Chuo Kikuu cha Dodoma kwa kushirikiana na Tume ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano wameendesha programu maalum ya uhamasishaji kwa wanafunzi wa mwaka wa mwisho wa Tehama, ikiwa ni sehemu ya kuwajengea uelewa kuhusu umuhimu wa usajili wa kitaaluma kwa wataalamu wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano kabla na baada ya kuingia katika soko la ajira.
Programu hiyo iliyofanyika Juni 6, 2026, imelenga kuhakikisha wahitimu wa Tehama wanatambuliwa rasmi kama wataalamu waliothibitishwa, hatua inayotarajiwa kuimarisha ubora wa huduma za kidigitali, kuongeza weledi na kulinda viwango vya taaluma nchini.
Akizungumza katika hafla hiyo, mwakilishi kutoka Tume ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano alieleza kuwa taasisi hiyo ina jukumu la kusimamia maendeleo ya sekta ya TEHAMA nchini, ikiwemo kutambua na kusajili wataalamu wa fani hiyo ili kuhakikisha huduma za kidigitali zinakuwa za viwango vya juu na salama.
Alisisitiza kuwa usajili wa wataalamu wa Tehama ni muhimu katika kuongeza uaminifu, kuimarisha maadili ya kitaaluma, pamoja na kulinda viwango vya sekta ya teknolojia nchini.
Katika warsha hiyo, wanafunzi wa mwaka wa mwisho wa Tehama walipata elimu kuhusu mchakato wa usajili na umuhimu wake katika maandalizi ya kuingia kwenye soko la ajira. Maafisa Tehama Gibson Mwasenga na Haji Lunga walikuwa miongoni mwa wawezeshaji, wakitoa maelekezo ya hatua za kujisajili pamoja na faida zake kwa wahitimu.
Gibson Mwasenga ni mmoja kati ya wawezeshaji katika warsha hiyo alisema:
“Usajili wa kitaaluma unampa mhitimu utambulisho rasmi unaomsaidia kuongeza ushindani wake katika soko la ajira na kumuwezesha kutambulika kitaifa.”
Kwa upande wake, Haji Lunga aliongeza:
“Sekta ya TEHAMA inabadilika kwa kasi kubwa. Ni muhimu kwa wahitimu kuendelea kujifunza na kuboresha ujuzi wao ili kuendana na mabadiliko ya teknolojia duniani.”
Mwisho wa programu hiyo, wanafunzi wa mwaka wa mwisho wa TEHAMA walihimizwa kutumia fursa ya usajili wa kitaaluma kama sehemu ya maandalizi yao ya kazi, huku wakisisitizwa kushirikiana na taasisi za elimu na serikali ili kujijenga kuwa wataalamu wenye ushindani katika soko la ajira.