Hapana Tumkabidhi José Eduardo

Hapana Tumkabidhi José Eduardo

Rubawa

JF-Expert Member
Joined
Dec 25, 2015
Posts
2,055
Reaction score
3,254
NA MOHAMMED ABDULRAHMAN

Historia ya Afrika kama ilivyo ya dunia kwa ujumla, kimsingi imejaaa masimulizi ya wanasiasa mbali mbali. Lakini waadilifu hasa ni wachache. Jina la Lucio Rodrigo Leite Barreto de Lara ni maarufu sana katika historia ya ukombozi wa Mwanamapinduzi Comrade Lucio Lara ni mwanasiasa aliyekuwa mmoja wa waasisi wa Movimento Popular de Libertação de Angola (MPLA) Chama cha Umma cha Ukombozi wa Angola mwaka 1956 na alichaguliwa Katibu mkuu wa kwanza wa chama hicho Desemba 1962. Kabla ya kujimwaga katika siasa alikuwa mwalimu wa hesabati na fizikia nchini Ureno. Ni mtu aliyekisimamia chama hicho na kuuongoza ujumbe wa kwanza ulioingia mji mkuu Luanda baada ya Ureno kusalimu amri na kukubali kuyapa uhuru makoloni yake barani Afrika baada ya vita virefu vya wapigania ukombozi nchini Angola, Msumbiji, Guinea Bissau na visiwa vya Cape Verde na pia Sao Tome na Principe.

Lucio Lara alimuapisha kiongozi wa MPLA Agostinho Neto kuwa Rais wa kwanza wa Jamhuri ya Watu wa Angola Novemba 1975. Neto alipoiaga dunia Septemba 1979 kutokana na matatizo ya afya,
Kuanzia wapambe hadi viongozi wengi wa ngazi ya juu walimsihi Comrade Lucio (kama makada na wafuasi wa MPLA walivyopenda kumwita) awe mrithi wake, lakini bila kusita alikataa. Badala yake akaitisha kikao cha dharura cha kile kilichoitwa mkutano mkuu wa chama. Kwa mshangao wa wengi, Lara akampendekeza José Eduardo dos Santos awe Rais licha ya kuendelea kushinikizwa azibe pengo aliloliachaComrade Neto.

Lucio hakuwa mtu mwenye uchu wa uongozi bali mwanasiasa muadilifu, mfuasi wa nadhari ya Marx na Lenin aliyeweka mbele masilahi ya MPLA na Angola. Ulikuwa wakati mzito, kipindi cha vita dhidi ya waasi wa União Nacional para a Independência Total de Angola (UNITA) Umoja wa Kitaifa kwa ajili ya Uhuru kamili wa Angola, walioongozwa na Jonas Savimbi, vilivyoibuka mara tu baada ya Uhuru na MPLA kuutwaa mji mkuu Luanda na kuunda serikali. Awali Unita kilichoasisiwa 1966, kilipigana bega kwa bega na MPLA wakati wa mapambano ya uhuru na majeshi ya Ureno.

Wakati waasi hao waliungwa mkono na utawala wa kibaguzi wa Afrika Kusini na Marekani wakati wa vita vya pili baada ya uhuru , ilikuwa ni kutokana na urafiki alioujenga Lucio na Cuba serikali ya MPLA iliweza kupata msaada wa wanajeshi wa Cuba kuisaidia . Urafiki huo ulianzia 1965, alipokutana na mwanamapinduzi Ernesto Che Guevara mjini Brazzaville nchini Congo Che alikuwa´katika barani Afrika, akielekea Congo –Leopoldville ( sasa DRC) na kikundi kidogo cha wapiganaji wa Kicuba kuwasaidia wanaharakati waliokuwa wakipigana na utawala wa Mobutu Sese Seko baada ya kupinduliwa na kuuwawa Patrice Lumumba.

Tatizo la urangi na ukabila limekuweko ndani ya MPLA tangu miaka ya 1960. Miongoni mwa watu walioingiwa na sumu hiyo ni aliyekuwa Makamu wake Daniel Chipenda. Chipenda sio tu alikuwa chanzo cha mivutano bali pia uchu wa madaraka. Aliandaa njama ya kumpindua hata Dk Neto. Aliposhindwa akaihama MPLA 1974 na akajiunga kwa muda na Frente Nacional de Libertação de Angola (FNLA) Muungano wa Kitaifa wa Ukombozi wa Angola, kilichoongozwa na Holden Roberto. FNLA kilichoundwa 1954 kikiwa chama cha kwanza nchini Angola, kiliungwa mkono na Marekani na utawala wa Mobutu kikiwa na wafuasi wengi kutoka kabila la Bakongo walioko katika mataifa yote mawili, Angola na Congo.

Waliomfahamu Chipenda kwa karibu wanaamini ni vita vya madaraka vilikuwa nyuma ya uamuzi wake, kwani wakati wote akitaka kuwa kama si kiongozi basi awe makamu. Alikwenda kuishi uhamishoni Ureno na kuruidi Angola baada ya kuanzishwa mfumo wa vyama vingi 1992, kwa nia ya kugombea Urais katika uchaguzi uliofuatia mkataba wa amani kumaliza vita kati ya serikali ya MPLA na UNITA. Chipenda alipata kura kidogo mno zilizomfedhehesha na akaamua kurudi tena Ureno alikobakia hadi alipofariki Februari 1996.

Pengine mtu atajiuliza kwanini nimemtaja sana Chipenda. Kwa hakika nimefanya hivyo kwa sababu ya mbili: Kwanza kwasababu ya nafasi yake ya juu katika MPLA akiwa mmoja wa watu wanasiasa wa kwanza waliokiongoza chama zilipoanza harakati za ukombozi akiwa mjumbe wa kamati kuu. Hasa ni kuonesha jinsi ubaguzi wa kikabila na rangi ulivyoanza kuota mizizi, tena dhidi ya watu waliojitolea kutetea haki na uhuru wakiamini kwamba walikuwa ni Waangola kama wengine na kukandamizwa kwa Waangola kuliwagusa wananchi wote bila kujali rangi bali utu wao.

Comrade Lucio Lara aliyefariki 2016 akiwa na umri wa miaka 86,hakuwa peke yake. Wanasiasa wengine waliokuwa wamechanganya damu ndani ya MPLA ni pamoja na Henrique Teles Carreira maarufu IKo Carreira, shujaa aliyeongoza vita dhidi ya majeshi ya Ureno na Paulo Texeira Jorge, waziri wa kwanza wa mambo ya nchi za nje wa Angola huru . Iko alikuwa mkuu wa majeshi ya Angola na waziri wa ulinzi 1975 hadi 1980, akiwa pia mjumbe wa kamati kuu ya kisiasa. Wakati wa kipindi kizito baada ya kifo cha Neto,Iko pia alikataa kuchukua uongozi wa taifa wakati alipopendekezwa na akaungana na Lucio kumpendekeza dos Santos.

Pamoja na kila mmoja wao kuombwa mara kadhaa alau kufanya hivyo kwa kipindi cha mpito , wote walishikilia mtu muwafaka alikuwa dos Santos. Hata hivyo muda si mrefu wakawa muhanga wa mwanasiasa huyo kijana waliyempigania. Muda si mrefu mara tu baada ya kuhisi ameshajizatiti madarakani dos Santos akawapunguzia madaraka, Lucio akaondolewa ukatibu mkuu wa chama na kamati kuu ya kisiasa na kubakia mjumbe wa kawaida . Iko pia akaondoshwa kuwa waziri wa ulinzi na kuteuliwa balozi nchini Algeria na baadae mwambata wa kijeshi Ubalozi wa Angola Uhispania. Alifariki dunia Mei mjini Madrid 2000 , alikobakia kwa sababu ya kuuguwa kwa muda mrefu.

Wachambuzi wanaamini sababu hasa ya Rais dos Santos kuwaengua wanasiasa wawili mbali na hisia zake za urangi,ni msimamo wao na kuunga mkono kwao sera za falsafa ya ujamaa walioi amini na kuisimamia kivitendo. Mageuzi, ya dos Santos aliyebaki madarakani karibu miaka 40 yakabadili dira na Angola taratibu na kimya kimya ikaanza kukumbatia sera ya ubepari na kurekebisha uhusiano wake na nchi za magharibi. Alihakikisha ili kuyatekeleza hayo, ilikuwa lazima watu kama Lucio wawekwe kando. Ujamaa ulionekana ni “hadithi ya kale.” Ushahidi wa hayo ni kuibuka pengo kubwa kati ya walionacho na wasio nacho katika taifa hilo lenye utajiri mafuta na almasi.

Lucio aliendelea kuyapinga mabadiliko ya mkondo wa kisiasa akisema , “ hivi ni vita vya mabeberu , wanataka tufanye kazi na watu wao wanaosema ndiyo bwana mkubwa.” Kokote alikotokeza alizungukwa na raia kila mmoja akitaka kupeyana mkono na mwanasiasa huyo mahiri aliyetangaza Jamhuri ya Watu wa Angola na kumuapisha omrade katika mapambano na rafiki yake wa Chanda na pete Angostinho Neto kuwa rais wa kwanza wa Angola.

Lucio Lara na Iko Carreira waliokuwa wanasiasa werefu , makini na waadilifu,waliisoma na kuielewa vilivyo hali ya kisiasa ya Angola. Wadadisi wanaamini uadilifu wa Lucio ulimsaidia kutambua hali halisii ya kisiasa na huenda alikataa kuwa Rais kunusuru kukigawa chamani kutokana na kuingia hisia hizo za kibaguzi. Pia aliiiona hatari ya kuwepo na uwezekano wa wale waliojizingatia kwamba ni wazawa kuungana na kumpindua . Kwa hakika hayo ndiyo yaliomfika baadae Rais wa kwanza wa Guinea Bissau Luis Cabral ambaye mahasimu wake wakidai wazee wake walizaliwa Cape Verde.

Kwao Lucio na Iko kubwa na muhimu lilikuwa ni ukombozi wa Angola, nchi waliozaliwa pamoja na kuwa walikuwa waliochanganya damu. Wamelinda heshima yao na utu wa binadamu kuliko wale walijaribu kutumia sumu ya ukabila. Heshima hiyo inaonekana hadi leo unapoyataja majina yao na wapiganaji wengine waliochanganya damu. Chembelecho rafiki yangu kutoka Cape Verde koloni jengine la zamani la Ureno Antonio Rocha, “a história da luta pela independência Angolana nunca esta completa sem nomear os camaradas Lucio Lara e Iko Carreira,”(historia ya mapambano ya kupigania uhuru wa Angola haitokuwa sahihi bila ya kuwataja comrade Lucio Lara na Iko Carreira ). Kwa bahati mbaya hayo si masahibu ya Angola pekee, siasa za ubaguzi wa rangi, kabila ,dini , eneo na kanda bado zingali katika kadhaa barani Afrika na hazina budi kupigwa vita.

Unapozingatia hulka na tabia za binadamu Kina Lucio Lara ni mifano ya aina yake . Kuna wanaotwaa madaraka kwa mguvu, kuna wanaopewa kwa ridhaa ya wananchi wakakataa kuondoka na kujiongezea mihula, lakini kinyume wao walishawishiwa watawale wakakataa. Uadilifu ni kusimamia kivitendo unachoamini .


RAIA MWEMA, Twitter:mamkufunzi, Baruapepe:mamohamed55@ hotmail.com




Sent using Jamii Forums mobile app
 
Back
Top Bottom