MALIPO KITANDANI 💔
KISOLO CHA O3
Usiku kucha Erick hakulala, aliwaza mambo mengi ambayo alishawahi kufanya na Amidu, machozi yalimtiririk lakini hakuthubutu kumuamsha mkewe.
Taratibu aliamka kutoka kitandani akaenda kulilia nje, alikuwa anapata uchungu hasa, alijua kabisa mazishi ya Amidu hayatachukua muda mrefu, alijua atazikwa siku itakayofuata.
Saa kumi na mbili asubuhi, usingizi ulimuisha Aneth, na tena bila kufumbua macho alinyoosha mkono na kuuweka juu ya meza ndogo iliyokuwa karibu na kitanda akaanza kupapasa ili kuitafuta simu yake ambayo aliamini ameiweka pale usiku kabla ya kulala.
Alipopasa alishangaa kutokuigusa, akafumbua jicho moja na kuitazama ile meza, akagundua hakuna simu yake, alishtuka na kugeuka huku akiita “Erick” lakini cha kushangaza Erick hakuwepo pale ndani.
“Mh” aliguna halafu akatazama mlangoni, bado ulirudishiwa “We Erick” alisema kwa sauti kubwa na kuinuka akaketi kitandani na kujinyoosha huku akipiga miayo, ndipo akaangaza kule na huku lakini hakufanikiwa kuiona simu yake vile vile.
“Khaa kaondoka nayo?” Aliwaza na kushuka kitandani akasimama halafu akaita “Erick” huku akichungulia dirishani ndipo akamuona Erick akiwa amegemea vyuma vya baraza.
Kwa kuwa binti alikuwa hajavaa, ilibidi ajifunge kitenge hadi kifuani halafu akafungua mlango na kuchungulia. Bado Erick hakumtazama, aliendelea kuwaza huku akiangalia mbali.
“We Erick. Mume wangu” alisema binti na kufungua mlango akatazama, kulikuwa ni ghorofani
Erick aligeuza macho na kumtazama mwanamke wake bila kuongea chochote. Aneth alipomuangalia machoni, aliona macho ni mekundu, yanaonekana yamelia sana, uso umemkakamaa mtaalam, na alionekana hajalala.
Wasiwasi ulimjaa binti, hasa pale alipotazama mikono ya Erick alikuwa ameshikilia simu zote mbili ya kwake na ya mke wake. Hili lilimfanya mkewe akahisi labda Erick amekuta message au kitu chochote kibaya katika simu yake.
Aliwaza haraka haraka lakini akagundua kuwa hakuna chochote kibaya mbona, aliogopa na kuuliza
“Mume wangu uko sawa?”
Aneth alishaanza kutetemeka kwa wasiwasi, lakini Erick alisikitika na kufyonza kidogo kisha akasema “Kaoge uvae vizuri usikae hapa uchi” aliongea kwa hasira kidogo
“Lakini mbona kama hauko s.....”
“Kaogee”
Binti alitetemeka na kuingia ndani akiwa na wasiwasi zaidi, kwanini jamaa amfokee wakati ndoa ndo kabisa ni changa mno haina hata wiki moja.
Aneth alirudi ndani bado kichwani alijiuliza kwanini mumewe anakosa raha kiasi kile, alijua labda kuna kitu amemkosea, lakini kumbe Erick alikuwa na huzuni kisa amepata taarifa juu ya kifo cha kijana wake wa nguvu aliyefahamika kwa jina la Amidu Hassani kijana wa kiluguru halisi na rasmi.
Pia Erick alikuwa amechukua simu ya mkewe wakati akiwa amelala ili akiamka asiingie mtandaoni maana aliamini mkewe akiingia tu, lazima atakutana na ile habari kwamba Amidu amefariki na ataianza siku vibaya.
Aneth akiwa anaoga bafuni, basi huku nje Erick alipata simu kutoka kwa kijana mmoja aitwaye Dullah, pia wote hao walikuwa ni crew moja na kina Elisha pamoja na marehemu Amidu.
Erick aliipokea kwa sauti hafifu ili mkewe akiwa ndani asisikie
“Niambie kaka”
Dullah akamuambia “naamini una taarifa za kifo cha Amidu”
“Ndio kaka”
“Anapelekwa leo, mapema sana akazikwe, embu tuambie unafika?”
“Duuh kaka ni ngumu sana, kumbuka hatujakata tiketi ya ndege, tafadhali chelewesheni maiti tutakuja kesho asubuhi sana”
“Pamoja kaka, nitajitahidi”
“Sawa”
Erick alikata simu haraka baada ya kusikia mlango wa bafu umefunguliwa na mkewe.
Aneth alipofika pale, Erick alitabasamu ili kumuonyesha furaha lakini binti alipomtazama aligundua mumewe hayuko sawa.
“Erick niambie ukweli” alisema binti
“Ukweli wa nini?”
“Umekutana na kitu kibaya kwenye simu yangu? Mbona ulikuwa nayo na macho yameonekana yamekasirika na hata kulia”
“Hahahaaa.....hapana mpenzi, sijapata usingizi kabisa leo, nilikuwa na mawazo tele kuhusu biashara hasa baada ya kutompata tena Amidu.....anyway nimepata furaha ghafla baada ya Dullah kunipigia simu na kuniambia Amidu alikamatwa na polisi ndio maana tulikuwa hatumpati, hata hivyo yuko kituo cha polisi tutaenda kesho tukalishughulikie atoke maana biashara zitakwama” alisema Erick lakini ni dhahiri kwamba alikuwa anamdanganya mkewe, hakutaka mkewe ajue kwamba Amidu kafariki maana alijua binti atapaniki na anaweza kumletea matatizo makubwa zaidi ni heri akamficha ili warudi kwanza bara
“Mh kweli?” aliuliza binti
“Ndio”
“Kwani alikamatwa kwa kosa gani Amidu?”
“Nasikia alimgonga mtu na pikipiki”
Kidogo hili jibu lilimpa faraja mtoto wa kike maana nia yake alikuwa anataka tu Amidu awe na afya njema. Hakujua kwamba mumewe anamdanganya
Kule bara, Shekilango, Ubungo, Dar es Salaam kina Elisha, Dullah na marafiki wengine walikuwa wameingia katika chumba cha marehemu Amidu na walikuwa wanataka kuchukua vitu vyake ili wasafirishe pamoja na mwili kuelekea mkoani Morogoro
Katika kupekua pekua ndani, Elisha alikutana na barua mezani, akaichukua ile barua ambayo ilikuwa imeandikwa siku moja kabla ya kujiua kwa marehemu Amidu.
Elisha alianza kuisoma ile barua, ikamfanya akatoka jasho mwili mzima maana maneno yaliyokuwa yameandikwa kule ndani yalikuwa ni maneno mazito kweli kweli....JE BARUA ILIKUWA IMEHUSIANA NA NINI? USIKOSE KISOLO CHA 04
#L