Hadithi ya umslopagaas

Naaaam mkuu, wacha niifaidi apa kwa uzuri
 
SURA YA NNE
Tulipokwisha kula tulitembea kuzitazama nyumba na mashamba na bustani za mission. Nadhani ni mahali pazuri kupita pote nilipopata kupaona katika nchi ya Afrika.

Kisha tulirudi tukakaa barazani, nikamwona Umslopogaas anazisafisha bunduki zetu. Alikuwa amekaa chini, na shoka lake la vita likiegemea ukutani nyuma yake, akawa anaisafisha kila bunduki kwa uangalifu sana. Kila bunduki aliipa jina.


Moja kubwa sana aliita ‘’Mngurumaji,’’ nyingine ndogo aliita ‘’Yule mdogo anayelia kama mchapo wa mjeledi,’’ nyingine zilizotoa risasi mfulizo aliziita ‘’Wanawake wanaosema upesi sana, hata huwezi kutambua neno moja linapokwisha na jingine linapoanza,’’ na bunduki sita za vivyo hivyo, aliziita ‘’watu tu,’’ na vivyo hivyo.

Alipokuwa akizisafisha, alisema nazo kama kwamba ni watu, akazisimulia habari za matendo aliyoyafanya katika vita alivyopigana.


Pia alizoea kusema na shoka lake ambalo alilifanya kama ni sahibu yake. Aliliita shoka lake ‘’Inkosikazi’’ kwa Kizulu maana yake, mke wa mfalme. Nililitwaa shoka hilo ili nilitazame vizuri.

Kipini chake kilifanywa kwa pembe kubwa sana ya faru, na urefu wake ulipata futi tatu na inchi tatu, na unene wake kadiri ya inchi moja na robo, na mwisho wa kipini ulikuwa kama rungu, yaani kisiweze kuponyoka mkononi.


Kipini hicho kiliweza kupindika kama henzarani lakini kilikuwa na nguvu sana, hata hivi kilizungushiwa nyuzi za shaba huko na huko.

Karibu na sehemu iliyoingia katika shoka lenyewe, kilichorwa alama nyingi, ndiyo hesabu ya watu waliouawa kwa shoka hilo katika vita.

Basi,ndiyo lilivyokuwa shoka la Umslopogaas aliloliita Inkosikazi, naye ni shida sana kuliacha popote wakati wowote isipokuwa anapokula, na hamu wakati huo aliliweka chini ya miguu yake.

Sikuweza kufahamu kwa siku nyingi kwa nini aliliita Inkosikazi, yaani mke wa mfalme, na siku moja nilimwomba anieleze. Akasema ya kuwa kwa hakika shoka ni mwanamke, maana ni desturi yake kupeleleza sana katika mambo, tena kwa hakika ni malkia au mke wa mfalme kwa sababu watu wote huanguka mbele yake wameshangaa kwa uzuri na nguvu zake.


Tena alieleza ya kuwa amezoea kumuuliza shauri akipatikana na shida, kwa sababu halikosi lina akili nyingi kwa sababu limechungulia katika ubongo wa watu wengi!

Basi, nilipokwisha kulitazama sana shoka, nikamrudishia Umslopogaas, akaendelea katika kazi yake ya kuzisafisha bunduki.

Hapo mtoto wa Bwana Mackenzie aitwaye Flossie akaja akanichukua nikayatazame maua yake katika bustani. Mengine yalikuwa mazuri sana nisiyopata kuyaona mpaka siku hiyo.

Nikamuuliza kama anayo maua ya namna Fulani ambayo nilisikia habari zake zamani kuwa ni mazuri mno.

Mtoto Flossie alitambua namna yake, akaniambia kuwa alijaribu kuyapanda katika bustani yake yasiote, akasema ya kuwa anadhani ataweza kunipatia ua moja la namna ile.

Baadaye wale watu waliotumwa na Bwana Mackenzie kupeleleza habari za Wajivuni walirudi, wakatuambia kuwa wametafuta kila mahali katika mwendo wa maili kumi na tano wasione hata Mjivuni mmoja, wakafikiri wamekwisha rudi walikotokea.

Tuliposikia habari hizi tulifurahi. Basi, watu wote walipoondoka tulizungumza, na halafu tukaenda kulala.
 
Naam [emoji39] [emoji39]
 
SURA YA TANO


Asubuhi tulipokuwa tunakula chakula sikumwona mtoto Flossie; nikamuuliza mama yake, ‘’Yuko wapi?’’

Akaniambia, ‘’Nilipoamka asubuhi niliona barua hii imewekwa nje ya mlango wa chumba changu amesema lakini isome mwenyewe.’’

Akanipa ile barua, nikaisoma.

‘’Mpenzi mama, ndiyo kwanza kunapambazuka sasa nami nakwenda milimani nimpatie Bwana Quatermain ua analolitaka, basi nitarudi halafu. Nimechukua punda weupe na yaya, na watumishi wawili wanafuatana nami tena nimechukua chakula cha kutosha, maana nimekusudia kulipata lile ua, hata kama ni kazi ya kutembea mwendo wa maili ishirini. Flossie’’.

Basi, nilianza kuona shaka, nikasema, ‘’Natumaini hatapatwa na mabaya, sikutaka aende na kushughulika hivi kulipata lile ua.’’

Mama yake akasema, ‘’Flossie anaweza kujitunza vizuri, na mara nyingi huenda hivi kama mtoto wa kweli wa mwituni.’’

Hapa, Bwana Mackenzie aliingia chumbani, akaisoma ile barua, nikaona ya kuwa anaona shaka, lakini hakusema neno.

Tulipokwisha kula chakula cha asubuhi, nilimchukua upande nikamuuliza kama itawezekana kutuma watu kumrudisha Yule mtoto, maana nilifikiri kuwa labda Wajivuni wengine wapo karibu na mtoto atadhurika.

Akajibu, ‘’Naona haiwezekani; labda amekwisha fika mbali mwendo wa maili kumi na tano, tena haiwezekani kujua njia ipi aliyofuata.’’

Nikasema afadhali tupande katika mti ule mrefu ulio mbele ya nyumba tuangalie kila mahali kwa darubini, basi tulifanya hivyo, na Bwana Mackenzie alituma watu wengine wajaribu kuzifuata nyayo za Flossie.

Tulipopanda katika mti ule, tuliangaza sana kila upande tusione hata alama ya Flossie wala punda wake, tukashuka tumefadhaika sana, tukarudi barazani tena.

Hapa nilimkuta Umslopogaas amekaa analinoa shoka lake Inkosikazi, kwa kinoo, nikamuuliza, ‘’Unafanya nini Umslopogaas?’’

Akajibu, ‘’Nasikia harufu ya damu.’’ Wala hakusema neno jingine ila hayo tu.
Tulipokwisha kula chakula cha mchana tuliupanda tena mti ule mrefu, tukatizama kila mahali kwa darubini, tusione kitu.

Tuliposhuka tena Umslopogaas alikuwa angali analinoa shoka lake, ingawa makali yake yalikuwa kama wembe.

Bwana Mackenzie akasema, ‘’Asema anasikia harufu ya damu? natumaini si kweli. Ninaanza kuona hofu kwa ajili ya mtoto wangu mdogo. Hana budi amekwenda mbali sana, kama sivyo, saa hizi, angalikuwa amerudi. Sasa ni saa tisa na nusu.’’

Nilimkumbusha ya kuwa mtoto amechukua chakula pamoja naye, na labda alikuwa hana nia kurudi mpaka jioni; lakini hata hivi moyo wangu ulijaa mashaka, na hofu na mashaka niliyoyaona yalikuwa dhahiri.

Baadaye kidogo watu wale waliotumwa na Bwana Mackenzie kumtafuta Flossie walirudi, wakasema walizifuata nyayo za punda kwa mwendo wa maili mbili, kisha zikapotea katika njia yenye mawe, wala hawakuweza kuziona tena.

Walikuwa wametafuta kila mahali wasimwone. Basi, saa zilikawia sana, na jioni ilipofika bila kuwapo dalili ya Flossie, mashaka tuliyoona yalizidi sana.

Mama yake maskini alikuwa ameshikwa sana na majonzi, lakini baba yake alijipa moyo.

Kila pambo lililowezekana kufanywa lilifanywa; watu walitumwa kila njia, tukapiga bunduki zetu ziwe ishara, tukaendelea kuangalia toka katika mti ule mrefu, lakini yote yalikuwa kazi bure.

Basi, giza likaingia, na hata sasa hakuna dalili ya Yule mtoto mzuri Flossie. Saa mbili tulikula chakula cha usiku. Kilikuwa chakula cha huzuni, na Bibi Mackenzie hakuja mezani.

Sisi watatu tulikaa kimya kabisa, maana pamoja na mashaka tuliyoyaona kwa ajili ya mtoto, ulielemewa na fikra ya kuwa kuja kwetu kumeleta msiba huu juu ya mkarimu wetu.
 
Chakula kilipokuwa karibu kwisha, niliomba ruhusa niondoke mezani. Nilitaka kwenda nje, nikafikiri juu ya mambo.

Nikaenda barazani, nikakitia moto kiko changu, nikakaa katika kiti karibu na mwisho wa baraza.

Nilikuwa nimeketi muda wa dakika sita saba, nikafikiri nimesikia mlango wa ukuta wa boma unafunguliwa, Nikatazama huko nisione kitu, nikafikiri ni mawazo yangu tu, Ulikuwa usiku wa giza, na mwezi haujapanda juu bado.


Baada ya kupita dakika moja tena, kitu kama tufe kilianguka juu ya sakafu ya baraza, kikaviringika kikapita mahali nilipokuwa nimekaa.

Kwanza sikuondoka, nilikaa nikifikiri ni kitu gani. Kisha nilifikiri labda ni mnyama mdogo. Ndipo wazo jingine likanijia, nikaondoka hima.

Kile kitu kilikuwa kimelala mbali kidogo, nikaunyosha mkono wangu karibu nacho, kisijongee, basi ni dhahiri si mnyama. Nikakigusa. Kilikuwa laini chenye uvungu na kizito. Nikakitwaa kwa haraka, nikakiinua katika mwangaza wa nyota. Kilikuwa ni kichwa cha mwanadamu ndio kwanza kimekatwa!


Mimi ni mtu aliyezoea mambo mengi, wala sichafukwi na moyo upesi, lakini lazima nikiri ya kuwa nilipokitazama kichwa kile, moyo wangu ulielea, nikataka kutapika. Kilifikaje hapa? Cha nani? Nilikiweka chini nikaukimbilia ule mlango mdogo.

Sikuweza kuona kitu wala kusikia mtu. Nilianza kutoka na kwenda katika giza nene, lakini nilikumbuka ya kuwa nikifanya hivyo nitakuwa ninajiweka katika hatari ya kuchomwa mkuki.

Nikarudi, nikaufunga mlango, nikatia komeo. Kisha, nilirudi barazani, nikamwita Sir Henry kwa sauti ambayo nilijaribu kuifanya kama hakuna jambo lililotokea.

Lakini naona sikuweza, maana si Sir Henry tu aliyetoka, ila Bwana Good na Bwana Mackenzie, wote wakaondoka mezani wakaja nje mbio. Bwana Mackenzie akauliza, ‘’Kuna nini?’’ Basi, ikawa sina budi kuwaambia.


Rangi ya uso wa Bwana Mackenzie ilibadilika, ikawa kama ya mfu. Tulikuwa tumesimama nje ya mlango wa sebule, na humo ndani mlikuwamo taa.

Akakishika kile kichwa kwa nywele zake, akakiinua ili akione vizuri, akasema, ‘’Ni kichwa cha mtu mmoja katika wale waliofuatana na Flossie.

Namshukuru Mungu si chake!’’ Sote tulisimama tukatazamana, tumetunduwaa, lakini tufanyeje! Hapo mlango ukabishwa, na sauti ikalia, ‘’Fungua baba, fungua!’’

Basi, tuliufungua mlango, na mtu alijiingiza amejaa hofu. Alikuwa mmoja wapo wa watu wale tuliowatuma kupeleleza habari.

Akasema, ‘’Baba yangu Wajivuni wanatujia! Jeshi kubwa limepita kuzunguka mwinuko, na sasa linaliendea lile boma la mawe la zamani la ng’ombe lililoko karibu na mto. Baba yangu, ujikaze moyo! Katikati yao nilimwona Yule punda mweupe na juu yake amekaa bibi Flossie.

Mjivuni mmoja alikuwa anamwongoza punda, na yaya alikuwa anatembea ubavuni analia. Sikuwaona wale watu waliofuatana nao asubuhi.’’

Bwana Mackenzie aliuliza kwa sauti iliyopwaya ‘’Mtoto yu hai?’’
Yule mtu akajibu, ‘’Ni mweupe kama theluji, lakini hakudhurika, baba yangu. Walipita karibu sana nami, nikauona uso wake.’’

Bwana Mackenzie akaguna, akasema, ‘’Mungu amsaidie yeye na sisi pia.’’
Nikauliza, ‘’Wako Wajivuni wangapi?’’

Akajibu, ‘’Zaidi ya mia mbili na hamsini.’’

Tukatazamana tena, tukaulizana kimoyo moyo, ‘’Tufanyeje?’’
Ndipo tuliposikia sauti inalia kwa uthabiti nje ya mlango. Ikasema, ‘’Fungua mtu mweupe, fungua mlango! Nimetumwa kusema nawe.’’

Umslopogaass alikimbilia ukutani, akainyosha mikono yake mirefu akajiinua aweze kutazama juu ya ukuta, akasema, ‘’Namwona mtu mmoja tu. Anazo silaha, tena amechukua kapu mkononi mwake.’’


Nikasema, ‘Fungua mlango,’’ Umslopogaas, akatwae shoka lako ukasimame hapa karibu na mlango. Mwache mtu mmoja tu apite ndani, mwingine akijaribu kuingia, muue.


Basi, mlango ulifunguliwa. Katika kivuli cha ukuta Umslopogaas alisimama ameliinua shoka lake juu tayari kupiga.

Hapo mwezi ukaangaza. Kukawa kimya muda kidogo, kisha, Mjivuni mmoja akaingia amevaa mavazi ya vita kama yale niliyoeleza, tena, amechukua kapu kubwa.

Mwezi uliung’arisha mkuki wake alipokuwa akijongea. Alikuwa mtu mshupavu, mwenye umri upatao miaka thelathini na mitano.

Alipofika karibu alisimama, akaliweka lile kapu chini, akaukita mkuki wake katika ardhi. Ukasimama wima. Akasema , ‘’Tuongee, Tarishi wa kwanza tuliye mtuma hakuweza kuongea,’’ akaonyesha kile kichwa kilicholala barazani kitu cha kutisha katika mwangaza wa mwezi.

‘’Lakini ninayo maneno ya kusema kama ninyi mnayo masikio ya kuyasikia. Tena, nimeleta zawadi.’’ Akaonyesha lile kapu, akacheka kwa ufedhuli na kiburi kisichoweza kuelezeka, na hata hivi hatuna budi kumsifu, hali amezungukwa na adui.
 
Bwana Mackenzie akasema, ‘’Haya, sema.’’

Akasema, ‘’Mimi ni mkubwa wa sehemu ya Wajivuni wa Guasa Amboni. Mimi na watu wangu tumewafuata watu weupe hawa watatu,’’ akawaonyesha Bwana Henry, na Bwana Good na mimi, ‘’lakini walikuwa werevu wakatushinda, wakaokoka wakaja hapa. Tuna kisa nao, nasi tutawaua.’’

Nikasema moyoni mwangu, ‘’Labda, rafiki yangu!’’

Akaendelea, ‘’Katika kuwafuata watu hawa asubuhi tuliwakamata watu wawili, mwanamke mmoja, punda mweupe na mtoto mwanamke mweupe. Tulimuua mtu mmoja kichwa chake ni kile pale barazani, Yule wa pili aliwahi kukimbia.


Yule mwanamke na mtoto mweupe na punda mweupe tumewateka nao wa pamoja nasi sasa.

Nimeleta kapu hili alilochukua Yule mtoto liwe ushuhuda.

Je, kapu hili si la mtoto wako?’’

Bwana Mackenzie akakubali, na Yule Mjivuni akaendelea, ‘’Vyema! Hatuna kisa na wewe wala na mtoto wako, wala hatutaki kuwadhuru, isipokuwa ng’ombe zako ambao tumekwisha kuwateka mia mbili na arobaini.’’

Hapa Bwana Mackenzie aliguna, maana aliwathamini sana ng’ombe aliowafuga kwa uangalifu mwingi sana.

‘’Basi, mtaachiliwa ila ng’ombe zako, hasa kwa sababu naona mahali hapa patakuwa pagumu sana kupashambulia.

Lakini habari za watu hawa ni shauri jingine. Tumewafuata siku kudha wa kadha mchana na usiku, na kwa hivi hatuna budi kuwaua. Tukirudi kwetu bila kuwaua, wanawake wetu watatucheka na kutudharau. Basi, shauri liwe na matata namna gani, kufa hawana budi kufa.’’

‘’Sasa nina shauri ninalotaka kukuambia. Hatutaki kumdhuru Yule mtoto mweupe; ni mzuri sana, tena moyo wake mkuu.

Utupe mmojawapo katika watu hawa watatu maisha kwa maisha nasi tutamwacha mtoto salama huru, tena tutamwacha na Yule mwanamke pia. Hili ni shauri la haki, mtu mweupe.

Tunataka mmoja tu, si watatu; hatuna budi kungojea nafasi nyingine kuwaua wale wawili wengine. Hata kumchagua mtu mwenyewe simchagui, ingawa ningependa zaidi Yule mkubwa,’’ akamwonyesha Sir Henry; aonekana kama ana nguvu, naye atakufa polepole zaidi.’’

Bwana Mackenzie akasema, ‘’Je, nikikataa kumtoa mtu mmoja?’’

Yule Mjivuni akajibu, ‘’Usiseme hivyo mtu mweupe, maana kama ni hivyo mtoto wako atauawa kesho kutakapo pambazuka, na Yule mwanamke aliye pamoja naye asema kuwa huna mtoto mwingine. Nitamuua kwa mkono wangu mwenyewe, ndiyo, kwa mkuki huu huu. Waweza kuja kushuhudia kama utataka.

Nitakuongoza salama,’’ akasema Yule mtu mwovu na akacheka sana kwa neno lake la ukatili.’’

Huku nyuma nilikuwa ninafikiri sana na kwa haraka haraka, kama afikiriavyo mtu katika shauri la ghafla, nikanuia nijitoe mwenyewe ili Flossie aachiwe huru.

Sipendi sana kutaja habari hizi nisije nikafikiriwa visivyo Msifikiri lilikuwa shauri la ushujaa, hasha! Ila ni la akili na la haki.

Maisha yangu ni ya kizee, wala hayana thamani tena, yake ni ya ujana yenye thamani. Tena, Yule mtoto akiuawa, kufa kwake kutaelekea kumuua baba yake na mama yake pia, lakini hakuna mtu atakayepata hasara kwa kufa kwangu mimi.

Tena, kwa kweli Yule mtoto mpenzi yumo hatarini kwa matendo niliyo tenda mimi.

Mwisho, inafaa mwanaume akikabili kifo cha namna yoyote hata kama ni kibaya, kuliko Yule mtoto mwanamke mzuri kuuawa.

Fikira hizi zote zilinipita katika akili zangu katika muda mdogo sana, kisha, nikasema, ‘’Usihangaike Bwana Mackenzie, mwambie Yule mtu ya kuwa mimi nitajitoa ili Flossie aachiwe, ila lazima kwa sharti ya kuwa yeye awe salama nyumbani humu humu kabla hawajaniua.’’

Sir Henry na Bwana Good wakasema pamoja kwa sauti moja, ‘’Hapana kabisa, hivyo haiwezekani,’’
 
Bwana Mackenzie akasema, ‘’Hapana, hapana. Sikubali mauti ya mmoja yeyote iwe katka mikono yangu.

Kama ni mapenzi ya Mungu mtoto wangu afe kifo hiki kibaya, basi, mapenzi yake yatimizwe. Wewe ni mtu hodari, tena shujaa Bwana Quatermain, lakini kwenda, ng’o, hutakwenda.’’

Nikasema kwa uthabiti, ‘’Kama shaurio lingine halitokei, kwenda sina budi nitakwenda.’’
Bwana Mackenzie akamwambia Yule mkubwa wa Wajivuni, ‘’Shauri hili ni kubwa sana, nasi hatuna budi kulifikiri. Nitakupa jibu kesho kabla hakujapambazuka.’’

Yule Mjivuni akasema kama kwamba si kitu cha maana, ‘’Vyema, lakini ufahamu ya kuwa kama jibu lako likichelewa, kile kitumba chako cheupe hakitachanua kuwa ua, maana nitakuwa nimekwisha kikata kwa huu,’’ akaugusa mkuki wake.


‘’Ningeweza kufikiri labda ungefanya hila na kutushambulia usiku, lakini Yule mwanamke amekwisha niambia ya kuwa watu wako wote wamekwenda pwani, nawe umebaki hapa na watu ishirini tu.

Je, umefanya busara kubaki na watu wachache hao ishirini kulilinda boma lako? Vyema, kwa heri, na ninyi watu weupe wengine kwa herini, ambao makope yenu nitayafumba daima hivi karibuni, kutakapo pambazuka utaleta jibu lako. Kama sivyo basi, mambo yatakuwa kama nilivyosema.’’

Kisha, akageuka akamtazama Umslopogaas aliyekuwa amesimama nyuma yake kama anamlinda.

‘’Hebu, fungua mlango, upesi sana, haya upesi!’’

Amri, hii ilimchukiza sana, muda wa dakika kumi alikuwa amesimama kama kawaida anatamani kumpiga Yule Mjivuni.

Hapo basi hakuweza kustahimili zaidi, akauweka mkono wake mrefu juu ya bega la Yule Mjivuni, akamvuta kwa nguvu hata kumgeuza kabisa na kumfanya amtazame usoni, kisha aliupeleka uso wake mkali katika uso wanye duara ya manyoya ya Yule Mjivuni.

Akasema kwa sauti iliyonguruma;

‘’Waniona?’’
Yule Mjivuni akajibu,

‘’Ndiyo, nakuona kitwana.’’

Umslopogaas akasema,

‘’Waliona hili?’’
akaweka Inkosikazi mbele ya macho yake
.

Yule Mjivuni akasema,
‘’Ndiyo, kitwana, na ‘mchezo’ wako; ya nini?’’

Umslopogaas akasema,

‘’We Mjivuni mbwa, mpayapaya, wewe mjivuni, wewe mkamata wanawake kwa ‘mchezo ‘ huu nitavikongoa viungo vyako. Ni vyema ya kuwa u tarishi, ama sivyo, ninge vitawanya tawanya viungo vyako chini katika majani.’’
Yule Mjivuni akautikisa mkuki wake mrefu, akacheka sana kwa muda mrefu, akajibu, ‘’Laiti tungeweza kushindana mimi na wewe peke yetu, ningekuonyesha kazi.’’ Aligeuka aende zake huku anacheka.

Umslopogaas akajibu, na ‘sauti yake ingali ikinguruma,’

‘’Usiwe na shaka, tutashindana peke yetu mimi na wewe.’’
‘’Utashindana uso kwa uso na Umslopogaas, wa damu ya Chaka, wa kabila la Wazulu, mkuu wa jeshi la Nkomabakosi, kama wengi wengine walivyofanya; nawe utajisalimisha mbele ya Inkosikazi kama walivyofanya wengi wengine. Ndiyo, cheka, cheka ila mwisho wako nakuhakikishia fisi watakuwa wanacheka na huku wanavunja mifupa na kuzitafuna mbavu zako.’’
 
Barikiwa mkuu
 
Cookies are required to use this site. You must accept them to continue using the site. Learn more…