minda
JF-Expert Member
- Oct 2, 2009
- 1,068
- 67
Tuesday, 28 September 2010 04:36
Na Tumaini Makene
MGOMBEA ubunge Jimbo la Kawe kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Bi. Halima Mdee amesema zama za wananchi kufanya mabadiliko ya uongozi zimefika na hazitazuiliwa na mgombea au chama chochote kwa nguvu za hongo.
Amesema kuwa katika uchaguzi wa mwaka huu Watanzania maskini waliochoshwa na uongozi mbovu usiojali maslahi ya wananchi, watakwenda kupiga kura za kimapinduzi, bila kujali hongo wanazopewa na baadhi ya wagombea wa vyama mbalimbali wanaosaka madaraka.
Bi. Mdee aliyasema hayo juzi katika mfululizo wa mikutano yake ya kampeni akiomba ridhaa ya wananchi kuwa mbunge wa Jimbo la Kawe, jijini Dar es Salaam.
Alisema kuwa kama ambavyo imekuwa ikitokea miaka ya nyuma wakati wa uchaguzi, mwaka huu pia wamejitokeza wagombea na vyama vinavyotumia nguvu ya fedha kuwarubuni na kuwanunua wapiga kura, hivyo akawataka wananchi kutorudia makosa ya nyuma.
"Watanzania uchaguzi wa mwaka huu ni uchaguzi wa aina yake, ni uchaguzi ambao tunapaswa kupeleka salamu kwa watawala wa sasa wa CCM na wengine kuwa maskini wa Tanzania tuliopigika tunaweza kuamua kufanya mabadiliko dhidi ya matajiri wachache.
"Wanatumia wakati huu kuwahonga wananchi ili wapate kura, wachukue nafasi kujineemesha wenyewe huku wananchi walio wengi wakizidi kuwa maskini. Tunatuma ujumbe mzito, mwaka huu maskini wataamua mustakabali wa nchi dhidi ya matajiri kupitia sanduku la kura.
"Hatutaki kura za huruma, msipige kura za kutuhurumia, pigeni kura za kimapinduzi. Tunataka mabadiliko ya uongozi, tupate viongozi makini watakaoshirikiana na wananchi kusukuma gurudumu la maendeleo," alisema Bi. Mdee.
Mgombea huyo ambaye alikuwa Mbunge wa Viti Maalumu katika bunge lililopita kupitia CHADEMA, alisema anasikitishwa na hali ya jimbo hilo kuwa pamoja na kuwa liko mjini lakini liko nyuma katika miundombinu na huduma za jamii.
Alisema anashangazwa kuwa kuna kata hazina hata zahanati, baadhi ya shule zikiwa katika hali mbaya huku baadhi ya maeneo miundombinu ya barabara ikianza kufanyiwa marekebisho yasiyo na tija wakati huu wa uchaguzi.
"Jamani Watanzania lazima tuambizane ukweli, nanyi mmechangia kuifikisha nchi hapa ilipo kwa kukubali hongo na kuwapigia kura viongozi wabovu, sasa kama kweli wanawapenda kwa nini wasitumie fedha hizo kuwajengea walau zahanati au shule bora.
"Nasikia sasa wanapita pita usiku wanawagawia fedha, na pilau mmeshaanza kupikiwa, angalieni sana, kuweni makini, msirudie makosa mliyowahi kufanya. Mnawachagua watu wanaenda kwanza kujilipa vile walivyowahonga, maendeleo hakuna," alisema Bi. Mdee.
Aliwataka wananchi kujiandaa kwenda kupiga na kulinda kura Oktoba 31, ili kuachana na visingizo vya kura kuibiwa.
mwisho.
Source: Majira