Walianza zamani kumuondolea Uhuru Mtanzania.
Pale Mnazi Mmoja wakaweka uzio, hakuna mtu kuingia au kutoka. Labda vile vyuo vya India na China ndiyo vinaruhusiwa.
Wakaja kwenye sheria, moja baada ya nyingine zikatungwa. Sheria za mitandao. Sheria za vyombo vya habari. Sheria za uchaguzi. Moja baada ya nyingine ikawa taratibu na kwa kasi inaondoa uhuru wa Mtanzania.
Hizo zikawa hazitoshi. Wakaondoa sherehe za uhuru. Kwa miaka sasa wanajificha kwenye chaka la kutumia fedha za sherehe kufanya hiki au kile. Nia Watanzania wazoee kuona uhuru wao siyo jambo muhimu kuliko "miundombinu".
Sasa hamruhusiwi hata kulalamika kwa lolote. Hamruhusiwi kulia pale mnapofiwa na ndugu zenu au mnapopata majeraha ya risasi.
Kila lalamiko, kila kilio, kila maumivu uliyonayo ni kosa la jinai linalokurudia wewe mwenyewe Kibaya zaidi, unaweza ukahukumiwa bila hata kufikishwa mahakamani na hukumu haijulikani anatoa nani.
Watawala wakiendelea kutunisha vifua, watapata watakachostahili. Kama hawa watawala walitaka historia iwakumbuke, nadhani mpaka sasa wameshafanikiwa. Historia itawakumbuka.