Hatari ya Amonium Nitrate karibu na Kambi ya Jeshi, uwanja wa ndege Dar

Hatari ya Amonium Nitrate karibu na Kambi ya Jeshi, uwanja wa ndege Dar

Parabolic

JF-Expert Member
Joined
Dec 3, 2013
Posts
2,922
Reaction score
3,252
Gazeti la Nipashe la Oktoba 12, 2026 limeandika habari ya uchunguzi uwepo wa kemikali aina ya Ammonium Nitrate inavyohifadhiwa katika ghala lililoko eneo la Kipawa, karibu na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), Kituo cha Anga cha Jeshi na makazi ya wananchi.

Agosti 4, 2020, mlipuko mkubwa ulitokea katika mji wa Beirut, nchini Lebanon, baada ya tani 2,750 za kemikali ya ammonium nitrate kulipuka. Kemikali hiyo ilikuwa imetaifishwa mwaka 2014 kutoka kwenye meli ya mizigo ya MV Rhosus na kuhifadhiwa katika Bandari ya Beirut kwa kipindi cha miaka sita bila kuzingatiwa kwa hatua za kutosha za usalama.

Kemikali hiyo ililipuka baada ya moto kuzuka katika ghala lililokuwa karibu na eneo ilipohifadhiwa. Mlipuko huo ulisababisha vifo vya watu wasiopungua 218, wengine 7,000 kujeruhiwa na takribani watu 300,000 kupoteza makazi yao. Uharibifu wa mali ulikadiriwa kufikia dola za Marekani bilioni 15.

Nguvu ya mlipuko huo ilikadiriwa kuwa sawa na takribani tani 1,100 za TNT (kilotani 1.1), na kuufanya kuwa miongoni mwa milipuko mikubwa zaidi isiyotokana na silaha za nyuklia kuwahi kurekodiwa. Pia, ulitajwa kuwa mlipuko mkubwa zaidi wa mara moja kuwahi kutokea kutokana na kemikali ya ammonium nitrate.

Endelea….

******
Nipashe.jpg



KATIKA jiji ambalo shughuli za biashara, usafirishaji, viwanda na makazi ya watu zimeendelea kukua kwa kasi, usalama wa kemikali hatarishi unapaswa kuwa jambo lisiloachwa kwenye uamuzi wa kawaida ya kibiashara.

Lakini uchunguzi wa Nipashe umeibua maswali kuhusu namna kemikali aina ya Ammonium Nitrate inavyohifadhiwa katika ghala lililoko eneo la Kipawa, karibu na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), Kituo cha Anga cha Jeshi na makazi ya wananchi.

Uchunguzi huo uliofanyika kwa muda wa miezi minne umebaini kuwa kampuni ya Donito Investment Limited CFS 056 inahifadhi kemikali hiyo, ambayo hutumika katika shughuli mbalimbali za viwandani, ukiwamo uchimbaji madini.

Kemikali hiyo inaweza kusababisha madhara makubwa inapokutana na mazingira yasiyo salama, hususan inapohusika katika tukio la moto, uchafuzi au uchanganyaji usiofaa.

Jambo linalozua wasiwasi zaidi si kuwapo kemikali hiyo pekee, bali ni maswali kuhusu mazingira inayohifadhiwa, wigo wa vibali vilivyotolewa, uelewa wa wananchi wanaoishi jirani na utayari wa mamlaka husika kukabiliana na dharura.

Kwa mujibu wa vipimo vilivyofanywa na mwandishi wa ripoti hii, ghala hilo liko umbali usiofikia kilomita moja kutoka Kituo cha Anga cha Jeshi na chini ya kilomita mbili kutoka Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere. Eneo hilo pia limezungukwa na shughuli za kibinadamu, yakiwamo makazi ya wananchi na biashara ndogondogo.

JNIA ni miundombinu muhimu katika usafiri wa anga, biashara na uhusiano wa Tanzania na mataifa mengine. Kwa sababu hiyo, usalama wa eneo linalozunguka uwanja huo una umuhimu wa kipekee.

Hali hiyo inaibua maswali muhimu kwa mamlaka zinazohusika na usalama wa wananchi: Je, mazingira ya eneo hilo yanaendana na masharti yanayotakiwa kwa uhifadhi wa kemikali hatarishi, na je, hatua zote za usalama zinazohitajika zimekaguliwa na kuthibitishwa?

Maswali hayo yanapata uzito zaidi kutokana na maelezo yaliyotolewa na Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), ambalo linasema cheti cha Tathmini ya Athari kwa Mazingira (TAM) kilichotolewa kwa mradi huo hakikujumuisha uhifadhi wa Ammonium Nitrate.

Kwa upande mwingine, Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali (GCLA) inathibitisha kuwa iliisajili kampuni hiyo kama mhifadhi na msafirishaji wa kemikali. Tofauti hiyo ya maelezo inazua haja ya mamlaka hizo kuweka wazi nyaraka, masharti na msingi wa uamuzi wao.

Hata hivyo, ni muhimu kutofautisha uwezekano wa kutokea kwa janga na ushahidi kwamba janga hilo linakaribia kutokea.

Uchunguzi huu wa Nipashe haujathibitisha kuwa mlipuko unatokea au ni lazima utokee. Kinachojitokeza ni haja ya kuhakikisha hatari zinazoweza kuzuilika zinadhibitiwa kabla hazijageuka maafa.

Hata hivyo, kuruhusiwa kwa ghala hilo katika eneno hilo kunakinzana na mwongozo uliotolewa chini ya Sheria ya Usimamizi na Udhibiti wa Kemikali za Viwandani na Majumbani, Na. 3 ya mwaka 2003 pamoja na kanuni zake za mwaka 2020.

Mwongozo unaelekeza kuwa katika maeneo yenye msongamano wa watu, mwongozo unaelekeza kuwa maghala ya muda yasitumike kuhifadhi mzigo kwa muda mrefu; waingizaji wanatakiwa kuondoa mzigo ndani ya siku 60.

Kwa mujibu wa mwongozo huo, ghala la kudumu lenye uwezo wa kuhifadhi tani 1,000–20,000 linapaswa kuwa mbali na maeneo yenye makazi ya watu kwa umbali usiopungua kilomita 15 hadi 20 na ghala la kudumu lenye uwezo wa zaidi ya tani 20,000 linapaswa kuwa mbali na maeneo yenye watu kwa umbali usiopungua kilomita 20 hadi 25.

Hata hivyo, kama ilivyodokezwa awali, mwandishi wa ripoti hii alipima umbali wa kutoka liliko ghala hilo hadi katika makazi ya watu, uwanja wa ndege na kituo cha anga cha jeshi, akabaini kutozingatiwa kwa mwongozo huo.





ENEO LA KIMKAKATI

Ghala la Donito Investment Limited CFS 056 liko katika eneo lenye umuhimu mkubwa kwa usafiri wa anga, shughuli za ulinzi na maisha ya wananchi wa Kipawa. Ukaribu wake na miundombinu hiyo unafanya tathmini ya usalama ihitaji kuzingatia zaidi ya hali ya jengo la ghala lenyewe.

Uwanja wa ndege ni sehemu nyeti kwa sababu unahudumia abiria, wafanyakazi, ndege na shughuli mbalimbali zinazotegemea usalama wa miundombinu.

Kituo cha kijeshi nacho kina mahitaji yake maalumu ya kiusalama, huku makazi ya watu yakihitaji ulinzi dhidi ya hatari zinazoweza kusababisha vifo, majeraha, uharibifu wa nyumba na kuvurugika kwa maisha ya kila siku.

Mhandisi wa Migodi, Maloda Mandango, anasema kuwapo ghala hilo katika mazingira hayo kunapaswa kutazamwa kwa uzito mkubwa kutokana na madhara yanayoweza kutokea iwapo kutatokea ajali kubwa.

Akizungumzia hatari hiyo, Mandango anasisitiza kuwa tukio la moto linalohusisha kemikali hatarishi haliwezi kuchukuliwa sawa na moto wa kawaida wa nyumbani au biashara ndogo.

“Moto wake si wa kawaida… kwamba ukitokea unaweza kuzimwa, hapana! Na hakuna mtu anaweza akasogea katika eneo hilo. Kwa hiyo, si kitu cha kuombea kitokee kabisa; ni hatari,” anasema.

“Upitiwe upya utaratibu uliotumika kumpa kibali cha kuhifadhi kemikali hiyo, ikiwezekana ahamishiwe sehemu nyingine salama zaidi na si kufukuzwa au kusitishiwa biashara yake kwa sababu amewekeza fedha na ameajiri watu wengi," Mhandisi Mandago.



UTATA WA VIBALI

Katika maelezo yake kwa Nipashe, Mkurugenzi wa NEMC, Dk. Immaculate Semes, anasema ghala hilo lilipewa Cheti cha Tathmini ya Athari kwa Mazingira chenye namba EC/EIA/2024/1443, kilichotolewa Aprili 12, 2025.

Kwa mujibu wa NEMC, cheti hicho kilihusu kuanzisha na kuendesha Kituo cha Kuhifadhi Makasha ya Mizigo (CFS), si kuhifadhi Ammonium Nitrate.

NEMC inasisitiza kuwa kupata cheti cha tathmini ya mazingira hakumpi mwekezaji rukhsa ya kufanya shughuli yoyote anayoona inafaa katika eneo lake. Mwekezaji anatakiwa kutekeleza shughuli zilizoainishwa kwenye taarifa ya tathmini, Mpango wa Usimamizi wa Mazingira na masharti yaliyoambatanishwa na cheti.

Maelezo hayo yanaweka wazi tofauti muhimu kati ya kuwa na cheti cha mazingira na kuwa na idhini ya kuhifadhi kila aina ya mzigo.

Kwa mujibu wa NEMC, uhifadhi wa Ammonium Nitrate haukuainishwa katika taarifa ya tathmini ya mradi huo. Hivyo, baraza hilo linasema linaendelea kuhakiki iwapo shughuli zinazofanyika zinaendana na wigo wa mradi ulioidhinishwa au zinahitaji tathmini ya ziada, marekebisho ya cheti au idhini nyingine kwa mujibu wa sheria.

Katika uchunguzi wake, mwandishi amebaini kuwa, ukaguzi wa NEMC uliofanyika Agosti 12, 2026, ulibaini kuwapo maghala matano yanayotumika kuhifadhi Ammonium Nitrate kwenye eneo tajwa, huku makasha yaliyokuwa nje yakihifadhi madini ya manganese.

Timu ya ukaguzi iliripoti kuwa kemikali hiyo ilikuwa imefungashwa katika mifuko maalumu na kuhifadhiwa ndani ya maghala yenye sakafu imara na njia za kuingia na kutoka. Hakukuonekana kemikali iliyomwagika wakati wa ukaguzi huo.

Hata hivyo, NEMC ilibaini maeneo yaliyohitaji maboresho, ukiwamo uwekaji alama na mabango ya tahadhari, upatikanaji vifaa vya kinga kwa wafanyakazi wote, vyombo vya kuhifadhi taka na kuondolewa kwa vyuma chakavu.

Maelezo hayo ya NEMC yanaonesha kuwa, hata kama baadhi ya masharti ya msingi yalionekana kutekelezwa wakati wa ukaguzi, bado kulikuwa na maeneo yaliyohitaji uboreshaji.

NEMC inaeleza kuwa inaweza kuchukua hatua za kiutawala au kisheria pale inapobainika kuwa mradi unaendeshwa nje ya masharti yaliyoidhinishwa.

Hatua zinazoweza kuchukuliwa, kwa mujibu wa NEMC, ni pamoja na kutoa maelekezo ya kurekebisha upungufu, kutaka tathmini ya ziada, kurekebisha au kusitisha cheti, kusimamisha shughuli husika kwa muda na kuwasilisha suala kwa mamlaka nyingine pale inapohitajika.





GCLA YAKIRI KIBALI

Tofauti na maelezo ya NEMC kuhusu wigo wa cheti cha mazingira, Meneja wa Kanda ya Mashariki wa GCLA, Dastan Mkapa, anathibitisha kuwa mamlaka hiyo iliisajili Donito kama mhifadhi na msafirishaji wa kemikali.

Mkapa anasema utoaji kibali cha kuhifadhi kemikali hiyo huambatana na masharti mbalimbali, ukiwamo ulinzi wa eneo, mpango wa kukabiliana na dharura, kuwapo alama za tahadhari, mafunzo kwa wafanyakazi na utekelezaji masharti ya usalama wakati wa usafirishaji.

Anasema pia kwamba, kwa utaratibu wanaoeleza, mzigo wa Ammonium Nitrate unaopitia katika ghala la muda haupaswi kukaa zaidi ya siku 60.

Anafafanua kuwa kibali kilitolewa kwa shughuli za kupokea na kusafirisha mzigo, akisema utaratibu huo unalenga kusaidia kupunguza msongamano wa mizigo bandarini.

Kwa maelezo yake, usafirishaji kemikali hiyo huambatana na taratibu maalumu, ukiwamo uangalizi wa kitaalamu na utoaji taarifa kwa vyombo vya usalama pale inapohitajika.

Hata hivyo, maelezo hayo yanaacha maswali kadhaa yanayohitaji majibu. Je, kibali kilichotolewa kwa kampuni hiyo kinataja wazi Ammonium Nitrate na aina ya shughuli inayoruhusiwa? Je, kuna masharti yanayobainisha kiwango cha juu cha mzigo unaoweza kupokewa kwa wakati mmoja? Je, kumbukumbu zinaonesha muda ambao kila mzigo umekaa katika ghala hilo? Na je, masharti ya mazingira na usalama yamethibitishwa na mamlaka zote zinazohusika?

Mkapa anasema mamlaka yake hukagua nyaraka na kufuatilia utekelezaji wa masharti ya usalama, huku akieleza kuwa ukaguzi wa kina hufanyika mara mbili kwa mwaka na pia wakati wa kuingia kwa mizigo.

Anakiri kuwa kumekuwa na changamoto zinazohusisha madereva wasiokuwa na nyaraka au vyeti vinavyokidhi matakwa ya usalama.

Anasema katika mazingira hayo mamlaka huchukua hatua zinazostahili, ikiwamo kutoza faini pale ukiukwaji unapothibitishwa.



MAMLAKA ZATOFAUTIANA

NEMC inasema Ammonium Nitrate haikujumuishwa katika taarifa ya tathmini ya mazingira iliyotumika kutoa cheti cha mradi. Kwa upande mwingine, GCLA inasema iliisajili kampuni hiyo kama mhifadhi na msafirishaji wa kemikali.

Maelezo hayo yanaweza kuhusiana na majukumu tofauti ya kisheria ya taasisi hizo, lakini yanaibua swali kuhusu namna vibali vinavyoratibiwa na jinsi taarifa za shughuli hatarishi zinavyoshirikishwa baina ya mamlaka.

GCLA yenyewe inasema, katika utaratibu wa utoaji kibali, nyaraka za mazingira kutoka NEMC ni miongoni mwa mambo yanayopaswa kuangaliwa.

NEMC inaeleza kuwa cheti cha mazingira kilitolewa kwa ajili ya kituo cha makasha ya mizigo na kwamba uhifadhi wa Ammonium Nitrate haukuainishwa. GCLA nayo inasema ilijua kampuni hiyo inahifadhi kemikali hiyo na iliipa kibali kwa kuzingatia masharti yake.

Uchunguzi wa mwandishi wa ripoti hii umebaini kuwa GCLA ililisajili ghala hilo kama mhifadhi na msafirishaji kemikali. Kibali kilichopo kinaanzia Mei 6, 2026 hadi Februari 2, 2027.



"HATUNA TAARIFA"

Wakati mamlaka zikijadili vibali na masharti ya uhifadhi, baadhi ya wakazi wa Kipawa wanasema hawajui kwa uhakika shughuli zinazofanyika ndani ya ghala hilo.

Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Kipawa Uwanja wa Ndege, Octavian Msofe, anasema hakuwa na taarifa kwamba kampuni hiyo inahifadhi Ammonium Nitrate.

Anachokifahamu, kwa mujibu wa maelezo yake, ni malalamiko ya wakazi kuhusu vumbi linalotokana na shughuli za upakiaji na upakuaji mizigo.

Msofe anasema kampuni ilipoanza shughuli zake, ilijitambulisha kama mtoa huduma za makasha ya mizigo.

Anasema: “Sifahamu kama wanahifadhi hiyo kemikali hatarishi, Ammonium Nitrate. Sijui vitu vingi; wakati mwingine mambo yanaweza kufanyika bila sisi kujua kwa sababu wanaamini sheria hairuhusu kufanya biashara hiyo katika baadhi ya maeneo.”

Anaongeza kuwa angependa kupata taarifa sahihi ili aweze kutekeleza wajibu wake wa kuwatetea wananchi anaowaongoza.

Hata kama baadhi ya taarifa za kiufundi zinaweza kuhitaji kudhibitiwa kwa sababu za kiusalama, wananchi wanaoishi karibu na shughuli hatarishi wanapaswa kupewa maelezo yanayowawezesha kuelewa hatari, kujua tahadhari za kuchukua na kufahamu pa kupata msaada wakati wa dharura.

Mkazi wa eneo hilo, Ashraf Sauge, anasema hajui kwa hakika aina ya mzigo unaoshughulikiwa ndani ya ghala, lakini amekuwa akiona magari makubwa yakiingia na kutoka, wakati mwingine yakisindikizwa na ulinzi.

Anasema shughuli hizo huambatana na vumbi na kelele zinazowasumbua wakazi jirani.

“Huwa linatimka vumbi na kelele; hatulali. Sijajua huwa wanashusha na kupakia vitu gani, lakini hizo kelele zake ni kero kubwa,” anasema.



KAULI YA KAMPUNI

Mwanasheria wa kampuni hiyo, Mohamed Muya, anakiri kuwapo malalamiko ya vumbi na anasema kampuni ina mpango wa kujenga sakafu imara ya zege ili kupunguza vumbi linalotokana na shughuli za uendeshaji.

Kwa upande mwingine, mkazi Gadiosa Mfinanga anasema amewahi kusikia kuwa ghala hilo linaweza kuwa linahifadhi Ammonium Nitrate, lakini hajawahi kupewa maelezo ya kutosha kuhusu madhara yake.

Anasema: “Kama ni kweli humo ndani inahifadhiwa kemikali hatarishi, ni bora tungefahamishwa ili, kama inawezekana, tuhame au tulipwe fidia tuondoke katika eneo hili.”





AMMONIUM NITRATE

Kwa mujibu wa Mhandisi Migodi, Mandago, Ammonium Nitrate ni kemikali inayotumika, miongoni mwa matumizi mengine, katika utengenezaji mbolea na shughuli zinazohusiana na uchimbaji madini. Katika mazingira fulani ya matumizi ya viwandani, hutumika katika mifumo ya vilipuzi maalumu.

Anafafanua kuwa ingawa kemikali hiyo inaweza kushughulikiwa kwa usalama inapofuatwa taratibu sahihi, hatari huongezeka inapohifadhiwa au kushughulikiwa kinyume cha masharti yanayotakiwa.

Anasema hali ya joto, moto, uchafuzi, uchanganyaji na vitu visivyooana nayo, pamoja na mazingira ya uhifadhi, vinaweza kuchangia kutokea kwa tukio hatari.

Kwa hiyo, usalama wake hauwezi kutegemea kauli kwamba mifuko imefungwa vizuri au kwamba wafanyakazi wamepata mafunzo pekee.

Unahitaji mfumo mzima wa udhibiti unaojumuisha tathmini ya eneo, ufuatiliaji wa kiasi cha kemikali, ukaguzi wa majengo, udhibiti wa vyanzo vya moto, utunzaji kumbukumbu na maandalizi ya kukabiliana na dharura.

Katika eneo la Donito, mwandishi alibaini kuwapo biashara ya chipsi inayotumia moto wa mkaa nje ya ghala.

Ni hali inayohitaji tathmini ya usalama inayofanywa na wataalamu ili kubaini kama shughuli hiyo inakidhi masharti yanayotakiwa kuhusiana na umbali wa vyanzo vya moto na maeneo ya kuhifadhi kemikali.



MATUKIO DUNIANI

Historia ya kimataifa inaonesha kuwa matukio yanayohusisha Ammonium Nitrate na kemikali nyingine hatarishi yanaweza kusababisha maafa makubwa pale usalama unaposhindwa.

Agosti 4, 2020, mlipuko mkubwa ulitokea katika Bandari ya Beirut, Lebanon. Taarifa zilizoripotiwa wakati huo zilisema takribani tani 2,750 za Ammonium Nitrate zilikuwa zimehifadhiwa kwa miaka kadhaa katika ghala la bandari. Mlipuko huo ulisababisha vifo vya zaidi ya watu 220, maelfu ya majeruhi na uharibifu mkubwa wa majengo na makazi.

Tukio hilo lilionesha madhara yanayoweza kujitokeza pale kemikali hatarishi inapokaa kwa muda mrefu katika mazingira ambayo usimamizi wake haukidhi kiwango cha usalama kinachohitajika.

Aprili 16, 1947, katika Jiji la Texas nchini Marekani, meli iliyokuwa imebeba takribani tani 2,300 za Ammonium Nitrate ilihusika katika tukio la moto na mlipuko bandarini. Maafa hayo yalisababisha vifo vya mamia ya watu na majeraha kwa maelfu, huku uharibifu mkubwa ukikumba eneo la bandari na maeneo jirani.

Nchini China, Agosti 12, 2015, milipuko ilitokea katika eneo la kuhifadhi kemikali bandarini Tianjin. Takribani watu 173 walifariki dunia na mamia kujeruhiwa. Uchunguzi wa tukio hilo ulihusisha masuala ya usimamizi wa kemikali na uhifadhi wa mizigo hatarishi.

Vilevile, Septemba 21, 1921, mlipuko katika kiwanda cha Oppau nchini Ujerumani ulihusisha mchanganyiko wa Ammonium Nitrate na Ammonium Sulfate. Watu 561 waliripotiwa kufariki dunia katika tukio hilo na sehemu kubwa ya eneo la Oppau iliharibiwa.

Matukio haya hayamaanishi kwamba hali ya Donito ni sawa na mazingira ya majanga hayo, wala hayathibitishi kuwa tukio kama hilo litatokea Kipawa.

Hata hivyo, yanaonesha kwa nini uhifadhi wa kemikali hatarishi unahitaji tahadhari za hali ya juu, udhibiti wa muda wa kukaa kwa mzigo, ukaguzi wa mara kwa mara na mipango ya dharura inayoweza kutekelezwa kwa vitendo.



MIONGOZO, WAJIBU

Ibara ya 14 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 inatambua haki ya kila mtu kuishi na kupata ulinzi wa maisha yake kutoka kwa jamii kwa mujibu wa sheria.

Katika mazingira ya shughuli zinazohusisha kemikali hatarishi, haki hiyo inatoa msingi muhimu wa kutaka hatua za usalama zichukuliwe kwa wakati na mamlaka zinazohusika zitekeleze wajibu wao.

Katika maelezo yaliyotolewa kwa Nipashe, GCLA inasema kuna tofauti kati ya ghala linalohifadhi kemikali kwa muda mrefu na kituo kinachopitisha mzigo kuelekea eneo lingine.

Kwa maelezo ya mamlaka hiyo, baadhi ya masharti ya umbali yanahusiana na aina ya uhifadhi na mazingira ya shughuli husika.

Akijibu maswali ya Nipashe, Mwanasheria wa Donito Investment Limited, Mohamed Muya, anasema kampuni imechukua tahadhari za usalama na imekuwa ikitoa mafunzo kwa wafanyakazi wake ili kuzuia ajali.

Muya anathibitisha kuwa kampuni inahifadhi Ammonium Nitrate na anakiri kuwa kemikali hiyo inaweza kusababisha madhara makubwa iwapo itahusika katika mlipuko.

Akizungumzia hatari hiyo, anasema: “Humu ndani sisi tunahifadhi Ammonium Nitrate, na ikiripuka inaweza kuteketeza uwanja wa ndege wote. Unahitaji utulivu kidogo kwa sababu ya hatari yake.”

Muya anasema kampuni imefuata taratibu za serikali na imepewa cheti cha tathmini ya mazingira. Anaongeza kuwa kampuni imekuwa ikifanya kazi kwa kuzingatia masharti inayopaswa kufuata na kwamba wakazi wa jirani wamekuwa wakilalamikia zaidi vumbi linalotokana na shughuli za upakiaji na upakuaji.

Anasema kampuni ina mpango wa kuweka sakafu ya zege ili kupunguza vumbi na kuimarisha uhusiano na majirani.
 
Mimi sikuwahi kujua kuhusu kuhifadhi Aluminum Nitrate lakini nilikuwa najiuliza yaani unaweka Container Freight station mbele ya Kambi ya jeshi, tena kwenye lango kuu la kuingilia, inakuwepo mbele ya Lango la Airport tena sio KM 2 kama mwandishi alivyosema pale labda 1km. Kiukweli kuna udhaifu mkubwa sana kwenye hili tunafahamu sehemu nyingi zilizopo CFS kunaleta foleni na namna n.k
 
Back
Top Bottom