Nov 05, 2023 06:46 UTC
Televisheni ya Al Jazeera imemnukuu, Osama Hamdan, mmoja wa viongozi wa ngazi za juu ya harakati ya HAMAS akisema kuwa ana uhakika wa kushindwa utawala wa Kizayuni katika vita vya #Kimbunga_cha_al-Aqsa.
Amesema: Wavamizi hawajaweza kufanikisha hata lengo moja la kijeshi. Wanachofanya wao ni kushambulia maeneo ya raia na kuua watu wasio na hatia. Mamia ya wanajeshi wa Israel wameangamizwa na kujeruhiwa. Pamoja na kwamba viongozi wa Israel wanachuja sana habari na wanaficha idadi halisi ya wanajeshi wao wanaongamizwa na kujeruhiwa, lakini idadi ni kubwa kiasi kwamba inakuwa vigumu kuficha kila kitu.
Katika sehemu nyingine ya matamshi yake, Osama Hamdan amesema: "Ulimwengu unashuhudia jinai kubwa za utawala wa Kizayuni unaoikalia kwa mabavu Baytul Muqaddas, lakini haufanyi lolote. Wapalestina kamwe hawataamini kuwa amani itapatikana bila ya kuangamizwa utawala unaoukalia kwa mabavu wa Quds Tukukfu."
Vile vile amesema: Utawala unaoikalia kwa mabavu wa Quds umeshashambulia vituo 105 vya afya na tiba na kuziondoa kikamilifu hospitali 5 katika mchakato wa kutoa huduma. Hospitali katika Ukanda wa Gaza hazina uwezo wa kupokea idadi kubwa ya watu wanaoojeruhiwa. Tunazilaumu Marekani na rais wake kwa kuhusika moja kwa moja katika mauaji ya kijinai ya wananchi wa Ghaza.
Ameongeza kwa kusema: "Misaada inayoingia Ghaza kupitia kivuko cha Rafah haikidhi hata mahitaji ya chini kabisa ya watu wetu. Misimamo rasmi ya nchi za Kiarabu ni dhaifu na hailingani na jinai zinazotendwa na adui. Tunataka Marekani ishinikizwe zaidi ili ikomeshe jinai na uhalifu dhidi ya taifa letu."