Na Mwandishi Wetu
Mafanikio ya Hashim Thabiti Manka a.k.a Hasheem Thabeet ni gumzo hivi sasa nchini, kila mmoja anapiga mayowe kwa staili yake bila kujua msoto ambao alikumbana nao enzi hizo za pangu pakavu tia mchuzi, gazeti hili linalo la kukumegea...
Ijumaa Wikienda linaweza kuthubutu kutoa picha ya zamani ya Hasheem kama kielelezo cha safari ndefu ya kimaisha aliyopitia kabla hajafikia ‘levo' ya utajiri anauogelea kwa sasa.
Kwa mujibu wa kumbukumbu za dawati pamoja na nyongeza kutoka kwa watu wa karibu na ‘tall man' huyo, Hasheem kabla hajapata ngekewa ya kwenda Marekani anakoishi, alipitia vipindi vigumu nchini, ikiwemo kuonekana kituko mitaani.
Hapo kabla, urefu wa Hasheem haukuonekana kama ni mtaji, badala yake akina ‘yahe' walimuona kituko na kuthubutu hata kumcheka walipomuona akikatiza mitaani.
Katika hilo, huko nyuma mara nyingi Hasheem alijaribu kujishughulisha na mambo mengi akiamini yangeweza kumtoa kimaisha na kugonga mwamba.
Habari ambazo zimethibitishwa na Hasheem mwenyewe kupitia ‘intavyuu' mbalimbali ambazo amekuwa akifanya ni kwamba staa huyo wa NBA amewahi kuwa mcheza soka wa kujituma ingawa hakukumtoa.
Hasheem, alikiambia kituo cha Redio Clouds FM wiki iliyopita kuwa kabla mambo hayajamkalia juu ya mstari, alikuwa mcheza soka wakati huo akiwa hana dira sahihi ya kimaisha.
"Nilikuwa nacheza sana soka, ni wakati ambao nilikuwa nimetoka kufiwa na baba yangu, kwahiyo nilikuwa naangalia fursa yoyote itakayoweza kunitoa," alisema Hasheem na kuongeza:
"Nilipokuwa naangalia kikapu pale Chuo Kikuu ndipo kocha wa Outsiders UDSM aliponiona na kunishawishi nicheze kikapu."
Mbali na hilo, gazeti hili linazo data kwamba Hasheem alitaka sana kujiingiza kwenye muziki wa kizazi kipya akiamini ungeweza kumtoa lakini alikumbana na vikwazo kwakuwa ‘maprodyuza' wengi waliikataa sauti yake.
Picha ya zamani ukurasa wa kwanza, ni kwenye Tamasha la Fiesta 2003 ambapo alipanda jukwaani kama mcheza shoo wa Kundi la Solid Ground Family lilipokuwa linatumbuiza wimbo wake wa Bush Party ndani ya Wet & Wild Hotel, Kunduchi, Dar.
Aidha, gazeti hili linazo data nyingine kwamba kutokana na ‘ulemavu' wa watu kumuona Hasheem kituko, alikuwa akipata usumbufu mkubwa wa usafiri kwenye daladala hasa wakati huo akiwa mwanafunzi.
Katika hilo, makondakta wengi walipenda kumnyanyapaa, kwa sababu urefu wake ulikuwa unamfanya ashindwe kusimama vizuri kwenye gari na alipoketi kwenye siti, alilipishwa bei ya mtu mzima bila kupenda.
Hivi karibuni, Hasheem alisajiliwa na Klabu ya Memphis Grizzlies inayoshiriki Ligi Kuu ya Chama cha Mpira wa Kikapu Marekani (NBA), hivyo kuwa Mtanzania wa kwanza kufikia mafanikio hayo.
Kabla ya hapo, alicheza timu ya Chuo Kikuu cha Connecticut, UConn Huskies ambayo inashiriki mashindano ya vyuo na kupata mafanikio makubwa, ikiwemo kutajwa kama beki bora wa mwaka wa ligi na muda wote katika timu yake.