SoC04 Hatua gani zichukuliwe kwa ubadhirifu unaobainishwa kwenye ripoti ya CAG ili kuchochea uwajibikaji?

SoC04 Hatua gani zichukuliwe kwa ubadhirifu unaobainishwa kwenye ripoti ya CAG ili kuchochea uwajibikaji?

Tanzania Tuitakayo competition threads
Joined
May 19, 2024
Posts
14
Reaction score
9
Nini maana ya UBADHIRIFU? Ubadhirifu ni hali ya kukosa uwezo wa kujizuia au kujidhibiti, katika matumizi ya Fedha au Rasilimali mbalimbali, na hii hutokea kwa wale waliopewa mamlaka za kuongoza Serikali ama Taasisi mbalimbali katika jamii zetu.

Je, nini kifanyike ili kuchochea Uwajibikaji dhidi ya wabadhirifu?

1.MIRADI YOTE YA SERIKALI HASA UJENZI SERIKALI ITOE VIFAA SIO PESA.
Tumeshuhudia mara nyingi katika Ripoti za kila mwaka za CAG, ambazo huwasilishwa kabla au tarehe 31 Machi kila mwaka, madudu mengi kwenye Taasisi za Umma huhusisha Fedha, hivyo tunaweza kudhibiti kwa sehemu fulani kwa kutoa vitendea kazi na si kutoa Pesa kwenye Taasisi hizo.
Nb; Picha ni kwa msaada wa Google

2:UBADHIRIFU ITANGAZWE KAMA JANGA LA TAIFA.
Serikali makini duniani kote ni ile inayokubali kuwajibika, Hasa pale madhaifu yanapotokea serikalini, ni lazima serikali ikubali kuwa jambo hili ni janga la Taifa, itakapokubali na kulitangaza rasmi, kuanzia hapo kama Taifa tutachukua hatua madhubuti, ikiwemo kubadili baadhi ya Sheria butu, ambazo zimekuwa hazina makali, watuhumiwa wameendelea tu kula maisha kila mwaka, kwakuwa Ripoti hizi kwao zimekuwa haziwashtui hata kidogo.

3:TEUZI ZA VIONGOZI SERIKALINI ZISIHUSISHE MAKADA WA VYAMA, HASA CHAMA TAWALA.
Nashauri kuwa ili tuitengeneze Tanzania tuitakayo, kwa miaka 25 ijayo, ni pale tutakapoamua kuwa, hizi nafasi za kuteuliwa Makada kuwa viongozi wa Taasisi au Serikali zikome, kwakuwa hapa ndipo penye dudumizi kubwa, mara nyingi tumeshuhudia baadhi ya Makada hawa wateuliwa, wanapotuhumiwa na kashfa za Ubadhirifu, wamekuwa wakikingiwa kifua na serikali yao, hivyo kudidimiza haki na kuendelea kukuza janga hili, wateuliwe kulingana na Taaluma zao, si kulingana na ukada wao.

4:KATIBA IFANYIWE MABADILIKO MADOGO JUU YA NI NANI AKABIDHIWE RIPOTI YA CAG.
Kulingana na Katiba yetu ya 1972 inazungumza kuwa, baada ya Mapitio yote na kukamilika kwa Ripoti, Mkaguzi mkuu wa serikali yaani CAG ataikabidhi Ripoti hiyo kabla au Tarehe 31 Machi kila mwaka kwa Rais, ninashauri kwa sehemu kubwa ili kuharakisha hatua kuchukuliwa mapema, Ripoti hii ikabidhiwe kwa Jaji mkuu na kisha Katiba imuelekeze Jaji mkuu kuwa, ndani ya Kipindi fulani, atoe mrejesho kupitia Televisheni ya Taifa, hatua zilizochukuliwa dhidi ya Watuhumiwa, kabla ya kuruhusu Ripoti nyingine kutoka, ili kupunguza mlundikano wa Ripoti kila mwaka, ambazo tumekuwa tukizipokea na kuishia Kusikitika tu.
Nb; Picha ni kwa msaada wa Google

5:MAMLAKA YA CAG IONGEZWE KIKATIBA
Ninashauri Mamlaka ya CAG iongezwe kikatiba, awe ni chombo huru kinachoweza kukamata, kufanya uchunguzi na kufungua Jalada kisha kuwafikisha watuhumiwa wa ubadhirifu huo mahakamani, pia katiba impe mamlaka CAG Kuwa, pindi anapotoa Ripoti yake ya mwaka mzima ya ukaguzi, wanaotajwa kama watuhumiwa, siku hiyo hiyo waachie nyadhifa zao, ili kuruhusu vyombo vya sheria kufanya taratibu za kiuchunguzi kwa uhuru, na pale itakapothibitika baadhi yao hawana hatia, ndipo warudishwe kazini.

6:KIUNDWE CHOMBO MAALUMU CHA KUPOKEA MAOMBI YA KAZI, MAMLAKA ZOTE ZA UTEUZI ZIONDOLEWE SERIKALINI.
Hebu kama Taifa kama kweli tumechoshwa na hali hii ya Ubadhirifu, hebu tukubali nafasi zote serikalini ziombwe na si kuteuliwa, maana baadhi ya mamlaka za uteuzi hazina uwazi, hivyo kuruhusu mianya mingi ya kujuana, na hii imefanya wengi wa viongozi wanaoteliwa, kutokuwa na sifa stahiki, hebu tuwape vijana wenye taaluma zao kazi, kisha tuwape imani hapo tutarudi baada ya miaka kadhaa na majibu mazuri, kwakuwa baadhi ya teuzi zimekuwa za kustaajabisha sana, baadhi yao huteuliwa ili wakapumzike huko kwakuwa wamekosa nafasi fulani fulani maeneo mengine, na kweli wamekuwa wakipumzika sana kuliko kuwajibika zaidi.

HITIMISHO
Tanzania niitakayo kwa miaka 25 ijayo, ni ile iliyochoshwa na Ubadhirifu, na ikaamua kuchukua hatua stahiki nilizozielekeza hapo juu, hapo ndipo kama Taifa tutashuhudia mabadiliko makubwa sana ya Kisekta katika Taasisi zetu za Umma.

NGUVU YA KUTHUBUTU NA KUFANYA ndiyo itakayoamua hayo yote kuwazekana.
000411_238562112_be525406.jpg
cag-pic-data.jpg
 
Upvote 7
Back
Top Bottom