Bwana Good akaruka ameshtuka sana, na mimi vile vile nikaruka nikatazama, na haya ndiyo niliyoona.
Pale yapata hatua ishirini kutoka nilipokuwa nimesimama mimi, na hatua kumi kutoka alipokuwako Bwana Good, niliona watu wamesimama. Wote walikuwa warefu na weusi, lakini wekundu kidogo kama rangi ya shaba nyekundu, na wengine walivaa manyoya marefu meusi na ngozi za chui; basi haya ndiyo niliyoona kwanza.
Mbele niliona kijana mwenye umri wa miaka kumi na saba amesimama kama ndiyo kwanza autupe mkuki. Mshale ule wa nuru niliouona ulikuwa mwangaza uliomulikwa na mkuki alioutupa.
Nilipokuwa nikitazama, mzee mmoja aliyekuwa kama askari akaja mbele akamshika mkono Yule kijana akasema naye, kisha wote wakatujia.
Bwana Henry na Bwana Good na Umbopa wote walishika bunduki zao wakaelekeza. Lakini wale watu wakazidi kutujia.
Basi niliona kuwa hawa kujua bunduki ni kitu gani, maana wangalijua wasingezi dharau hivyo. Basi nikawaambia waweke bunduki zao chini, maana watambue kuwa usalama wetu u katika kutafuta suluhu.
Wakafanya nilivyotaka, kisha nikaenda mbele kuonana na wale watu, nikamwambia Yule mzee kwa Kizulu. Maana nilibaatisha tu, lakini nilipoona kuwa wanafahamu maneno yangu nilistaajabu.
Yule mzee akaitikia, lakini maneno yake yaliachana kidogo na maneno ya Kizulu ila si sana, na mimi na Umbopa tuliweza kuyafahamu mara. Yule mzee akauliza, ‘Mmetoka wapi? Nyinyi ni nani? Kwa nini sura za nyinyi watatu ni nyeupe na huyu wanne ni kama sura zetu?’
Akapeleka mkono kumwonyesha Umboka. Nikamtazama Umbopa na nikajua kuwa anasema kweli. Sura yake ilikuwa kama sura za watu wale waliokuwa wamesimama mbele yetu, na maungo vile vile yalifanana nao. Nikamjibu, ‘sisi ni wageni tumekuja kwa amani, na mtu huyu ni mtumishi wetu.’
Akasema, ‘’Unasema uwongo, wageni hawawezi kuvuka ile milima.
Lakini uwongo wenu utafaa nini? Ikiwa nyinyi ni wageni lazima mtakufa, maana wageni wowote hawana ruhusa kuishi katika nchi hii ya Wakukuana. Hii ndiyo amri ya Mfalme. Basi mjiwekeni tayari kufa, e nyinyi wageni’’ Niliposikia maneno hayo nilifadhaika, na hasa nilipoona mikono ya wale watu inashuka na kushika visu vikubwa vilivyofungwa viunoni mwao. Bwana Good akauliza, ‘Je, mtu huyu anasema nini?’ Nikamjibu, ‘Anasema kuwa tutauawa .’
Bwana Good akaghumia, na kama ilivyokuwa desturi yake anapokuwa kwenye shida yeyote, alitia vidole kinywani akashika meno yake akayavuta chini, kisha akayaacha yarudi juu tena kwa kishindo. (Maana alikuwa ametiwa meno yaliyotengenezwa, kwa kuwa meno yake yameng’olewa).
Jambo hilo lilituokoa, maana mara walipoona hivyo, wale watu wakashtuka wakapiga kelele kwa hofu, wakaruka nyuma hatua mbili tatu. Nikasema, ‘Je, kuna nini?’ Bwana Henry akaninong’oneza akasema, ‘Ni meno ya Bwana Good nadhani alipoyavuta chini; wale watu wameona ni ajabu.
Haya, Bwana Good, yatoe kabisa.’ Basi akayatoa akayaficha upesi katika mkono wa shati lake.
Basi wale watu sasa walishikwa na udadisi wakasahau hofu yao kidogo, wakaja mbele, sasa ile habari ya kutuua waliisahau.
Yule mzee akaelekeza mkono wake kumwonyesha Bwana Good, naye amesimama amevaa shati na viatu tu, na tena amenyoa upande mmoja tu wa uso wake, akasema, ‘Ee nyinyi wageni, imekuwaje kuwa huyu mnene amevaa nguo maungoni ila miguu ni mitupu, na pia ndevu zaota kwa upande mmoja tu wa uso wake, naye, analo jicho moja ambalo linapenya nuru? Imekuwaje anaweza kuyatoa meno yake nakuyarudisha apendavyo?’
Nikamwambia Bwana Good, ‘Funua kinywa chako.’ Akafunua midomo yake kama mbwa mkali, wakaona kuwa hana meno kabisa, waliouona ni ufizi tu. Basi wale watu wakashtuka sana, wakasema, ‘Meno yake yako wapi sasa? Tulioyaona kwa macho yetu sasa hivi!’
Basi Bwana Good akageuza kichwa chake kidogo akainua mkono wake akayaweka meno ndani kwa siri, kisha akacheka. Kumbe! Kinywa chake kimejaa meno tena. Basi walipoona hivyo, Yule kijana alijiangusha chini akalia kwa hofu; na magoti ya Yule mzee yaligongana kwa kuogopa, akasema, na sauti yake ilitetemeka.
‘Naona kuwa nyinyi ni mizuka, maana hapana mtu aliyezaliwa na mwanamke mwenye ndevu upande mmoja tu wa uso, wala jicho moja linalopenya nuru, wala meno yanayotoweka na kuonekana tena. Ee mabwana, mtuwie radhi.’
Basi nikaona kama ni bahati yetu tena, nikamjibu kwa sauti kali, ‘Basi, msiogope; nitawataarifu habari za kweli. Sisi ni wanaume kama nyinyi lakini tumetoka katika ile nyota kubwa inayozidi kung’aa usiku.
Tumekuja kukaa pamoja nanyi kwa muda kidogo na kuwaleteeni neema. Mnaona rafiki zangu, nimejifunza lugha yenu ili niwe tayari.’
Wakaitika, ‘Ni kweli, ni kweli.’ Nikaendelea nikasema, ‘Na sasa, rafiki zangu, labda mnaogopa, mnafikiri kuwa tutamuua Yule kijana aliyemtupia mkuki huyu mwenzetu mwenye meno yanayotoka na kurudi tena. Maana mmetupokea vibaya baada ya safari ndefu tuliyoifanya ili kufika hapa.’
Yule mzee akasema, ‘Mabwana, mtusameheni nawasihi, maana yeye ni mwana wa mfalme na mimi ni mjomba wake. Akidhurika lazima mimi nitauawa.’ Yule kijana akaitikia, akasema, ‘Ndiyo, hayo ni kweli kabisa.’
Nikasema, ‘Labda mnafikiri kuwa hatuna nguvu za kujilipiza kisasi, lakini nitakuonyesheni. Haya wewe (nikamwita Umbopa kwa ukali sana) nipe mwanzi wangu wa uchawi unaosema.’ (Nikamwashiria anipe bunduki yangu).
Umbopa alitambua mara moja niliyotaka, akanipa bunduki yangu huku akiinamisha kichwa, na akasema, ‘Ni huu, bwana wa mabwana.’ Basi kabla sijamwambia anipe bunduki niliona swala amesimama juu ya mwamba kadiri ya mwendo wa hatua mia moja, nikanuia kumpiga.
Basi niliwaonyesha huyo swala, nikasema, ‘Niambieni kama yupo mtu aliyezaliwa na mwanamke anayeweza kumuua Yule mnyama kwa mshindo tu!
Yule mzee akajibu, ‘Hapana mtu, wala haiwezekani kabisa.’ Nikajibu, ‘Lakini mimi nitamuua.
Nikaelekeza bunduki yangu, Yule mnyama alikuwa mdogo lakini nilijua kuwa ni lazima nimpige. Nikavuta pumzi nikakaza mtambo wa bunduki kwa taratibu. Yule swala alisimama kimya kabisa. Bunduki ikalia, na mara Yule swala akaruka juu, akaanguka juu ya mwamba amekwisha kufa.
Basi, hapo wale watu waliguna kwa hofu, nikasema, ‘Haya, mkitaka mnyama nendeni mkamchukue huyo.’ Yule mzee akamwashiria mtu mmoja, na akaenda akamleta mnyama, wakamzungukia wakatazama tundu iliyoingia risasi.
Nikasema, ‘Kama hamsadiki hata sasa, basi mtu mmoja asimame mwambani nimfanye kama nilivyomfanya huyo swala. Hapo mtafahamu kuwa mimi sisemi maneno ya bure.’
Hapana aliyetaka kufanya hivyo mpaka Yule mwana wa mfalme aliposema, ‘Umesema vema. Wewe, mjomba wangu, nenda ukasimame mwambani, Uchawi ule umeua mnyama tu, hauwezi kumuua mtu.’
Lakini Yule mzee hakupenda shauri lile, akaudhika, akasema, ‘Hapana! Hapana! Macho yangu ya kizee yameona mambo ya kutosha. Watu hawa ni wachawi wa kweli kweli. Tuwachukue kwa mfalme.
Lakini ikiwa mmoja wenu anataka ushuhuda zaidi, basi na yeye asimame mwambani na ule mwanzi wa uchawi utasema naye.’
Hapo wote wakaanza kukataa. Na mmoja akasema, ‘Hapana, uchawi wa namna hiyo usipotee bure kwa ajili yetu. Sisi tumeridhika. Uchawi wote wa watu wetu hauwezi kufanya jambo kama hilo.’
Yule mzee akasema, ‘Ni kweli. Bila shaka ni kweli. Na sasa nyinyi watoto wa nyota, sikilizeni, nyinyi watoto wenye macho yanayong’aa, meno yanayotoweka, nyinyi mnaonguruma kwa ngurumo inayoweza kuua kwa mbali. Mimi ni Infadus, mwana wa Kafa, aliyekuwa mfalme wa watu wa Kukuana.
Huyu kijana ni Skraga, mwana wa Twala aliye mfalme mkuu wa Kukuana, Mlinzi wa Njia Kuu, Mtishaji wa adui zake, Mwenye elimu ya uchawi, Jemedari wa askari mia elfu, Twala mwenye chongo, Mweusi, Mtishaji.’
Nikasema kwa maneno ya dharau, ‘Mn, basi na tuongoze kwa Twala. Sisi hatutaki kusema na watu wanyonge na wadogo.’
Yule mzee akajibu, ‘Vema, mabwana wangu. Sisi tunawinda muda wa siku tatu kutoka mji wa mfalme, lakini mabwana muwe na subira na sisi tutawaongozeni.’ Nikajibu, ‘Vema, wakati wote upo mikononi mwetu, maana sisi hatufi.
Tu tayari mtuongoze. Lakini wewe Infadus, na wewe Skraga, angalieni! Msitudanganye, msijaribu kututega, maana tutatambua fikra zenu duni kabla hazijaingia katika akili zenu, na hatutakosa kujilipiza kisasi.
Nuru ile inayotoka katika jicho la Yule mwenye miguu mitupu na ndevu upande mmoja tu wa uso, itakuaribuni, itapita katika nchi yenu. Meno yake yanayotoweka yatajibana mikononi mwenu na yatakuleni nyinyi na wake zenu na watoto wenu; mianzi ya ajabu itasema nanyi kwa sauti na itawafanyeni kuwa kama takataka.
Angalieni.’ Basi maneno yangu yaliwatisha sana, na yule mzee alijibu, ‘Koom! Koom!’
Baadaye nilipata kufahamu ya kuwa yale maneno ndiyo wanayoyatumia kwa kumwamkia mfalme.
Akageuka akawaamuru watu wake, na mara upesi wakashika vitu vyetu ili wavichukukue, ila bunduki hawakushika, maana waliziogopa. Hata na nguo za Bwana Good wakazishik, naye alipoona hivi akataka kuzitwaa, ‘Ee, Bwana mwenye jicho linalong’aa na meno yanayoyeyuka, usitwae nguo, maana watumishi wako watazichukua.’
Bwana Good akasema kwa Kiingereza, ‘Ndiyo, lakini nataka kuziva.’ Umbopa akatafsiri maneno yake, na Infadus akajibu, ‘Hapana Bwana, usifiche miguu yako mizuri iliyo meupe tusiione tena? Tokea sasa lazima uvae shati na viatu na miwani yako tu basi.’
Na mimi nikaongeza, ‘Ndiyo, na tena lazima uache ndevu upande mmoja tu wa uso wako. Ukijibadili kwa namna yoyote watu hawa watafikiri kuwa tunawadanganya. Nakusikitikia, lakini kweli, lazima ufanye hivyo. Kama wakishuku habari hizi si za kweli, basi maisha yetu yatapotea kabisa.’
Bwana Good akasema, ‘Je, unasema kweli?’ Nikamjibu, ‘Ndiyo, nasema kweli kabisa, maana miguu yako meupe mizuri na miwani yako imekuwa ni umbo lako na lazima uvumilie tu.’ Akavumilia lakini hakuzoea, mpaka baada ya kadiri ya siku kumi, kwenda akivaa nguo chache hivi.