Uchaguzi wamuondoamkurugenzi wa Hai Wednesday, 29 September 2010 18:55 0diggsdigg
Daniel Mjema, Moshi
MKURUGENZI mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Hai, Nicholaus Mtega ameondolewa ghafla katika wadhifa huo na kuhamishiwa makao makuu ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) mjini Dodoma.
Uhamisho wa Mtega, ambaye pia ni msimamizi wa uchaguzi wa jimbo hilo, unaonekana kuwachanganya watumishi wengi wa halmashauri hiyo, hasa kutokana na uvumi kuwa uhamisho wake una msukumo wa kisiasa.
Uhamisho wa mkurugenzi ni wa tatu kufanywa kwa watumishi wa serikali katika mazingira yanayohusishwa na uchaguzi mkuu baada ya mkurugenzi wa Jiji la Arusha, Raphael Mbunda kupata uhamisho siku chache baada ya kutupilia mbali pingamizi la CCM dhidi ya mgombea wa Chadema wa Jimbo la Arusha, Godbless Lema.
Pia kamanda wa Takukuru wa Kilimanjaro, Alexander Budigira alishushwa cheo katika mazingira ya kutatanisha siku chache baada ya maofisa wake kumkamata mkuu wa wilaya ya Kasulu, Betty Machangu kwa tuhuma za kuhusika katika vitendo vya rushwa wakati wa mchakato wa kura za maoni ndani ya CCM.
Habari zilizopatikana jana zinaeleza kuwa Mtega pia ameondolewa ghafla kwenye cheo chake wakati masuala ya uchaguzi yakizidi kupamba moto. Nafasi yake imechukuliwa na Melkizedeck Humba ambaye alikuwa afisa mipango wa Wilaya ya Same na jana aliripoti ofisini na kukabidhiwa ofisi.
Waziri wa Tamisemi, Celina Kombani hakupatikana kutoa ufafanuzi wa sababu ya kuhamishwa ghafla kwa mkurugenzi huyo wakati huu ambao wakurugenzi wa halmashauri ni nyenzo muhimu kwenye uchaguzi mkuu, lakini Mtega mwenyewe alikiri kuwa amehamishwa baada ya kubanwa sana.
"Hizo sababu unazonieleza kwamba zimechangia uhamisho wangu, mimi sizijui ndio kwanza nazisikia kwako lakini nataka nikuambie barua yangu imesema tu imeamuliwa uhamishiwe Dodoma basi," alisema Mtega.
Mtega alisema sababu zilizoelezwa katika barua yake hazionyeshi kama uhamisho huo ni wa adhabu bali ni wa kawaida na kwamba kama unavyoteuliwa hakuuliza sababu za uteuzi wake hata hilo hana sababu ya kuulizia.
Lakini vyanzo mbalimbali vimeidokeza Mwananchi kuwa tangu Mtega alitupilie mbali pingamizi la CCM dhidi ya mgombea ubunge wa jimbo hilo kwa tiketi ya Chadema, Freeman Mbowe amekuwa akionekana kama msaliti kwa chama hicho tawala.
Pingamizi hilo ambalo kama lingekubaliwa lingeweza kuifanya CCM ipate ushindi mwepesi, liliwasilishwa na mgombea ubunge kwa tiketi ya chama hicho, Fuya Kimbita.
Kimbita alimwekea Mbowe pingamizi hilo akidai amekwepa kulipa kodi zinazofikia Sh40 milioni kwenye hoteli yake ya kitalii ya Protea Aishi anayoimiliki, pingamizi ambalo lilitupwa baada ya Mbowe kuwasilisha utetezi wake.
Mbali na suala hilo, inadaiwa kuwa kigogo mmoja wa serikali wa ngazi ya wilaya (jina tunalo) amekuwa akimchukulia Mtega kama mfuasi wa vyama vya upinzani kwa kuwa amekuwa akikataa maombi mengi ya kuisaidia CCM.
"Nakwambia uhamisho wake una mkono wa huyo kigogo... ndiye amejenga hoja kuwa kwa vile Mtega anakataa kusaidia kuipa CCM mafuta ya kampeni, lazima ni (mfuasi wa) Chadema na huyo kigogo amekuwa akitamka hayo waziwazi," alidokeza mpashaji wetu wa habari hiyo.
Fitina nyingine anayodaiwa kuzushwa na kigogo huyo pamoja na baadhi ya viongozi wa CCM ni kwamba msimamizi huyo alihudhuria mkutano wa kampeni wa mgombea urais kwa tiketi ya Chadema, Dk Willibrod Slaa wakati alipozuru wilaya hiyo.
"Wanadai eti alihudhuria mkutano wa Dk Slaa, lakini akakacha ule wa mgombea urais wa CCM (Jakaya Kikwete)... sisi watumishi tumeshtushwa sana na tuhuma hii ya uongo na ya kutungwa dhidi ya Mtega," alidai mtumishi mmoja.
Watumishi hao ambao waliomba majina yao yahifadhiwe, walidai kuwa siku Kikwete alipofika Uwanja wa Bomang'ombe wilayani humo, Mtega alikuwepo uwanjani akiwa kwenye gari la halmashauri na watumishi wengine.
Lakini, duru nyingine zilidai kutosainiwa kwa mkataba kati ya halmashauri na Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Kaskazini wa kuipandisha hadhi Hospitali ya Machame kuwa teule nako kumechangia.
Vyanzo hivyo vimeidokeza Mwananchi kuwa Kikwete alitoa agizo hilo mwaka 2007, lakini mkataba huo haukusainiwa baada ya KKKT kushindwa kutimiza masharti muhimu, ikiwamo idadi ya watumishi waliokuwa wanatakiwa.
Inadaiwa KKKT walichukulia agizo hilo la halmashauri la kutaka vigezo hivyo muhimu vya kisheria vitimizwe kwanza kabla ya kusainiwa kwa mkataba kama ni usumbufu na kuandika barua nzito ya kulalamika kwenda Ikulu.
Habari hizo zinadai kuwa CCM wanachukulia kutosainiwa kwa mkataba huo kuwa huenda kukainyima kura hasa baada ya askofu wa dayosisi hiyo, Dk Martin Shao kulalamika hadharani kuhusu kutekelezwa kwa agizo hilo la rais.
Source Mwananchi