakishika kitasa cha mlango ule na kuufungua.
Christina alikuwa amelala kitandani, afya yake haikuonekana kuwa nzuri kabisa, mwili wake ulikuwa umekonda sana hali ambayo ilionyesha kwamba alikuwa katika uuguzi wa ugonjwa wa UKIMWi ambao ulikuwa umekwishaanza kuonyesha dalili katika mwili wake. Mwili wake haukuwa na nguvu, kila wakati alikuwa mtu wa kukohoa tu, kilio, kwake ndicho kilikuwa kitu ambacho kimetawala maisha yake katika kipindi hicho.
Alikuwa kitandani katika mateso makali, kitu ambacho alikuwa akikisubiria kwa wakati huo ni kufa tu. Maisha yalikuwa yameonekana kwenda kwa kasi sana, wazazi wake walikuwa wamefanya kila kilichowezekana kuhakikisha kwamba wanamsaidia mtoto wao lakini hali haikuonekana kubadilika kabisa, bado Christina alikuwa akiumwa vilevile.
Mara baada ya Puma kuingia ndani ya chumba kile, akasimama huku akimwangalia Christina ambaye alikuwa hoi kitandani. Christina alionekana dhahiri kusubiri kifo mahali pale. Badala ya kutekeleza kile ambacho alikuwa ametumwa, Puma akasimama kwa muda huku akimwangalia Christina ambaye alikuwa hoi kitandani pale. Mvutano mkubwa ulikuwepo moyoni mwake katika kipindi hicho, upande mmoja wa moyo wake ulikuwa ukimwambia kukamilisha kile ambacho kilikuwa kimempeleka mahali pale lakini upande wake mwingine wa moyo wake ulikuwa ukimkataza kumuua.
Puma alimwangalia Christina kwa muda fulani na kisha kuondoka ndani ya chumba kile huku akiwa hajafanya kitu chochote. Hali ambayo alikuwa nayo Christina ilionekana kumhuzunisha kupita kawaida, alijua fika kwamba hata kama asingemuua katika kipindi kile basi ilikuwa ni lazima ugonjwa ule umuue kitandani pale, tena ndani ya siku chache zijazo.
“Vipi? Fresh?” Mchina alimuuliza Puma.
“Tuondokeni” Puma aliwaambia.
Hawakutaka kubaki ndani ya nyumba ile, walichokifanya ni kutoka nje huku wakiwaambia kwamba hawakutakiwa kusimama kwani walikuwa wanataka kukaa dirishani kuongea na hivyo kwa yeyeote ambaye angesimama au kupiga kelele zozote basi wangeweza kumfyatulia risasi. Moja kwa moja wakalifuata geti na kisha kulifungua na kuingia garini huku Puma akionekana kuwa na mawazo lukuki.
“Vipi! Umeua kama tulivyoagizwa?” Os D aliuliza.
“Washikaji nyie acheni tu” Puma aliwaambia.
“Tuache nini?”
“Ugonjwa wa UKIMWI noma. Ugonjwa huu unatisha zaidi ya unavyojua wewe” Puma aliwaambia.
“Hatukuelewi una maana gani kutuambia hivyo. Umemuua?” Mchina alimuuliza Puma.
“Hapana” Puma alijibu hali iliyomfanya Os D kusimamisha gari kwa ghafla.
“Haujamuua?”
“Ndio”
“Kwa nini sasa?”
“Mtu mwenye anaumwa ngoma aisee. Yaani yupo hoi kabisa. Sikuona haja ya kumuua kwani alivyoonekana siku yoyote kuanzia sasa atakufa. Ila pamoja na hayo, ugonjwa wa UKIMWI noma sana. Usikiieni tu kwenye kwenye redio na usiombee kumuona mtu anayeumwa ugonjwa huo mbele ya macho yako. Hali inatisha” Puma aliwaambia.
Kila mmoja alibaki akimshangaa Puma, hawakuamini kama Puma yule ambaye walikuwa wakimfahamu leo hii alikuwa na huruma juu ya mgonjwa ambaye alikuwa hoi kitandani, kwao, siku hiyo Puma alionekana kubadilika kupita kawaida. Roho yake ya ukatili ikaonekana kupotea katika kipindi ambacho alikuwa amemuona Christina alivyokuwa akiteseka kitandani. Huruma ambayo alikuwa ameionyesha siku hiyo ilikuwa kubwa sana kiasi ambacho mpaka yeye mwenyewe ikaonekana kumshangaza.
“Ila kwa nini bosi ametuagiza tumuue huyu msichana?” Puma aliwauliza wezake huku Os D akiwahsa gari.
“Hatujui. Yeye alichoagiza ni kumuua tu” Mchina alimjibu Puma.
“Nahisi kuna kitu hapa. Halafu nimekumbuka. Yule demu sio mgeni kabisa machoni mwangu. Nahisi nilikwishawahi kumuona sehemu fulani” Puma aliwaambia wenzake huku akionekana kama kutaka kukumbuka kitu.
“Uliwahi kumuona wapi?”
“Kwenye magazeti. Hebu subiri nikumbuke” Puma aliwaambia huku akiyainua macho yake juu.
“Kwa hiyo ni supastaa?”
“Yeah! Nimemkumbuka sasa”
“Ni nani?”
“Alikuwa demu wa The Ruler”
“Acha utani bwana! Sasa kwa nini Papaa anataka kumuua?”
“Mmmh! Sijui. Ila Papaa Pipo si rafiki wa The Ruler?”
“Ndio”
“Halafu si kuna tetesi zinasema kwamba The Ruler kababuka?”
“Ndio”
“Mmekwishapata picha hapo?” Puma aliuliza.
“Picha gani?”
“Kwamba huyu demu atakuwa kamuambukiza The Ruler gonjwa hili na ndio maana anataka kumuua” Puma aliwaambia.
“Sasa mbona Papaa Pipo ndio katutuma?”
“Inawezekana hataki kujulikana”
“Na vipi kuhusu yule daktari”
“Inawezekana kwamba nae anajua kwamba jamaa ameathirika. Ila tuachane na hayo yote. Yule demu siku yoyote ile anakufa kwa hiyo cha msingi tumwambiaeni Papaa kwamba tumemuua. Mmesikia?” Puma aliwaambia.
“Haitokuwa msala?” Mchina aliuliza.
“Msala gani? Kwani atakuja kuhakikisha? Hakuna kitu kama hicho, ataamini kila tutakachomwambia” Puma aliwaambia.
Safari bado ilikuwa inaendelea mpaka pale ambapo walifika katika nyumba ya Papaa Pipo ambapo wakaingia ndani na kisha kumsubiria bosi wao ambaye alikuwa chumbani. Baada ya dakika tano, Papaa Pipo akatoka chumbani na kisha kuelekea pale sebuleni. Akapokelewa na tabasamu zito kutoka kwa vijana wale hali iliyoonyesha kwamba kila kitu kilikwenda salama kama kilivyotakiwa.
“Kwa hiyo kila kitu poa?” Papaa Pipo aliwauliza.
“Kama kawa huwa haturembi kwenye kazi zetu. Tumekamilisha basi hata wewe pia utatakiwa kutukamilishia mzigo wetu uliobakia” Puma alimwambia.
Papaa Pipo akasimama na kisha kuanza kuelekea katika chumba chake ambako huko alikaa kwa dakika kama kumi na pia kurudi sebuleni pale huku akiwa na bahasha kubwa ya kaki na kisha kuwakabidhi. Papaa Pipo aliwaamini vijana wake kwamba walikuwa wamekamilisha kile ambacho alikuwa amewaagiza kukifanya katika kipindi kile, kuwaua watu wote ambao alitaka wauawe. Mara baada ya kukabidhiwa fedha zao zilizobakia, wakaondoka mahali hapo huku kila kitu kikionekana kukamilishwa moyoni mwa Papaa Pipo.

je nini kitaendelea?
 
MTUNZI: NYEMO CHILONGANI.
MAHALI: DAR ES SALAAM.
SIMU: 0718 069 269.

NITAKAPOKUFA 17

Msichana Pamela ndiye ambaye alikuwa akitamba kwa uzuri katika kipindi hicho kiasi ambacho wanamuziki mbalimbali walikuwa wakimtaka kwa ajili ya kuonekana katika video zao mbalimbali ili video hizo ziweze kuangaliwa sana na watu kutokana na uwepo wa msichana huyo ambaye alionekana kuwa mrembo kupita kawaida. Pamela alikuwa akivuma sana katika kipindi hicho, kuvuma huko kulianzia katika kipindi ambacho alikuwa amechaguliwa kushiriki urembo wa Vyuo ngazi ya taifa.
Kila mtu ambaye alikuwa akimwangalia Pamela alikuwa akimtamani msichana huyo ambaye alikuwa ameumbika vizuri kupita kawaida jambo ambalo liliwafanya watu kuona kwamba Mungu alikuwa ametoa nafasi ya upendeleo kwake au katika kipindi ambacho alikuwa akimuumba, alikuwa katika utulivu mkubwa. Pamela alikuwa ameumbika vizuri sana, umbo lake lilikuwa la kimisi, hipsi zake zilikuwa zimetokeza japo si sana, sura yake ilikuwa ya kitoto huku mashavu yake yalikuwa yakipendezeshwa na vishimo viwili ambavyo vilikuwa vikionekana kila alipokuwa akicheka au kutabasamu.
Ngozi yake ilikuwa laini sana, kwa mbali alionekana kuwa na mchanganyiko wa rangi. Kifuani kulionekana kuridhisha kabisa, hakuwa na haja ya kuvaa sidiria, alikuwa akipendelea kutovaa chochote kile kwa ndani hasa maeneo ya kifuani jambo ambalo lilikuwa likimvutia kila mwanaume lijari ambaye alikuwa akimwangalia. Mvuto wa Pamela katika kipindi hicho ulikuwa mkubwa sana, hakukuwa na msichana maarufu ambaye alikuwa akivutia kama jinsi ambavyo alikuwa akivutia kwa kipindi hicho.
Mwendo wake ulikuwa ni wa kimisi hasa, alikuwa akipendelea kutembea kwa mwendo wa madaha hata kama alikuwa akitakiwa kuwahi sehemu ambayo alikuwa akihitajika. Si wanamuziki wote ambao walikuwa wakikubaliwa na Pamela kuonekana katika video zao za muziki, ni wanamuziki wachache sana ndio ambao walikuwa wakipata nafasi hiyo adimu, nafasi ambayo walikuwa wakiitumia vilivyo. Wanaume wengi ambao nao walikuwa wakionekana katika video mbalimbali za muziki ambazo Pamela alikuwa akionekana ndio ambao walikuwa wakiharibu zaidi hasa pale ambapo walikuwa wakimtongoza Pamela kiasi ambacho kilimfanya kuwalalamikia sana wanamuziki ambao walikuwa wamemuhitaji katika kipindi hicho.
“Nimekuja kufanya kazi na si kutafuta bwana. Umenielewa?” Pamela alimwambia mwanamuziki, Shabby ambaye alikuwa na umaarufu kidogo ndani ya nchi ya Tanzania.
“Nafahamu. Ila nadhani hii ni nafasi yangu ya kukwambia kile ambacho nilikuwa nikitamani sana kukwambia toka zamani” Shabby alimwambia Pamela ambaye alionekana kuanza kukasirika.
“Sikiliza Shabby, ulitaka nionekane kwenye video yako ili itazamwe sana na watu, si ndio hivyo?” Pamela alimwambia Shabby na kumuuliza.
“Ndio”
“Na nimefanya kile ulichokitaka, si ndio?”
“Ndio”
“Basi sawa. Nimalizie fedha zangu nisepe manake ushaanza kunikera” Pamela alimwambia Shabby.
“Ila si ninaomba unisikilize kidogo Pamela”
“Hata kama nikikusikiliza Shabby, una lipi jipya la kuongea ambalo utanifanya nikukubalie. Nisikilize kwa makini na unielewe. Kama kutongozwa nimekwishatongozwa sana, nimesikia maneno mengi sana mazuri na matamu ya mapenzi na nidhani mengine ni matamu hata zaidi ya hayo ambayo utataka kuniambia. Watu wamelia sana mbele ya macho yangu lakini hakukuwa na mtu ambaye nimemkubalia. Ninajiheshimu sana, mambo mengine usitake mpaka tukayaongee kwa waandishi wa habari na kuanza kuchafuana. Nipe changu nisepe” Pamela alimwambia Shabby huku akionekana kuzidi kukasirika.
Maneno yale ambayo aliongea Pamela yakaonekana kumchoma sana Shabby, akabaki kimya kwa muda huku akimwangalia pamela. Hakuamini kama msichana ambaye kila siku alikuwa akimtamani leo hiyo alikuwa mbele ya macho yake huku akiwa anataka kumtongoza na kuambiwa maneno ambayo yalimfanya kutokuzungumza kile ambacho alikuwa akitaka kumwambia. Kadri ambavyo alivyokuwa akimwangalia Pamela ndivyo ambavyo alizidi kumtamani zaidi na zaidi.
“Kama hautaki kunipa mkono kwa mkono basi utanitumia kwenye akaunti yangu ya simu. Kupitia namba zangu hizo hizo ulizonitafutia” Pamela alimwambia Shabby na kisha kuanza kuondoka mahali hapo.
Shabby hakutaka kukaa na deni, alichokifanya ni kuanza kupiga hatua kumfuata Pamela na kisha kumuomba radhi kwa kile kilichotokea na kisha kumpatia fedha zake alizokuwa akizihitaji kama malipo ya kazi ya kuonekana katika video yake kama ambavyo walivyokubaliana kabla. Huku akionyesha dharau, Pamela akazichukua zile fedha na kuondoka mahali hapo.
Hayo ndio yalikuwa maisha yake. Katika kipindi cha mwaka mzima, hakukuwa na msanii ambaye alifanikiwa kutembea na Pamela. Msichana huyo alionekana kuwa mgumu hasa, wanamuziki wengi pamoja na waigizaji walikuwa wamekwishajaribu bahati zao lakini hakukuwa na mtu ambaye alifanikiwa kumtia katika mikono yake.
Wazee waliokuwa na fedha zao hawakubaki nyuma, nao wakaanza kumvizia Pamela kwa fedha walizokuwa nazo lakini bado msichana huyo alionekana kuwa mgumu sana kupatikana. Pamela hakuonekana kuzishobokea fedha, kwake, kiasi kile ambacho alikuwa akikipata kilikuwa kikubwa na kilionekana kumtosha kwa matumizi yake ya kila siku.
Siku zikaendelea kukatika, kadri ambavyo alivyokuwa akionekana sana kwenye video na ndivyo ambavyo alizidi kujipatia umaarufu zaidi na zaidi mpaka kuzidi kusikika zaidi nchini tanzania na hata nje ya nchi ya Tanzania. Wasanii waliendelea kumiminika kufanya nae kazi, mapedeshee nao waliendelea kumtunza fedha lakini Pamela hakuwa radhi kuvua nguo yake ya ndani na kuyapanua mapaja yake, alikuwa akiendelea na msimamo wake ule ule wa kutotaka kutembea na mwanaume yeyote ambaye alikuwa maarufu au kuwa na fedha.
“Kwa hiyo tumuweke nani kwenye video yako mpya?” Muongozaji wa kampuni ya Video ya The Troy, Jafari alimuuliza Yusufu.
“Msichana yeyote mzuri” Yusufu alijibu.
“Kama ni mzuri basi ngoja tuwasiliane na msichana fulani anaitwa Misajo” Jafari alimwambia Yusufu.
“Hakuna tatizo”
“Na hii video itabidi tuifanyie katika hoteli ya Serena kwani inatakiwa iwe ya kimataifa zaidi” Jafari alimwambia Yusufu.
“Hapo umeongea. Ila hatuwezi kumtafuta msichana mzuri zaidi ambaye anaonekana kuwa na hadhi ya kufanana na hoteli ile?” Yusufu aliuliza.
“Au labda tumchukue Pamela”
“Dah! Nilikuwa nimekwishamsahau Pamela. Anafaa sana. Wasiliana nae” Yusufu alimwambia Jafari huku akionekana kuwa na furaha.
“Ngoja nimpigie sasa hivi” Jafari alisema huku akiichukua simu yake mfukoni.
“Umesema video ifanyikie wapi?” Yusufu alimuuliza Jafari
“Pale Serena hotel”
“Achana napo. Tunasafiri na kwenda Madagaskar, sehemu ambayo ina hoteli kubwa na nzuri zaidi. Ukimpigia simu na kukubaliana nae, mwambie ajiandae na safari kwani itaanza kesho kutwa” Yusufu alimwambia Jafari.
“Sawa”
Yusufu akaondoka mahali hapo. Katika kipindi kirefu sana alikuwa akitamani sana kufanya mawasiliano na msichana Pamela. Alijua fika kwamba msichana yule alikuwa mgumu sana kumkubalia mwanaume aliyekuwa na fedha au supastaa ila kwake aliamini kwamba msichana huyo asingeweza kusumbua hata kidogo. Kwa jinsi pamela alivyokuwa akifuatwafuatwa na wavulana wengi, Yusufu aliamini kama angefanya nae mapenzi basi kungekuwa na watu wengi ambao wangemfauata na kuangamia.
Siku hiyo kwake ikaonekana kuwa ya furaha. Alichokifanya mara baada ya kufika nyumbani ni kuangalia video ambazo Pamela alikuwepo huku akili yake kwa kipindi hicho ikiwa inamfikiria msichana huyo. Kadri ambavyo alivyokuwa akimwangalia na ndivyo ambavyo alizidi kumtamani zaidi na zaidi, mzuka wa kufanya nae ngono ukazidi kumkamata zaidi na zaidi. Kila alipoangalia kama kulikuwa na dalili za msichana Pamela kunusurika kutoka katika mikono yake, hakuona hata dalili moja, kila alichokuwa akikifikiria mahali hapo ni kumpata Pamela kwa gharama yoyote ile.
“Hawezi kukataa. Atakataa vipi na wakati maisha yangu yamejaa mvuto! Nina mvuto kiasi ambacho hakuna atakayeweza kunikataa. Nikifika nae Madagaska ndipo ambapo nitakamilisha kila kitu” Yusufu alijisemea huku akiendelea kumwangalia Pamela katika video zile na baada ya saa moja akajikuta akipitiwa na usingizi.
Siku iliyofuata ndio ilikuwa siku ambayo Yusufu alitakiwa kukutana na Pamela na kisha kupanga namna ambavyo video ile itakavyokuwa. Japokuwa jambo hilo likaonekana kuwa tofauti na wengine, Yusufu akaamua kwamba matendo ambayo yalitakiwa kufanyika katika video ile ni lazima yachukuliwe mazoezi. Hapo ndipo alipoanza kuwasiliana zaidi na Pamela na kisha kutaka kuonana nae katika hoteli ya Serena kwa ajili ya kufanya mazoezi.
Pamela hakuonekana kuhofia, kwake, kila kitu kilionekana kuwa sawa kabisa. Saa kumi na robo jioni, Pamela akaanza safari ya kuelekea katika hoteli hiyo ambapo alipokelewa na Yusufu na kisha kupelekwa katika chumba ambacho Yusufu alikuwa amechukua. Pamela alionekana kushangaa kila alichokuwa akikiona kwa wakati huo. Ni kweli kwamba alikwishawahi kuingia katika vyumba vya hoteli nyingi kubwa lakini chumba cha hoteli ile kikaonekana kumshangaza kupita kawaida.
Yusufu akabaki kimya akimwangalia Pamela kisiri huku akiandaa sehemu ambazo walitakiwa kuchukulia mazoezi. Mara baada ya kupanga sehemu hizo vizuri, Yusufu akamuita Pamela na kisha kukaa nae katika viti ambvyo vilikuwa vimezunguka meza ya kioo. Wote wakabaki wakiangalia kama watu ambao walikuwa wakisubiriana kufanya mambo fulani, baada ya sekunde chache, Yusufu akachukua glasi iliyokuwa na soda na kisha kupiga fundo moja.
“Najua wewe si undreground. Kwa hiyo jiamini. Hapa nitataka kuangalia uwezo wako, ukinivutia basi nitakuwa nikikutumia katika video zangu nyingi ambazo zinaangaliwa Afrika nzima” Yusufu alimwambia Pamela.
“Usijali” Pamela alijibu.
Hapo mazoezi ya kizushi yakaanza mara moja. Kama mazoezi, yalikuwa ni mazoezi hasa, Yusufu hakutaka kuonyesha ishara zozote zile, tayari alijiona kutokuwa na presha katika kitu chochote ambacho alitakiwa kukifanya mahali hapo. Alimfananisha pamela na kuku wake, kamwe hakutakiwa kumchukulia manati na kumpiga nayo, akimtaka tu, anamkamata bila kipingamizi. Mazoezi hayo yaliendelea mpaka saa mbili usiku na kisha kuondoka magali hapo.
Siku hiyo kwa Pamela ikaonekana kuwa tofauti, madawa ya mvuto ya kishirikina ambayo alikuwa amepewa Yusufu yakaonekana kuanza kumsumbua pamela. Muda mwingi alikuwa akiweweseka kitandani huku akimmfikiria sana Yusufu ambaye alikaa nae kwa zaidi ya masaa manne katika chumba cha hoteli. Moyo wake ukaanza kumfikiria Yusufu, hakuamini kama yule Yusufu ambaye alikuwa akimuona sana katika televisheni ndiye alikuwa yule Yusufu ambaye alikuwa ametoka kukaa nae katika hoteli ile.
Katika hali ambayo wala hakuitegemea, Pamela akaanza kujishikashika mwilini mwake, tayari hali ikaonekana kuanza kubadilika, Yusufu akaanza kuonekana kuwa mtu wa ajabu ambaye alikuwa amekutana nae katika maisha yake. Pamela aliendelea kujishikashika kwa muda wa dakika kadhaa, moyo wake ukaonekana kumhitaji Yusufu katika muda ule.
Usingizi haukupatikana kirahisi siku hiyo, muda mwingi alikuwa akimfikiria Yusufu ambaye alikuwa ameuteka moyo wake kwa kipindi kichache sana. Siku iliyofuata, siku moja kabla ya safari, pamela akapanga kuonana na Yusufu lakini Yusufu akajifanya kuwa bize sana na mambo yake kwa hivyo asingeweza kuonana nae mpaka pale ambapo wangeanza safari ya kuelekea Madagaska.
Kwa Pamela jambo lile likaonekana kuwa kama pigo, asingeweza kuendelea kuishi zaidi kama asingeweza kumuona Yusufu siku hiyo. Alichokifanya pamela ni kuondoka nyumbani kwao na kisha kuanza kuelekea Sinza kwa ajili ya kuonana na Yusufu. Alipofika huko, akakaribishwa na kisha kuingia ndani. Macho ya Pamela yalipotua usoni mwa Yusufu ambaye alikuwa ametokea chumbani na kuja pale sebuleni alipokaribishwa na mfanyakazi, Pamela akauhisi moyo wake ukipata faraja ambayo wala hakuweza kuipata kablsa.
Kabla ya salamu, Pamela akasimama na kisha kumfuata Yusufu, alipomfikia, akamkumbatia kwa nguvu kana kwamba hakutaka atoke katika mikono yake. Kumbatia lile likamshangaza sana Yusufu lakini hakuonekana kujali, tayari aliona kwamba mvuto ule ambao alikuwa nao ndio ambao ulimfanya Pamela kuwa katika hali ile.
“Vipi Pamela?” Yusufu alimuuliza Pamela ambaye hakuwa akitaka kutoka kifuani mwake.
“Nakupenda” Pamela alimwambia Yusufu kwa sauti ya chini iliyojaa mahaba.
“Unasemaje?”
“Nakupenda The Ruler” Pamela alimwambia Yusufu.
Yusufu akajifanya kushtuka, moyo wake ulijawa na furaha kubwa, tayari aliona kwamba kile ambacho alikuwa amekikusudia ndicho ambacho kilionekana kutokea katika muda huo. Alichokifanya Yusufu ni kumchukua Pamela na kisha kumpeleka kochini na kumkalisha na kuanza kumwangalia.
“Unanishangaza Pamela. Ulisemaje?” Yusufu aliuliza huku akijifanya kutokusikia kile ambacho alikuwa ameambiwa.
“Ninakupenda The Ruler” Pamela alimwambia Yusufu.
“Hilo ni tatizo kubwa sana. Kazi haiwezi kufanyika kama kuna mapenzi kati yetu” Yusufu alimwambia Pamela.
“Nimeshindwa kuvumilia The Ruler, usiku wa jana ulikuwa usiku wa shida sana katika maisha yangu, nilishindwa kulala kwa sababu yako. Nimeweweseka peke yangu usiku kwa ajili yako. Ninakupenda sana The Ruler” Pamela alimwambia Yusufu.
“Acha utani Pamela”
“Ndio hivyo The Ruler”
“Sasa kwa nini umekuja usiku hivi?” Yusufu alimuuliza Pamela.
“Nimekuja kulala nawe usiku wa leo”
“Unasemaje?”
“Nimekuja kulala nawe usiku wa leo” Pamela alilirudia jibu lake”
Kitu kama hicho kilikuwa moja ya kitu ambacho alikuwa akitarajia kukisikiaYusufu kutoka kwa Pamela, kwake, mvuto mkubwa wa mapenzi ambao alikuwa nao katika kipindi hicho ulionekana kumwewesekea msichana yeyote ambaye alikuwa akimtaka katika kipindi hicho. Ingawa Pamela alionekana kuwa mgumu kwa wanaume wengi maarufu na tajiri lakini kwa Yusufu hakuonekana kuwa na ugumu wowote ule.
Moja kwa moja Yusufu akamchukua Pamela na kisha kumpeleka chumbani. Wakavua nguo na kisha kuelekea bafuni kuoga na baada ya hapo, kilichofuatia kilikuwa ni kuvunja amri ya sita tu. Kwa pamela, tukio lile likaonekana kumfariji huku kwa Yusufu, tukio lile likaonekana kumfurahisha kutokana na ugonjwa wa UKIMWI ambao alikuwa amemuambukiza Pamela katika kipindi hicho.
Siku hiyo ilikuwa ni siku ya kufanya ngono usiku tu. Walikesha wakifanya ngono mpaka miili yao ikachoka. Walipoamka asubuhi, wakajiandaa tayari kwa safari ya kuelekea katika visiwa vya Madagaska tayari kwa kuanza kutengeneza video ya wimbo ambao walikuwa wameupanga kuurekodi.
Matendo yao ya ngono yakaendelea zaidi visiwani Madagaskar, ngono ikaonekana kuwatawala mpaka katika kipindi ambacho wakaamua kurudi nchini Tanzania huku wakiwa wametumia siku tatu kukaa nchini Madagaskar. Kama ilivyo kawaida, mara baada ya Pamela kufanya mapenzi na Yusufu, akaanza kuonekana kuwa msichana mwepesi, mapepo ambayo yalikuwa yamemuingia kupitia kwa Yusufu yakamfanya muda mwingi kutamani kufanya ngono.
Hapo ndipo ambapo Pamela akaanza kuwapanga wanaume. Wanamuziki wote ambao walikuwa wakimtaka akaanza kufanya nao ngono huku akiwa anakataa katakata kutumia mpira. Kutokana na uzuri ambao alikuwa nao katika kipindi hicho, Pamela alitembea na wanaume wengi huku zoezi lake la kuwaambukiza ugonjwa huo likiwa limefanikiwa kwa asilimia kubwa.

Je nini kitaendelea?
Itaendelea kesho.
 
MTUNZI: NYEMO CHILONGANI.
MAHALI: DAR ES SALAAM.
SIMU: 0718 069 269.

NITAKAPOKUFA 18

Ugonjwa wa UKIMWI ukaendelea kuua kama kawaida. Wasichana warembo zaidi ya mia na mbili nchini Tanzania walikuwa wakiugua vilivyo katika vitanda vyao huku kila dalili za kuathirika zikiwa zinaonekana miilini mwao. Hilo likaonekana kuwa pigo kubwa kwa wavulana ambao walikuwa wamewahi kutembea na wasichana hao ambao walikuwa wakisikitisha sana vitandani.
Watu wakaanza kuhoji kwamba ni nani angefuatia mara baada ya hao. Mbele yao kukaonekana kuwa na mnyororo mkubwa sana ambao ungewajumuisha wanaume wengi ambao walifanya mapenzi na wanawake wale. Hakukuwa na mtu ambaye alifahamu kwamba wasichana wale wote walikuwa wamefanya mapenzi na mwanamuziki The Ruler ambaye kazi yake ilikuwa ni kutembea na wasichana hao na kuwaambikiza UKIMWI.
“Hali inatisha sana, sijui kama atapona mtu” Kijana mmoja alimwambia mwenzake.
“Hawa wasichana warembo wanaougua watakuwa wanaondoka na watu wengi sana. Hapa ni kumuomba Mungu tu” Jamaa mmoja aliwaambia wenzake.
Hali ikaonekana kuogopesha katika kipindi hicho, wanawake ambao walikuwa warembo wakaonekana kuogopwa kutokana na idadi kubwa yao kuathirika na ugonjwa huo. Wasichana ambao walikuwa wakitarajia kugombea urembo wa Tanzania, wengi wao walikuwa wakiugua ugonjwa huo ambao ulikuwa umewaweka kitandani katika kipindi hicho.
Ukiachilia hao, pia hata msichana ambaye alikuwa akitikisa kwa mvuto na uzuri nchini Tanzania, Pamela, nae alikuwa miongoni mwa wasichana ambao walikuwa wakiugua ugonjwa huo ambao ulionekana kuwapuputisha vijana wengi nchini tanzania. Watu wote ambao walitembea na Pamela wakaanza kuishi kwa matumaini hata kabla hawajaenda kupima afya zao na kuangalia kama walikuwa wameathirika au la.
Kuanzia vyuoni, katika shule za Sekondari mpaka maofisini, wasichana warembo walikuwa wameambukizwa ugonjwa huo. Uchunguzi juu ya ugonjwa huo ulipoanza kufanyika, hali ikaonekana kuwa ngumu sana kumjua mtu ambaye alikuwa chanzo kutokana na watu hao kufanya mapenzi na wanaume mbalimbali tena hata bila kutumia mpira.
Serikali jaikutaka kulifumbia mambo jambo hili jambo ambalo wakaanza kufanya uchunguzi wa kimya kimya. Kila msichana mrembo ambaye alikuwa akiugua ugonjwa huu alipofuatwa na kuwataja wavulana ambao alikuwa ametembea nao, Yusufu alikuwa mmoja wapo. Jambo hilo likaonekana kuwatia wasiwasi, halikuwa jambo la kawaida kwa wanawake zaidi ya mia moja kusema kwamba wote walikuwa wamewahi kufanya mapenzi na mtu mmoja, msanii ambaye alikuwa akiingiza kiasi kikubwa cha fedha kwa wakati huo.
Tume ndogo ya siri ikaandaliwa kwa kuendelea kuwahoji wasichana zaidi na zaidi, na kwa kila msichana, jina la Yusufu lilikuwa la kwanza kutajwa jambo ambalo liliendelea kuwashtua. Walichokiamua kwa wakati huo, ilibidi Yusufu atafutwe na kisha kuambiwa kupimwa kwa kulazimishwa. Japokuwa hiyo haikuwa haki lakini hawakuwa na jinsi kwa wakati huo, ilikuwa ni lazima Yusufu apimwe na kisha kuangaliwa kama alikuwa ameathirika au la, na kama alikuwa ameathirika basi aandaliwe kesi ya kuua kwa kukusudia.
Mchakato huo ukafanyika na Yusufu kuanza kusubiriwa kwani kwa kipindi hicho hakuwa nchini Tanzania, alikuwa nchini Afrika Kusini kikazi. Yusufu alichukua muda wa mwezi mmoja na ndipo akarudi nchini Tanzania na kisha kuhitajika katika ofisi ya Waziri wa Afya.
“Kuna nini?” Yusufu aliuliza huku akionekana kuwa na wasiwasi.
“Wewe njoo tu, kuna maswali kadhaa tungependa kukuuliza” Waziri yule, Bwana Mkude alimwambia Yusufu.
Yusufu akakata simu, moyoni mwake akaanza kuwa na wasiwasi, tayari alikwishaona kwamba mambo yalikuwa yameharibika kwa wakati huo. Maswali kibao yakaanza kumiminika kichwani mwake na mwisho wa siku alikuja kufahamu kwamba alikuwa akihitajika kutokana na wanawake wale kuulizwa na jina lake kutajwa kwa kila msichana.
“Mmmh! Je wakinikuta nao itakuwaje? Ila poa, ngoja nikawasikilize. Inawezekana najitia wasiwasi kumbe huko naitiwa kitu kingine” Yusufu alijisema na kisha kutoka nje na kuanza safari ya kuelekea katika ofisi ya waziri huyo iliyokuwa Posta Mpya.
Mara baada ya kufika katika eneo la ofisi hiyo moja kwa moja Yusufu akateremka na kuanza kuelekea katika mlango wa kuingilia katika ofisi ile. Alikaribsihwa vizuri na kisha kukaa kitini huku akimwangalia Waziri Mkude ambaye alikuwa amekaa nyuma ya meza kubwa ya vioo.
Muda wote ule, Yusufu alikuwa na wasiwasi, mapigo yake ya moyo yalikuwa yakidunda kupita kawaida. Kila alipokuwa akimwangalia waziri Mkude, moyo wake ulikuwa ukiendelea kukosa amani mahali hapo. Bwana Mkude wala hakuonekana kuwa na haraka, akaanza kupiga stori na Yusufu kama mtu ambaye alikuwa akitafuta mazoea.
“Umewezaje kuwa na mashabiki wengi namna hiyo kwa muda mfupi sana wa miaka miwili?” Bwana Mkude aliuliza.
“Kujituma. Kila siku nimekuwa mtu wa kujituma sana maishani mwangu” Yusufu alimwambia Bwana Mkude.
“Na unapigana vipi na changamoto za hapa na pale?”
“Changamoto zipo na wala siwezi kuzizuia maishani mwangu. Ili nifanikiwe katika maisha yangu, haina jinsi kuzipokea changamoto mbalimbali. Kuna watu watakuja na kusema kwamba unataka sifa kwa wasichana, kuna wengine watasema unatumia uchawi na kuna wengine watasema kwamba madj ndio watu wanaokupaisha sana” Yusufu alimwambia Bwana Mkude.
“Ila kutaka sifa kutoka kwa wasichana si ndio zenu wasanii?”
“Baadhi yao lakini sidhani kama mimi nipo kama wao” Yusufu alijitetea.
“Sawa. Ila mbona haupendi hata kusaidia watu wenye matatizo mbalimbali katika jamii?” Bwana Mkude aliuliza.
“Si kweli. Katika maisha yangu nimekuwa nikijitoa sana kuwasaidia watu wenye matatizo mbalimbali. Najua nilipotoka, kwa kipindi kirefu sana nimekuwa na matatizo kama wao, kwa hiyo ninapowaona watu wenye matatizo huwa ninapata hamasa ya kuwasaidia” Yusufu alimwambia Bwana Mkude.
“Na vipi kuhusu mambo yetu yale?” Bwana Mkude aliuliza.
“Mambo gani?”
“Acha hizo bwana. Si wale watoto wa kike” Bwana Mkude alisema kwa sauti ya utani.
“Huwa sipendi kuwafuatilia sana”
“Kwa nini sasa?”
“Unakumbuka kwamba nilikuwa na mke? Yeye ndiye aliyenifanya nisiwatamani watu hawa” Yusufu alisema.
“Kwa nini sasa?”
“Basi tu”
“Ila mbona kila kona watoto wa kike wanakuitaita tu. Kweli utawakosa hata kufanya nao mambo fulani na wakati wewe bado kijana na damu inachemka?” Bwana Mkude alisema huku akiendelea kumtoa woga Yusufu.
“Bado. Naangalia maisha kwa sasa, halafu mapenzi baadae” Yusufu alijibu.
“Sasa mbona kila msichana anasema kwamba ameshalala na wewe?” Bwana Mkude alisema kitu kilichomfanya Yusufu kushtuka.
“Hapana”
“Kweli tena. Wanawake kama mia wamesema wamelala na wewe”
“Si kweli mheshimiwa”
“Kwa nini si kweli? Kwani unashindwa na wakati wewe ni supastaa, kila kona linaitwa jina lako?”
“Idadi kubwa sana hiyo kwangu”
“Sawa. Kama idadi kubwa wewe umekwishawahi kulala na wangapi?”
“Na wanawake watatu”
“Uliwahi kutumia mpira?”
“Yaap! Huwa ninatumia sana kwani bado najipenda” Yusufu alimwambia.
“Mara yako ya mwisho kupima damu ilikuwa lini?”
“Mwezi mitatu iliyopita”
“Majibu yalikuwaje?”
“Nilikuwa fiti. Damu safi”
“Kama ulipima miezi mitatu iliyopita, ilitakiwa urudi tena baada ya miezi mitatu. Utarudi lini?” Bwana Mkude aluliza.
“Wiki ijayo”
“Na itakuwaje kama tukikwambia kwamba upime sasa hivi?”
“Sasa hivi! Hapana bwana, sijajiandaa” Yusufu alijibu huku akionekana kushtuka.
“Kwani jambo hili linahitaji maandalizi?”
“Ndio”
“Kama yapi”
“Maandalizi ya kawaida tu”
“Acha woga The Ruler. Kwani mara baada ya kupima miezi mitatu iliyopita na kuonekana upo fiti, ulifanya mapenzi na mtu yeyote?”
“Hapana”
“Sasa unaogopa nini? Acha woga” Bwana Mkude alisema huku akisimama.
Bwana Mkude akaanza kuelekea nje ya ofisi ile. Yusufu alibaki ndani ya kile chumba akitetemeka, kwa jinsi maongezi yalivyokuwa yamekwenda na kwa jinsi yalivyomaliziwa yalionekana kuwa tofauti kabisa, Yusufu alibaki akitetemeka, katika kichwa chake alikuwa akijifikiria mambo mawili, cha kwanza kilikuwa ni kuwagomea lakini cha pili kilikuwa ni kuwakimbia.
“Nifanye nini sasa?” Yusufu alijiuliza hakini hata kabla hajajua nini cha kufanya, mara mlango ukafunguliwa na Bwana Mkude kuingia huku akitangulizana na mtu ambaye alikuwa amevalia koti kubwa jeupe.
“Samahani kwa kukutisha. Huyu ni daktari kutoka katika hospitali ya muhimbili anaitwa Dokta Musa. Yeye anashughulika zaidi maabara na kitu ambacho tumeamua kukifanya kwa sasa kama serikali ni kuchangisha damu kutoka kwa watu mbalimbali kwa ajili ya watoto ambao wamekuwa na upungufu wa damu hospitalini. Tunaanza na wasanii kwa sababu hata baadae tukiwafuata watu wengine na kuwaambia kwamba wasiogope kwani The Ruler mwenyewe ametoa damu yake, watu watakubali, si unajua wanataka kufanya kama supastaa anavyofanya” Bwana Mkude alimwambia Yusufu huku maneno yake mengi yakionekana kumtoa wasiwasi.
Dokta Musa akauchukua mkanda fulani na kisha kumfunga Yusufu mkononi kwa juu kwa ajili ya kuiruhusu mishipa yake ya damu kuonekana. Mishipa ilipoonekana, dokta Musa akamchoma sindano na kuchukua damu na kisha kwenda nayo kwenye gari lao walilokuja nalo mahali pale.
“Kwanza tunahitaji kucheki damu yako kama safi halafu tutaichukua. Unajua damu za watu wengine zinakuwa chafu, yaani hazina ubora wa kufanya kupewa mtu mwingine” Bwana Mkude alimwambia Yusufu.
Furaha yote ambayo alikuwa nayo Yusufu ikapotea katika kipindi hicho, mawazo yake yalikuwa juu ya ile damu yake ambayo ilikuwa imechukuliwa kwa ajili ya vipimo. Mapigo ya moyo katika kipindi hicho yalikuwa yakidunda sana, mara mbili zaidi ya udundaji wake wa kawaida. Bwana Mkude alikuwa akiendelea kuongea maneno mengi tu mahali hapo lakini kwa Yusufu hayakuonekana kueleweka hata kidogo.
Mawazo yake yalikuwa yakifikiria majibu ya damu ambayo ilikuwa imechukuliwa kwa ajili ya kupimwa. Moyoni mwake alijua wazi kwamba alikuwa ameathirika, kitendo cha kuchukuliwa damu yake na kisha kwenda kupimwa tena kingemfanya Bwana Mkude aufahamu ukweli kwamba alikuwa ameathirika.
Dokta Musa alichukua dakika kadhaa akarudi ndani ya ofisi ile na moja kwa moja kumpa karatasi ya majibu Bwana mkude na kuanza kuiangalia. Katika kipindi hicho, uso wa Yusufu ulikuwa ukionyesha wasiwasi dhahiri, mapigo yake ya moyo yakazidi kudunda zaidi na zaidi kwa kuona kwamba Bwana mkude alikuwa akienda kuujua ukweli kwamba alikuwa ameathirika. Mwili wake ukamnyong’onyea huku kijasho chembamba kikimtoka kwa kuona kwamba ukweli wa kila kitu ulikuwa ukienda kujulikana siku hiyo.
****
Tabasamu pana bado lilikuwa likiendelea kuonekana usoni mwa Bwana Mkude ambalo lilionekana kuwa tabasamu lililomfanya kugundua kitu fulani. Aliiangalia karatasi ile kwa dakika kadhaa na kisha kuyapeleka macho yake usoni mwa Yusufu ambaye bado alikuwa na wasiwasi mwingi usoni mwake.
“Safi sana The Ruler. Damu yako safi na wala haina maambukizo ya virusi vya UKIMWI” Bwana Mkude alimwambia Yusufu.
Maneno yale yakaonekana kumshtua sana Yusufu, akamwangalia mara mbili mbili Bwana Mkude huku akionekana kutokuamini kile ambacho alikuwa amekisikia, alichokifanya ni kunyanyuka na kisha kuichukua karatasi ile na kuanza kuiangalia. Yusufu hakuonekana kuamini, neno NEGATIVE lilikuwa likionekana vizuri tena likiwa limeandikwa kwa herufi kubwa.
Furaha ambayo alikuwa nayo Yusufu katika kipindi hicho ikamfanya kumuinua bwana Mkude na kisha kumkumbatia kwa nguvu. Kwake majibu yale yalionekana ni zaidi ya masikini wa kutupa kushinda bingo ya kiasi cha shilingi milioni mia moja. Bila kutarajia, machozi ya furaha yakaanza kumtoka Yusufu, alikuwa akifurahia kupita kawaida.
Hapo hapo akachukua simu yake na kisha kumpigia Papaa Pipo na kisha kumpa taarifa ile. Furaha yake katika kipindi hicho ilionekana kuwa kubwa hata zaidi ya kuushinda mwili wake. Alikuwa akiruka ruka kila wakati, hakuamini kama kweli alikuwa na damu safi, hakuwa ameathirika na ugonjwa wa UKIMWI.
“Siamini” Yusufu alimwambia Papaa Pipo mara baada ya simu yake kupokelewa.
“Haumani nini? Mbona unaonekana kuwa na furaha kubwa?” Sauti ya Papaa Pipo ilisikika simuni.
“Nimetoka kupima sasa hivi, tena kwa dokta ambaye anaaminikia na serikali, sijaathirika ugonjwa wa UKIMWI” Yusufu alimwambia Papaa Pipo.
“Unasemaje?”
“Sijaathirika na ugonjwa wa UKIMWI. Damu yangu ni safi kabisa” Yusufu aliema kwa sauti kubwa iliyojaa furaha huku Bwana Mkude akimwangalia kwa uso uliojaa tabasamu.
“Unanitania Yusufu”
“Ndio hivyo. Damu safiiiiiiiii, haina mdudu hata mmoja wa kusingiziwa” Yusufu alimwambia Papaa Pipo.
“Hebu njoo nyumbani uniambie vizuri manake ushaanza kunichanganya” Papaa Pipo alimwambia Yusufu na kisha kukata simu.
Bado Yusufu alionekana kuwa na furaha, hakuamini kama kweli damu yake haikuwa imeathirika na ugonjwa ule wa UKIMWI kama vile ambavyo alikuwa ameambiwa na Dokta Lyimo miezi kadhaa iliyopita. Yusufu alibaki akiiangalia karatasi ile huku akionekana kutokuamini dhahiri kile ambacho alikuwa akikiangalia kwenye karatasi ile.
“Mbona hauamini na wakati haujafanya chochote ndani ya miezi mitatu iliyopita?” Bwana Mkude alimuuliza.
“Skendo. Watu wamekuwa wakiongea sana mambo mengi kuhusiana na afya yangu. Nadhani hata wewe utakuwa umezisoma sana au kusikia sana skendo zile kwamba nimeathirika” Yusufu alimwambia bwana Mkude.
“Ndio maana nikakwambia kwamba wewe kama supastaa kuna mambo mengi sana yataongelewa juu yako. Yakupasa kuwa na moyo wa chumba kuyavumilia” Bwana Mkude alimwambia Yusufu.
“Hicho ndicho ninachofanya japokuwa wakati mwingine tetesi hizi zinanifanya kutokuwa na raha kabisa. Majibu haya, ikiwezekana ni lazima yawekwe kwenye magazeti na kutangazwa sehemu nyingine ili watu wajue kwamba zile ni skendo chafu za kunichafua” Yusufu alimwambia bwana Mkude.
Yusufu hakutaka kukaa sana mahali hapo, bado moyo wake ulikuwa katika furaha kubwa kupita kawaida, kwa wakati huo alikuwa akitaka kuonana na Papaa Pipo macho kwa macho na kisha kumwambia vizuri juu ya majibu ya afya yake yalivyokuwa. Yusufu akaondoka ndani ya ofisi ile na kisha kulifuata gari lake na kisha kuanza kuondoka mahali hapo.
Ndani ya gari, Yusufu alionekana kuwa mwingi wa furaha, hakuamini kama majibu ya damu yake yalionyesha kwamba yalikuwa safi kabisa. Kila wakati garini alikuwa akitabasamu kupita kawaida, alijiona kuwa mtu pekee ambaye alikuwa na furaha kubwa sana duniani kuliko mtu yeyote yule.
Mara baada ya kufiika magomeni hospitali, Yusufu akalipaki gari lake pembeni na kuteremka. Yusufu akavuka barabara na kisha kuanza kumfuata ombaomba mmoja ambaye alikuwa akiomba fedha kwa kila mwananjia ambaye alikuwa akipita mahali hapo na kisha kumsaidia kiasi cha fedha.
Watu wote ambao waliliona tukio lile wakaonekana kumsifia Yusufu kwa kile ambacho alikuwa amekionyesha mahali pale. Watu ambao walikuwa na simu zenye kamera wakaanza kumpigia pichwa, uadimu wa Yusufu kutokuonekana mitaani ukamfanya kuwa wa thamani katika macho ya watu.
“Jamaa anataka tumuone kama yeye anasaidia sana watu masikini” jamaa mmoja ambaye alionekana kuwa na bifu lake aliwaambia wenzake.
“Acha roho ya kwa nini wewe. Mtoto mdogo utakuja kufa na kiroho chako kibaya. Mtu amejaribu kuonyesha kujali kwake kwa watu masikini halafu unaponda tu. Hapo angepita bila kumsaidia ungeanza kuongea maneno kwamba anaringa. Badilika bwana, utakuja kuzeeka kabla ya muda wako” jamaa mwingine alimwambia jamaa yule maneno ambayo yaliwafanya watu wote waliokuwa mahali hapo kuanza kucheka.
Yusufu alipoona watu wameridhika kumpiga picha, akaanza kulifuata gari lake na kisha kuingia na kuondoka mahali hapo. Bado furaha yake moyoni ilikuwa kubwa, hakumsaidia ombaomba yule kiasi cha fedha kwa sababu alijisikia kumsaidia, ila alimsaidia kutokana na furaha kubwa ambayo alikuwa nayo moyoni mwake katika kipindi hicho.
“Sasa hapa hata wakisema wanailinda afya yangu nitakuwa nikikubaliana nao” Yusufu alijisemea katika kipindi ambacho alichukua barabara ya kuelekea Tandale huku lengo lake likiwa ni kutaka kufika kwa Mtogole ambapo angekata kulia na kuchukua barabara ya Kijitonyama na kisha kuanza kuelekea katika mtaa wa Hollywoody aliokuwa akiishi Papaa Pipo. Yusufu alijiona kutokufika haraka kiasi ambacho wakati mwingine alitamani gari lake liote mabawa na hivyo lipae na kutua katika geti la nyumba ya Papaa pipo.
Yusufu alichukua dakika kadhaa mpaka kufika katika nyumba hiyo ambapo mlinzi akaufungua mlango na kisha kuliingiza gari katika eneo la nyumba ya Papaa Pipo. Mara baada ya kulipaki, moja kwa moja akateremka na kisha kuanza kuufuata mlango wa kuingilia sebuleni na bila kupiga hodi akaufungua na kuingia ndani na kumkuta Papaa Pipo.
“Bora umekuja, hebu niambie vizuri” Papaa Pipo alimwambia Yusufu hata kabla ya kuongea chochote. Alichokifanya Yusufu ni kumrushia karatasi ile ambayo ilikuwa na majibu ya damu yake. Papaa Pipo akaichukua na kisha kuanza kuiangalia.
“Mmmh! Mbona imekuwa hivi tena?” Papaa Pipo alimuuliza Yusufu huku akiigeuza karatasi ile nyuma na kuona kama kulikuwa na maandishi mengine.
“Hata mimi mwenyewe nilishangaa sana. Vipimo vya Dokta Lyimo havikuwa sahihi, tulifanya uamuzi mzuri kumuua. Angeweza kuniua kwa presha” Yusufu alisema huku akicheka kwa furaha.
“Kwa hiyo mambo safi?”
“Wewe si unaona mwenyewe”
“Nani alikupima?”
“Mmoja wa madaktari wa hospitali ya Muhimbili, tena mbele ya macho ya Waziri Mkude” Yusufu alimwambia Papaa Pipo.
“Mbele ya macho ya Waziri Mkude?”
“Ndio”
“Mmmh!”
“Nini tena?”
“Mbona unanichanganya?”
“Nakuchanganya kivipi?”
“Ulikuwa ukifanya nini na Waziri?” Papaa Pipo aliuliza huku akionekana kushtuka.
“Aliniita”
“Ili?”
“Sijui. Nafikiri kupimwa”
“Inawezekana vipi?”
“Labda zamu zamu. Mimi si ndio Baba Lao la mastaa wote Bongo ndio maana nimekuwa wa kwanza” Yusufu alimwambia Papaa Pipo.
“Sawa nimekuelewa. Kwa hiyo ni nini kinachofuata sasa hivi?”
“Mwendo wa kula bata mpaka kuku waone wivu” Yusufu alisema huku akisimama.
“Bata wapi sasa?”
“Popote tu ili mladi tuhakikishe bata wanaliwa kweli”
“Basi poa. Kama vipi Kilimanjaro hoteli huku tukiwa tumezungukwa na watoto wa Kiarabu na Kizungu” Papaa Pipo alimwambia Yusufu.
“Hakuna tatizo”
“Au ulikuwa unataka watoto wa Kiswahili?”
“Achana nao. Nimewavua sana mpaka nimechoka. Twende kwa hao hao watoto wa Kiarabu na Kizungu. Ni mwendo wa pushapu mpaka asubuhi hadi kitanda kiombe poo” Yusufu alimwambia Papaa Pipo na kisha kutoka nje ya nyumba hiyo ambapo wakachukua gari la Papaa Pipo na kuanza kwenda Kilimanjaro hoteli kwa ajili ya kula starehe tu kama kusherehekea usafi wa damu ya Yusufu.


Wanawake warembo wa tanzania wanaangamizwa na supastaa Yusufu.
Je nini itakuwa hatima ya warembo hawa?
Je nini itakuwa hatima ya Yusufu?
 
MTUNZI: NYEMO CHILONGANI.
MAHALI: DAR ES SALAAM.
SIMU: 0718 069 269.

NITAKAPOKUFA 19

Mwanaume huyu alikuwa na fedha nyingi katika maisha yake, kila siku, kazi yake kubwa ilikuwa ni kusafirisha madawa ya kulevya kupeleka katika nchi za Asia kwa wafanyabiashara wakubwa wa kazi hiyo ambao walikuwa wakiyanunua madawa hayo kwa kiasi kikubwa cha fedha. Katika maisha yake yote, mwanaume huyu ambaye alikuwa akijulikana kwa jina moja la Anko, alikuwa akimiliki kiasi kikubwa cha fedha ambacho kilimfanya kujenga nyumba mbalimbali za kifahari pamoja na kuendesha magari mengi ya kifahari.
Utajiri wake mkubwa ambao alikuwa akimiliki ndio ambao ukamfanya kuwa mrtu wa kwanza mpaka sasa kuingiza gari la kifahari la Lamboghin ambalo alilinunua kwa gharama ya shilingi milioni mia tisha kutoka nchini Marekani. Utajiri wa Anko ulikuwa ukiongezeka kila siku, kulala na wanawake ndio ilikuwa kawaida yake kila siku.
Utajiri mkubwa ambao alikuwa akiumiliki ndio ambao ulikuwa ukimfanya kuonekana kichaa wakati mwingine. Alikuwa akinunua magari mengi na kisha kuyatelekeza gereji kwa kuona kwamba mpaka unafikia hatua ya kulipelekea gari gereji, tayari lilikuwa bovu na halikutakiwa kutembelewa na mtu kama yeye.
Sifa zake za utajiri zilikuwa zikiendelea kusikika sana ndani ya jiji la Dar es Salaam, umwagaji wake wa fedha ambao alikuwa akiufanya mara kwa mara ndio ambao uliwafanya watu wengi kumfahamu Anko ambaye alikuwa akikupa fedha endapo tu ungemsifia kwa staili yoyyote ile. Maishani mwake, Anko hakuwahi kupenda, alikuwa akikutana na wanawake wengi wazuri ambao alikuwa akifanya nao ngono kila siku, kuhusu wasichana, kwake hakukuonekana kama kulikuwa na msichana ambaye alikuwa mzuri.
Ingawa alikuwa akila sana raha lakini kamwe hakuiacha biashara yake ya usafirishaji wa madawa ya kulevya kwenda barani Asia. Mara kwa mara alikuwa akiwatafuta vijana ambao walikuwa na shida ya fedha na kisha kuwapa mzigo wa kwenda nao katika nchi hizo. Usafiri ambao mara kwa mara alikuwa akiuamini ulikuwa ni wa meli tu, kamwe hakuamini kama angetumia usafiri wa anga mizigo yake ingeweza kufika salama.
Vijana wengi walikuwa wakitaani kufanya kazi pamoja nae, malipo ambayo alikuwa akiwalipa vijana ambao walikuwa wakisafirisha mizigo hiyo yallikuwa makubwa kiasi ambacho alikuwa akibadilisha maisha ya kila kijana ambaye alikuwa akifanya nae biashara ya kusafirisha mizigo hiyo. Ingawa kila siku katika maisha yake alikuwa akitumia fedha sana lakini kamwe fedha zake hazikuonekana kupngungua kabisa zaidi ya kuzidi kuongezeka zaidi na zaidi.
Watu wengi walikuwa wakimheshimu Anko kutokana na fedha ambazo alikuwa akizipata kila siku na kutanua nazo katika klabu mbalimbali hasa nyakati za usiku. Kwa vijana ambao walikuwa wakiuhitaji ukaribu pamoja nae, iliwapasa kumpapatikia sana na hata wakati mwingine kumuabudu kana kwamba alikuwa Mungu kwao.
Katika maisha yake yote, Anko alikuwa akiamini katika fedha. Moyoni mwake aliamini kwamba kama unataka kumpata msichana yeyote katika maisha yako basi ilikupasa kuwa na fedha tu au hata ukitaka kumiliki vitu vizuri basi ilikuwa ni lazima upate fedha. Fedha kwake zikaonekana kuwa sumaku huku wanawake wote akiwaona kuwa na vyumba miilini mwao kiasi ambacho angeweza kuwavuta kila walipokuwa wakipita karibu nae.
Ingawa alikuwa akijijua kwamba alikuwa akimiliki bunduki ndogo ambayo alikuwa akitembea nayo katika kila sehemu alizokuwa akienda kwa sababu ya usalama wa maisha yake lakini kamwe hakutaka kuwa peke yake hasa katika maisha yake ya mizunguko. Kila sehemu ambayo alikuwa, walinzi walikuwa pamoja nae huku wakihakikisha ulinzi mkubwa katika maisha yake.
Hakukuwa na mtu ambaye alidiriki kumgusa Anko, nguvu ya fedha ambayo alikuwa nayo ikawapelekea hata baadhi ya viongozi serikalini kuanza kumuogopa kwa kumuona kuwa na nguvu hata zaidi yao. Kila kona, Anko alikuwa akituimia fedha. Barabarani, alikuwa akimwaga fedha ovyo kwa askari wa barabarani kiasi ambacho hata pale alipokuwa akivunja sheria makusudi, hakukuwa na mtu ambaye alimnyooshea kidole.
“Hivi nikitaka kuinunua Tanzania itanipasa kutoa kiasi gani?” Anko alimuuliza rafiki yake wa karibu, Martin katika kipindi ambacho walikuwa wanakunywa huku walinzi wake wakiwa pembeni.
“Hii nchi kuinunua si fedha nyingi, kidogo tu, nchi inakuwa yako na wewe unakuwa rais” Martin alimjibu Anko hali iliyowafanya wote waliokuwa mahali pale kuanza kucheka.
“Nimekuwa na fedha nyingi mpaka najichukia Martin”
“Basi itakubidi fedha nyingine usaidie watoto yatima” Martin alimwambia Anko.
“Haiwezekani bwana. Siwezi kusaidia watoto yatima. Huwa ninachukia watoto” Anko alimwambia Martin.
Kila siku Anko alikuwa akizidi kutumia fedha kadri alivyotaka lakini wala fedha hizo hazikuonekana kupungua katika akaunti yake zaidi ya kuongezeka tu. Tabia yake ya kuchukua wanawake iliendelea kuongezeka zaidi na zaidi mpaka pale ambapo alikuja kukutana na msichana Manka, msichana ambaye akatokea kumpenda kwa mapenzi ya dhati.
Manka kwake akaonekana kuwa msichana wa tofauti kabisa, kwa mara ya kwanza ndani ya miaka mitano ya kuwa na fedha akajiona akianza kuangukia kwenye mapenzi ya dhati kwa msichana. Uzuri wa Manka kwake ukaonekana kuwa hata zaidi ya uzuri wa Malaika. Katika siku ya kwanza ambauyo alikuwa amekutana na msichana huyo, mapigo yake ya moyo yalikuwa yakidunda sana.
Siku hiyo ilikuwa ni siku ya sherehe yake ya kuzaliwa, siku ambayo alikuwa amewaarika watu wengi kusherehekea pamoja nae. Kati ya watu ambao alikuwa amewaalika katika sherehe hiyo alikuwepo msichana Debora ambaye aliamua kuja pamoja na rafiki yake kipenzi, Manka. Mara baada ya macho ya Anko kutua usoni mwa Manka, utulivu ukapungua kabisa, kila wakati alikuwa akitaka kuongea na msichana huyo ambaye kwa kasi sana alikuwa amekwishaingia moyoni mwake na mbaya zaidi alikuwa amekwishavuta kiti na kutulia.
Kila alipotaka kumfuata Manka na kuongea nae, watu walikuwa wakimzuia kwa kupiga nae stori za hapa na pale bila kujua kwa kufanya vile walikuwa wakimkasirisha sana. Moyo wake ukawa na uhitaji mkubwa sana wa kumfuata Manka na kisha kumwambia kile ambacho kilikuwa kimejengeka moyoni mwake, alijiona kuwa na uhitaji mkuhwa wa kumfuata msichana huyo na kumwambia ukweli kwamba katika kipindi hicho alikuwa amempenda kupita kiasi.
“Hebu subirini kwanza” Anko aliwaambia watu ambao alikuwa nao mara baada ya kuona hawaondoki. Akaanza kupiga hatua kumfuata Manka.
“Mambo mrembo” Anko alimsalimia Manka ambaye alikuwa amekaa pembeni ya bustani ya maua huku akinywa kinywaji cha Reds. Manka akageuza macho yake na kumwangalia mtu aliyemsalimia.
“Poa. U mzima mtoto?” Manka alimuuliza Anko huku akionyesha tabasamu ambalo lilionekana kumchanganya sana Anko.
“Nipo poa tu. Mbona umejitenga hivi?” Anko aliuliza kwa sauti ya upole.
“Najisikia kuchoka sana, halafu nahisi kichwa kinauma” Manka alisema kwa sauti ya chini, sauti iliyojazwa kila aina ya mvuto.
“Umekunywa dawa?”
“Hapana”
“Kwa nini sasa?”
“Kimenianza sasa hivi” Manka alijibu huku kwa mbali sauti yake ikisikika kuanza kudeka.
“Ungependa nikuletee dawa?”
“Yeah! Itakuwa vizuri”
“Nikuletee dawa gani?”
“Yaani hata dawa ya kutuliza maumivu ya kichwa hauijui?” Manka aliuliza huku akitoa tabasamu.
“Siijui”
“Sawa. Niletee panado”
“Afadhali umeniambia kwani nilikuwa nawaza kukuletea Pritoni” Anko alimwambia Manka ambaye alianza kucheka kimapozi.
Anko hakutaka kubaki mhali hapo, hiyo ikaonekana kuwa nafasi kubwa sana ya kumpata Manka, alichokifanya ni kuanza kuondoka kuelekea ndani ya nyumba yake. Ingawa watu walikuwa wakimuita lakini hakuonekana kusikia, mawazo yake kwa wakati huo yalikuwa yakimuwaza Manka ambaye tayari alikuwa ameanza kuiteka akili yake kwa wakati huo.
Mara baada ya kufika ndani, moja kwa moja akaanza kuelekea jikoni ambapo akafungua kabati katika droo ambayo alikuwa akihifadhia dawa zake na kisha kuanza kutafuta vidonge vya panado. Wala hakuchukua hata sekunde zaidi ya ishirini, akakiona kifuko cha karatasi ambacho kilikuwa na dawa hizo na kisha kuanza kuondoka kuelekea nje huku akiwa amekwishapitia maji ya kumezea dawa.
“Hizi hapa” Anko alimwambia Manka huku akimpa dawa zile pamoja na maji na kisha kunywa.
“Unajisikiaje sasa hivi?” Anko alimuuliza Manka.
“Kwani dawa zinaanza kufanya kazi muda huo huo? Ngoja kama dakika kumi halafu nitakwambia” Manka alimwambia Anko ambaye mpaka katika kipindi hicho, alikuwa amevutiwa na Manka mara tatu zaidi ya kipindi kichache kilichopita ambacho hakuwa ameongea nae.
“Unaitwa nani?” Anko aliuliza huku akimsogelea.
“Nani? Mimi?”
“Yeah! Nakuuliza wewe mrembo”
“Naitwa Manka Temba”
“Unaishi wapi hapa Dar? Au sitakiwi kujua?”
“Naishi Upanga”
“Upanga ipi?”
“West”
“Unamaanisha Magharibi”
“Hapana. Kusini” Manka alijibu na wote kuanza kucheka.
Kila mmoja kwa wakati huo alikuwa akijitahidi kuuonyesha uchangamfu kwa mwenzake, muda mwingi walikuwa wakiongea huku wakicheka pamoja. Anko akaonekana kujisahau kabisa kama alitakiwa kujuika na watu wengine katika sherehe hiyo, yeye bado alikuwa akimng’ang’ania Manka tu.
“Saa ngapi hapo?” Manka alimuuliza Anko ambaye akaanza kuangalia saa yake.
“Saa nane na robo”
“Mchana au usiku?”
“Asubuhi” Anko alijibu na kisha wote kuanza kucheka.
“Nahitaji kuondoka. Najisikia kuchoka sana” Manka alimwambia Anko kwa sauti ya chini.
“Mbona unawahi sana?”
“Wewe unataka nilale hapa hapa?”
“Kama ikiwezekana”
“Mmmh! Baba yangu mkali sana, utafuatwa na polisi asubuhi” Manka alimwambia Anko.
“Kisa nini? Kwa sababu ya mtoto wake kulala kwangu?”
“Ndio”
“Kwani hilo tatizo?”
“Ni tatizo kubwa sana”
“Hapana bwana. Lala hapa leo” Anko alimwambia Manka.
“Haiwezekani”
“Sasa hauoni mimi mtoto leo nitasumbua sana usiku?”
“Nitakuachia chupa ya kunyonyea” Manka alijibu na wote kuanza kucheka tena.
Manka hakuendelea kukaa sana mahali hapo, alichokifanya ni kumuita Debora na kisha kumwambia kwamba walitakiwa kuondoka muda huo kwa sababu alionekana kuchelewa sana. Debora hakuonekana kukubaliana nae, sherehe ile ndio kwanza ilionekana kuchangamka kwa wakati huo.
“Kwa nini tusikae hadi asubuhi?” Debora alimuuliza Manka.
“Hata mimi nilimshauri hilo”
“Hapana. Siwezi. Nahitaji kulala” Manka aliwaambia.
“Kalale ndani. Si kuna vyumba vya wageni?” Debora aliuliza huku akimwangalia Anko.
“Vipo vingi tu na vyote vina viyoyozi” Anko alijibu.
“Hapana. Sijazoea kulala kwa watu. Nahitaji kuondoka” Manka alisema.
“Basi usijali. Naomba nikupeleke. Upanga si mbali sana kutoka hapa” Anko alimwambia Manka.
“Siendi Upanga”
“Uko si ndio kwenu! Unakwenda wapi tena usiku huu?”
“Hosteli”
“Kumbe unakaa hosteli halafu unaogopa!”
“Hapana. Nahitaji kwenda kupumzika”
“Usijali. Twende nikupeleke” Anko alimwambia Manka.
Alichokifanya Anko ni kumwambia Debora ampe nafasi ya kumsindikiza Manka nafasi ambayo bila wasiwasi wowote ule akapewa na kisha kuanza kuelekea nae katika sehemu ambayo ilikuwa ikitumika kupakia magari na kuchukua gari lake aina ya Range na kisha kuondoka mahali hapo huku Manka akiwa katika kiti cha pembeni.
“U mzuri sana Manka” Anko alimwambia Manka.
“Asante”
“Uzuri huo umeutoa wapi? Kwa mama au kwa shangazi?” Anko alimuuliza huku akionekana kuwa na furaha muda wote.
“Kwa mama”
“Mpe hongera zake. Nimeupenda uzuri wako” Anko alimwambia Manka ambaye muda mwingi alikuwa akitabasamu tu.
Siku hiyo Anko hakutaka kuongea kitu chochote kile kuhusiana na mahusiano, tayari akili yake ilikuwa imekwishamsoma Manka kwamba hakuwa miongoni mwa wanawake ambao walikuwa wakichukulika kiulaini endapo ungeamua kuwaambia ukweli wa moyo wako. Fedha zake kwa Manka zikaonekana kuwa si kitu, msichana huyo hakuonekana kama alikuwa akizitamani fedha zake kama wanawake wengine, hicho kikaonekana kuwa kitu ambacho kilimuongezea thamani ndani ya moyo wa Anko.
“Nishushe hapo hapo” Manka alimwambia Anko mara baada ya kufika Magomeni Mapipa.
“Tumekwishafika?”
“Hapana. Ila ningependa unishushie hapa” Manka alimwambia Anko.
“Kwa nini tena?”
“Hosteli ipo mbali kutoka hapa na ninapita katika vichochoro ambavyo havina uwezo wa kupitisha magari” Manka alimwambia Anko.
“Ningependa nikusindikize” Anko alimwambia Manka.
“Mmmh! Hauogopi usiku huu watu wanaweza kuiba gari lako?”
“Hilo si tatizo. Wakiiba hili, saa kumi na mbili asubuhi nitakuwa nimenunua jingine” Anko alimwambia Manka.
Wote wakateremka kutoka garini na kisha kuanza kuelekea katika vichochoro hivyo ambavyo wakapita pita mpaka kutokea katika jengo moja kubwa ambalo liliandikwa ANNIE MARIE HOSTEL. Manka hakutaka kuendelea mbele zaidi, akasimama na kumgeukia Anko ambaye alikuwa akiangalia huku na kule kama mlinzi.
“Nimefika. Unaweza kurudi” Manka alimwambia Anko.
“Ok! Usijali. Ila ningependa ukaribu wetu uendelee zaidi ya hapa, yaani tuwe tunaonana zaidi ya leo” Anko alimwambia Manka.
“Usijali. Tutaonana tu”
“Unasoma wapi?”
“Nipo I.F.M”
“Mwaka wa ngapi?”
“Mwaka wa kwanza”
“Ok! Nitaweza kupata namba yako ya simu?”
“Usijali” Manka alijibu na kisha kuchukua simu yake na kisha kumpitgia Anko ambaye akaikata na kisha kuihifadhi.
Huo ndio ukawa mwanzo wa ukaribu kati ya Anko na msichana Manka Temba, msichana ambaye alikuwa mzuri sana, uzuri ambao ulifananishwa na uzuri wa malaika. Kuanzia siku hiyo, wawili hao wakaanza kuwasiliana zaidi na zaidi, kwa Anko bado hakuonekana kuwa na presha kubwa, katika kipindi hicho bado kuna vitu vingi sana ambavyo alikuwa akitaka kuvifahamu kuhusiana na Manka.
Manka hakuonekana kuwa msichana mwepesi, kila siku Anko alikuwa akijaribu kumwambia maneno haya na yale lakini bado Manka hakuonekana kujirahisisha kwake. Ilimchukua Anko mwezi mzima na ndipo ambapo Manka akaamua kuwa nae, tena baada ya kuona kwamba ameangaika sana.
Mahusiano hayo ya kimapenzi pamoja na Manka yakamfanya Anko kutulia, uzuri wa Manka ukaonekana kuwa chachu kubwa ya kutotaka kuwatamani wasichana wengine ambao walikuwa wakijigongagonga sana katika maisha yake. Manka alimchukulia msichana wa muhimu sana katika maisha yake, alimchukulia Manka kuwa kama yai au sahani ya udongo ambayo ilihitaji uangalizi wa hali ya juu katika kuitunza.
Kila kitu ambacho Manka alikuwa akikitaka alikuwa akipewa. Alinunuliwa gari la kutembelea bila kuomba huku akaunti yake ikijazwa fedha mpaka yeye mwenyewe kushangaa. Manka akazidi kubadilika, fedha za Anko zikaonekana kumbadilisha kupita kawaida. Shepu yake ikaongezeka mvuto, maringo yakazidi kuongezeka zaidi na zaidi kiasi ambacho wanachuo wa chuo cha I.F.M kuzidi kumtamani zaidi na zaidi.
Anko hakutaka kuumizwa, aliyajua vilivyo maumivu ya mapenzi kwa jinsi yalivyokuwa yakiwatesa watu. Kila siku alikuwa akimsisitizia Manka kuhusiana na uaminifu katika maisha yao, hakukuonekana kuwa na sababu yoyote ya kumkaribisha mtu yeyote kuingilia katika mapenzi yao. Maneno yale yalieleweka sana masikioni mwa Manka lakini wala hayakuonekana kukaa kabisa kichwani mwake.
Anko akawaandaa vijana wake ambao walikuwa na kazi ya kumlinda Manka bila kujua. Vijana hao waliifanya kazi yao kwa uaminifu mkubwa sana huku wakimpa taarifa Anko kuhusiana na kila mvulana ambaye alikuwa akimsumbua Manka. Anko hakutaka kuumizwa kichwa chake jambo ambalo lilikuwa likimfanya kutoa amri moja tu ya kufanya mauaji kwa kila mvulana ambaye alikuwa akimsumbua sumbua Manka.
Vijana wengi ndani ya chuo cha I.F.M wakaanza kuuawa jambo ambalo likaanzisha wasiwasi kwamba kulikuwa na msichana jini ambaye alikuwa akiwaua vijana hao. Mauaji yote ambayo yalikuwa yakifanyika, yalikuwa yakifanyika ufukweni. Ndani ya miezi mitatu, vijana sita tayari walikuwa wameuawa huku polisi wakiwa hawajui ni nani hasa alikuwa nyuma ya mauaji hayo.
Hali ikaonekana kuzidi kutisha, wavulana wa chuo cha I.F.M wakazidi kuogopa zaidi na zaidi bila kujua ni kwa namna gani ambayo walitakiwa kuepukana na vifo hivyo ambavyo wala chanzo chake hakikuwa kikijulikana. Ulinzi na upelelezi ukaimarishwa zaidi, wanachuo wakaanza kutembea kimakundi makundi ili kuepukana na wauaji ambao walikuwa wakiendelea kufanya mauaji kwa vija wa chuo kile.
“Sasa nani anahusika na vifo hivi?” Masatu, raisi wa chuo hicho aliwauliza wanachuo wenzake huku akionekana kukasirika.
“Labda kuna jini mwanamke ambalo linafanya mauaji” Mwanachuo mmoja alisikika akisema.
“Jini? Hainiingii akilini. Toka lini jini akaua kwa kumchoma mtu kwa kisu?” Masatu aliuliza.
“Sasa unafikiri hapo atakuwa nani? Au mapolisi wamesemaje juu ya hili?”
“Hawajasema chochote zaidi ya kusema upelelezi bado unaendelea kufanyika”
“Na utakwisha lini huo upelelezi?”
“Bado hatujajua”
Wanachuo walikuwa wakiendelea kuogopa kupita kawaida, mauaji ambayo yalikuwa yakiendelea kwa wanafunzi wa chuo hicho yalionekana kuwatisha kupita kawaida. Chanzo cha mauaji yale wala hakikuwa kikijulikana kabisa jambo ambalo likawapelekea watu wengi kutojua kama nao walikuwa njiani kuuawa au la.

Hahaha! Mambo yamezua mambo.
Huyu Anko ni muuza madawa ya kulevya mwenye fedha ambaye hataki hata kusalitiwa, anaua kila anaposalitiwa huku akijua kila mwenye binti mzuri lazima watu wamtolee macho.
Je nini kitaendelea?
Je uaminifu wa Manka utaendelea?
Je Anko ataweza kumuua kila atakayetembea na Manka?
Hebu chukua nafasi hii kutabiri halafu tuone nani atapatia.
Unaionaje hadithi? Hii hadithi ndio nilitaka iwe kitabu ambacho nilitaka kutoa mwaka huu mwezi wa tatu ila ikashindikana. Ipo vipi? Je ilifaa kuwa kitabu? Je ungejuta kutoa fedha yako?
Hadithi haikatishwi...itaendelea mpaka mwisho tuone mwisho wa Yusufu, Anko na binti mrembo, mwanachuo Manka.
Kama unaona mpaka tunafika sehemu ya 19 haujawahi kuLIKE, fanya hivyo leo ili nijue ni wangapi wanaikubali hadithi hii kwani kama ina watu wachache wanaoifuatilia, itaweza kukatishwa kitu ambacho huwa sipendi kitokee, napenda hadithi ipate kampani kubwa na itolewe yote.

Itaendelea saa nne usiku.
 
MTUNZI: NYEMO CHILONGANI.
MAHALI: DAR ES SALAAM.
SIMU: 0718 069 269.

NITAKAPOKUFA 20

Kijana mwenye akili nyingi, Emmanuel Kihampa alikuwa akiteremka kutoka garini mwake aliloliegesha nje ya eneo la chuo hicho na kisha kuanza kupiga hatua kuelekea katika geti la kuingilia chuoni humu. Miwani yake ya macho ilikuwa machoni mwake, saa yake ya thamani pamoja na bengi lililokuwa na laptop yake vilikuwa mikononi mwake. Mwendo wake wala haukuwa wa haraka haraka, alikuwa akipiga hatua kulifuata geti la kuingilia chuoni humo.
Mara baada ya kulifikia geti, akaonyesha kitambulisho chake kwa walinzi waliokuwa pale getini na kisha kuingia ndani ya eneo la chuo kile. Emmanuel alikuwa akiangalia huku na kule kana kwamba alikuwa akimtafuta mtu fulani siku hiyo. Siku hiyo, kwake ikaonekana kuwa siku nzuri, siku ambayo alikuwa akijiona kwamba aliamka vizuri kuliko siku nyingine.
Mara baada ya kuingia darasani, akajiweka kitini na kumsubiria mfundishaji aingie darasani humo. Darasa lilikuwa kimya, wanachuo wengine wakaonekana kuwa bize kujisomea katika kipindi hicho, kwa Emmanuel, hakujisikia kusoma kabisa kwani kwa wakati huo kichwa chake kilikuwa kikimfikiria msichana Manka tu.
Uzuri wa Manka ulikuwa umemchanganya sana Emmanuel kiasi ambacho kwake alionekana kama kuwa mwanaume sahihi ambaye alikuwa ameandaliwa kuwa na msichana huyo ambaye alikuwa akivutia sana chuoni hapo. Kitendo cha kupenda kuangalia sana na Manka katika mtazamo wa kimahaba ndio ambao ulionekana kumchanganya sana Emmanuel na kumpa uhakika kwamba msichana yule ambaye alikuwa akimpenda sana, nae alikuwa akimpenda kama ambavyo alivyokuwa akipenda.
Kila wakati macho yake yalikuwa yakiangalia saa yake, katika kipindi hicho alikuwa na presha kubwa ya kumuona Manka, msichana ambaye alikuwa na mapenzi yake ya dhati. Kiti cha Manka kilikuwa wazi darasani mule hali iliyomaanisha kwamba hakuwa amefika chuoni hapo katika muda huo. Ilipofika saa 8:11, msichana Manka akaanza kuingia darasani humo.
Kwanza harufu ya manukato ambayo alikuwa amejipulizi ndio ambayo yakamshtua Emmanuel kutoka katika lindi la mawazo ambalo alikuwa nalo. Alikuwa akiitambua sana harufu ya manukato ambayo alikuwa akijipulizia Manka, yalikuwa ni manukato ya kike ambayo yalikuwa yakiuzwa kwa bei ya gharama kubwa sana dukani. Emmanuel akayageuza macho yake nyuma, Manka alikuwa akipiga hatua kuelekea katika kiti chake.
Muda wote huo Emmanuel alikuwa akimwangalia Manka, siku hiyo alionekana kuwa tofauti sana katika uwepo wa macho yake, alikuwa akivutia zaidi ya siku nyingine. Darasa zima likatawaliwa na harufu ya manukato ambayo alikuwa amejipulizia Manka mwilini mwake. Emmanuel hakutaka kubaki sana kitini mwake, alichokifanya ni kuinuka na kisha kuanza kumfuata Manka na kukaa juu ya meza yake.
“Mambo” Emmanuel alimsalimia huku akiachia tabasamu.
“Poa. Karibu” Manka alimwambia Emmanuel huku nae akirudisha tabasamu pana ambalo lilionekana kuuongeza uzuri wake machoni mwa Emmanuel.
“Unakumbuka ulichoniambia jana?” Emmanuel alimuuliza.
“Kitu gani?”
“Nilijua tu ungesahau”
“Lakini si uniambie”
“Inawezekana labda hakikuwa muhimu”
“Sidhani”
“Labda kwa sababu mimi sio mtu muhimu kwako”
”Si kweli”
“Sasa kama nimekuwa miongoni mwa watu muhimu, kwa nini ukisahau nilichokwambia na ulichoniambia?”
“mambo mengi sana Emmanuel. Nisamehe kwa hilo” Manka alimwambia Emmanuel.
“Usijali”
“Naomba unikumbushe uliniambia nini”
“Kwamba nilikuwa nataka nikutoe chakula cha mchana leo”
“Sawasawa. Nimekumbuka. Usijali”
“Kwa hiyo fresh?”
“Yeah! Usijali”
“Basi poa. Ngoja nikitoka nikimbilie ATM kabisa” Emmanuel alisema huku akionekana kuwa na furaha na kisha kurudi kitini mwake.
Emmanuel alionekana kufurahia kupita kawaida, siku hiyo, kwake ikaonekana kuwa siku moja nzuri sana na ya furaha kupita kawaida. Kitendo cha Manka kukubali kumtoa mtoko kwa ajili ya chakula cha mchana kikaonekana kumfurahisha kupita kawaida kwa kuona kwamba kila kitu kilikuwa kinakwenda kukamilika huko huko.
“Tutakwenda kama marafiki. Tukirudi tayari tutakuwa wapenzi” Emmnuel alijisemea moyoni.
Siku hiyo ikaonekana kuwa tofauti na siku nyingine chuoni hapo, kitendo cha kupewa uhakika kwamba Manka alikuwa tayari kwenda kula chakula cha mchana pamoja nae kikaonekana kumfurahisha kupita kawaida. Siku hiyo, dakika kwake zilionekana kwenda taratibu sana kiasi ambacho mpaka akawa anashangaa yeye mwenyewe.
Ilipofika saa sita kamili, wakatoka darasani na hivyo Emmanuel kumchukua Manka na kisha kuanza kwenda nae katika mghahawa uliokuwa Posta mpya, Kingstone na kisha kuanza kupata nae chakula cha mchana.
Muda mwingi macho ya Emmanuel yalikuwa yakimwangalia Manka ambaye kwake kwa siku hiyo alionekana kuwa mrembo zaidi na zaidi. Katika macho yake, Manka alionekana kuwa kama malaika ambaye alikuwa ameshushwa katika dunia hii kwa bahati mbaya, na kama ilikuwa si bahati mbaya, basi alikuwa ameshushwa kwa ajili yake.
“Mbona unaniangalia hivyo?” Manka alimuuliza Emmanuel huku akitabasamu.
“Uzuri wako unanichanganya sana” Emmanuel alimjibu Manka.
“Hahaha! Aya bwana. Nimekwishazoea kusikia maneno hayo mdomoni mwako” Manka alimwambia Emmanuel.
“Ila nadhani leo unayasikia katika hali ya tofauti sana” Emmanuel alimwambia Manka.
“Kivipi?”
“Leo nipo serious sana”
“Mbona naona upo kawaida sana”
“Hapana. Leo nipo serious. Ni muda mrefu sana nimekwambia kwamba ninakupenda. Hivi kwa nini hautaki kunielewa?” Emmanuel alimuuliza Manka.
“Sikuelewi au hatuelewani?”
“Haunielewi”
“Hapana. Sema hatuelewani”
“Kivipi?”
“Ni mara ngapi na wewe nimekwambia kwamba tayari nina mtu? Ulinielewa kweli?” Manka alisema na kumuuliza Emmanuel.
“Nafahamu uliniambia ila sidhani kama kuwa na mtu wako kutanifanya niache kukwambia kwamba nakupenda, sidhani kama kuna siku nitakaa kimya nisikwambie maneno haya” Emmanuel alimwambia Manka.
“Umechelwa mno Emmanuel”
“Vizuri. Ila utaweza kunifikiria vipi mimi?”
“Kivipi?”
“maisha bila wewe”
“Mbona kawaida sana. Kwani ulikuwa ukiishi vipi bila mimi?”
“Hiyo ilikuwa kabla”
“Utaweza tu Emmanuel. Halafu kwangu, nakuchukulia kama rafiki. Naomba na wewe unichukulie hivyo hivyo” Manka alimwambia Emmanuel.
Moyo wa Emmanuel ukanyong’onyea kupita kiasi. Hakuamini kile ambacho alikuwa amekisikia kutoka mdomoni mwa Manka, msichana ambaye alikuwa akimpenda zaidi ya msichana yeyote katika kipindi hicho. Macho yake wala hayakubanduka usoni mwa Manka, aliendelea kumwangalia zaidi na zaidi huku bado akiwa na hamu ya kutaka kukubaliwe kile ambacho alikuwa akikihitaji.
“Kwa hiyo unataka kunichukulia kama kaka yako na mimi nikuchukulie kama dada yangu?” Emmanuel alimuuliza Manka.
“Yeah! Itakuwa vizuri sana”
“Nitaweza vipi kumchukulia kama dada yangu mtu ninayempenda?” Emmanuel aliuliza.
“Wakati mwingine yakupasa kujitahidi tu. Haijalishi kama utaweza au hautoweza”
“Nitashindwa”
“Basi yakupasa kutokunifikiria kabisa katika moyo wako kwani naamini kwamba sitoweza kuwa sehemu ya maisha yako kama mpenzi” Manka alimwambia Emmanuel.
Maneno yale ya mwisho ndio yakawa msumali mkubwa wa mwisho uliokuwa wa moto ndani ya moyo wa Emmanuel. Machoni mwake akaanza kuyahisi machozi yakianza kumlenga, maneno yale yalimuumiza kupita kawaida. Mtu ambaye alikuwa akimpenda sana na kumuhitaji, leo hii alikuwa mbele yake akiongea nae huku akitaka kumchukulia kama dada yake kwani asingeweza kuwa sehemu ya maisha yake kama mpenzi.
Emmanuel hakutaka kuendelea kubaki mahali hapo, alichokifanya kwa wakati huo ni kumwambia Manka waondoke mahali hapo. Wakatoka na kisha kulifuata gari na kuondoka mahali hapo. Muda wote ndani ya gari, Emmanuel alikuwa kimya, kichwa chake kwa wakati huo bado kilikuwa kikiyafikiria maneno ambayo alikuwa ameyaongea Manka mbele ya macho yake.
“Huu ni mwanzo tu, siku zote wanawake mioyo yao huwa myepesi” Emmanuel alijisemea moyoni mwake.
****
Yusufu alikuwa akiendelea kupata skendo mbaya kwamba alikuwa akiwaambukiza wasichana warembo ugonjwa wa UKIMWI jambo ambalo alikuwa akilipinga kila siku. Skendo zile hazikuisha, kila siku watu walikuwa wakizungumza mengi na menhine mapya kuzidi kuibuka zaidi na zaidi. Katika kipindi hicho, Yusufu hakutaka kukaa kimya tena, alichokifanya ni kuwafuata waandishi wa habari na kisha kuwaonyeshea ile karatasi ambayo ilikuwa na majibu yake.
Kila mmoja akaonekana kushangaa, hawakuamini kama Yusufu alikuwa hajaathirika na ugonjwa ule na wakati kila kona habari zilikuwa zimesambaa kwamba alikuwa ameathirika. Hapo ndipo Yusufu alipowaambia waandhsi wale wa habari juu ya hatua za upimaji wa hiyari ambao alikuwa ameuchukua tena ikiwa mbele ya Waziri wa Afya, bwana Mkude.
“Kwa sababu nyie ndio mlioandika habari juu ya kuathirika kwangu, basi nanyi pia inabidi mtoe taarifa kwamba sijaathirika kama majibu yanavyoonyesha” Yusufu aliwaambia waandishi wale wa habari.
“Sisi tuliandika kutokana na tetesi ambazo zilikuwa zikisikika mitaani” Mwandishi John alimwambia Yusufu.
“Sawa. Ukweli wenyewe ndio huu. Utoeni” Yusufu aliwaambia.
Siku mbili zilizofuata, magazeti mengi ya udaku yakaanza kuandika kuhusiana na hali ya Yusufu ambayo alikuwa nayo katika kipindi hicho. Karatasi ile ambayo ilikuwa na majibu yake ikatolewa katika magazeti hayo jambo ambalo watu wakaonekana kushangazwa. Damu ya Yusufu ilikuwa safi kiasi ambacho kila mtu alikuwa amepigwa na mshangao. Tetetsi zile zilizosema kwamba alikuwa ameathirika zikawekwa kapuni na kuonekana skendo mbaya ambazo zilikuwa zimeanzishwa kwa lengo la kumchafua tu.
“Wabongo sasa tumezidi” Msichana mmoja aliwaambia wasichana wenzake huku akiwa ameshika moja ya magazeti ambayo yalikuwa yametoa taarifa kuhusiana na majibu ya damu ya Yusufu.
“Tumezidi kwa lipi?”
“Majuzi juzi tu waliandika kwamba kuna uwezekano Yusufu akawa ameathirika” Msichana yule alimwambia.
“Kwani uongo?”
“Uongo. Si unaona leo wametoa kwamba hajaathirika na majibu yake haya hapa” Nsichana yule alisema huku akimuonyeshea gazeti lile.
“Mmmh! Au ya kutengeneza”
“Iweze yawe ya kutengeneza na wakati zoezi limesimamiwa na Waziri wa Afya, Bwana Mkude?”
“Kama ni hivyo, basi kweli tumezidi”
Kila mtu ambaye alikuwa akiiona taarifa ile alikuwa akiwashangaa waandishi wa habari mambo ambayo walikuwa wame=yaandika katika kipindi cha nyuma kwamba Yusufu alikuwa ameathirika. Japokuwa zile zilikuwa ni tetesi ambazo hazikuwa na uhakika, lakini hawakupaswa kutoa katika vyombo vya habari mpaka pale ambapo wangehakikisha juu ya kile ambacho kilikuwa kikiendelea kusikika mitaani. Kuanzia hapo, wasichana wote ambao walikuwa wakisema kwamba walikuwa wametembea na Yusufu au The Ruler kama alivyojulikana na wengi, wakaonekana kudanganya kwa kutaka kumchafua msanii huyo ambaye uwezo wake ulikuwa ukizidi kupanda juu.
Kuanzia hapo, nyota ya Yusufu ikazidi kung’aa zaidi huku wapenzi wengi hata wale ambao hawakuwa wakimpenda kuanza kumpenda. Yusufu akaonekana kuwa na bahati katika maisha yake, idadi kubwa ya mashabiki ambayo alikuwa nayo katika kipindi hicho ilimfanya kuwa juu zaidi na zaidi. Mara kwa mara alikuwa akitoka nchini tanzania na kuelekea katika nchi mbalimbali za Afrika na kusfanya matamasha ambayo yalikuwa yakimuingizia fedha nyingi sana.
Kwa wakati huo, jina lake likawa kubwa kupita kawaida, mkataba wa kuiuza nafsi yake ukaonekana kumnyooshea mambo yake yote. Hapo, hakutaka kuvunja masharti tena, mara kwa mara alikuwa akizivaa zile pete ambazo alikuwa akiambiwa azivae pamoja na kuvaa fulana ambazo alikuwa akiambiwa azivae katika kipindi ambacho alikuwa jukwaani akiimba. Pete zile pamoja na fulana zile zile ambazo alikuwa akizivaa ndizo ambazo ziliyarubuni macho ya watu kwa kuona kwamba alikuwa akifanya vizuri sana jukwaani kuliko wasanii wote wa muziki.
Kutokana na biashara zake ambazo alikuwa akizifanya pamoja na muziki, Yusufu alikuwa akiingiza zaidi ya milioni sabini kwa mwezi jambo ambalo likamfanya kuwa msanii ambaye alikuwa akiingiza kiasi kikubwa cha fedha. Yusufu hakuishia hapo, bado aliendelea kujenga nyumba mbalimbali, nyumba nzuri na za kifahari pamoja na kufungua biashara nyingine nyingi ambazo ziliendelea kumuingizia kiasi kikubwa cha fedha. Miaka miwili ya mafanikio yake, alikuwa amefanya mambo mengi na makubwa ambayo wala hakukuonekana kama kungetokea msanii yeyote kufanya mambo makubwa kama aliyokuwa ameyafanya.
Wakenya hawakuonekana kuridhika, mara kwa mara walikuwa wakimuita Yusufu kwa ajili ya kutumbuizia sehemu mbalimbali nchini humo. Katika kipindi hiki ndicho kilikuwa kipindi ambacho Wakenya walikuwa wakisherehekea sikukuu ya Uhuru ambayo walipangwa wasanii mbalimbali kwa ajili ya kutumbuiza siku hiyo. Ingawa viongozi walikuwa wakiwataka wasanii wa Kenya peke yao kutumbuiza lakini watu wengi wakaanza kulilia kwamba ilikuwa ni lazima Yusufu awepo katika sherehe hizo ili wapate burudani kutoka kwa msanii huyo.
Hakukuwa na mtu ambaye alibisha, mara moja mawasiliano kati ya Waziri wa Mambo ya Ndani na Nje, Bi Agness na Yusufu yakaanza kufanyika na hivyo Yusufu kutakiwa kuelekea nchini kenya kwa ajili ya kufanya shoo katika sikukuu ya Uhuru nchini humo ambayo ilitarajiwa kufanyika baada ya siku mbili. Yusufu akaanza kufanya maandalizi ya nyimbo mbalimbali ambazo alitarajiwa kuzifanya siku hiyo na kisha kuanza kuelekea siku iliyofuata kuanza kuelekea uwanja wa ndege.
“The Ruler...!” Ilisikika sauti ya msichana mmoja ambaye alimuita Yusufu.
Japokuwa Yusufu alikuwa amevaa miwani ya jua pamoja na kofia lakini msichana yule akaonekana kumtambua Yusufu. Watu wote ambao walikuwa katika maeneo ya uwanja wa ndege wakageuka na kumwangalia msichana yule ambaye alikuwa akimfuata Yusufu aliyekuwa amesimama na Kelvin ambaye alikuwa akiondoka nae siku hiyo. Msichana yule aliendelea kupiga hatua mpaka pale alipomfikia.
“Mambo vipi!” msichana yule alimsalimia Yusufu.
“Poa mrembo. U mzima?”
“Nipo poa”
Yusufu akaonekana kutokuridhika kiasi ambacho kikamfanya kuvua miwani yake. Macho yake yalikuwa yakimwangalia msichana yule kwa mshangao. Msichana yule alionekana kuwa mrembo kupita kawaida. Japokuwa katika maisha yake alikuwa amekutana na wasichana wengi lakini kwa msichana yule, Yusufu alijihisi akitetemeka. Msichana huyo alikuwa mrembo ambaye alikuwa amekamilika katika kila idara. Macho yake yalikuwa ni macho mazuri ambapo kama ungemwangalia kwa haraka haraka basi ungejua kwamba alikuwa akisikia usingizi.
Sura yake ilikuwa ni ya kitoto huku akionekana kuwa na mvuto mkubwa. Yusufu hakuishia hapo, akaanza kushuka chini. Kiunoe chake kilikuwa kimeumbika vizuri huku akiwa amevaa fulana ambayo iliruhusu kitofu chake kuonekana. Yusufu akabaki akikiangalia kitofu kile kwa sekunde kadhaa, aliyahisi mapigo yake yakiongeza kasi ya udundaji.
“Nimefurahi sana kuonana na wewe” Msichana yule ambaye alijitambulisha kwa jina la Manka alimwambia Yusufu.
“Nimefurahi kukuona pia. Na wewe pia ni msafiri?” Yusufu alimuuliza msichana yule.
“Hapana. Nimekuja kumsindikiza baba ambaye anaondoka kuelekea Mbeya kwenye msiba wa babu” Manka alijibu huku akitoa tabasamu pana ambalo lilimchanganya sana Yusufu.
“Kwa nini usingeenda nae sasa? Au ulikuwa haumpendi babu?” Yusufu aliuliza huku muda wote akiliruhusu tabasamu lake kuonekana.
“Nilikuwa nampenda, ila si unajua masomo”
“Kumbe unasoma! Unasoma wapi?”
“Nipo hapo IFM”
“Ok! Nimefurahi kukuona”
“Hata mimi. Naomba nipige nawe picha” Manka alimwambia Yusufu.
“Usijali” Yusufu alijibu.
Manka akachukua kamera yake na kisha kumpa Kelvin ambaye aliichukua na kisha kusimama karibu na Yusufu na kisha kupiga picha pamoja. Watu walikuwa wakiwaangalia tu, kwa jinsi ambavyo uzuri wa Manka ulivyokuwa, kila mmoja alimuona Yusufu kwenda kufaidi. Mara baada ya picha kadhaa kupigwa, Yusufu hakutaka kulaza damu, alichokifanya ni kumuomba namba ya simu Manka ambaye huku akionekana kuwa na furaha, akampatia Yusufu namba ya simu yake.
“Poa Manka. Nikirudi kutoka Kenya nitakutafuta” Yusufu alimwambia Manka.
“Usijali. Utanipata tu. Asante kwa namba yako”
“Usijali. Siku njema” Yusufu alimwambia Manka na kisha kuanza kuondoka pamoja na Kelvin.
“Kwa hiyo na huyu nae unataka umvue sketi?” Kelvin alimuuliza Yusufu.
“Ukitaka kuulizia makofi polisi, unaweza kupata kipigo. Hilo ni jibu, cha msingi, pigia mstari” Yusufu alimwambia kelvin huku wakielekea sehemu ambayo walikuwa wakihitajika kama wasafiri.

Je nini kitaendelea?
Je Anko atajua kinachoendelea?
Na akijua nini kitatokea?
Tukutane kesho.
 
MTUNZI: NYEMO CHILONGANI.
MAHALI: DAR ES SALAAM.
SIMU: 0718 069 269.

NITAKAPOKUFA 21

Siku ya sikukuu ya Uhuru wa nchi ya Kenya ndio ilikuwa imefika. Watu wengi zaidi ya elfu sitini walikuwa wamekusanyika katika uwanja huo wa mpira ambao ulikuwa ukiingiza watu elfu sitini na tano. Idadi kubwa ya watu wale ndani ya uwanja huo hasa katika siku kama hiyo ikaonekana kumshangaza kila mmoja. Haikuwahi kutokea siku ambayo uwanja ule ulionekana kujaza sana hasa katika siku kama zile za Uhuru. Ila siku hiyo, watu walikuwa wamejaa kupita kiasi, kila wakati, jina la The Ruler ndilo ambalo lilikuwa likisikika midomoni mwa watu ambao walikuwa wamehudhuria katika uwanja huo.
Yusufu ndiye abaye alionekana kumvutia kila mtu mahali hapo, Yusufu ndiye ambaye alikuwa ameufanya uwanja ule kujaza kupita kawaida. Kila mtu ambaye alikuwa amefika katika uwanja huo, alikuwa akitaka kumuona Yusufu, msanii ambaye alikuwa kipenzi cha watu kwa wakati huo. Wasanii mbalimbali wa hapo Kenya wakaanza kutumbuiza kwa zamu katika kila kipindi ambacho walikuwa wakihitajika jukwaani hapo kwa ajili ya kutoa burudani tu.
Wasanii wengine waliokuwa wakitumbuiza katika sikukuu ya Uhuru nchini Kenya walionekana kupooza kupita kawaida kiasi ambacho watu hawakuwa wakiwashangilia kwa sana. Kila msanii ambaye alikuwa akipanda hapo jukwaani, alikuwa akijitahidi kuimba lakini hakukuwa na mtu ambaye alionekana kuhamasika zaidi. Wasanii wote wa Kenya wakaimba na mara baada ya kumaliza, Yusufu au The Ruler kama alivyokuwa akijulikana akakaribishwa katika jukwaa.
Uwanja mzima ukaripuka kwa shangwe, watu wale ambao walikuwa wakijisikia uchovu mwingi mwilini, uchovu wote ukawaisha na kuanza kuruka kwa furaha katika kipindi ambacho Yusufu alikuwa akipanda jukwaani. Kwa mbwembwe nyingi, Yusufu akaanza kuingia jukwaani hapo, uwanja mzima ukasimama na kuanza kuruka ruka kwa furaha.
Yusufu akaanza kutoa burudani mahali hapo. Watu wote ambao walikuwa wameingia ndani ya uwanja huo wakaanza kuruka ruka kwa furaha huku hata watu ambao walikuwa wakipita nje ya uwanja huo na kusikia kwamba The Ruler alikuwa uwanjani hapo akitumbuiza, watu wakakatisha safari zao na kisha kuingia ndani ya uwanja huo.
Katika kitu ambacho watu wengi hawakukiamini, hata viongozi mbalimbali wa nchi ambao walikuwa wamekaa katika jukwaa maalumu nao wakaanza kuruka ruka pamoja na watu wengine katika uwanja ule. Raisi, Kibaki ndiye ambaye alikuwa akiongoza msafara wa viongozi ambao walikuwa wakicheza katika jukwaa lile maalumu. Siku hiyo ikaonekana kuwa siku maalumu kwa Wakenya, siku hiyo ikaonekana kuwa siku maalumu kwa watu kupata bure kile ambacho hawakuwa wakikitarajia.
Kadri Yusufu alivyokuwa akiendelea kutumbuiza jukwaani, watu walikuwa wakiendelea kuruka ruka kwa furaha jambo ambalo likawafanya kutoka katika viti ambavyo vilikuwa vimezunguka uwanja huo na kuingia katikati na kuanza kucheza. Yusufu hakutaka kuimba jukwaani tu jambo ambalo likamfanya kuanza kuteremka na kujumuika uwanjani, Kila mtu ambaye alikuwa uwanjani pale alikuwa akitamani kumshika Yusufu. Kwao, Yusufu akaonekana kuwa kama nabii ambapo kama ulikuwa ukipata nafasi ya kumgusa basi kama ulikuwa na ugonjwa unapotea muda huo huo.
“Kuna siku mtaniabudu tu....Nimekwishakuwa mungu wenu mioyoni mwenu” Yusufu alijisemea huku akiwaambia watu wanyooshe mikono juu.
Siku hiyo Yusufu akaonekana kuweka rekodi ya kuujaza uwanja huo. Watu hawakuizungumzia sikukuu ya Uhuru bali walikuwa wakizungumzia kuhusiana na jinsi Yusufu alivyoweza kuwakonga nyoyo zao. Mara baada ya kufanya kila alichotaka kufanya, akaomba kurudi Tanzania kwani kulikuwa na kazi ambayo alikuwa akitakiwa kuifanya kwa haraka sana.
“Ila si wamesema rais anakuhitaji Ikulu kwa ajili ya kula chakula cha usiku?” Kelvin alimuuliza Yusufu mara baada ya kuambiwa kwamba jioni ya siku hiyo ilitakiwa kurudi Tanzania.
“Namuwahi mtoto aiseee” Yusufu alimwambia Kelvin.
“Mtoto gani? Mtoto wako, Nasri?”
“Hapana. Mtoto wa uwanja wa ndege”
“Unamaanisha Manka?”
“Ndio”
“Yaani huyo ndiye anakufanya hata kuikataa ofa ya kuingia Ikulu ya Kenya na kula chakula cha usiku na rais?” Kelvin aliuliza huku akionekana kushtuka.
“Ndio maana yake. Muda wote nimekuwa nikimfikiria huyu mtoto Manka” Yusufu alimwambia Kelvin.
“Sasa Manka na Rais nani muhimu?”
“Muhimu Manka na ndio maana tunarudi Tanzania”
“Ila Manka si yupo?”
“Na hata raisi nae si yupo? Tatizo lipo wapi tena?”
“Kuna tatizo hapo Yusufu”
“Hakuna tatizo. Raisi ni binadamu wa kawaida sana. Achana nae. Kwanza naweza kwenda huko nikavutiwa na mkewe na kisha kutembea nae. Tuwaachie chakula chao, kama na wewe shida yako ni chakula, niambie twende kwenye hoteli gani Tanzania tule chakula ukipendacho. Na kama shida yako ni kula pamoja na Raisi, nitamwambia rais wetu atuandalie chakula cha usiku pamoja nae Ikulu tukale wote” Yusufu alimwambia Kelvin.
Kama alivyoamua ndivyo ambavyo alitaka iwe. Kwake, kula chakula cha usiku Ikulu pamoja na rais na viongozi mbalimbali wa Kenya halikuonekana kuwa jambo muhimu kwake, kitu ambacho alikuwa akikitaka kwa wakati huo ni kuonana na msichana mrembo ambaye alikuwa amekutana nae uwanja wa ndege, Manka. Tayari katika kipindi hicho msichana huyo akaonekana kuuteka sana moyo wake, hakutaka kumuona akipita hivi hivi bila kutembea nae. Kwa kila alivyokuwa akimkumbuka jinsi alivyokuwa, alikuwa akijipa kila sababu za kutembea nae.
“Nikifika tu, jambo la kwanza kuonana nae hotelini” Yusufu alimwambia Kelvin huku wakiwa tayari wapo ndani ya ndege.
“Mbona haraka haraka hivyo Yusufu. Hotelini kote kufanya nini na wakati bado mapema?” Kelvin aliuliza.
“Hotelini kufanya nini tena?”
“Yeah! Au unaanza na stori za hapa na pale”
“Hakuna stori. Nipige nae stori kwani yeye dada yangu? Huko ni mwendo wa kazi tu” Yusufu alimwambia Kelvin.
“Ila kuwa makini bwana. Usikione kila king’aacho ni dhahabu”
“Najua kwamba mengine huwa mabati. Basi tufanye Manka ni bati halafu hilo hilo bati linafanana na dhahabu. Hata kama wewe hutapeliwi maeneo ya Manzese?” Yusufu aliuliza huku uso wake aionyesha tabasamu.
“Tatizo lako maneno mengi”
“Na wewe tatizo lako ushauri mwingi kama Angaza” Yusufu alimwambia Kelvin.
Ndege ilipotua uwanja wa ndege hawakutaka kuendelea kukaa zaidi, walichokifanya ni kutoka nje ya uwanja ule ambapo Papaa Pipo kama kawaida yake alikuwa amekuja kuwapokea na kisha kuondoka uwanjani hapo. Muda wote huo Yusufu alikuwa akimfikiria Manka, hakujua angejisikiaje kama angepata nafasi ya kutembea na msichana huyo ambaye kwake alionekana kuwa mrembo kupita kawaida.
****
Emmanuel alikuwa chumbani kwake akisoma notes zake ambazo zilikuwa katika kompyuta yake ya mapajani, akili yake alikuwa ameituliza kimasomo kwa wakati huo japokuwa akili yake kwa wakati mwingine ilikuwa ikimfikiria Manka ambaye bado moyo wake ulikuwa ukimpenda kupita kawaida. Alikuwa akisoma lakini kila alipokuwa akipumzika, alikuwa akimfikiria Manka ambaye alitoka kula nae chakula katika siku hiyo.
Bado moyo wake haukutaka kumsahau Manka, mara nyingi alikuwa akiishika simu yake na kisha kutaka kumpigia Manka lakini moyo wake ulikuwa ukisita kufanya hivyo. Emmanuel aliendelea kukaa katika hali hiyo mpaka pale ambapo aliamua kuzifunga notes zake zile alizokuwa akizisoma na kisha kuanza kuangalia picha kadhaa za Manka ambazo zilikuwa katika kompyuta yake.
Huku akiendelea kuangalia picha zile, mara akasikia mlio mlio wa meseji ukiwa umeingia katika simu yake, alichokifanya ni kuupeleka mkono katika simu yake ambayo ilikuwa pembeni ya kitanda kile na kisha kuichukua na kuanza kuliangalia jina la mtu ambaye alikuwa amemtumia meseji hiyo katika usiku huo wa saa nne. Emmanuel hakuonekana kuamini, jina la Manka lilikuwa likionekana katika kioo cha simu yake, kwa haraka haraka, akaifungua meseji ile.
‘NAOMBA TUKUTANE NJOMBE ROYAL HOTEL, UBUNGO SAA TANO LEO USIKU’ Hiyo ilikuwa jinsi meseji ile ilivyokuwa ikisomeka.
Emmanuel akashtuka, hakuamini kama angeweza kutumiwa meseji ile na Manka, alichokifanya kabla ya kuifunga meseji ile ni kuanza kuisoma zaidi na zaidi, aliisoma zaidi ya mara kumi na ndipo akaifunika. Emmanuel hakutaka kuchelewa, japokuwa mara kwa mara alikuwa akichelewa sana katika sehemu ambazo alikuwa akihitajika lakini siku hiyo hakuonekana kuwa radhi kuchelewa kule ambapo alikuwa ameitwa na Manka, alichokifanya ni kuinuka kutoka pale kitandani, akaingia bafuni haraka haraka na kisha kuanza kuoga.
Moyo wake haukuamini kama kweli usiku ule alikuwa amepokea meseji kutoka kwa Manka, alijiona kama mtu ambaye alikuwa akiota ndoto fulani yenye furaha katika maisha yake. Tofauti na siku zote, siku hiyo alitumia muda mchache sana kuoga, alipomaliza akatoka na kuanza kujiandaa kwa kasi ya ajabu. Dakika nazo zilikuwa zikizidi kusonga mbele, alipoiangalia saa yake, ilikuwa saa 4:20 usiku. Alichokifanya mara baada ya kumaliza kujiandaa, akachomoka kutoka chumbani kwake na kuanza kuelekea nje.
“Unakwenda wapi usiku wote huu?” Mama yake, Bi Happy alimuuliza.
“Nimepigiwa simu na rafiki zangu mama” Emmanuel alijibu.
“Lakini haujanijibu swali langu”
“Nakwenda kwenye pati”
“Pati gani tena? Mbona haukusema toka mapema?”
“Nilijisahau. Nimepigiwa simu kukumbushwa kwamba nilikuwa nahitajika mimi tu” Emmanuel alidanganya.
“Sawa, nenda ila kuwa makini barabarani. Usiku huu, madereva wengi wanakuwa wamelewa” Bi Happy alimwambia Emmanuel.
“Usijali mama. Ila ningeomba kitu kimoja” Emmanuel alimwambia mama yake, Bi Happy.
“Kitu gani?”
“Gari lako”
“Gari langu! Lako lina nini?”
“Najua kwenye pati kutakuwa na watu wengi mama, halafu wanione nashuka kwenye Rav 4, haipendezi. Leo nataka nionekane tofauti. Niazime Prado lako” Emmanuel alimwambia mama yake.
“Hapana. Utapata nalo ajali kwa mambo yenu ya kutaka kukimbizana barabarani”
“Siko hivyo mama. Naomba uniazime, nazidi kuchelewa”
“Sawa. Kachukue ufunguo pale kwenye droo ya kitanda chumbani. Ila kumbuka kwamba yakupasa kuwa makini barabarani” Bi Happy alimwambia Emmanuel.
“Usijali” Emmanuel alimwambia mama yake na kisha kuanza kuelekea chumbani kwa mama yake ambapo akachukua ufunguo na kutoka.
“Kuna kingine mama”
“Kipi? Hela ya mafuta?”
“Hapana”
“Kumbe kipi?”
“Usimwambie baba kama nimekwenda kwenye pati”
“Kwa nini?”
“Nikija nitakwambia kwa nini, ila akiuliza mwambie nimekwenda kwa kina James kujisomea pamoja nae” Emmanuel alimwambia Bi Happy.
“Sawa. Nakukumbushia kwamba yakupasa kuwa makini barabarani”
“Usijali mama” Emmanuel aliitikia.
Emmanuel hakutaka kuendelea kukaa mahali hapo, alijiona kama alikuwa akichelewa. Akayapeleka macho yake katika saa yake ya mkononi, ilikuwa tayari imefikia saa 4:35 usiku. Moja kwa moja akaanza kupiga hatua na kulichukua gari la mama yake na kisha mlinzi kumfungulia geti na kutoka ndani ya eneo hilo.
Kila wakati Emmanuel alikuwa akiangalia saa yake, alijiona kama alikuwa akichelewa kufika pale ambapo Manka alikuwa akitaka kuonana nae kwa wakati huo. Kasi ambayo alikuwa akiitumia aliona kama ilikuwa ndogo vile hali ambayo ilimfanya kuongeza kasi zaidi na zaidi. Ilipofika saa 4:55, alikuwa amekwishafika katika hoteli hiyo ambapo akalipaki gari katika sehemu za maegesho na kisha kuteremka.
Akaanza kupiga hatua za haraka haraka kuelekea ndani ya eneo la kupata vinywaji huku macho yake yakiangalia huku na kule akimtafuta Manka ambaye hakuwa akimuona mahali hapo. Alichokifanya Emmanuel ni kuchukua simu yake na kisha kuanza kumpigia Manka, kwa wakati huu, simu ilikuwa ikiita tu.
“Pokea simu baby” Emmanuel alijisemea wakati simu ilipokuwa ikiita.
Simu ile iliita mpaka ilipokata. Emmanuel hakuonekana kujali, tayari alijua kwamba inawezekana kwamba Manka alikuwa ameiacha simu ile mahali fulani. Alichokifanya ni kuisogelea meza iliyokuwa jirani ambayo wala haikuwa na mtu na kisha kutulia kitini huku akimsubiria Manka. Emmanuel alikaa kwa dakika kadhaa, alichokifanya ni kuchukua simu yake tena na kisha kumpigia Manka. Simu ikaanza kuita kama kawaida, baada ya sekunde kadhaa, ikapokelewa na sauti ya Manka kusikika.
“Mambo vipi Emmanuel” Manka alisikika akimsalimia.
“Poa. Upo wapi wewe? Mbona sikuoni hapa?” Emmanuel aliuliza.
“Nipo nyumbani. Hunioni wapi?” Sauti ya Manka ilisikika ikiuliza.
“Si hapa Njombe Royal Hotel ulipotaka tukutane saa tano. Nimefika kitambo sana” Emmanuel alimwambia manka.
“Nimekwambia tuonane?” Sauti ya Manka ilisikika ikiuliza kwa mshangao.
“Wewe si umenitumia meseji na kuniambia kwamba tuonane mahali hapa?”
“Hapana Emmanuel. Utakuwa umechanganya namba”
“Mimi ni mtu mzima na akili timamu Manka. Siwezi kuchanganya namba. Ni wewe ndiye ambaye umenitumia meseji”
“Si mimi. Angalia vizuri” Manka alisema na kisha kukata simu.
Emmanuel akaanza kuangalia vizuri katika sehemu za meseji. Namba ilikuwa ni ya Manka kabisa, akaanza kuiangalia namba ile vizuri kabisa, ilikuwa ni namba ya Manka. Maswali mengi yakaanza kumiminika kichwani mwake kwamba kwa nini Manka alikuwa akikataa kwamba ile haikuwa namba yake ambayo ilitumika kutuma meseji ile? Kila kitu ambacho alikuwa akijaribu kujiuliza mahali hapo, alikosa jibu.
Huku akiwa hajui ni kitu gani ambacho alitakiwa kufanya kama kilikuwa ni kurudi nyumbani au kumpigia Manka simu na kumtaarifu kwamba namba ile ilikuwa ni yake, mara ghafla akajikuta akishikwa bega kwa nyuma, alipogeuka, walikuwa vijana wanne ambao walikuwa na miili iliyojazia. Emmanuel akaonekana kushtuka, hakuwa akiwafahamu watu wale ambao walionekana kufika mahali hapo kishari zaidi.
“Vipi tena?” Emmanuel aliuliza huku akionekana kuwa na wasiwasi.
“Inuka twende. Ukibisha, tunakuua” Kijana mmoja alisema kwa sauti nzito ambayo ilijaa utetemeshi.
Emmanuel hakubisha, alichokifanya ni kufanya kile ambacho vijana wale walimtaka kukifanya kwa wakati huo. Wakamchukua na kisha kuelekea katika gari lao na kisha kumuingiza ndani huku Emmanuel akionekana kuwa na hofu moyoni mwake kwa kuona kwamba alikuwa akienda kuuawa kwani muonekano wa watu wale wala haukuonekana kama ulikuwa muonekano wa amani.
“Wapi sasa?” Kijana mmoja ambaye alishikiria usukani aliuliza.
“Kama kawa. Kule kule kwa siku zote” Kijana mwingine alijibu huku Emmanuel akiwa katikati ya vijana wawili waliokuwa siti za nyuma.
“Coco Beach?”
“Pigia mstari” Kijana mwingine alisema maneno ambayo yalimfanya Emmanuel kugundua kwamba kulikuwa na uhakika kwamba vijana wale walikuwa miongoni mwa watu ambao walikuwa wakiwaua vijana wa chuo cha I.F.M na miili yao kukutwa katika ufukwe wa Coco.
****
Vijana waliokuwa wakimtaka Manka ambao walikuwa wakisoma katika chuo cha IFM bado walikuwa wakiendelea kuuawa jambo ambalo vyanzo vya vifo vyao wal havikuwa vikijulikana kabisa. Katika mipango ya kila kitu ambacho kilikuwa kikifanyika, mwanachuo, Urassa alikuwa akifahamu kila kitu. Urassa alikuwa akitumiwa na Anko kuwa kama mlinzi wa Manka chuoni hapo, kazi kubwa ya Urassa ilikuwa ni kumtaarifu Anko ni mvulana gani katika kipindi hicho alikuwa akimfuatilia Manka.
Urassa alikuwa akiifanya kazi kwa juhudi kubwa, kiasi cha milioni mbili ambacho alikuwa akilipwa kila baada ya mwezi kilionekana kuwa kiasi kikubwa cha fedha ambacho kilimfanya kuifanya kazi ile kwa moyo mmoja na uaminifu mkubwa. Yeye ndiye ambaye alikuwa akimpa Anko namba za simu za watu ambao walikuwa wakimfuatilia Manka na hivyo kila kitu kumalizwa na Anko ambaye alikuwa akiwaandaa vijana wake katika kufanya mauaji kwa vijana hao.
Anko alikuwa akimuamini sana Urassa kiasi ambacho wakati mwingine alikuwa akimpa marupurupu kama shukrani juu ya kazi ile ambayo alikuwa akiendelea kuifanya kwa nguvu zote. Urassa alikuwa akionyesha uaminifu mkubwa, kwa Anko, alijiona kupata kila kitu ambacho alikuwa akikihitaji kwa wakati huo.
“Unasemaje?” Anko aliuliza.
“Ndio hivyo. Yaani huyu jamaa, leo alimtoa out kula chakula cha mchana” Urassa alimwambia Anko.
“Muda gani?”
“Saa sita mchana baada ya masomo”
“Huyo kijana anaitwa nani?”
“Emmanuel Kihampa”
“Asante. Nitakutumia lakini tano kwenye akaunti yako ya simu baadae. Umenifurahisha kwa taarifa hiyo” Anko alisema na kisha kukata simu.
Anko alionekana kuchanganyikiwa, hakuamini kama kweli kungekuwa na kijana ambaye angediriki hata kumtoa mtoko msichana wake, Manka na kwenda kula chakula cha mchana. Akili yake haikukaa sawa siku hiyo, alichokifanya mahali hapo ni kuanza kuwasiliana na Manka kwamba angependa kuwa pamoja nae katika usiku huo ndani ya hoteli ya White Elephant iliyokuwa Msasani.
“Nitakuja” Manka alimwambia Anko simuni.
Usiku wa saa mbili walikuwa wote chumbani huku wakicheza michezo mbalimbali kama kupigana na mito pamoja na michezo mingine. Katika kipindi chote ambacho walikuwa wakicheza michezo hiyo, akili ya Anko ilikuwa ikifikiria jambo jingine kabisa, alichokuwa akikitaka ni kuichukua namba ya simu ya Manka na kisha kuangalia namba ya mtu aliyeitwa Emmanuel.
Waliendelea kucheza na kufanya mambo mengi mpaka pale ilipofika saa nne na ndipo Manka alipohitaji kwenda kuoga. Ingawa Manka alikuwa akitaka kuoga pamoja na Anko lakini siku hiyo Anko hakutaka kwenda kuoga nae, alitaka kubaki chumbani pale kwa ajili ya kufanya kitu kimoja ambacho kwake kilionekana kuwa muhimu, kuangalia namba ya Emmanuel.
Manka alipoondoka na kuelekea bafuni kuoga, kwa haraka haraka Anko akaichukua simu ya Manka na kisha kuanza kuangalia majina, akaanza kulitafuta jina la Emmanuel, alipoliona, akaandika meseji ya haraka haraka na kisha kuituma. Alipoona meseji ile imekwenda, akaifuta kabisa ili Manka asiweze kufahamu kitu chochote kile. Alipoona kila kitu kimekamilika, akawapigia simu vijana wake.
“Mmefika hapo Njombe Royal Hotel?” Anko aliwauliza.
“Ndio tunakata kona ya hapa Legho”
“Fanyeni haraka. Yule mjinga anaweza kuwa njiani kuwa mahali hapo” Anko aliwaambia.
Anko akatulia kitandani huku moyoni mwake akiwa ameridhika kwa kuona kwamba kila kitu kwa wakati huo kilikuwa kinakwenda kama ambavyo kilitakiwa kwenda. Mara baada ya dakika kadhaa, simu ya Manka ikaanza kuita tena, Anko akainyanyua simu ile na kuangalia mpigaji, alikuwa Emmanuel, wala hakuipokea, akairudisha pale kitandani huku akiwa ameifunika ili mwanga usionekane.
Baada ya dakika kadhaa, Manka akarudi chumbani pale na kisha kuanza kuelekea kitandani. Akapokelewa kwa mikono miwili na kisha kuanza kushikana shikana hapa na pale. Japokuwa Anko alionekana kuwa na furaha mahali hapo lakini akili yake ilikuwa ikifikiria kazi ambayo alikuwa amewapa vijana wake ambayo alitaka ifanyike kwa haraka sana kama ambavyo ilivyofanyika kwa watu wengine ambao walionekana kuwa na tamaa kwa Manka.
“Nenda kaoge mpenzi” Manka alimwambia Anko”
“Usijali” Anko alisema na kisha kuinuka kitandani hapo na kuchukua taulo na kisha kuelekea bafuni ambapo akaanza kuoga. Manka akabaki chumbani pale kitadani, mara akaisikia simu yake ikianza kuita, alichokifanya akaisogelea na kisha kuichukua na kuanza kuangalia kioo cha simu ile, mpigaji alikuwa Emmanuel, akaipokea na kuipeleka sikioni.
“Mambo Emmanuel......Nipo nyumbani...Hunioni wapi?...Nimekwambia tuonane?....Hapana, utakuwa umechanganya namba....Si mimi, angalia vizuri” Manka alisema na kisha kukata simu
Manka akabaki kimya kitandani huku akiiangalioa simu yake. Alionekana kutokumuelewa Emmanuel maneno yale ambayo alikuwa amemwambia kwa wakati ule kwamba walitakiwa kuonana. Alichokifanya ni kuanza kuangalia sehemu za meseji, hakukuwa na meseji yoyote ile ambayo alikuwa amemtumia Emmanuel wala kumpigia, hakuelewa ni sababu ipi ambayo ilimfanya Emmanuel kusema maneno yale kwamba walitakiwa kuonana.

Je nini kitaendelea?
Je Emmanuel atauawa?
Je nini kitaendelea kwa Manka na Yusufu?
Tukutane kesho.
 
MTUNZI: NYEMO CHILONGANI.
MAHALI: DAR ES SALAAM.
SIMU: 0718 069 269.

NITAKAPOKUFA 22

Bara baada ya kumaliza kazi zake za siku mbili, Yusufu akaanza kuwasiliana na Manka na kisha kuanza kuongea nae. Muda huo, Yusufu alionekana kuwa mwingi wa furaha, hakuamini kama msichana ambaye alikuwa amemvutia kupita kawaida, Manka alikuwa akiongea nae katika kipindi hicho. Waliongea kwa muda mwingi sana huku kila mmoja akisikika kuwa na furaha na kisha kupanga kuonana.
Kwa Manka ikaonekana kuwa kama tukio moja la ajabu na lenye furaha ambalo hakuwa amelitegemea katika maisha yake, hakuamini kabisa kama siku hiyo alikuwa akitakiwa kuwa meza moja pamoja na Yusufu, msanii mkubwa mwenye fedha ambaye alikuwa akiheshimika sana barani Afrika. Manka hakutaka kulaza damu, siku ambayo walipanga kuonana, alijitahidi kujipendezesha kuliko siku nyingine.
Siku ya kuonana ikatimia, Manka akavaa mavazi yake mapya ambayo alikuwa ameyanunua kwa ajili ya siku hiyo ambayo kwake ikaonekana kuwa muhimu sana. Japokuwa katika kipindi cha nyuma alikuwa amejiapiza kutokutembea na supastaa yeyote yule lakini siku hiyo kiapo chake kikaonekana kuvunjwa, Yusufu akaonekana kuwa mwanaume wa ajabu ambaye alikuwa amejaa mvuto mkubwa kupita kiasi.
Manka akalifuata gari lake ambalo alikuwa amenunuliwa na Anko na kisha kupanda na kuondoka mahali hapo. Muda wote ndani ya gari Manka alikuwa akionekana kuwa na furaha, hakuamini kama siku hiyo alikuwa njiani kwenda kumuona Yusufu, mwanaume ambaye alikuwa amevutiwa nae kupita kawaida. Baada ya dakika thelathini, Manka akalisimamisha gari lake katika hoteli ya La Vista Inn iliyokuwa Magomeni, hoteli ambayo Yusufu alikuwa akipenda sana kuitumia kwa ajili ya kulala na wasichana mbalimbali aliokuwa akitembea nao.
Mara baada ya macho ya Manka kutua kwa Yusufu, mvuto wa Yusufu ukaongezeka zaidi machoni mwake, akamuona Yusufu kuwa mwanaume mzuri kuliko wanaume wote ambao aliwahi kukutana nao katika dunia hii. Wote wakaanza kusogeleana na kisha kukumbatiana kwa nguvu kiasi ambacho kilimshangaza hata Yusufu mwenyewe.
“Unanukia vizuri” Manka alimwambia Yusufu.
“Hata wewe pia” Yusufu alimwambia Manka.
Mwili wa Yusufu kwa wakati huo ulikuwa umekwishabadilika kabisa, kitendo cha kukumbatiana na Manka kiliufanya mwili wake kusisimka kimapenzi kupita kawaida. Akashindwa kujizuia, japokuwa alikuwa akihitaji kukaa na Manka tu mahali hapo na kunywa pamoja na kula lakini kwa hali ya mwili wake ilivyobadilika, akaamua kuchukua chumba kitendo ambacho wala hakikupingwa na Manka.
Walipofika chumbani, Manka akajilaza kitandani. Yusufu akabaki akimwangalia Manka tu pale kitandani. Ni kweli kwamba mpaka katika kipindi hicho alikuwa amefanya ngono na wasichana wengi katika maisha yake lakini kwa Manka, alionekana kuwa msichana wa tofauti sana. Mvuto wa Manka ulikuwa mkubwa sana katika macho yake.
Yusufu hakutaka kusubiri, alichokifanya ni kuanza kuzivua nguo zake huku Manka akiwa amebaki kitandani pale akitabasamu tu. Alipoona amemaliza kuzivua nguo zake, akamsogelea Manka na kisha kuanza kumvua nguo zile alizokuwa amezivaa. Kwa mara ya pili toka waonane, hawakuwa wameongea neno lolote la kuonyesha kwamba walikuwa wakitakana, wakajikuta wakifanya mapenzi kwa mara ya kwanza.
Kwa kipindi hicho, Manka hakuwa akimfikiria Anko, Yusufu ambaye alikuwa juu ya kifua chake kwa wakati huo ndiye ambaye alionekana kuwa mwanaume sahihi. Kitanda kilikuwa kikilia tu huku kila mtu akitoa miguno yake. Kwa Manka wala hakuwa akifahamu kwamba mtu ambaye alikuwa akifanya nae mapenzi kwa wakati huo alikuwa ameathirika, mbaya zaidi walikuwa wakifanya ngono zembe, ngono ambayo wala mpira haukuwa ukitumika.
****

Mapenzi kati ya Manka na Yusufu yakaonekana kuanza kuchanganya, kila wakati walikuwa pamoja huku muda mwingi Manka akiwa na hamu ya kuwa na Yusufu ambaye alionekana kuwa kwenye mapenzi nae ya dhati. Yusufu hakutaka kuzificha hisia zake, alikuwa wazi kumwambia kila mtu kwamba kwa wakati huo alikuwa pamoja na Manka ambaye nae alikuwa akimpenda kwa dhati.
Watu ambao walikuwa wakipewa taarifa juu ya uhusiano ule wakaonekana kufurahia huku wengine wakionekana kukasirika. Uzuri wa Manka haukuonekana kama alistahili kuwa na Yusufu japokuwa walijua kwamba kijana huyo alikuwa mtu maarufu na mwenye fedha nyingi. Manka alionekana kustahili kuwa na mtu mwenye fedha lakini asiyekuwa maarufu kwani watu wengi ambao walikuwa maarufu hawakuonekana kuwa na mapenzi ya dhati.
Tetesi zile ambazo zilikuwa zikiendelea kusikika ndizo ambazo zilimfikia Anko ambaye alionekana kuchanganyikiwa kupita kawaida. Katika kipindi cha kwanza, Anko hakutaka kutilia maanani sana kile ambacho alikuwa amekisikia kutokana na kujua kwamba zile zilikuwa tetesi tu ambazo zilikuwa zikivuma, ila mara baada ya kuusikia wimbo ambao Yusufu alikuwa ameutunga kwa ajili ya mpenzi wake mpya, Manka, hapo ndipo alipopata uhakika kwamba tetesi zile hazikuwa tetesi tu bali lilikuwa jambo la kweli ambalo lilikuwa likiendelea.
Moyo wake ukaumia kupita kawaida, aliuhisi ukiwa umepigwa na msumali mkubwa wa moto, tena ukiwa msumali ambao ulikuwa na ncha kali. Mawazo yakaanza kujaa kichwani mwake, hakuonekana kuamini kile ambacho alikuwa akikisikia katika wimbo ule ambao alikuwa ameutunga Yusufu kwa ajili ya mpenzi wake, Manka.
Anko hakutaka kukubali, alichokifanya ni kuanza kumtafuta Manka ili apate kujua ukweli juu ya kile ambacho kilikuwa kikiendelea. Simu ya Manka ilikuwa ikiita kila siku lakini wala haikuwa ikipokelewa. Anko akaanza kujuta moyoni, hakujuta juu ya fedha ambazo alikuwa amezitumia kwa ajili ya Manka au vitu mbalimbali ambavyo alikuwa amempa, alikuwa akijuta kutokana na muda wake ambao alikuwa ameupoteza, muda ambao alikuwa ameutumia kumpenda Manka na kumthamini.
Anko hakuonekana kukubali kwa wakati huo, alijiona kwamba kila kitu kilikuwa kimekwenda tofauti na jinsi alivyopanga, aliona kulikuwa na kila sababu ya kuirudisha furaha ambayo ilikuwa imepotea moyoni mwake katika kipindi hicho. Hakukuwa na njia nyingine ya kufanya ili furaha yake irudi tena moyoni mwake, alijiona kutakiwa kufanya kitu kimoja kwa wakati huo, kumuua Manka pamoja na Yusufu tu.
Kadri siku zilivyozidi kwenda na ndivyo ambavyo Anko alivyozidi kuumia zaidi na zaidi, kila alipokuwa akiziona picha ambazo Yusufu alikuwa akipiga pamoja na Manka ambazo zilikuwa zikitolewa katika magazeti mbalimbali, Anko alikuwa akikasirika kupita kiasi. Japokuwa alikuwa amepanga kuanza kuwatafuta na kuwaua baada ya mwezi mmoja, lakini picha zile zikamfanya kusitisha mpango wake mrefu, akaweka mpango wa muda mfupi.
Alichokifanya ni kuwaandaa vijana wake ambao alitaka kufanya nao kazi ya kutekeleza kile ambacho alikuwa amekipanga kwa wakati huo. Vijana ambao walikuwa wakimfanyia kazi ya kuwaua wanachuo wa chuo cha IFM ndio ambao walitakiwa kuifanya kazi ambayo alikuwa ameipanga kufanyika kwa wakati huo. Alichokifanya ni kuwapigia simu na kutaka kuonana nao, tena nyumbani kwake, sehemu ambayo aliiona kuwa salama katika mipango yake yote.
“Kwa hiyo wewe unatakaje bosi?” Sudi aliuliza.
“Unamaanisha nini sasa kwa swali lako?” Anko aliuliza huku akionekana kuwa na hasira.
“Yaani tuwaue na kukuletea japo damu zao kwenye vidumu au tuwateke na kisha uje kuwaua wewe mwenyewe?” Sudi alimuuliza.
“Nyie mnaona zuri lipi hapo?”
“Chagua wewe”
“Nisaidie lipi zuri hapo”
“Labda tuwateke halafu uje kuwauwa wewe mwenyewe”
“Kwa nini msimalize kazi ninyi wenyewe na kuniletea damu kwenye vidumu kama ulivyosema?” Anko aliuliza.
“Tunahofia lawama?”
“Lawama zipi?”
“Kama tukikuletea damu kwenye vidumu unaweza kusema kwamba ni damu ya ng’ombe” Sudi alimwambia Anko.
“Hilo nalo neno. Watekeni halafu nije kufanya yangu”
“Poa bosi”
Sudi pamoja na wenzake, Kemo na Yati hawakutaka kupoteza muda, kwa kuwa kiasi cha shilingi milioni nne walikuwa wamekwishakabidhiwa kama nusu ya malipo ya kufanya kazi ile, wakaanza kuondoka kuelekea katika maskani yao kwa ajili ya kupanga juu ya namna ambavyo mchakato ule ulivyotakiwa kufanyika katika siku ya tukio ambalo walitakiwa kulifanya.
Usiku mzima walikuwa wakipanga ni kwa namna gani ambayo walitakiwa kukamilisha kile ambacho walikuwa wameambiwa kukamilisha, kuwateka Yusufu na Manka na kisha kuwasiliana na Anko ambaye angefika sehemu ambayo watakuwa wamewahifadhi kwa ajili ya kufanya kile ambacho alikuwa akitaka kuwafanyia.
Mipango kabambe ikapangwa usiku huo na ilitakiwa kufanyika katika siku ambazo watu hao wangekuwa pamoja hivyo kuwateka na kisha kufanya kile ambacho wangetakiwa kukifanya katika siku hiyo. Walipoona kwamba kila kitu kilikuwa tayari na ni ufanyaji wa kazi tu ndio ambao ungebakia, wakalala huku wakiwa wamepanga kila kitu.
****
“Sijui ni kitu gani ambacho kinaendelea chuoni kwetu” Manka alimwambia Yusufu.
“Kwa nini unasema hivyo?”
“Wanaume wanauawa sana na watu wasiojulikana” Manka alimwambia Yusufu huku wakiwa mezani wakipata chakula cha usiku.
“Nazisikia sana habari hizo. Kwa nini wanauawa?”
“Hata mimi sifahamu mpenzi. Halafu mbaya zaidi, kila aliyeuawa basi alikuwa akinitaka” Manka alimwambia Yusufu.
“Au wewe jini?” Yusufu alitania,
“Hapana bwana”
“Sasa ni nani anawaua?”
“Labda........” Manka alisema na ghafla kukaa kimya.
Hapo hapo kumbukumbu zake zikaanza kurudi nyuma kama mkanda wa video na kuanza kukumbuka baadhi ya matukio ambayo yalikuwa yametokea. Ni kweli wanaume wengi ambao walikuwa wakisoma katika chuo cha IFM walikuwa wakiuawa, swali lilikuja, kwa nini wanaume ambao walikuwa wakiuawa ni wale ambao walikuwa wakimtaka kimapezi?
Mtu wa kwanza kuuawa alikuwa Joseph na maiti yake kisha kutupwa katika ufukwe wa Coco, mtu wa pili kuuawa alikuwa Steve ambaye maiti yake pia ilitupwa katika ufukwe wa Coco. Ukiachana na hao, watu waliofuatia kuuawa walikuwa zaidi ya kumi na tano na mtu wa mwisho kabisa kuuawa alikuwa Emmanuel, kijana ambaye alikuwa na akili nyingi sana darasani. Wanaume wote hao ambao walikuwa wameuawa walikuwa wakimtaka kimapenzi, ni ndani ya wiki moja ya mishemishe zao za kumpata zilipokuwa zikiendelea, walikuwa wakiuawa.
Mpaka kufikia hatua hiyo, tayari Manka akahisi kwamba kulikuwa na kitu kinaendelea nyuma ya pazia. Haikuwezekana kwamba kila mwanaume ambaye alikuwa akiuawa ni yule ambaye alikuwa akimtaka kimapenzi. Hapo akaonekana kugundua kitu, hapo ndipo hisia zake zilipokwenda moja kwa moja kwa mpenzi wake wa nyuma, Anko ambaye alikuwa na fedha nyingi.
“Anko” Manka alijikuta akisema.
“Ndiye nani huyo?” Yusufu aliuliza.
“Ndiye aliyeuwa watu wanaume wa pale chuoni” Manka alimwambia Yusufu.
“Ndiye nani huyo?”
“Alikuwa mpenzi wangu kabla ya kuwa na wewe. Nadhani alikuwa akimuua kila mvulana ambaye alikuwa akitamani kuwa na mimi” Manka alimwambia Yusufu.
“Kwa hiyo kila aliyetaka kuwa na wewe alimuua?”
“Ndio”
“Kwa hiyo ina maana hata mimi ataweza kuniua?”
“Inawezekana” Manka alijibu na kumfanya Yusufu kuanza kucheka.
“Usicheke mpenzi. Unahitaji kuwa makini kwa sasa” manka alimwambia Yusufu.
“Hawezi kuniua. Kila aliyetaka kuniua, aliuawa yeye” Yusufu alimwambia Manka huku akiendelea kucheka.
“Inakupasa kuwa makini mpenzi, hili si jambo la kulipuuzia” Manka alimwambia Yusufu ambaye bado alikuwa akiendelea kucheka.
“Kuna watu wapo makini kwa ajili ya maisha yangu. Usiogope” Yusufu alimwambia manka.
Bado waliendelea kula chakula kama kawaida. Walipomaliza kula, bia zikaletwa mezani hapo na kisha kuanza kuzinywa kwa fujo. Kila walipokuwa wakimaliza chupa tatu, mfanyakazi alikuwa akiwaletea chupa nne. Usiku huo ulikuwa ni usiku wa kunywa pombe tu kiasi ambacho kiliwafanya kuwa hoi.
Wote wakainuka na kisha kushikana, kilichofuata baada ya hapo ni kuanza kupelekana chumbani huku wakiyumba yumba kupita kawaida. Walipoufikia mlango, wakaufungua na kisha kuingia na kujilaza kitandani. Wote wakabaki wakiangaliana kwa macho ya mahaba kitandani hapo, Manka hakutaka kukubali, alichokifanya ni kuanza kumsogelea Yusufu na kisha kuanza kumshikashika kifuani jambo ambalo likaanza kuziamsha hisia za Yusufu.
“Unataka tufanye nini mpenzi?” Yusufu aliuliza kwa sauti iliyojaa ulevi.
“Nataka tufanye mapenzi” Manka alimjibu huku akiendelea kukichezea kifua cha Yusufu.
“Hapana baby. Leo Jumapili” Yusufu alimjibu Manka kwa sauti ya chini iliyojaa kilevi.
“Nafahamu baby. Leo jumapili, walokole walikwenda kanisani asubuhi” Manka alimwambia Yusufu.
“Kama unajua leo Jumapili, sasa kwa nini unataka tufanye mapenzi?” Yusufu aliuliza huku akionekana kuzidiwa.
“Kwa sababu leo ni siku ya mapumziko”Manka alijibu.
Katika kila jibu ambalo alikuwa akilitoa Manka na ndivyo ambavyo alikuwa akizidi kumvua Yusufu nguo moja baada ya nyingine na kisha kuanza kuzivua nguo zake. Baada ya dakika mbili, wote wakabaki watupu. Japokuwa Yusufu alijua fika kwamba siku hiyo ilikuwa ni Jumapili, siku ambayo hakutakiwa kufanya mapenzi lakini akaonekana kushindwa kumzuia Manka kwani mwili wake haukuwa na nguvu kabisa kutokana na kulewa kupita kiasi pamoja na kuzidiwa katika suala zima la msisimko wa mwili wake.
Manka akamlalia Yusufu kifuani na kisha kuanza kufanya mapenzi kama kawaida yao. Kitendo kile kilipoanza, Yusufu hakutaka kukumbuka tena, hakutaka kukumbuka kwamba siku hiyo ilikuwa ni siku ya Jumapili, siku ambayo ilionekana kuwa mbaya kwake kama ambapo angefanya kile ambacho alikatazwa kukifanya siku hiyo. Kadri muda ulivyozidi kwenda mbele na ndivyo ambavyo waliendelea kufanya zaidi na zaidi mpaka pale ambapo wote wakahisi kuchoka na kisha kulala.

Yusufu amevunjwa moja ya masharti aliyopewa kwenye ulimwengu wa kuzimu kwa kufanya mapenzi na manka katika siku ya Jumapili.
Je nini kitaendelea?
Je Yusufu atapewa adhabu gani?
Kumuua mama yake, mtoto wake, mtalaka wake au kumuua Papaa Pipo?
Itaendelea.
 
MTUNZI: NYEMO CHILONGANI.
MAHALI: DAR ES SALAAM.
SIMU: 0718 069 269.

NITAKAPOKUFA 23

Yusufu akaamka asubuhi na kisha kuanza kujiangalia kitandani pale. Alipojiona kwamba yupo mtupu na Manka nae alikuwa kama alivyokuwa, Yusufu akaonekana kuwa na wasiwasi. Kitu cha kwanza ambacho alikuwa amekifikiria kwa wakati huo ni siku hiyo ya siku hiyo. Ilikuwa ni siku ya Jumatatu, kwa maana hiyo ilimaanisha kwamba siku iliyopita ilikuwa ni siku ya Jumapili.
Kama mtu aliyechanganyikiwa, Yusufu akainuka kutoka kitandani, akaanza kumwangalia Manka mara mbili mbili huku akionekana kutokuamini kile ambacho kilikuwa kimetokea usiku uliopita. Japokuwa katika usiku uliopita alikuwa amelewa lakini alikumbuka dhahiri kwamba walikuwa wamefanya mapenzi, Yusufu akachanganyikiwa kupita kawaida.
“Manka....Manka...” Yusufu akaanza kumwamsha Manka.
Manka alikuwa mzito kuamka. Yusufu aliendelea kumwamsha zaidi na zaidi mpaka pale ambapo manka akaamka na kisha kuanza kumwangalia Yusufu usoni ambaye alionekana kuwa kama mtu aliyechanganyikiwa. Yusufu hakuongea kitu, kwanza akaanza kumwangalia Manka kwa makini huko uso wake ukionekana kuwa na wasiwasi mwingi.
“Hivi tulifanya mapenzi usiku uliopita?” Lilikuwa swali la kwanza lililotoka mdomoni mwa Yusufu.
“Ndio tulifanya” Manka alijibu na kisha kujilaza tena.
“Kwa nini tulifanya?” Yusufu alimuuliza Manka ambaye wala hakuonekana kujali zaidi ya kuendelea kulala.
Akili ya Yusufu kwa wakati huo ilikuwa imekwishachanganyikiwa. Hakuamini kama hiyo ilikuwa ni mara yake ya pili kuvunja masharti ambayo alikuwa amewekewa katika ulimwengu wa giza. Akaanza kuikumbuka siku ambayo alivunja sharti la kwanza na hivyo kupewa adhabu ya kumuua baba yake jambo ambalo lilikuwa limemuuma kupita kawaida.
Siku hiyo, kwa mara ya pili akawa amevunja sharti la pili ambalo alikuwa amepewa la kutofanya mapenzi katika siku ya Jumapili. Tukio lile likamuuma sana Yusufu kwa kuona kwamba ilikuwa ni lazima viumbe wa ulimwengu ule wa giza wampe adhabu, adhabu ambayo aliamini ingekuwa kali sana katika maisha yake.
Yusufu hakutaka kuendelea kubaki ndani ya chumba kile, alichokifanya ni kutoka na kuanza kuelekea nje huku akiwa ameuchukua ufunguo wa gari lake. Machozi yakaanza kutoka machoni mwake, moyoni mwake alikuwa ameumia kupita kawaida. Tayari akajiona kuwa mtu ambaye hakuuonea raha utajiri na umaarufu wake ambao alikuwa amepewa. Kwake, tayari vitu vile ambavyo alikuwa amepewa aliviona kumnyima uhuru kabisa kwa kumuwekea masharti ambayo yalikuwa mazito sana kuyaepuka.
Yusufu akaingia ndani ya gari lake na kisha kuanza kuelekea nyumbani kwa Papaa Pipo, Kijitonyama. Kichwa chake kwa wakati huo kilikuwa kimechanganyikiwa kupita kawaida. Hakuamini kama tayari alikuwa amevunja sharti jingine, sharti ambalo halikumtaka kufanya mapenzi katika siku ya Jumapili. Yusufu aliendelea kuendesha gari huku akiwa na mawazo mengi, mpaka katika kipindi hicho, hakujua ni adhabu gani ambayo angepewa.
Baada ya dakika kadhaa akawa amekwishafika nje ya nyumba ya Papaa Pipo ambapo akateremka na kisha kuanza kulifuata geti lile. Hakutaka kuliingiza gari lake ndani ya eneo la Papaa Pipo, kwa wakati huo akili yake ilikuwa imechanganyikiwa kupita kiasi. Alipolifikia geti akaanza kugonga kifujo fujo na mlinzi kutokea na kufungua.
“Karibu The Ruler” Mlinzi alimkaribsha.
Yusufu hakuongea kitu chochote kile, alichokifanya ni kuingia ndani ya nyumba ile huku akili yake ikiwa bado haijakaa sawa kabisa. Alipoufikia mlango wa kuingilia sebuleni akaugonga na mfanyakazi wa ndani kuja kuufungua. Mfanyakazi wa ndani alionekana kushangaa sana, katika maisha yake yote hakuwahi kumuona Yusufu akifika nyumbani hapo asubuhi sana tena huku akionekana kuwa ovyo ovyo kama ambavyo alivyokuwa kwa wakati huo, hakuwa amenawa, na alikuwa amevaa bukta tu pamoja na kaoshi.
“Karibu” Yule mfanyakazi wa ndani alimkaribisha huku akionekana kushangaa.
“Asante” Yusufu aliitikia na kisha kuingia ndani.
Hakutaka kukaa sebuleni hapo, alichokifanya ni kuanza kupiga hatua kuelekea katika chumba alichokuwa akilala Papaa Pipo. Alipoufikia mlango wa chumba kile, akaanza kuugonga na baada ya muda Papaa Pipo kutokea na kisha kumfungulia huku akionekana kumshangaa Yusufu. Yusufu akaingia na kisha kukifuata kitanda na kutulia.
“Vipi tena? Mbona asubuhi asubuhi kama mtu aliyeitwa kwenye usaili?” Papaa Pipo alimuuliza Yusufu huku akionekana kushangaa.
“Nimevunja sharti la pili” Yusufu alimwambia Papaa Pipo.
“Unasemaje?” Papaa Pipo aliuliza huku akionekana kushtuka.
“Nimevunja sharti la pili” Yusufu alimwambia Papaa Pipo.
“Samiah amepata mtoto wa pili?” Papaa Pipo aliuliza
“Hapana. Nimefanya mapenzi jana na Manka” Yusufu alimwambia Papaa Pipo.
“Acha kunitania Yusufu”
“Huo ndio ukweli Papaa Pipo. Nimefanya mapenzi na Manka usiku uliopita” Yusufu alimwambia Papaa Pipo.
“Sasa kwa nini ulikubali kufanya mapenzi?”
“Nilikuwa nimelewa”
“Kwa nini ulewe siku kama ile, siku ambayo unajua fika kwamba ni siku ya majanga?”
“Hata sijui kwa sababu gani. Yaani hapa nilipo nimechanganyikiwa” Yusufu alimwambia Papaa Pipo.
“Kwa hiyo tufanye nini?”
“Hata sijui. Labda niwaombe msamaha wakiniita” Yusufu alimwambia Papaa Pipo.
“Kukusamehe ni jambo gumu sana. Ni lazima uitumikie adhabu” Papaa Pipo alimwambia Yusufu.
Yusufu akabaki kimya, hakuwa akiamini kile ambacho kilikuwa kimemtokea kwa mara ya pili katika kipindi hicho. Masharti yote ambayo alikuwa amepewa tayari alikuwa amekwishayavunja ndani ya miaka mitatu tu ya mafanikio yake. Aliikumbuka siku ile ambayo alivunja sharti la kwanza mara baada ya kupata mtoto kitu ambacho hakutakiwa kukipata katika maisha yake yote. Kuvunjika kwa sharti lile, lawama zote alikuwa akimpa mtalaka wake, Samiah ambaye alifanya kitendo kile kwa makusudi bila kumpa taarifa.
Yusufu aliumia sana mara baada ya kupewa adhabu ya kumuua baba yake tena kwa mkono wake mwenyewe. Leo hii, tayari alikuwa amevunja sharti jingine. Hakutaka kumlaumu sana Manka katika kuvunja sharti lile bali lawama zote alikuwa akijipa yeye mwenyewe kwa kuruhusu kunywa pombe na hatimae kuvunja sharti la kufanya mapenzi katika siku ambayo hakutakiwa kufanya mapenzi. Jambo hilo ndilo ambalo lilikuwa likimuumiza sana kichwa kwa wakati huo, hakujua ni kitu gani alitakiwa kukifanya.
“Siadhibiwi” Yusufu alisema kwa sauti kubwa huku akionekana kuwa na hasira.
“Unasemaje?” Papaa Pipo aliuliza kana kwamba hakuwa amesikia.
“Siadhibiwi. Sipo tayari kupokea adhabu yoyote kwa sasa” Yusufu alimwambia Papaa Pipo na kisha kuondoka mahali hapo.
Njia nzima Yusufu alikuwa na mawazo, hakuamini kama kitendo chake cha kukubali kupata mvuto pamoja na utajiri vingemfanya kufikia hatua ile. Japokuwa utajiri na mvuto ule vilikuwa vitu vizuri sana katika maisha yake lakini muda wingi vilikuwa vikimkosesha sana amani jambo ambalo wakati mwingine lilimfanya kujuta kupita kawaida kwa uamuzi ambao alikuwa ameuchukua. Kwa wakati huo, aliiona dunia ikiwa imemuinamia, hakuamini kama matokeo ya kuchukua uamuzi ule yangekuwa namna ile.
“Ulikwenda wapi mpenzi?” Ilikuwa ni sauti ya Manka ambayo ilisikika masikioni mwake mara baada ya kufika nyumbani.
“Nilikwenda sehemu fulani”
“Mbona haukuniaga jamani baby wangu?”
“Nilikuamsha ili nikuage lakini ukalala tena” Yusufu alimwambia Manka ambaye alikuwa akimwangalia kwa mshangao.
“Ila unaonekana haupo sawa. Kuna nini?” Manka alimuuliza Yusufu.
“Hakuna kitu. Mbona nipo sawa tu”
“Hapana. Haupo sawa kabisa. Nieleze kitu gani kimetokea”
“Nipo sawa mpenzi. Ni uchovu wa asubuhi tu” Yusufu alimwambia Manka.
Bado kichwa cha Yusufu hakikukaa sawa kabisa kwa wakati huo, mawazo yake yalikuwa yakifikiria juu ya adhabu ambayo angepewa mara tu baada ya kuitwa katika ulimwengu wa giza. Hakujua ni kitu gani ambacho angetakiwa kukifanya kama ni kukubali adhabu ambayo angepewa au kukataa kuipokea. Yusufu alikaa katika hali ya mawazo mpaka pale ambapo Manka akahitaji kuondoka, akaamua kumsindikiza.
“Ila bado unaonekana kutokuwa sawa kabisa. Naomba uniambie ni kitu gani kinaendelea” manka alimwambia Yusufu.
“Mbona nipo kawaida tu”
“Hapana. Haupo kawaida. Asubuhi ulisema kwamba ulikuwa na uchovu, sidhani kama uchovu wa asubuhi unaweza kuendelea mpaka sasa hivi, jioni hii” Manka alimwambia Yusufu.
“Siko sawa mpenzi”
“Kwa nini tena?”
“Sipo sawa” Yusufu alimwambia Manka kwa sauti yenye ukali.
Manka akaonekana kuogopa, siku hiyo Yusufu alionekana kuwa mtu wa tofauti kabisa. Toka alipoanza kumfahamu, hakuwahi kumuona Yusufu akiwa katika hali hiyo, alikuwa akimuona kuwa katika hali ya furaha na utulivu mkubwa sana. Siku hiyo, Yusufu hakuonekana kuwa sawa, alijua fika kwamba kulikuwa na kitu ambacho kilitokea lakini kila alipokuwa akijaribu, Yusufu hakuonekana kuwa radhi kumwambia.
Hali ile bado ilikuwa ikimtia Manka wasiwasi, hakupenda kumuona mpenzi wake akiwa katika hali ile, alitamani amwambie ni kitu gani ambacho kilikuwa kimeendelea ili hata kama alikuwa na uwezo wa kumsaidia basi afanye hivyo. Yusufu alionekana kuwa mgumu kujiweka wazi kwa Manka, kumwambia ukweli kwamba alikuwa amevunja masharti aliyokuwa amepewa lisingeonekana kuwa jambo sahihi kwake kwani hakutaka Manka afahamu jambo lolote lile.
“Nataka kwenda chuo” Manka alimwambia Yusufu ambaye akainuka kutoka kitandani na kuchukua ufunguo wa gari.
Garini, bado Yusufu hakuonekana kuwa sawa kabisa, alionekana kuwa mwingi wa mawazo, akili yake ilikuwa ikiwafikiria wale viumbe wa ajabu ambao walikuwa wakipatikana katika ulimwengu wa ajabu pamoja na adhabu ambayo wangempa mara baada ya kumuita katika moja ya vikao vyao.
Manka alionekana kuwa na wasiwasi mwingi, hali ambayo alikuwa nayo mpenzi wake ilionekana kumhuzunisha kupita kawaida. Hakuzoea kumuona Yusufu akiwa katika hali hiyo, alikuwa amezoea kumuona Yusufu akiwa katika hali ya furaha huku wakiyafurahia mapenzi yao ambayo yalionekana kuzidi kukua kadri siku zilivyozidi kwenda mbele.
Walichukua dakika thelathini na ndipo walipofika Mabibo ambapo Yusufu akalisimamisha gari lile na kisha kuanza kumwangalia Manka usoni huku ikiwa imetimia saa kumi na mbili na robo jioni. Hata kabla manka hajateremka kutoka katika gari lile, akayapeleka macho yake usoni mwa Yusufu ambaye bado alionekana kuwa mwingi wa mawazo.
“Nakuomba uniambie simuni baadae kile kinachokusumbua” Manka alimwambia Yusufu.
“Hakuna kinachonisumbua mpenzi. Nipo sawa tu” Yusufu alimwambia manka.
“Hapana. Sijazoea kukuona katika hali hiyo. Naomba uniambie mpenzi” Manka alimwambia Yusufu ambaye akashusha pumzi ndefu na kumwangalia usoni.
“Usijali. Nitakwambia” Yusufu alimwambia Manka ambaye akaanza kuteremka garini.
Yusufu hakutaka kuendelea kubaki, alichokifanya ni kuondoka mahali hapo na kurudi nyumbani kwake. Mwendo wa gari ulikuwa ni wa taratibu sana, bado hali ya mawazo hayakuweza kumtoka, adhabu ambayo alikuwa akitarajia kuipata ndio ambayo ilimfanya kuwa kwenye hali hiyo ambayo haikuonekana kuwa ya kawaida kabisa.
Kutokana na foleni kubwa ya Ubungo, magari yalikuwa yakitembea tembea taratibu huku yakisimama kila baada ya hatua kadhaa. Huku akiwa amelisimamisha gari katika foleni ile, mara mwanaume mmoja ambaye alionekana kuwa kama kijana wa mitaani akatokea mbele ya gari lake na kisha kujifanya kuosha kioo cha gari lake. Yusufu alitamani kumwambia aache kufanya hivyo lakini hata nguvu ya kumwambia akaiona kupotea kabisa.
Huku macho yake yakimwangalia kijana yule ambaye alikuwa akiendelea kuosha kioo cha gari lake, mara akasikia kioo cha gari lake cha mlangoni kikigongwa, alipoangalia, alikuwa muuza magazeti. Yusufu akakifungua kioo kile na kisha kuanza kumwangalia kijana yule ambaye alikuwa ameshika magazeti mengi.
“Utataka gazeti moja kaka?” Kijana yule alimuuliza Yusufu.
“Hapana” Yusufu alijibu huku akijiandaa kupandisha kioo cha mlango ule.
Huku hata kabla hajaanza kukipandisha kioo kile, macho yake yakatua katika mkono wa muuza magazeti yale, mkono ambao ulikuwa umeshika magazeti yale, ulikuwa umeshika bunduki kwa chini, sehemu ambayo hakukuwa na mtu mwingine yeyote ambaye angefanikiwa kuiona kutokana na kufunikwa na magazeti yale.
“Ukileta ubishi wowote hapa, nakifumua kichwa chako” Kijana yule alimwambia Yusufu huku mdomo wa bunduki ukiwa umemlenga usoni mwake.
“Fungua mlango huo huko” Kijana yule alimwambia Yusufu ambaye bila ubishi akaufungua mlango wa upande wa pili na kisha huku akionekana kushangaa, kijana yule ambaye alikuwa akikiosha kioo cha gari lake akiufuata mlango, akaifungua na kisha kuingia ndani.
Yusufu akatakiwa kutulia katika usukuni ule huku kijana yule ambaye alikuwa na bunduki akiufungua mlango wa nyuma na kuingia ndani. Yusufu akaonekana kuwa na wasiwasi, hakuamini kama kwa mara ya pili tena alikuwa amewekwa chini ya ulinzi wa watu asiowajua, alichokifanya mahali hapo, ni kufanya kile ambacho watu wale walitaka akifanye.
“Unatakiwa uendeshe gari mpaka katika barabara ya Sam Nujoma, pembezoni mwa jengo la Mawasiliano” Sudi alimwambia Yusufu.
Yusufu akatulia, mdomo wa risasi ambao alikuwa ameelekezewa na Sudi ambaye alikuwa katika viti vya nyuma ulionekana kumtia wasiwasi, alikuwa akitetemeka huku kijasho chembamba kikianza kumtoka. Foleni ile ilichukua muda wa dakika ishirini na ndipo wakafanikiwa kuvuka katika maunganisho ya barabara ya Morogoro na kisha kuingia katika barabara ya Sam Nujoma.
Safari iliendelea zaidi na zaidi mpaka pale ambapo walifika karibu na jengo la Mawasiliano na kisha kutakiwa kulisimamisha gari lake pembeni ya barabara karibu kabisa na mahali ambapo Yati alipokuwa amesimama. Gari liliposimamishwa, Yati akaufungua mlango na kisha kuingia ndani huku nae akionekana kuwa na bunduki.
“Wapi sasa” Kemo, ambaye alikuwa pembeni ya Yusufu katika viti vya mbele aliwauliza.
“Kwanza shikilia usukani na huyo mjinga aje huku nyuma” Sudi alimwambia Kemo ambaye alimwambia Yusufu ampishe katika kiti kile na kisha kukaa yeye huku Yusufu akielekea katika kiti cha nyuma na kuwekwa katikati.
“Tanganyika Pakers” Sudi alimwambia Kemo ambaye akawasha gari na kisha kuondoka mahali hapo na safari ya kuelekea katika uwanja wa Tanganyika Pakers uliokuwa Kawe kuanza.
Katika muda wote wa safari ile Yusufu alionekana kuwa na wasiwasi, hakuamini kama kweli katika siku hiyo angeweza kuwa mikononi mwa watu ambao wala hakuwa akiwajua kabisa. Wasiwasi wake ulizidi kuongezeka mara baada ya kugundua kwamba tayari alikuwa amevunja sharti hivyo aliona kama ulinzi kwake usingekuwepo kabisa kutoka katika ulimwengu wa giza.
Kutokana na foleni za hapa na pale, walichukua saa moja na dakika kumi na tano na ndipo walipofika katika viwanja hivyo na kisha kulipaki gari huku tayari ikiwa imetimia saa mbili kasoro kumi usiku. Hapo hapo wakamtaka Yusufu kuteremka pamoja nao huku wakiwa pamoja nae na kisha kumtanguliza mbele katika jumba moja bovu ambalo lilionekana kutelekezwa ambalo lilikuwepo katika uwanja huo.
“Mpigie simu bosi” Sudi alimwambia Kemo huku wakiingia ndani ya jumba lile bovu.
“Ila si bado msichana?”
“Wewe mpigie tu. Hatuna muda. Ni bora tuanze na huyu halafu huyo demu atafuata” Sudi alimwambia Kemo.
Kemo akachukua simu yake na kisha kuanza kumpigia Anko na kisha kuanza kumpa taarifa ile kwamba kile kitu ambacho aliwataka wakifanye tayari kilikuwa kimekwishafanyika na katika kipindi hicho walikuwa pamoja na Yusufu katika uwanja wa Tanganyika Pakers uliokuwa Kawe.
“Nakuja. Na vipi kuhusu yule malaya?”Ilisikika sauti ya Anko.
“Yule bado ila tu.....” Kemo alisema lakini hata kabla hajamalizia, Anko akaingilia.
“Msijali. Huyo mjinga ndio wa muhimu zaidi ya yule malaya. Yule malaya hasumbui, nitamtafuta hata kesho. Nisubirini nakuja hapo hapo ndani ya dakika ishirini kwani nipo hapa Leaders Club” Sauti ya Anko ilisikika na kisha kukata simu.
“Amesemaje?” Sudi alimuuliza Kemo.
“Anakuja ndani ya dakika ishirini kwani yupo hapo Leadres Club” Kemo alijibu.
Yusufu akaamriwa kukaa chini, bado alikuwa na wasiwasi tele, hakuamini kama katika kipindi hicho alikuwa mateka na muda wowote ule kuanzia hapo angeweza kuuawa. Tayari akaonekana kufahamu kwamba inawezekana kwamba mtu ambaye alikuwa amemzungumzia Manka ndiye ambaye alikuwa nyuma ya mipango yote ya kutekwa kwake.
Japokuwa toka aishi maisha yake ndani ya jiji la Dar es Salaam hakuwahi hata kwenda msikitini, kwa wakati huo akaanza kumuomba Mungu amuepushe na hatari ambayo ilikuwa mbele yake. Yusufu hakuishia hapo, alichokuwa akikijua yeye ni kwamba alikuwa akienda kufa na hivyo alihitaji Mungu amsamehe kwa kila kitu ambacho alikuwa amekifanya.
“Hata ukimuomba Mungu! Ni lazima tukuue tu” Sudi alimwambia Yusufu huku akimgonga gonga na bunduki yake kichwani.

Je nini kitaendelea mahali hapo?
Je Anko ataweza kumuua Yusufu ambaye ametekwa na watu wake?
Kama atafanikiwa kumuua Yusufu, ataweza kumuua Manka pia?
Je nini hatma ya kila kitu katika simulizi hii?
Itaendelea.
 
MWANDISHI: NYEMO CHILONGANI
MWASILIANO: 0718 069 269
MAHALI: DAR ES SALAAM

NITAKAPOKUFA 24

Anko akabadilika, uso wake ukaonekana kuwa kwenye furaha kubwa, hakuamini kile ambacho alikisikia kutoka simuni mwake, alichoambiwa na Kemo. Japokuwa alikuwa katika uwanja wa Leaders akiiangalia bendi ya Twanga Pepeta ambayo ilikuwa ikitumbuiza mahali pale, hakujali, akasimama na kisha kuanza kuondoka mahali hapo.
Moja kwa moja akalifuata gari lake ambalo alikuwa amelipaki katika uwanja wa mpira uliokuwa mahali hapop, akaufungua mlango wa gari na kuanza kuondoka mahali hapo. Moyo wake ulikuwa kwenye furaha tele, hakuamini kama wakati huo vijana ambao aliwaambia wamkamate Yusufu pamoja na Manka walikuwa wamekwishafanikisha kile alichowaambia. Hakuwa na wasiwasi na Manka, alijua kwamba kazi kubwa ilikuwa kwa huyu Yusufu, mtu ambaye alikuwa akionekana kuwa makini katika kipindi chote.
Mwendo wake haukuwa mdogo, alikuwa akiendesha gari lake kwa kasi kuelekea Kawe katika viwanja vya Tanganyika Pakers huku lengo lake likiwa ni kuonana na vijana wale ambao alikuwa amewatuma pamoja na kufanya kile ambacho alikuwa akikitaka, kumuua Yusufu na kuondoka zake huku moyo wake ukianza kuwa na amani.
Akajipapasa kiunoni mwake, bunduki yake ilikuwa vizuri mahali hapo, hakuridhika, akaitoa na kuanza kuiangalia vizuri huku mkono mmoja ukiwa umeshika usukani wa gari lake. Risasi za kutosha bado zilikuwepo ndani ya bunduki ile ambayo wala haukuwa umepita muda mrefu tangu ainunue nchini Uganda, na alikuwa akiimiliki kinyume na sheria.
Mwendo wake bado haukuwa wa taratibu, alikuwa akiendesha gari kwa kasi kwa kuona kwamba kama angechelewa basi Yusufu angeweza kuwatoroka watu hao kitu ambacho hakutaka kitokee mahali hapo. Mara baada ya kufika Mikocheni B karibu kabisa na mtaa wa Mbuni, mbele yake kukaonekana umati mkubwa wa watu ambao walikuwa wamevaa nguo nyeupe tupu huku watu hao wakiwa wameshika majeneza mengi wakielekea upande wa baharini kuzika.
Anko akapigwa na mshtuko kupita kawaida, hakuamini kile ambacho alikuwa akikiona machoni mwake kwa wakati huo, ilikuwaje watu waelekee kuzika muda kama huo, usiku tena mbaya zaidi wakielekea baharini, sehemu ambayo wala haikuwa na makaburi yoyote yale. Hayo yakaonekana kuwa mauza uza kwake, akawaangalia watu wale vizuri, hawakuwa watu weusi, walikuwa waarabu tupu huku idadi yao ikiwa kubwa kupita kawaida.
Wale watu ambao walikuwa wakivuka barabara kwenda baharini kuzika huku wakiwa na majeneza hawakuweza kuisha, bado walikuwa wakiendelea kuvuka barabara ile huku wakiimba nyimbo ambazo wala hakuwa akizielewa kabisa. Alikaa kwa zaidi ya nusu saa, idadi ile bado haikuonekana kuisha mahali pale, bado watu wale walikuwa wakiendelea kuvuka barabara kuelekea kuzika.
Mpaka kufikia hatua hiyo, Anko akaonekana kuchanganyikiwa kupita kawaida, hakujua ni kitu gani ambacho alitakiwa kukifanya zaidi ya kuteremka kutoka garini na kisha kuanza kuangalia huku na kule. Barabarani, hakukuwa na gari lolote lile zaidi ya gari lake. Hilo nalo kwake likaonekana kuwa la mauza uza, hakutegemea muda kama huo wa saa tatu kusiwe na gari lolote mahali hapo, Anko alionekana kuchanganyikiwa.
Muda bado ulikuwa ukizidi kwenda mbele, watu wale ambao walikuwa wakielekea kuzika hawakuisha, bado walikuwa wakiendelea kuvuka barabara ile huku majeneza yakiwa mikononi mwao. Anko akaonekana kuchoka, alichokifanya ni kurudi garini mwake na kisha kuanza kupiga honi kadhaa lakini watu wale wala hawakuonekana kusikia, na kama walisikia basi hawakuonekana kujali.
Anko hakuwa na jinsi, kwa wakati huo alikuwa amevumilia kupita kawaida, alichokifanya ni kurudisha gari nyuma na kuchukua uamuzi mmoja tu, kuwagonga watu hao ambao walikuwa hawaishi kuvuka barabara ile kuelekea makaburini baharini. Alipoona amerudisha gari lake umbali wa kutosha, hapo ndipo alipopiga gia na kisha kuanza kuliondoa gari lile kwa kasi ya ajabu na kuwagonga watu wale ambao walikuwa mbele yake ambao ghafla wakapotea. Gari lake likakosa muelekeo, likatoka nje ya barabara na kuuvamia mtaro uliokuwa pembeni mwa barabara ambapo kulikuwa na mtaro na gari lile kujibamiza kwa nguvu hivyo yeye mwenyewe kutolewa nje ya gari lile.
Kichwa chake kilikuwa kimepiga kioo cha mbele cha gari lile na hivyo kutolewa nje ambapo akakibamiza kichwa chake katika ukuta wa mtaro huo, kichwa kikapasuka, ubongo ukatoka, damu zikatapakaa mahali hapo. Hiyo ikaonekana kuwa ajali moja kubwa ambayo ilionekana kuwa ya kizembe kupita kawaida.
Ndani ya sekunde ishirini tu, watu wakafika mahali hapo na kisha kuanza kuuangalia mwili wake ambao ulikuwa mtaroni. Ile ikaonekana kuwa ajali mbaya sana, kichwa kilikuwa kimepasuka kabisa huku ubongo ukiwa mtaroni katika maji machafu. Waliokuwa na simu zenye mwanga wakaanza kupiga picha mwili huo bila mtu yeyote kujua kwamba mtu yule alikuwa Anko.
“Mmmh! Inatisha” Jamaa mmoja aliwaambia wenzake.
“Hivi ilikuwaje? Unajua sijaiona hii ajali” Jamaa mmoja aliuliza.
“Huyu dereva sijui alikuwa amelewa. Yaani hadi nashangaa” Jamaa mwingine alisema.
“Kwani ilikuwaje?”
“Huyu dereva alikuwa amelisimamisha gari barabarani bila sababu yoyote ile kwa zaidi ya nusu saa” Jamaa yule alielezea.
“Alisimamisha gari barabarani?”
“Ndio. Kila akipigiwa honi alikuwa hatoi gari. Bado alikuwa amelisimamisha tu”
“Au lilikuwa limeharibika?” Jamaa mwingine aliuliza.
“Hakuna. Yaani nilishangaa nini kimetokea. Madereva wa magari mengine hawakuonekana kujali, wakawa wakimpita na kuendelea na safari zao”
“Sasa kwa nini hukwenda kumshtua?”
“Nilitaka kufanya hivyo ila kila nilipotaka kwenda, nilikuwa mzito kweli”
“Sasa ikawaje? Mbona yupo mtaroni?”
“Baada ya kusimama kwa muda mrefu, nikaona anarudisha gari kwa nyuma na kisha kuliendesha kwa mwendo wa kasi. Cha kushangaza sasa, akaanza kuufuata mtaro kwa mwendo huo huo wa kasi. Kilichotokea ndicho hiki mnachokiona” Jamaa huyo alielezea.
“Kwa hiyo hii ni ajali ya kujitakia?”
“Asilimia mia moja. Ila inawezekana alikuwa amelewa” Jamaa yule alimalizia.
****
Muda ulikuwa ukizidi kwenda mbele lakini wala Anko hakuonekana kufika mahali hapo. Sekunde zilikuwa zikisogea huku dakika zikizidi kusonga mbele lakini bado Anko hakuweza kufika mahali hapo. Mara kwa mara walikuwa wakimpigia simu yake, simu ilikuwa ikiita tu lakini wala haikuwa ikipokelewa jambo ambalo lilikuwa likimkasirisha kila mtu mahali pale.
Tayari mtu ambaye alikuwa akimhitaji kwa udi na uvumba alikuwa mikononi mwao, yeye ndiye ambaye alikuwa akisubiriwa tu mahali hapo na kisha kumkabidhi mtu wake ambaye angemfanya kitu chochote kile ambacho angetaka kumfanya mahali hapo. Muda mwingi walikuwa wakiangalia saa zao lakini wala Anko hakuweza kutokea mahali hapo.
Mpaka inatimia saa tano usiku, bado Anko hakuwa mahali hapo. Kila walipokuwa wakipiga simu masaa ya nyuma ilikuwa ikiita tu, kwa sasa hata kuita haikuwa ikiita, ilikuwa haipatikani kabisa jambo ambalo lilimshangaza kila mmoja mahali hapo. Wakaanza kujadiliana ni kitu gani ambacho walitakiwa kukifanya mahali hapo, hapo ndipo ambapo simu ile ambayo walikuwa wameitumia kumpigia Anko ilipoanza kuita, Kemo akaipokea na kuipeleka sikioni.
“Unasemaje?....Amepata ajali?...... Wapi?.... Muhimbili?... Hapana, mimi ni rafiki yake tu. Sawa nakuja........” Kemo aliongea na mtu simuni na kisha kukata simu ile.
“Vipi?” Yati alimuuliza.
“Anko amepata ajali na mwili wake kupelekwa hospitalini?” Kemo alijibu huku akionekana kuchoka.
“Kwa hiyo amekufa ajalini?” Sudi aliuliza.
“Sijui”
“Sasa inakuwaje amesema mwili wake umepelekwa hospitalini? Hivi angekuwa hai angesema mwili umepelekwa hospitalini? Atakuwa amekufa tu” Sudi aliwaambia.
“Sasa inakuwaje?” Kemo aliuliza
“Kuhusu nini? Kuelekea hospitalini?”
“Hapana. Hospitalini siendi. Sio ndugu yangu yule. Nauliza kuhusu huyu mpumbavu” Kemo alijibu huku akimwangalia Yusufu.
“Huyu tumuacheni tu. Amesalimika. Au nyie mnaonaje?” Sudi aliwaambia na kuwauliza.
“Hiyo sawa sawa. Tuondokeni tu” Yati aliwambia.
Hawakutaka kubaki mahali hapo, walichokifanya ni kuondoka mahali hapo na kuanza kushuka chini ya jengo lile kuu kuu. Walipolifikia gari lile la Yusufu, Kemo akashikilia usukani na kisha kuanza kuondoka mahali hapo. Wala hawakufika mbali, Kemo akasimamisha gari huku akionekana kushtuka.
“Vipi?” Sudi alimuuliza kemo.
“Hivi tumemuacha Yusufu hai?”
“Kwani hatukumuua?” Sudi aliuliza.
“Hapana. Nafikiri tumemuacha hai. Kwa nini tumemuacha hai?” Kemo aliuliza huku akiteremka kutoka garini huku akiwa na bunduki.
“Tulimuacha hai? Kivipi?” Sudi aliuliza huku akiteremka garini pamoja na Yati.
“Tulimuacha hai. Haiwezekani. Kwa nini hatukumuua?” Kemo aliuliza.
“Mmmh! Kweli tulimuacha hai!” Sudi alisema kwa mshangao.
Hapo hapo wakaanza kukimbia kuelekea katika jengo lile. Wote wakaonekana kuchanganyikiwa kupita kawaida, hawakuamini kama kweli walikuwa wamemuacha Yusufu hai katika jengo lile pasipo kumuua. Ni kweli kwamba mtu wao ambaye alikuwa amewatuma kumuua Yusufu alikuwa amekufa lakini hiyo haikuwa sababu ya kumuacha Yusufu hai, ilibidi wamuue tu.
Mara baada ya kufika katika jengo lile kule juu, Yusufu hakuwepo jambo ambalo lilionekana kuwashangaza kupita kawaida. Wakabaki wakiangaliana, hapo ndipo wakakumbuka kwamba walikuwa wameshauriana kwamba wamuache Yusufu hai. Kila mmoja alionekana kujishangaa kwa kupanga uamuzi ule, hakukuwa na mtu ambaye alitambua kwamba kulikuwa na nguvu ya ziada, nguvu ambayo iliwaingia na kuanza kumuonea huruma Yusufu.
Huku wakiwa wamepigwa na butwaa katika jengo lile, kwa mbali wakaliona gari lile la Yusufu ambalo walikuwa wamekuja nalo mahali pale likiwa linaanza kuondoka katika viwanja vile vya Tanganyika Pakers. Kila mmoja akashtuka na kujua kwamba yule mtu ambaye alikuwa ameingia ndani ya gari lile alikuwa Yusufu.
Hapo ndipo walipoanza kuteremka ngazi kwa kasi ya ajabu kuelekea chini huku wakiwa na lengo la kulifuata gari lile. Mpaka wanafika chini ya jengo lile, gari lile likawa limekwishaingia katika barabara ya lami na kisha kuendeshwa kwa mwendo wa kasi kuondoka katika maeneo hayo.
“Tumemkosa...!” Sudi alisema huku akijishika kichwa chake kwa hali ya kusikitika.

je nini kitaendelea?
 
MTUNZI: NYEMO CHILONGANI.
MAHALI: DAR ES SALAAM.
SIMU: 0718 069 269.

NITAKAPOKUFA 25

Yusufu alikuwa akitetemeka kwa woga kwani alijua muda wowote ule kuanzia kipindi hicho mtu ambaye alikuwa akisubiriwa kwa ajili ya kazi moja ya kumuua basi angefika mahali hapo na kumuua. Bado sala ya kimoyo moyo ilikuwa ikiendelea moyoni mwake huku akimtaka Mungu amuepushe na kile ambacho kilitaka kutokea mahali pale.
Alijua fika kwamba toka aingie ndani ya jiji la dar es Salaam hakuwahi kuingia msikitini, alijua fika kwamba ulimwengu wa giza ndio ambao alikuwa akiuabudu katika maisha yake yote ila katika siku hiyo, moyo wake ulikuwa ukimuomba Mungu aweze kumuokoa katika hali ambayo alikuwa nayo mahali pale.
Yusufu hakuonekana kuamini mara baada ya kusikika kwamba mtu ambaye alikuwa akitarajiwa kufika mahali hapo alikuwa amepata ajali. Hiyo ikaonekana kuwa furaha kwake, alijua kwamba ule ulimwengu wa giza bado ulikuwa katika upande wake, haukutaka kuacha auawe katika kipindi hicho kwa sababu bado walikuwa wakiendelea kumhitaji.
Alipowasikia Sudi na wenzake wakipanga shauri la kumuacha hai mahali pale, moyo wake ukafurahi zaidi kwa kuona kwamba kila kitu ambacho alikuwa akitaka kifanyike kilikuwa kinafanyika kama alivyokuwa akitaka. Sudi na wenzake hawakuendelea kubaki ndani ya jumba lile, walichokifanya ni kuondoka mahali hapo.
Yusufu hakutaka kubaki, alichokifanya nae ni kuanza kushuka ngazi katika jumba lile bovu na kuanza kukimbia kuelekea upande wa kaskazini. Yusufu alikimbia kwa muda fulani na kisha kusimama. Moyo wake akauhisi kuanza kujawa na uzito fulani hali iliyomuonyesha kwamba hakutakiwa kukimbilia kule alipokuwa akikimbilia bali alitakiwa kwenda kule kulipokuwa na gari lake.
Yusufu hakutaka kujiuliza mara mbili mbili, japokuwa aliliona gari lake likiwa linaanza kuondoka mahali pale, akaanza kuelekea kule lilipokuwa. Alipolifikia, akaingia huku likiwa limeendeshwa kwa umbali fulani. Bahati ilikuwa upande wake, ufunguo wa gari ulikuwa mule garini, alichokifanya ni kuutekenya ufunguo ule na kisha kuliondoa gari mahali pale huku akiwa hajui sababu ambayo iliwafanya vijana wale kuliacha gari lake huku wakiwa wameliendesha kwa umbali fulani.
“Asante Mungu kwa kusikia maombi yangu” Yusufu alisema huku akiwa amekwishaingia barabara ya lami na kuanza kuelekea nyumbani kwake.
****
Yusufu hakutaka kukaa kimya, siku iliyofuata akaamua kuwafuata waandishi wa habari na kisha kuwaambia kwamba alikuwa ametekwa na watu wasiojulikana kwa lengo la kuuawa ila Mungu alikuwa upande wake na hivyo kumsaidia. Maneno yale yakaonekana kumshtua kila mtu aliyeyasikia, roho ya Yusufu ikaonekana kuwa dili kwa watu ambao walikuwa wakimtafuta katika kipindi hicho.
Yusufu hakumpa taarifa Manka kwamba mtu ambaye alikuwa mwanaume wake ndiye ambaye alikuwa amewatuma vijana ambao walikuwa wamemteka na hatimae kutaka kumuua katika jumba bovu lililokuwa katika viwanja vya Tanganyika Pakers. Magazeti pamoja na vyombo mbalimbali vya habari vikaandika jambo lile ambalo lilizidi kumpaisha Yusufu zaidi na zaidi. Japokuwa kila siku maisha yake alikuwa akijulikana sana lakini bado katika kipindi hicho alizidi kusikika zaidi na zaidi.
Yusufu akazidi kuitwa katika matamasha mbalimbali ambayo yalikuwa yakimuingizia kiasi kikubwa cha fedha. Katika kipindi cha miaka mitatu tu, Yusufu alikuwa amepata kiasi kikubwa cha fedha ambacho kilimfanya hata wakati mwingine kufikiria kuchana na muziki na kujiingiza katika mambo ya biashara.
Japokuwa alikuwa akitanua kila siku lakini bado kichwa chake kilikuwa kikifikiria kitu kimoja tu, kuitwa katika ulimwengu wa giza na kisha kupewa adhabu juu ya kile ambacho kilikuwa kimetokea, kuvunja moja ya masharti ambayo walikuwa wamempa, kufanya mapenzi na Manka katika siku ya Jumapili, siku ambayo ilionekana kuwa mbaya kwake.
Alikunywa na kula lakini wakati mwingine alijiona kuwa kama kwenye kifungo kikubwa moyoni mwake, alijua kwamba ulimwengu ule wa giza ulikuwa umempa kila kitu lakini ulikuwa umemnyima uhuru wa kufanya kila kitu vikiwepo kupata mtoto na hata kufanya mapenzi katika siku ya Jumapili na Jumatano, siku ambazo alikuwa akishinda klabu za usiku pamoja na wanawake wazuri na kuondoka bila ya kufanya kitu chochote kwao.
Moyoni alijihisi upweke sana hali ambayo ikamfanya kuwa na mawazo kila wakati. Kuna wakati alijipa moyo kwamba inawezekana kwamba watu hao wa ulimwengu wa giza walikuwa wamesahau kumpa adhabu lakini katika kipindi kingine aliisikia sauti ikimwambia kwamba hawakuwa wamesahau ila kuna siku moja angeitwa na kuambiwa adhabu yake ingekuwa nini.
Alipata kila kitu katika maisha yake lakini uhuru ndicho kitu ambacho kilimfanya kujiona kuwa kwenye kifungo kikubwa sana. Kwa wakati mwingine alikuwa akitamani sana kuachana na vitu vile lakini alijua fika kwamba kama angeamua kufanya hivyo basi wangechukua kila kitu kilicho chao ambacho walikuwa wamempatia katika maisha yake.
Asingekuwa tena na utajiri, mvuto ungeondoka machoni mwa watu, wasichana wasingempenda tena na hivyo kurudi katika maisha ya kimasikini ambayo alikuwa akiishi katika kipindi cha nyuma. Kila alipokuwa akifikiria kuhusu wazo lake la kurudisha kila kitu ambacho alipewa, moyo wake ulikataa katakata kumruhusu kufanya hivyo.
“Ila inawezekana wakawa wameamua kuniacha kwa sababu nimewatumikia sana” Yusufu alijisemea.
“Mmmh! Inawezekana kweli wakawa na mioyo ya msamaha kirahisi namna hiyo? Lakini mbona hawaniiti na huu ni mwezi unakatika? Inawezekana wakawa wamenisamehe” Yusufu alikuwa akijiuliza maswali mengi na kujijibu.
Kwa wakati huo hakuwa na uhakika kama alikuwa amesamehewa au watu wa ulimwengu ule walikuwa wakisubiri siku maalumu ifike na hatimae kumuita tena katika sehemu yao ya makutanio na hatimae kumpa adhabu juu ya kile ambacho alikuwa amekifanya. Kama alivyokuwa akiwaza na ndicho kitu ambacho kilitokea.
Baada ya siku kadhaa huku akiwa chumbani kwake usiku, kioo kile ambacho kilikuwa mlango wake mkuu wa kuingilia katika ulimwengu wa giza kikaanza kuonyesha miale kadhaa ya radi huku kwa mbali ngurumo zikiwa zinasikika. Yusufu akashtuka kutoka usingizini, alipoiona miale ile ya radi, mapigo yake ya moyo yakaanza kudunda kwa kuona kwamba siku hiyo ilikuwa ni siku ya balaa.
Akaamka kutoka kitandani mwake na kisha kuvua nguo zote na kubaki mtupu. Akaanza kukifuata kioo kile na kisha kuingia katika ulimwengu huo. Siku hiyo kwake ikaonekana kuwa siku tofauti, mwili wake ulikuwa ukitetemeka kupita kiasi, woga ulikuwa umemtawala sana kwa kuona kwamba siku hiyo ilikuwa ni siku ya hatari sana kwake.
Alipofika katika mlango wa nyumba kubwa ambayo ilikuwa ikifanyika kama makutano yao, nje ya nyumba ile kulikuwa na mavazi ya aina mbili, mavazi yalikuwa na rangi nyeusi na rangi nyekundu. Akainamana na kutaka kuchukua mavazi meusi ambayo mara kwa mara alikuwa akiyavaa, akakatazwa na kutakiwa kuchukua mavazi mekundu, mavazi ambayo yalikuwa kama shuka kubwa.
Hapo ndipo Yusufu alipojua kwamba siku hiyo ilikuwa ni siku ya balaa ndani ya jengo lile kutokana na kutakiwa kuchukua mavazi mekundu, mavazi ambayo yalimaanisha umwagaji wa damu katika siku hiyo. Yusufu akaanza kupiga hatua kuelekea ndani ya jengo lile. Alipoingia ndani, wenzake walikuwa wamekwishafika kitambo na hali ilionyesha kwamba ni yeye tu ndiye ambaye alikuwa akisubiriwa mahali hapo.
Yusufu akawa anatembea taratibu huku akionekana kuwa mwenye wasiwasi mwingi. Kiumbe cha ajabu, kiumbe ambacho kilikuwa na mwili wa kibinadamu ila baadhi ya viungo vilikuwa kama vya paka akatokea mahali hapo na kisha kumtaka yusufu kusimama. Yusufu akatii, akasimama na kisha kuanza kukiangalia kiumbe kile.
Mapigo yake ya moyo yalikuwa yakiongezeka kudunda kupita kawaida, siku hiyo ikaonekana kuwa siku ya hatari tupu. Viumbe wengine wawili wakatokea mahali pale na kisha kuanza kumwangalia, bado Yusufu alikuwa akitetemeka tu.
“Umevunja moja ya masharti yetu” Kiumbe kile alimwambia Yusufu ambaye alibaki kimya huku akiwa ameuinamisha uso wake chini.
“Kwa sababu umevunja moja ya masharti yetu, tutakuadhibu” Kiumbe yule alimwambia Yusufu ambaye alikuwa kimya.
Yusufu akatakiwa kupiga hatua mbele mpaka karibu na kioo kile kilichokuwa mbele ya chumba kile. Kila mtu mahali hapo alikuwa kimya, watu ambao walikuwa wamezunguka katika kila sehemu ya chumba kile, nao walikuwa kimya huku wakiwa wameviinamisha vichwa vyao chini.
Yusufu akapiga hatua mpaka mahali pale. Chini ya kioo atika meza kulikuwa na kisu ambacho akaamriwa kukichukua, akakichukua huku mikono yake ikitetemeka kupita kawaida. Kioo kile ambacho hakikuwa kikionyesha kitu chochote kile, kikaanza kuonyesha mianga ya radi, sehemu ile ikajaa moshi mwekundu ambao kwa mtu wa kawaida ungemfanya kuogopa sana. Ghafla katika kioo kile ikatokea taswira ya mama yake, Bi Fatuma ambaye alikuwa amelala.
“Tunataka utoe kafala kwa kile ulichokifanya cha kuvunja moja ya masharti yetu” Kiumbe yule alimwambia Yusufu ambaye alikuwa akitetemeka kwa woga.
“Nimuue mama yangu?” Yusufu aliuliza huku akionekana kutokuamini.
“Ndicho unachotakiwa kukifanya” Kiumbe yule alimwambia Yusufu.
Yusufu akabaki kimya kwa muda, akaanza kuwaangalia watu wale ambao walikuwa wamekusanyika ndani ya ukumbi wa nyumba ile na kisha kuyapeleka macho yake kwenye taswira ya mama yake katika kioo kile, bado Yusufu alikuwa akitetemeka tu. Mawazo yake yakaanza kurudi nyuma toka katika kipindi ambacho alikuwa mtoto, kipindi ambacho mama yake alikuwa ameangaika sana kwa ajili yake.
Mambo mengi ambayo yalitokea katika miaka ya nyuma yakaonekana kuugusa moyo wake, kwa jinsi ambavyo mama yake alivyokuwa ameangaika kwa ajili ya maisha yake na leo hii amuue kwa kumtoa kafala, lilionekana kuwa jambo moja ambalo wala hakutaka litokee. Mama yake ndiye mtu pekee ambaye alikuwa amembakisha katika dunia hii, kumuua mama yake kulimaanisha kwamba alikuwa akimpoteza mtu muhimu sana maishani mwake.
“HAIWEZEKANI. SIWEZI KUMUUA MAMA YANGU” Yusufu alisema kijasiri huku akikitupa kisu kile chini.
Watu wote ambao walikuwa wamekusanyika ndani ya ukumbi ule wakaonekana kushtuka, maneno ambayo aliyaongea Yusufu kwa wakati huo yalimshtusha kila mmoja mahali pale. Hilo lilikuwa tukio la kwanza kutokea kwa mtu kukataa kumtoa kafala mtu ambaye aliambiwa amtoe kafala katika kipindi ambacho alivunja moja ya masharti aliyopewa.
“Siwezi kumuua mama yangu. Ametoka mbali sana pamoja nami. Amenilea katika mazingira ya shida sana. Yeye ndiye mtu pekee ambaye amebaki katika maisha yangu. Kumuua mama yangu, hicho ni kitu kisichowezekana kabisa. Mliniambia nimuue baba yangu, nilifanya hivyo, bado hamjaridhika, mnaitaka roho ya mama yangu, hakika sitoweza kuunyanyua mkono wangu kumuua mama yangu” Yusufu aliwaambia huku akianza kulia.
“Kama hautaki kufanya hivyo, tunavunja mkataba na wewe. Utatakiwa kurudisha pete zetu, nguo zetu., mali zetu, utajiri wetu na kila kitu ulichochukua kutoka kwetu” Kiumbe yule alimwambia Yusufu.
“Sirudishi kitu chochote kile. Pete siwapi, utajiri siwarudishii, yaani kwa kifupi ni kwamba siwapi kitu chochote kile. Kama mtaweza, mtavichukua kinguvu, ila kiukweli siwezi kuwakabidhi vitu hivi” Yusufu aliongea kwa sauti ya juu iliyojaa hasira.
Muda huo alionekana kama mtu aliyechanganyikiwa, Yusufu alionekana kuwa radhi kwa kila kitu katika kipindi hicho, hakuwa radhi kurudisha kitu chochote kile ambacho alikuwa amepewa katika kipindi cha nyuma. Alikuwa radhi kupokonywa kinguvu lakini si kurudisha kwa mkono wake.
“Tunachukua kila kitu tulichokupa. Ulinzi wetu juu ya afya yako tunauchukua kuanzia sasa na kuuacha ugonjwa wa UKIMWI ukutafune mpaka kifo chako. Ndani ya mwezi mmoja tu, usiporudisha kitu chochote kile tunakuua kwa ugonjwa huo. Tarehe 2 mwezi ujao ndio utakuwa mwisho wako wa kuvuta pumzi ya dunia hii. Tutakumaliza kwa ugonjwa huu. Tutakifanya kifo chako kuwa kifo cha aibu kwa kila mtu atakayekisikia” Kiumbe yule alimwambia Yusufu huku siku hiyo ikiwa ni tarehe 2 mwezi wa tano.
“Fanyeni chochote kile lakini siwezi kurudisha chochote mikononi mwenu. Binadamu ni mavumbi na mavumbini atarudi” Yusufu alisema na hapo hapo kuanza kuondoka. Yusufu hakutaka kutembea, akaanza kukimbia kutoka ndani ya nyumba ile. Kila kitu ambacho alikuwa amewaambia ndicho alichokifanya, hakurudisha kitu chochote kile ambacho alikuwa amepewa kutoka katika ulimwengu wa giza. Alikuwa tayari kufanya kitu chochote lakini si kumuua mama yake wala kurudisha vitu ambavyo alikuwa amepewa awe navyo.


Itaendelea kesho.
 
MTUNZI: NYEMO CHILONGANI.
MAHALI: DAR ES SALAAM.
SIMU: 0718 069 269.

NITAKAPOKUFA 26

ANGALIZO:
Ukiona huko chini imekuandikia "SEE MORE" au "NEXT PAGE" Basi fanya kushare au nenda kwenye WALL yangu utaiona yote.



Yusufu hakuonekana kuwa na raha hata mara moja, muda mwingi alionekana kuwa mtu wa mawazo kupita kawaida. Adhabu ambayo alikuwa amepewa ya kuweza kumuua mama yake kwake ilionekana kuwa kubwa kubebeka kwa mkono wake mwenyewe. Njia nzima alikuwa akifikiria, hakutaka kujiona akimpoteza mama yake ambaye kwake alionekana kuwa mtu muhimu kuliko mtu yeyote ambaye alikuwa amebaki katika dunia hii katika kipindi hicho.
Alipofika nyumbani, kitu cha kwanza alichokifanya ni kulala usingizi mzito. Asubuhi ilipoingia, moja kwa moja akaanza safari ya kuelekea Bagamoyo. Huko, akaenda kuonana na mama yake. Kitendo cha kumtia mama yake machoni mwake, machozi ya uchungu yakaanza kumlenga na hatimae kumtoka.
Moyoni alijisikia uchungu, alikuwa akimpenda mama yake kupita kawaida katika maisha yake. Alichokifanya ni kumsogelea mama yake na kisha kumkumbatia. Bi Fatuma hakuelewa ni kitu gani ambacho kilikuwa kikiendelea katika kipindi hicho, yeye mwenyewe alikuwa akijisikia uchungu sana kila alipokuwa akimwangalia mtoto wake wa pekee, Yusufu akiwa analia.
“Nakupenda mama” Yusufu alimwambia mama yake.
“Nakupenda pia” Bi Fatuma alimwambia Yusufu.
Siku hiyo walikaa na kuongea mengi, muda mwingi Yusufu alionekana kuwa mtu wa huzuni, alijua fika kwamba hakuwa na siku nyingi za kuishi ndani ya dunia hii. Alifahamu fika kwamba alikuwa njiani kuelekea kaburini jambo ambalo lilikuwa likimhuzunisha kupita kawaida.
“Mbona leo unaonekana kuwa hivyo Yusufu?” Bi Fatuma alimuuliza Yusufu ambaye alionekana kuwa na huzuni kipindi chote.
“Ninataka kumrudia mke wangu mama” yusufu alimjibu mama yake.
“Unataka kumrudia Samiah?”
“Ndio mama. Ninataka kumrudia mke wangu. Ninataka kuishi na familia yangu” Yusufu alimwambia mama yake.
“Hilo ndilo linalokufanya kuwa hivyo mwanangu? Au kuna kitu kingine?” Bi Fatuma alimuuliza.
“Hapana mama. Ni hilo tu”
“Hakuna tatizo. Umekwishaongea nae juu ya hilo?”
“Hapana”
“Hata haujaongea nae simuni?”
“Sijaongea nae”
“Ongea nae kwanza”
“Hapana mama. Nataka twende Dodoma pamoja” Yusufu alimwambia mama yake.
Haikuwa na jinsi, walichokifanya ni kuelekea jijini Dar es Salaam ambapo huko wakakata tiketi ya ndege na kisha kuanza kuelekea Dodoma. Bado Yusufu hakuonekana kuwa na furaha kabisa, tofauti na kuihitaji familia yake lakini alionekana kwamba kulikuwa na kitu kingine ambacho kilikuwa kimemsibu moyoni mwake.
Ndege ilichukua dakika sitini na ndipo ilipoingia katika uwanja wa ndege wa Dodoma ambapo wakateremka na kisha kukodi teksi ambayo iliwapeleka mpaka katika mtaa wa Area C ambapo alikuwa akiishi Samiah.
Kitendo cha Yusufu kuonekana ndani ya eneo la nyumba hiyo lilionekana kumshtua kila mtu ambaye alikuwa akimwangalia. Yusufu hakutaka kujali sana, alichokifanya ni kuanza kuelekea katika nyumba hiyo pamoja na mama yake na kisha kukaribishwa.
Siku hiyo hakukuwa na sababu ya kupoteza muda, Bi fatuma akaanza kuongea kile ambacho kilikuwa kimewaleta mahali pale kwamba Yusufu alikuwa akitaka kurudiana na mke wake, Samiah. Jambo hilo lilionekana kuwa gumu kukubalika moyoni mwa Samiah kwani alijua fika kwamba kulikuwa na uwezekano wa mwanaume huyo kuwa katika matatizo makubwa na ndio maana alikuwa akiwahitaji.
“Ila aliniacha kwa dharau sana” Samiah alimwambia mama yake, Bi Warda.
“Hata kama Samiah. Kumbuka kwamba alikupa talaka moja” Bi Warda alimwambia Samiah.
Bi Warda alichukua muda wa dakika arobaini na tano kumbembeleza Samiah. Samiah akaonekana kuelewa kitu ambacho kilimfanya kuelekea sebuleni pale huku akionekana kuwa mwingi wa huzuni. Alichokifanya Yusufu mara baada ya kumtia machoni Samiah, akasimama, akamsogelea na kisha kumkumbatia.
Yusufu akaanza kulia, hakuamini kama kweli Samiah alikuwa amemsamehe kwa kila kitu na kwa kipindi hicho alikuwa akirudi nae kuishi maisha kama zamani. Baada ya kukumbatiana kwa muda mrefu huku wote wakilia, mtoto Nasri akaletwa mahali hapo, Yusufu akamchukua na kisha kumbeba huku akionekana kuwa mwingi wa furaha.
“Huyu ndiye atakuwa mrithi wangu wa kila kitu” Yusufu alisema huku akiwa amembeba nasri mikononi mwake.
Kilichoendelea ni kulala Dodoma na kisha kesho asubuhi kurudi jijini Dar es Salaam huku Yusufu akiwa amekwishawaambia marafiki zake wote kwamba alikuwa akirudi jijini huku akiwa pamoja na familia yake. Hiyo ikaonekana kuwa furaha kwa marafiki zake ambao wakawapelekea taarifa ile waandishi wa habari.
Asubuhi ya saa nne waandishi wa habari tayari walikuwa wamekwishafika katika uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere kwa ajili ya kumpiga picha Yusufu huku akiwa pamoja na familia yake.
Ndege ya precision Air ilipoanza kuingia, waandishi wa habari wakajiandaa vilivyo. Yusufu alipotoka katika jengo la uwanja wa ndege, waandishi wakaanza kumpiga picha na huku wengine wakianza kumfuata kwa ajili ya kumhoji maswali machache.
“Ndugu mwandishi. Mke ni mke na familia ni familia. Ninampenda sana mke wangu na ninampenda sana mtoto wangu” Yusufu alimwambia mwandishi wa habari.
“Na vipi kuhusu Manka?”
“Sijali chochote kile. Yeye alikuwa msichana wa mpito kama walivyokuwa wengine, sitotaka kujali chochote kuhusu yeye. Ninachokijali ni familia yangu tu” Yusufu alimjibu mwandishi.
“Kwa hiyo tutegemee nini kutoka kwako?”
“Mengi. Ila mnatakiwa kutegemea albamu yangu iitwayo NITAKAPOKUFA pamoja na kitabu cha maisha yangu cha NITAKAPOKUFA ambacho ningependa vianze kuuzwa tarehe 2 mwezi ujao” Yusufu alimwambia mwandishi wa habari.
“Mbona albmu yako hiyo pamoja na kitabu cha maisha yako umevipa jina linalofanana tena likiwa na msismko mkubwa?” Mwandishi alimuuliza.
“Duniani tunapita tu, bado tupo safarini kwa sasa. Ni lazima tujue kwamba kuna siku tutakufa, sisi tutaendelea kuwa mavumbi na mavumbini tutarudi” Yusufu alimwambia mwandishi wa habari.
Hawakutaka kukaa sana mahali hapo, moja kwa moja wakaanza kuelekea garini ambapo Kelvin alikuwa amekuja kuwachukua mahali hapo. Njiani, kidogo japo si sana Yusufu alikuwa akionekana kuwa na furaha, uwepo wa familia yake ulionekana kumfurahisha kupita kawaida.
Walipofika nyumbani, moja kwa moja wakaelekea ndani ambapo wakakaa kochini huku Yusufu akionekana kuwa katika hali ambayo ilionyesha kwamba hakuwa na furaha kabisa japo tabasamu la kinafiki lilikuwa likionekana usoni mwake.
“Nataka kuandika kitabu cha maisha yangu” Yusufu aliwaambia.
“Mbona mapema sana?” Kelvin alihoji.
“Yeah! Hiyo ni kwa sababu sina muda mrefu wa kuishi” Yusufu alijibu.
“Mmmh! Kuna nini tena?” Bi Fatuma aliuliza huku akionekana kushtuka.
“Nitakufa, tena si muda mrefu kuanzia sasa” Yusufu aliwaambia.
“Mbona unaonekana kutokuwa sawa Yusufu. Kuna nini mpenzi?” Samiah alimuuliza Yusufu mbaye akaanza kutoka na machozi.
“Naombeni mnisamehe kwa kila kitu. Sina muda mrefu wa kuishi kuanzia sasa. Naomba unisamehe mama” Yusufu alisema huku akiinuka kutoka katika kochi na kupiga magoti mbele ya mama yake.
“Nimekwishakusamehe. Ila kuna nini Yusufu? Mbona unatuchanganya?” Bi Fatuma alimuuliza Yusufu.
“Ninahitaji kuishi na familia yangu katika hizi siku za mwisho mama. Nimekuwa mtu muovu sana katika maisha yangu” Yusufu alimwambia mama yake.
“Yusufu, mbona unaonekana kutokueleweka rafiki yangu?” Kelvin aliuliza.
“Ninakwenda kufa Kelvin. Ninakwenda kuacha kila kitu nilichokuwa nacho. Ila kabla sijafa nahitaji mnisamehe sana” Yusufu aliwaambia.
“Tatizo nini Yusufu?” Samiah aliuliza huku akiinuka.
“Nilimuua baba” Yusufu alisema na kisha kuanza kulia.
Kila mmoja mahali hapo akaonekana kushtuka, hawakuamini kile ambacho kilikuwa kimesemwa mdomoni mwa Yusufu ambaye alikuwa akilia kupita kawaida kama ishara ya kuwaonyeshea kwamba alikuwa akihuzunika sana kwa kile ambacho alikuwa amekifanya katika maisha yake.
Katika hali isiyotarajiwa, Bi fatuma akaanza kulia, akaonekana kushtuka kupita kawaida. Hakukuwa na mtu ambaye alionekana kuyaamini maneno yale ya Yusufu moja kwa moja, kwao waliyaona maneno yale kuwa ya uongo.
“Nimemuua baba kwa tamaa zangu za fedha na umaarufu. Nimekuwa nikimtumikia shetani katika kipindi chote hiki” Yusufu aliwaambia maneno ambayo yalionekana kuwashtua zaidi.
“Imekuaje Yusufu? Usimlize Bi Mkubwa, hebu tueleze kipi kimetokea” Kelvin alimwambia Yusufu.
Hapo ndipo ambapo Yusufu akaanza kuelezea kila kitu ambacho kilikuwa kimetokea katika maisha yake toka siku ya kwanza ambayo alikuwa ameamua kuiuza nafsi yake katika ulimwengu wa giza. Ilikuwa ni stori ndefu na ya kusisismua ambayo ilionekana kumshtua kila mtu mahali pale. Stori hiyo ndefu ikasababisha kilio kikubwa kutoka kwa Bi fatuma na Samiah.
“Nimesababisha mauaji ya watu wengi maishani mwangu” Yusufu aliwaambia huku akiendelea kulia.
Kila mmoja mahali pale alionekana kuwa na huzuni kupita kawaida, historia ambayo Yusufu aliizungumza mahali pale ilikuwa imewagusa kupita kawaida. Hawakuamini kwamba Yusufu angeweza kufanya yale ambayo alikuwa ameyafanya. Umaarufu wote ambao alikuwa ameupata, mvuto wote ambao alikuwa ameupata vyote hivyo vilitokana na mkataba wa damu ambao alikuwa ameusaini katika ulimwengu wa giza.
Maneno yake yalimuuma kila mmoja mahali pale, Yusufu yule ambaye alikuwa amefanya mambo mengi katika maisha yake, mtu ambaye alikuwa amependwa na watu wengi katika maisha yake leo hii kila kitu kilikuwa kimejulikana katika familia yake.
“Kwa nini ulifanya haya Yusufu?” Mama yake, Bi Fatuma aliuliza huku akilia.
“Umasikini mama. Sikuwa nikiupenda umasikini, nilitaka kujiondoa katika maisha haya ambayo yalikuwa yakinikasirisha kila siku. Pamoja na hayo, nikatamani fedha, nikatamani kutembea na wanawake wazuri, nikatamani kuendesha magari ya kifahari pamoja na kumiliki nyumba nyingi za gharama. Hizo ndizo sababu ambazo zilinifanya kumtumikia shetani mpaka siku ambayo waliniambia nikuue na kukataa” Yusufu alimwambia mama yake.
Japokuwa moyoni alikuwa ameumia sana lakini hakukuwa na jinsi, Bi Fatuma akasimama kutoka pale alipokuwa amekaa na kisha kumsimamisha Yusufu na kukumbatia. Katika kipindi hicho, hakikuwa kipindi cha kupeana lawama kwa kile ambacho kilikuwa kimetokea, walitakiwa kusahau kile kilichopita na kupanga mambo mengine.
“Ninakufa mama. Ninakufa nikiwa mdogo sana, ninakufa nikiwa katika mafanikio makubwa sana” Yusufu alimwambia mama yake huku akiendelea kulia.
“Mungu atakuwa pamoja nawe kijana wangu”
“Hapana mama. Mimi ni muovu, moyo wangu umejaa dhambi, mikono yangu imejaa damu. Nimesababisha vifo vya watu wengi katika nchi hii, watu ambao walinionyeshea mapenzi, watu ambao hawakuwa na hatia” Yusufu alimwambia mama yake na kuendelea.
“Naombeni mnisamehe. Naombeni msamaha wenu kwa kila nilichokifanya” Yusufu alisema huku akiendelea kulia.
Siku hiyo ikaonekana kuwa ya huzini katika maisha ya kila mmoja aliyekuwa mahali hapo. Alichokifanya Yusufu ni kuingia ndani na kisha kuleta hati za nyumba zake pamoja na biashara zake na kisha kuliandika jina la mtoto wake, Nasri pamoja na mke wake, Samiah.
Yusufu hakuishia hapo, alichokipanga kukifanya ni kuzigawa fedha zake zote zilizokuwa benki ambazo zilikuwa ni zaidi ya bilioni mbili na kisha na kumgawia mama yake, mke na mtoto wake pamoja na mama yake.
“Sitakiwi kumiliki kitu kwa sasa. Ninakwenda kufa, haina jinsi, naomba mkubali kwamba ninakufa katika kifo kibaya sana” Yusufu aliwaambia.
****
Siku iliyofuata asubuhi na mapema, Kelvin akatumwa kwenda kumtafuta mwandishi bora wa vitabu katika kipindi hicho, George Iron Mosenya kwa ajili ya kumwandalia kitabu chake cha maisha yake kwa malipo makubwa. Mara baada ya Mosenya kufika katika nyumba ile, moja kwa moja akaanza kuongea na Yusufu.
“Ninataka uandike kitabu cha maisha yangu” Yusufu alimwambia Mosenya.
“Hakuna tatizo” Mosenya alijibu kwa haraka kwani nae aliona kama zali kuambiwa aandike kitabu cha mtu maarufu kama Yusufu.
“Ila ninataka kiuzwe kuanzia tarehe 2 mwezi ujao” Yusufu alimwambia Mosenya.
“Mmmh! Mbona haraka sana?”
“Ni kwa sababu sina muda mrefu wa kuishi katika dunia hii” Yusufu alimwambia Mosenya.
“Sawa. Hakuna tatizo ila itabidi hata malipo yake yawe makubwa kidogo” Mosenya alimwambia Yusufu.
“Hakuna tatizo. Unataka nikulipe kiasi gani?”
“Milioni nne”
“Hilo si tatizo. Nitakupa milioni tano” Yusufu alimwambia Mosenya.
Hapo ndipo Yusufu akamtahadhalisha Mosenya kwamba kila kitu ambacho angekwenda kumwambia muda huo kibaki siri yake na si kwenda kumwambia mtu yeyote yule mpaka kitabu kitakapotoka. Mwandishi Mosenya akakubali kwamba angekwenda kuitunza siri hiyo, hapo ndipo Yusufu alipoanza kumhadithia kila kitu.
Muda wote Mosenya alikuwa akimya huku akisikiliza kwa makini, kila kitu ambacho alikuwa akiambiwa alikisikiliza kwa makini kabisa huku akikataa kupitwa na kitu chochote kile hali iliyompelekea kuchukua simu yake na kisha kuanza kurekodi kila kitu ambacho aliongea Yusufu.
Ilikuwa ni stori ambayo ilimgusa sana Mosenya kiasi ambacho hakuonekana kuamini kwamba vile vitu ambavyo alikuwa akivisikia vilikuwa vikitokea na wala havikuwa simulizi kama ambavyo alivyokuwa akihisi katika kipindi cha nyuma.
Kila siku Mosenya alikuwa akifika nyumbani hapo na kuendelezewa stori ile mpaka wiki ya kwanza ilipokatika, katika kipindi ambacho Yusufu akaanza kuumwa. Kwanza akaanza kukonda, mwili wake ukaanza kukosa nguvu jambo ambalo lilimfanya kupelekwa hospitalini.
Kila mtu ambaye alikuwa amesikia hali ambayo alikuwa nayo Yusufu, alionekana kuumia kupita kawaida. Waandishi wa habari walipompiga picha na kutoa kwenye magazeti, watu walibaki wakishangaa kupita kawaida, hawakuamini kama yule ambaye alikuwa akionekana alikuwa Yusufu au mtu mwingine ambaye alionekana kuwa mfano wa Yusufu.
Kila mtu akaanza kuhoji ni kitu gani kilikuwa kimetokea mpaka ugonjwa wa ghafla vile kumpata lakini hakukuwa na mtu ambaye alipata jibu lolote lile.Yusufu aliendelea kuugua kitandani pale huku akiendelea kumwadithia mwandishi Mosenya kile ambacho kilikuwa kimeendelea katika maisha yake. Kadri siku zilivyokuwa kwenda mbele na ndivyo ambavyo alizidi kuugua zaidi na zaidi. Mara kwa mara watu walikuwa wakifika mahali hapo na kumpa pole.
“Hii ngoma aiseee” Jamaa mmoja alimwambia mwenzake.
“Ndio yenyewe. Daah! Jamaa kakonda mshikaji”
“Ndio hivyo. Kila siku tunaambiwa ugonjwa unaua lakini hatusikii. Sisi tunaendekeza kuwavua wanawake sketi bila kutumia kinga, tunaendelea kutumia vitu vyenye ncha kali tena kwa kuchangia pamoja. Majanga yake ndio huwa namna hii sasa” Jamaa mwingine alimwambia mwenzake.
“Albamu yangu ipo tayari na itaanza kuuzwa tarehe 2. Kitabu changu pia kinakamilika na kitaanza kuuzwa tarehe 2 pia. Fedha ambazo zitapatikana naomba ziwasaidie watoto yatima, zikiwezekana zijenge hospitali moja kubwa ya watoto mtaa wa Tandale. Kiasi kingine kitakachobaki naomba ipewe familia yangu pamoja na Kelvin ambaye ni rafiki wangu wa siku nyingi” Yusufu alimwambia mwanasheria wake.
“Hakuna tatizo. Sasa tugawe asilimia ngapi hapo?”
“Asilimia arobaini zitengeneze hospitali, asilimia kumi na tano apewe Kelvin, asilimia ishirini na tano ipewe familia yangu na asilimia ishirini apewe mama yangu” Yusufu alimwambia mwanasheria wake ambaye akaandika kila kitu.
Yusufu aliendelea kubaki kitandani pale zaidi na zaidi. Kutokana na jina lake kuwa kubwa sana, wanamuziki wengi kutoka barani Afrika wakafika nchini Tanzania kwa ajili ya kumuona Yusufu ambaye alikuwa amekonda sana kitandani. Viongozi mbalimbali wa nchi wakiwepo maraisi wa nchi mbalimbali nao hawakuachwa nyuma, walikuwa wakifika hospitalini hapo na kumuona Yusufu.
Yusufu akaonekana kuwa mfano mzuri kwa vijana wote ambao walikuwa wakiendekeza matendo ya ngono huku wakijifanya kutokujua ni kwa namna gani ugonjwa ule ulivyokuwa ukiua. Picha ya Yusufu kitandani pale ilikuwa ni fundisho tosha kwa kila mtu ambaye alikuwa akimwangalia.
Muda mwingi Yusufu alikuwa akilia. Hakuwa akilia kwa sababu alikuwa akifa, hapana, alikuwa akilia kwa sababu alikuwa amefanya mambo mengi sana ya kusikitisha katika ulimwengu huu hasa likiwa hili la kumtumikia shetani katika maisha yake.
“Ninakufa ila nitataka watanzania wajue kila kitu kuhusiana na maisha yangu ya nyuma” Yusufu aliwaambia waandishi wa habari katika kipindi ambacho walikuwa wamekusanyika hospitalini hapo.
“Hii ndio sababu ya kukufanya kuandaa kitabu na albamu yako ya mwisho ya NITAKAPOKUFA?”Mwandishi alimuuliza.
“Ndio”
“Kwa hiyo ulikuwa ukijua kwamba unakwenda kufa karibuni?”
“Ndio”
“Ulijuaje?”
“Majibu yote yatapatikana katika kitabu hicho” yusufu alijibu.
Taarifa ile ikatolewa katika magazeti mengi nchini kwamba siri ya kifo cha Yusufu ilikuwa ikipatikana katika kitabu cha stori ya maisha yake cha NITAKAPOKUFA ambacho kilitarajiwa kutoka tarehe 2 mwezi ujao, siku ambayo alisema kwamba ilikuwa siku ambayo atayafumba macho yake milele.
Kila mtu akawa na hamu ya kutaka kukisoma kitabu hicho, walitaka kufahamu mambo mengi katika kitabu hicho huku wakitaka kufahamu zaidi majina ya wasichana wengi ambao alikuwa amewaandika mule ambao alikuwa ametembea nao huku asilimia tisini na nane wakiwa wamekwishakufa kwa ugonjwa wa UKIMWI.
“Ninakupenda mke wangu. Ninaacha kila kitu katika maisha yako, sikutaka kumuachia hawala yeyote mali yangu yoyote, nimekuachia wewe mpenzi. Naomba uishi maisha mema, naomba umlee Nasri katika maisha bora mke wangu” Yusufu alimwambia Samiah ambaye muda mwingi alikuwa akilia.
“Nitafanya hivyo mume wangu” Samiah alimwambia Yusufu huku akiendelea kulia.
“Naomba uniahidi”
“Nakuahidi kufanya hivyo”
“Nashukuru. Nakuacha na maisha yako. Kufa kwangu haimaanishi kwamba nawe umeathirika, hapana. Katika kitabu changu nimejaribu kuelezea kwa kina kwamba niliporudiana nawe sikulala nawe kabisa. Ila katika yote kumbuka kwamba kuna wanaume wengi watataka kuja kukuoa, si kwamba wewe ni mzuri, bali wengi wao watakuja wakiwa na tamaa ya kumiliki kila ulicho nacho. Sikuzuii usiolewe, hapana. Kama ukitaka kuolewa, olewa ila yakupasa kuwa makini mke wangu” Yusufu alimwambia Samiah.
“Nimekuelewa mume wangu” Samiah alimwambia Yusufu ambaye macho yake akayageuza kwa Kelvin.
“Wewe ni rafiki yangu Kelvin” Yusufu alimwambia kelvin.
“Najua sana Yusufu. Wewe ni rafiki yangu ambaye kwangu nakuona ni ndugu yangu pia” kelvin alimwambia yusufu.
“Unaniona ninavyoteseka?”
“Ndio. Nakuona Yusufu”
“UKIMWI mbaya rafiki yangu. UKIMWI unatisha. Huu si ugonjwa wa kuchezea. Watu niliokuwa nawatumikia wameuacha huu ugonjwa unitese. Na kweli unanitesa sana hapa kitandani” Yusufu alimwambia Kelvin.
“Pole sana”
“Fedha nilizokuachia ni nyingi mno. Nakuomba usifanye mambo ya anasa, jaribu kuzifanyia mambo ya maana fedha hizo” Yusufu alimwambia Kelvin.
“Usijali”
“Ninakufa lakini nikiwa na uchungu sana. Nakufa nikiwa kijana mdogo sana. Nakuomba sana kelvin usifanye anasa. Nakusisitiza kwa mara nyingine, usifanye anasa” Yusufu alimwambia Kelvin.
“Usijali Yusufu” Kelvin alimwambia Yusufu ambaye akamgeukia mama yake.
“Umekuwa kila kitu kwangu mama. Wewe ndiye mtu ambaye nilikubakiza kwenye dunia hii, sikutaka kukuona unakufa ili niendelee kuishi katika maisha ya kitajiri, nilitamani kukuona ukiishi kila siku katika maisha yangu. Ninakufa sasa mama, ninahitaji umlee mtoto wangu ambaye ni mjukuu wako, Nasri katika malezi bora kama ambavyo ulivyokuwa ukinilea mimi” Yusufu alimwambia mama yake.
“Nitafanya hivyo Yusufu”
“Nakuomba usahau kila kilichopita mama”
“Usijali mwanangu. Siwezi kuvikumbuka tena” Bi Fatuma alimwambia Yusufu huku akilia.
Siku hiyo ndio ikawa siku ya mwisho kwa Yusufu kuongea nae, siku iliyofuata, siku ya tarehe 2 mwezi wa sita ikawa mwisho wa Yusufu kuvuta pumzi ya dunia hii. Alikufa huku pete zile ambazo alikuwa amepewa katika ulimwengu ule wa giza zikiwa vidoleni mwake ambapo baada ya dakika kadhaa, zikapotea.
Kioo pamoja na nguo ambazo alikuwa amekabidhiwa na kuviweka chumbani kwake navyo vikawa vimepotea. Hivyo ndivyo vitu ambavyo vilichukuliwa kutoka kwake. Fedha na mali nyingine vikaachwa kama vilivyo.
Huyo ndiye alikuwa msanii maarufu wa muziki barani Afrika, Yusufu au The Ruler kama alivyokuwa akijulikana na wengi. Maisha ya tamaa yalionekana kumkaribisha katika ulimwengu wa giza, ulimwengu ambao alikuwa ameamua kuutumikia kwa nguvu zote.
Siku hiyo ambayo alifariki ndio siku ambayo albamu yake aliyoiita NITAKAPOKUFA pamoja na kitabu cha stori ya maisha yake cha NITAKAPOKUFA vilipoanza kuuzwa. Vitabu na albamu ile vikagombaniwa sana mitaani. Kopi za vitabu zaidi ya milioni saba zikauzika, albamu yake ikauza zaidi ya kopi milioni tatu na nusu. Kiasi kikubwa sana cha fedha kikaingia, kiasi ambacho hakupata nafasi hata ya kutumia shilingi mia moja.
Japokuwa alikuwa amekufa, familia yake ikabaki kwenye utajiri mkubwa sana, rafiki yake, Kelvin nae akawa kwenye utajiri mkubwa sana. Yusufu akazikwa Bagamoyo, mazishi ambayo yalihudhuriwa na watu wengi zaidi ya mazishi ya mwalimu Nyerere au mwigizaji Steven Kanumba.
Maisha yake ya muziki pamoja na kazi zake zilionekana kuwa kumbukumbu vichwani mwa Watanzania ambao mpaka leo hii bado wanaendelea kumkumbuka kwa vile alivyokuwa amefanya hapa nchini. Japokuwa watu walijua fika kwamba alikuwa ametumia nguvu za giza lakini bado mapenzi yao yalikuwa makubwa kwa Yusufu, mvuto wake bado uliendelea kubaki mioyoni mwao.
“PUMZIKA KWA AMANI” Yalikuwa maneno ya kila mtu ambaye alikuwa akielekea Bagamoyo na kuliona kaburi lake.

MWISHO.
 
Cookies are required to use this site. You must accept them to continue using the site. Learn more…