Hajjat Messos: Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama ilitoa mikopo ya 10% yenye thamani ya Sh 500,598,000

Hajjat Messos: Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama ilitoa mikopo ya 10% yenye thamani ya Sh 500,598,000

DogoWaNjombe

JF-Expert Member
Joined
Feb 7, 2022
Posts
3,284
Reaction score
7,708
WhatsApp Image 2026-07-02 at 14.25.09.jpeg

Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama, Hajjat Asia Juma Messos​

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI: MWAKA MMOJA WA MAFANIKIO YA SERIKALI WILAYANI MKALAMA (2025/26)

Ndugu waandishi wa habari, wageni waalikwa, mabibi na mabwana,

Awali ya yote namshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema aliyetukutanisha mahali hapa leo hii.

Pili napenda kumshukuru Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuipatia Wilaya ya Mkalama rasilimali na fedha za maendeleo zinazowezesha utekelezaji wa miradi mbalimbali kwa manufaa ya wananchi wa Mkalama. Vilevile naishukuru OWM-TAMISEMI kwa usimamizi mzuri wa Halmashauri kwa kutoa maelekezo na miongozo mbalimbali ambayo imechangia katika kuisimamia na kuiendesha Halmashauri.

Ndugu waandishi wa habari, lengo la mkutano huu ni kuwasilisha kwa muhtasari taarifa ya mafanikio yaliyopatikana katika utekelezaji wa shughuli za serikali katika mwaka mmoja wa fedha mwaka ulioisha jana tarehe 30 Juni, yaani mwaka wa fedha wa 2025/26 pamoja na kutoa mwelekeo wa utekelezaji wa shughuli za maendeleo kwa mwaka huu wa fedha 2026/27 katika halmashauri ya Mkalama.

UWEZESHAJI WANANCHI KIUCHUMI
Katika mwaka wa fedha 2025/26, Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama ilitoa mikopo ya asilimia 10 yenye thamani ya Shilingi 500,598,000 kwa vikundi 52 vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu. Kati ya fedha hizo, vikundi 24 vya wanawake vilipokea Shilingi 208,011,000, vikundi 19 vya vijana Shilingi 259,787,000 na vikundi 9 vya watu wenye ulemavu Shilingi 32,800,000.

Katika kipindi hiki, kliniki tembezi ijulikanayo kama MAK (Mkalama Asilimia kumi Kliniki) ilianzishwa ili kusogeza karibu huduma za utoaji wa mikopo katika ngazi za vijiji. Kliniki hii imekuwa na mafanikio makubwa ambapo jumla ya wananchi 2,000,000 wamefikiwa kupitia mitandao ya kijamii ya Wilaya ya Mkalama na wananchi 2,000 kupitia mikutano ya hadhara iliyofanyika katika kata 17 na vijiji 70 vya Wilaya ya Mkalama.

Katika hatua nyingine Halmashauri imetoa mafunzo ya ujasiriamali na usimamizi wa biashara kwa wanachama 289 wa vikundi vilivyopata mikopo. Miongoni mwa wanachama hao, wanawake ni 146, vijana 124 na watu wenye ulemavu 19. Mafunzo haya yamechangia kuongeza fursa za ajira, kujiajiri, kuongeza kipato cha wananchi na kuimarisha shughuli za kiuchumi ndani ya halmashauri.

SEKTA YA BIASHARA
Halmashauri kupitia kitengo cha biashara kimefanya ziara katika maduka mbalimbali kwa lengo la kufanya tathimini ya muenendo wa biashara na kutoa elimu kwa biashara ambazo zimeonekana kutofanya vizuri. Jumla ya maduka 560 yametembelewa. Hii imesaidia kukuza biashara na kuimarisha uchumi wa mtu mmoja mmoja ndani ya halmashauri. Kupitia kitengo hiki uwekezaji umeongezeka kutoka wawekezaji 6 mwaka 2024/25 hadi kufikia wawekezaji 9 Juni 30, 2026. Uwekezaji huu ni wa sekta mbalimbali; madini, nishati, kilimo, ufugaji n.k. Hii imesaidia kuwawezesha wananchi kiuchumi kupitia ajira za muda mrefu na zile za muda mfupi.

SEKTA YA ELIMU
Sekta ya elimu imepata mafanikio makubwa katika kipindi cha mwaka wa fedha 2025/26. Halmashauri imeongeza shule mpya 4, zikiwemo shule mbili za sekondari za Kinyambuli na Kidarafa pamoja na shule mbili za msingi za Mlumba na Gracemesaki zilizojengwa kwa gharama ya jumla ya Shilingi 1,304,625,624.

Vilevile, miundombinu yenye thamani ya Shilingi 305,000,000 imejengwa ikiwemo madarasa 34, maabara 5 na bweni 1 vimejengwa ili kuboresha mazingira ya kufundishia na kujifunzia. Fedha hizi ni kutoka serikali kuu na pia mapato ya ndani. Idadi ya shule za Kidato cha Tano na Sita imeongezeka kutoka 3 hadi 6. Kwa ujumla hadi sasa halmashauri ina shule 99 za msingi na shule 22 za sekondari.

Kitaaluma, ufaulu wa Kidato cha nne umeongezeka kutoka asilimia 97.89 mwaka 2024 hadi asilimia 97.91 mwaka 2025, huku shule za kidato cha tano na sita zikiendelea kuwa na ufaulu wa asilimia 100. Aidha, ufaulu wa darasa la saba umeongezeka kutoka asilimia 68 hadi asilimia 71.85.

Mafanikio mengine ni kuimarika kwa utawala bora katika shule, kuendelea kupokea ruzuku ya elimu kutoka Serikali Kuu (EBM) jumla ya Shilingi 1,692,175,371 (shule za msingi Shilingi 770,696,327 na sekondari Shilingi 921,479,044) zimepokelewa katika mwaka 2025/26, kupungua kwa uhaba wa vitabu vya kiada ambapo jumla ya vitabu 45,848 na vifaa vya tehama 115 vimepokelewa kwenye shule za msingi. Ili kukabiliana na upungufu wa walimu Halmashauri imepokea walimu wapya 65, ambapo walimu 38 ni wa shule za sekondari na walimu 27 ni wa elimu ya awali na msingi.

SEKTA YA AFYA
Sekta ya imeendeleaa kuimarika kupitiaaa ujenzi wa zahanati 4 ambapo ni katika kijiji cha makulo, yulanson Kitumbili na tumuli na kituo cha afya kinachojengwa iguguno pamoja na ukarabati wa Majengo mbalimbali ya little huduma za afya. Vyote kwa Jumla vyenye thamani ya Shillingi 719,143,506 had sasa Halmashauri ina jumla ya vituo vya kutolea huduma 55 ambapo vituo 49 ni vya serikali ikiwemo hospitali 1, vituo vya afya 5 na zahanati 43. Aidha vituo binafsi ni 7 ambapo hospitali 1, vituo vya afya 2, na zahanati 3.

Upatikanaji wa dawa umeongezeka kutoka asilimia 92 hadi asilimia 93.8, huku dawa na vifaa tiba vyenye thamani ya Shilingi 850,968,855.17 vikininuliwa. Aidha, mashine mpya 11 za uchunguzi pamoja na vifaa tiba vyenye thamani ya Shilingi 200,000,000 vimesambazwa katika vituo vya kutolea huduma. Upatikanaji wa chanjo umefikia asilimia 100 na utoaji wa chanjo umeongezeka kutoka asilimia 102 hadi 105.

Katika kuimarisha afya za wananchi Halmashauri imeendelea na huduma za afya bila malipo kwa wazee wenye umri wa miaka 60 na zaidi wenye hali duni pamoja na watoto chini ya miaka mitano zimeendelea kutolewa katika vituo vyote vya afya ndani ya Mkalama.

Katika mwaka wa fedha 2025/26, wazee 5,501 walinufaika na huduma hizi, wakiwemo wanaume 1,762 na wanawake 3,739. Aidha, watoto 15,664 walipatiwa huduma za matibabu bila malipo, wakiwemo wavulana 7,699 na wasichana 7,965.

Thamani ya huduma zilizotolewa kwa msamaha wa matibabu ni Shilingi 104,024,958. Huduma hizi zimechangia kuboresha afya na ustawi wa wananchi, kupunguza gharama za matibabu kwa kaya na kuongeza upatikanaji wa huduma za afya kwa makundi maalum.

SEKTA YA MAZINGIRA
Katika kuunga mkono utekelezaji wa mkakati wa Miaka 10 (2024–2034) unaolenga kuhakikisha zaidi ya asilimia 80 ya Watanzania wanatumia nishati safi ya kupikia ifikapo mwaka 2034, Halmashauri katika mwaka wa fedha 2025/26 imesambaza jumla ya majiko 4,370. Kati ya hayo, majiko 3,255 ni ya gesi na majiko 1,115 ni majiko banifu.

Hatua hiyo inalenga kupunguza matumizi ya kuni na mkaa, hivyo kuchangia katika uhifadhi wa mazingira na kupambana na uharibifu wa mazingira unaosababishwa na ukataji miti ovyo.

Katika utunzaji na uhifadhi wa mazingira Halmashauri imeendelea na zoezi la upandaji wa miti ambapo miti 800,817 imepandwa kwenye maeneo ya wazi na maeneo ya nyumba za wananchi. Kitalu kimoja (1) kimeanzishwa chenye jumla ya miche 20,000 kwaajili ya kurahisisha zoezi la utoaji wa miche kwa wananchi na taasisi.

SEKTA YA KILIMO
Kilimo kimeendelea kuwa nguzo muhimu ya uchumi kwa wananchi wa Mkalama. Uzalishaji wa mazao ya chakula umeongezeka kutoka tani 116,948 katika msimu wa 2024/25 hadi tani 354,438 katika msimu wa 2025/26.

Kwa upande wa mazao ya biashara, uzalishaji umeongezeka kutoka tani 44,796 hadi tani 50,471 katika kipindi hicho.

Mafanikio haya yamechangiwa na kuongezeka kwa Maafisa Kilimo Ugani ambao Halmashauri imepokea kutoka 16 hadi 47, matumizi ya mbegu bora na mbolea kupitia ruzuku ya Serikali, ambapo jumla ya pembejeo za ruzuku zenye thamani ya Shilingi 9,488,500,000 zimesambazwa kwa wananchi, pamoja na utekelezaji wa mfumo wa stakabadhi za ghala ambao umeimarisha masoko ya zao la dengu na kuongeza kipato cha wakulima. Jumla ya Shilingi 8,143,989.09 zililipwa kwa wakulima kupitia mfumo huu na Shilingi 246,688,529 zililipwa kwa halmshauri ikiwa ni ushuru unaotokana na zao la dengu.

SEKTA YA MIFUGO
Sekta ya mifugo imeendelea kuimarika kupitia utoaji wa huduma za chanjo na tiba ambapo jumla ya mifugo 173,775 imehudumiwa, ikijumuisha ng’ombe 115,153, mbuzi 37,519 na kondoo 21,103.

Aidha, uzalishaji wa mifugo na bidhaa zake umeongezeka kutoka asilimia 65 mwaka 2024/25 hadi asilimia 80 mwaka 2025/26. Mafanikio haya yamechangiwa na kuongezeka kwa Maafisa Mifugo Ugani kutoka 28 hadi 35.

Hatua hizi zimeboresha huduma kwa wafugaji, kuongeza tija katika ufugaji na kuchangia kuongezeka kwa kipato cha wafugaji pamoja na maendeleo ya sekta kwa ujumla.

Sekta ya Mifugo imeendelea na usimamizi wa huduma ya kuosha/kuogesha mifugo ambapo jumla ya mifugo 379,196 wamehudumiwa, ikijumuisha ng'ombe 271,728, mbuzi 66,748, kondoo 40,197 na Mbwa 523.

Kwa upande wa dawa zilizopokelewa, Halmashauri ilipokea dozi za chanjo ya CBPP 150,000 zenye thamani ya Shilingi 37,500,000, dozi za chanjo ya PPR 143,000 zenye thamani ya Shilingi 50,050,000 na dozi za chanjo ya Newcastle 350,000 zenye thamani ya Shilingi 14,000,000. Kwa jumla, thamani ya dawa/chanjo zilizopokelewa ni Shilingi 101,550,000.

AJIRA NA UIMARISHAJI WA UTUMISHI WA UMMA
Katika mwaka wa fedha 2025/26, jumla ya watumishi 344 wameajiriwa katika kada mbalimbali zikiwemo elimu, afya, kilimo na utawala. Aidha watumishi wapatao 216 wamepandishwa madaraja kulingana na weledi wao wa kazi katika kada mbalimbali zikiwemo afya, elimu, kilimo na utawala.

Ajira hizi zimeimarisha utoaji wa huduma kwa wananchi na kuongeza ufanisi wa taasisi za umma katika Wilaya ya Mkalama.

MWELEKEO WA MWAKA HUU WA FEDHA (2026/27)
Kwa mwaka huu, Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama itaendelea kutekeleza miradi ya kimkakati ikiwemo miradi ya elimu ambapo, ujenzi wa shule mpya moja ya sekondari Ishenga itakayojengwa kupitia mradi wa SEQUIP kwa gharama ya Shilingi 544,225,626, ukamilishaji wa maabara 2 katika shule za sekondari (Isanzu na Mwangeza) kwa gharama ya Shilingi 60,000,000 (kutoka Serikali Kuu).

Ukamilishaji wa vyumba 3 vya madarasa katika shule za msingi (Ndala, Migunga na Mgolombyo) vyenye thamani ya Shilingi 37,500,000 (Mapato ya ndani), Ujenzi wa matundu ya 12 vyoo katika shule za msingi (Malaja, Ilunda na Kinandili) yenye thamani ya Shilingi 20,400,000 (Mapato ya ndani), Ukamilishaji wa nyumba moja ya Mwalimu shule ya msingi Kipamba yenye gharama ya Shilingi 12,500,000, utengenezaji wa vitanda 40 katika shule ya sekondari Mwangeza yenye thamani ya Shilingi 10,000,000 (Mapato ya ndani).

Ujenzi wa bweni katika shule ya sekondari Gunda yenye gharama ya Shilingi 30,000,000, Pamoja na ununuzi wa vifaa vya Tehama katika shule ya sekondari Nduguti vyenye thamani ya Shilingi 10,000,000 (Mapato ya ndani).

Miundombinu ya majengo ya utawala ambapo utafanyika ujenzi wa nyumba 3 za wakuu wa idara kwa gharama ya Shilingi 250,000,000. Miundombinu ya afya ikiwemo ukamilishaji wa hospitali ya Wilaya yenye gharama ya Shilingi 500,000,000, Pamoja na ukamilishaji wa vituo viwili vya afya vya Ilunda na Gumanga vyenye gharama ya Shilingi 200,000,000.

Aidha, juhudi za kuwawezesha wananchi kiuchumi na kuimarisha huduma za elimu, afya, kilimo na mifugo zitaendelea kupewa kipaumbele ili kuongeza ustawi wa wananchi na kuchochea maendeleo ya wilaya.

HITIMISHO
Katika mwaka wa fedha 2025/26, Wilaya ya Mkalama imeendelea kushuhudia mafanikio makubwa katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo na utoaji wa huduma kwa wananchi. Nendelea kumshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuendelea kuipatia Halmashauri fedha na rasilimali za kutosha ili kutekeleza shughuli za maendeleo ndani ya Mkalama.

Mafanikio haya yasingeweza kupatikana bila ya watumishi wote wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama, kwa dhati ya moyo wangu nawapongeza watumishi wote wa Halmashauri kwa utendaji kazi mzuri, maarifa na ubunifu katika kuiletea halmashauri maendeleo.

Namshukuru Mwenyekiti wa Halmashauri Mhe. Mohamed Juma Pamoja na baraza la madiwani kwa usimamizi mzuri wa rasilimali kwenye maeneo yao na kwa halmashauri kwa ujumla. Nawashukuru wananchi wote wa Mkalama kwa ushirikiano wao katika utekelezaji wa majukumu ya serikali niwaombe waendelee kushirikiana na halmashauri katika mwaka huu mpya na Halmashauri inaahidi kuendelea kutoa huduma bora kwao na niwakumbushe umuhimu wa kutunza amani ndani ya halmashauri yetu.

Wananchi wajiepushe na vitendo vyovyote vya uvunjifu wa amani au vinavyopelekea uvunjifu wa amani. Zaidi watoe taarifa kwa watendaji wa vijiji na kata endapo watabaini mienendo isiyofaa yenye viashiria vya uovu kwenye maeneo yao au wafike Ofisi ya Mkurugenzi kwaajili ya kutoa taarifa.

Mwisho, nawakumbusha watumishi wote kuwa safari ya kuiletea nchi yetu maendeleo makubwa zaidi imeanza leo Julai Mosi, 2026 ikiwa ni siku ya kwanza ya utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 “Dira 2050”. Nitoe rai kwa watumishi wote ndani ya Halmashauri ya Mkalama kuongeza kasi ya utendaji kazi, ubunifu na uwajibikaji ili kuendana na malengo yaliyomo kwenye Dira 2050.

Aidha ni vizuri kila mtumishi wa umma akaisoma na kuielewa mipango hii ili aweze kuiwekea mikakati ya kuifanyia kazi katika eneo analolitumikia. Mafanikio na maendeleo ya Halmashauri ya mkalama yapo mikononi mwetu watumishi wa umma tufanye kazi kwa umoja, upendo na mshikamo ili kwa pamoja tuyafikie malengo haya.
 

Attachments

  • WhatsApp Image 2026-07-02 at 14.25.09.jpeg
    WhatsApp Image 2026-07-02 at 14.25.09.jpeg
    255.7 KB · Views: 16
Back
Top Bottom