CCJ yaigusa Marekani
• Balozi nchini akana kuisaidia kifedha, kimkakati
na Waandishi Wetu
KUANZISHWA kwa Chama Cha Jamii (CCJ) kumeendelea kuchochea hali ya mikanganyiko inayotokana na kuwapo kwa taarifa mbalimbali zinazokinzana kuhusu ustawi na mfumo wa uendashaji wake; Tanzania Daima imebaini.
Siku tatu baada ya chama hicho kukabidhiwa cheti cha usajili wa muda kumeibuka taarifa zinazokihusisha chama hicho na misaada kutoka nje ya nchi ikiwa ni pamoja na kuanza kutumia mfumo wa kisasa wa mtandao wa kompyuta katika kusaka wanachama 200 kutoka mikoa minane ya Tanzania Bara na miwili ya Zanzibar.
Hata hivyo saa chache tu baada ya taarifa hizo kuifikia Tanzania Daima, Marekani, moja ya nchi ambazo zimekuwa zikitajwa chinichini kukisaidia chama hicho, ilitoa tamko la kukanusha kufanya hivyo kwa CCJ na kwa chama kingine chochote cha siasa hapa nchini.
Tamko hilo la Serikali ya Marekani lilitolewa jana na Balozi wa taifa hilo kubwa hapa nchini, Alfonso Lenhardt, wakati alipokuwa akijibu maswali ya waandishi wa vyombo mbalimbali vya habari aliokutana nao kuzungumzia uzoefu alioupata wa kuishi hapa nchini kwa siku 100 za kwanza, tangu alipowasili nchini Novemba 10, mwaka jana.
Balozi Lenhardt ambaye alikuwa akijibu swali, alisema sera ya Marekani ya kuchochea ustawi wa demokrasia duniani na Tanzania hailengi katika kuvisaidia kifedha au kimikakati vyama vya siasa na wala haitekelezwi katika misingi ya kutaka matokeo fulani kupitia katika sanduku la kura.
"Hatusaidii vyama vya siasa katika uchaguzi, tangu nimefika nimekutana na viongozi au wawakilishi wa vyama vitatu vyenye nguvu vya CCM, CUF na CHADEMA, ambavyo nadhani ndivyo vikubwa hapa...ndiyo nimekisikia hiki chama cha CCJ kupitia katika vyombo vya habari, sijakutana na viongozi wake na hata hawajulikani ni kina nani. Jambo la msingi, hatusaidii chama chochote cha siasa, tupo hapa kuwasaidia wananchi wa Tanzania," alisema balozi huyo.
Alipoulizwa alikuwa ana maoni gani kuhusu kauli iliyopata kutolewa hivi karibuni na kwa nyakati tofauti na Rais Jakaya Kikwete na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, ya kuyataka mataifa ya nje kutoingilia masuala ya ndani ya Tanzania, balozi huyo kwanza alisema anaamini matamshi hayo hayakuilenga nchi yake.
Akifafanua alisema alikuwa akiunga mkono kauli hizo kutokana na yeye mwenyewe kuwa na imani kwamba, Watanzania wenyewe ndio walio na wajibu wa kuamua hatima ya masuala yanayohusu nchi yao na si mataifa ya nje kama Marekani.
Balozi Lenhardt alisifia hatua mbalimbali za kukabiliana na masuala yanayohusu rushwa na utawala bora hapa nchini na akasema ni vyema viongozi wanaojiuzulu uongozi kutokana na kukabiliwa na tuhuma za rushwa wakafikishwa mbele ya vyombo vya sheria.
"Tunaona hatua zikipigwa katika mapambano dhidi ya rushwa na kuimarisha misingi ya utawala bora. Kuna viongozi wamejiuzulu kutokana na mambo hayo, nadhani ni jambo jema baada ya kujiuzulu uchunguzi ukafuata na watuhumiwa wakafikishwa mbele ya vyombo vya sheria," alisisitiza balozi huyo na kuongeza kuwa hatua za namna hiyo zinaonyesha namna serikali inavyopambana na rushwa ipasavyo.
Alipoulizwa ni kwa nini anaona ni vyema kwa Tanzania viongozi waliojiuzulu kwa tuhuma za rushwa wakashitakiwa ilhali nchini Marekani miaka ya 1970 wakati rais wa nchi hiyo, Richard Nixon, alijiuzulu kwa rushwa na hakushitakiwa, Balozi Lenhardt alisema kutoshitakiwa kwa rais huyo kulitokana na msamaha aliopewa na rais aliyefuata baada yake, Gerald Ford.
Wakati Balozi wa Marekani akitoa kauli hiyo, uongozi wa muda wa CCJ nao kwa upande wake uliihakikishia Tanzania Daima kwamba chama hicho kilikuwa hakijawahi hata siku moja kuwasiliana na kupata msaada wa aina yoyote kutoka nje ya nchi, kwani kinaendeshwa kwa kutumia rasilimali za wanachama na wananchi.
Akizungumza na gazeti hili, Mwenyekiti wa muda wa CCJ, Richard Kiyabo, alisema; "Hatujawahi kuomba fedha kutoka nchi yoyote, kwani uendeshaji wa chama chetu unatokana na vyanzo vyetu binafsi. Hatutarajii kufanya hivyo hata siku zijazo kutokana na sheria mpya ya fedha iliyopitishwa hivi karibuni."
Katika hatua nyingine, uongozi huo wa muda wa CCJ, umemtaka Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, John Tendwa, kuacha kutengeneza mazingira magumu ya kuwazuia kushiriki kwenye Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba.
Akizungumza na Tanzania Daima, Dar es Salaam jana, Katibu Mkuu wa CCJ, Renatus Muhabi, alisema kauli za msajili huyo zinatengeneza mazingira ya kuwazorotesha katika juhudi za kupita mikoani kwa ajili ya kuwapata wanachama.
Alisema wanatarajia kuwasilisha majina ya wanachama 200 kila mkoa kwa mikoa 10 mwanzoni mwa Aprili mwaka huu, hivyo kauli za msajili huyo kwamba atafuata sheria ya miezi sita, atawanyima haki wananchi wengi wenye matumaini na chama hicho.
"Kwa kauli zake, Tendwa anatengeneza mazingira ya kutunyima usajili wa kudumu mapema ili tusishiriki kwenye uchaguzi, sasa hili si jambo jema…asitafute sababu ili baadaye apate kitu cha kusema. Mategemeo yetu ni kushiriki Uchaguzi Mkuu.
"Sisi hadi mwanzoni mwa mwezi ujao (yaani Aprili), tutakuwa tayari tumekamilisha idadi ya wanachama wanaotakiwa kwa mujibu wa sheria… hatujawahi kufanya kazi za chama kabla ya kupata usajili wa muda," alisisitiza Muhabi.
Aidha, katibu huyo aliitaja mikoa minane ya Tanzania Bara watakayoitembelea kuwa ni Mara, Mwanza, Shinyanga, Mbeya, Iringa, Morogoro, Dar es Salaam na Pwani, ambapo kwa Zanzibar watafika Unguja na Pemba.
Alisema wakati wanatengeneza chama walifanya utafiti wa kutosha hivyo haitawawia vigumu kwao kuwapata wanachama 200 kwa mikoa watakayoitembelea huku akiahidi kuzunguka nchi nzima baada ya kupata usajili wa kudumu.
Akitolea mfano kwa Dar es Salaam, Muhabi alisema baada ya kupata usajili wa muda, wamejizolea wanachama rasmi wenye kadi za CCJ zaidi ya 4,000 na kubainisha kwamba hiyo ni dalili njema kwao.
Kuhusu uvumi kwamba wanatumia teknolojia ya mtandao kuwapata wanachama wanaotakiwa, katibu huyo alikanusha maneno hayo na kusisitiza kuwa wameshaanza kwenda mikoani kutafuta wanachama na ofisi za chama chao.
"Hatuna teknolojia hiyo, ingawa tunafikiria kuwa nayo ila kwa sasa bado… tukitafuta wanachama kwa njia hiyo itakuwa kazi ngumu kwa msajili kuhakiki majina ya wanachama na kujiridhisha kama kweli wanatoka kwenye mikoa tajwa," alisema katibu huyo akiwa na Mwenyekiti wake, Richard Kiyabo. Juzi, CCJ ilikabidhiwa cheti cha usajili wa muda kwenye ofisi za msajili wa vyama vya siasa huku msajili wake akionyesha wasiwasi wake kwa chama hicho kushiriki kwenye Uchaguzi Mkuu ujao kutokana na muda wa kutimiza matakwa ya sheria.
Tendwa, alisema ili chama kipate usajili wa muda kuna sheria ya miezi sita ili kutafuta wanachama 200 kila mkoa kwa mikoa 10 nchini, ambayo kwa mujibu wake anazingatia zaidi sheria zilizopo.