Date::9/18/2008
Hatimaye EU wakubali kutoa Sh860bilioni za maendeleo
Boniface Meena
Mwananchi
NCHI 14 washirika wa maendeleo katika Mpango wa Kuchangia bajeti ya Tanzania (GBS) wamepanga kuipatia serikali Sh860bilioni (sawa na Dola 750milioni za Marekani) kwa ajili ya mwaka wa fedha 2008/09 ambayo ni sawa na asilimia 12 ya bajeti yote ya serikali.
Kiwango hicho ni pungufu kwa asilimia 22 ukilinganisha na asilimia 34 ambazo washirika hao waliahidi kutoa katika bajeti nzima ya serikali ambayo ni Sh7.2 trilioni.
Uamuzi wa kutoa msaada huu umetokana na mazungumzo ya karibu baina ya washirika wa maendeleo pamoja na Serikali ya Tanzania, mazungumzo yaliyochukua miezi tisa baada ya kashfa za ufisadi kuwafanya wasitishe kuanza kutoa fedha hizo za msaada kwenye bajeti ya Serikali ya Tanzania.
Balozi wa Denmark nchini, Bjarne H Sorensen, ambaye kwa sasa ni mwenyekiti wa kundi la nchi 14 washirika wa GBS, alisema jana kuwa washirika wote wa mpango huo wamethibitisha kutoa mchango wao kwa mwaka huu wa fedha.
"Hii inadhihirisha kuheshimu ahadi zetu kwa maendeleo ya Tanzania," alisema balozi huyo. "Serikali ya Tanzania imeimarisha usimamizi katika Benki Kuu pamoja na kuchukua hatua za kinidhamu dhidi ya maofisa wanaohusika.
"Uchunguzi juu ya suala la EPA umefikia hatua nzuri, ikiwa ni pamoja na kuweza kurejeshwa kwa baadhi ya fedha zilizochukuliwa na kuwagundua wahusika. Serikali imetuhakikishia kuwa uchunguzi utaendelea mpaka kufikiwa kwa hitimisho kamili.
"Tanzania imepata maendeleo muhimu. Lakini hakuna shaka kwamba changamoto bado zipo. Tutazitilia mkazo changamoto hizi wakati washirika wa GBS na serikali kwa pamoja tutakapotathmini maendeleo yaliyofikiwa katika mkutano utakaofanyika Novemba mwaka huu."
Aisema washirika hao wanataka kufanya kazi na serikali na asasi za kiraia ili kupata fursa za kukuza uchumi, na kuhakikisha kwamba Watanzania walio masikini zaidi wananufaika na mpango huo.
Pia alisema: "Uwajibikaji wa ndani ni kitu muhimu sana. Na katika jambo hili tumetiwa moyo na mchango unaotolewa na vyombo vya habari, asasi za kiraia na Bunge katika kuendeleza uwajibikaji.
Mpango wa GBS unaipatia Serikali uwezo na motisha katika kuimarisha uwezo wake wa kubuni, kutekeleza na kufanikisha mipango yake ya maendeleo kwa muda mrefu na njia endelevu zaidi. Tutaendelea kufanya kazi pamoja na serikali kwa ukaribu ili kuhakikisha kuwa malengo na vipengele vya GBS vinaendelezwa, aliongeza Sorensen.
Washirika wa maendeleo ambao wako kwenye mpango huo wa GBS ni Benki ya Maendeleo ya Afrika (ADB), Canada, Denmark, Kamisheni ya Nchi za Ulaya, Finland, Ujerumani, Ireland, Japan, Uholanzi, Norway, Sweden, Uswisi, Uingereza na Benki ya Dunia.
Wakati washirika hao wakiridhia kutoa fedha hizo, serikali jana ilipokea kiasi cha Sh216 bilioni kutoka serikali ya Uingereza, ikiwa ni sehemu ya mpango wa GBS.
Akizungumza na waandishi wa habari, waziri wa Fedha na Uchumi, Mustafa Mkulo alisema serikali ya Uingereza ni moja ya nchi 14 washirika ambao husaidia bajeti kuu ya Tanzania kwa ajili ya kusaidia maendeleo.
Alisema misaada hiyo huenda moja kwa moja kwenye bajeti ya taifa na kuiwezesha serikali kutoa fedha katika sekta za maendeleo zilizopewa kipaumbele na kufanikisha Mkakati ya Kupunguza Umasikini na Kukuza Uchumi Tanzania (Mkukuta)
Taarifa ya maandishi kwa gazeti hili ya Julai 19 kutoka kwa Sorensen, ilithibitisha kwamba kundi la nchi hizo washirika lilifanya mkutano na Mkulo, ikiwa ni sehemu ya mikutano ya kawaida na mijadala wanayofanya na serikali hujadili na kuangalia maendeleo muhimu yatakayotoa fursa ya kuamua ni lini fedha hizo zianze kutolewa kwa bajeti ya mwaka 2008/09.
Katika taarifa hiyo, ilionekana kuwa washirika hao walikuwa wanasita kutoa fedha zao kusubiri hatua kuchukuliwa dhidi ya mafisadi, hasa katika sakata la wizi wa fedha za Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA), ufisadi ndani ya Benki Kuu ya Tanzania na taarifa ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Serikali (CAG).
Msimamo huu ulikwenda sambamba na kauli waliyotoa wakati wakiridhia kusaidia katika bajeti ya mwaka huu, waliposema: "Kabla ya kutoa fedha kusaidia bajeti hii, tunatazamia kupokea taarifa zaidi za utekelezaji wa namna serikali inavyopambana na tuhuma za rushwa, kuboresha utawala bora na utekelezaji wa mapendekezo ya CAG yaliyohusu ukaguzi wa hesabu za Benki Kuu ya Tanzania kwa mwaka wa fedha wa 2005/06."
Wafadhili hao waliahidi kuchangia asilimia 34 ya bajeti ya mwaka huu ya Sh7.2trilioni, hali ambayo iliiweka serikali kwenye wakati mgumu kama fedha hizo zisingetolewa kwa wakati kutokana na fedha hizo kutegemewa kwenye miradi mbalimbali ya maendeleo.
Mara ya mwisho washirika hao kuibana serikali katika bajeti yake ilikuwa wakati wa utawala wa serikali ya Awamu ya Pili iliyokuwa chini ya Rais Ali Hassan Mwinyi. Katika kipindi hicho, washirika hao walikataa kufadhili Tanzania kutokana na serikali kushindwa kukusanya kodi kiasi cha Sh70bilioni kwa wakati huo.
Wakati huohuo, serikali ya Marekani imesema Tanzania itahatarisha misaada yake kutoka nchini humo kama itagundulika kwamba misaada hiyo inatumika vibaya au kuishia katika mifuko ya viongozi mafisadi.
Akizungumza katika semina iliyoandaliwa na ubalozi wa Marekani nchini na kufanyika kwenye ukumbi wa hoteli ya Blue Pearl iliyo kwenye jengo la Ubungo Plaza, balozi wa Marekani nchini, Mark Green alisema wamarekani wanaisaidia sana Tanzania katika mambo mbalimbali, lakini iwapo watagundua kwamba misaada hiyo inatumika vibaya au kuishia katika mifuko ya viongozi mafisadi, watasitisha.
Sisi ni wakarimu sana, lakini si wapumbavu kama Rais George Bush alivyosema wakati alipoitembelea Tanzania Februari mwaka huu kwamba 'hatutoi fedha zetu kwa mataifa ya kifisadi,' alisema Green.
Alisema juhudi za Serikali ya Tanzania katika kupambana na ufisadi zinaonekana na imeifanya nchi kupata jina zuri katika jumuiya ya kimataifa, ikiwa kama mwanzilishi wa kweli wa vita dhidi ya ufisadi.
Alifafanua kuenea kwa programu za Mifumo ya Kufuatilia Matumizi ya Umma (PETS), kumesaidia sana katika kuipatia Tanzania jina zuri mbele ya jumuiya ya kimataifa.
PETS inawafanya watumishi wa Umma kukumbuka kwamba kuna watu wanawaangalia na sio viongozi tu, bali watu wa kawaida na imewasaidia Watanzania wa kawaida kujiamini kwamba serikali yao inalinda maslahi ya walio wengi na si ya mtu mmoja mmoja, alisema Green.
Alieleza kwamba katika hatua za awali za PETS wametoa mafunzo kwa zaidi ya waandishi 280 wa habari katika kuandika habari za uchunguzi, kutoa vifaa na mafunzo ya kupambana na ufisadi pamoja na kumsaidia mnunuzi mkuu wa vitu vya serikali katika kufanya ukaguzi wa manunuzi ndani ya mashirika mbalimbali ya kiserikali.
Katika hatua hiyo ya awali ambayo itamalizika mwishoni mwa mwezi huu alisema bila ya shaka kazi hiyo itaendelezwa na wale waliopatiwa mafunzo hayo.